07-28-2021, 08:04 AM
KISWAHILI KAMA CHOMBO CHA KUTANGAZA NA KUUZA VYOMBO VYA HABARI NCHINI KENYA
Mark A. Odawo na Jacktone O. Onyango
Ikisiri
Makala1 hii inatathmini ufaafu wa matumizi ya maneno ya Kiswahili kama anwani ya vituo vya redio vilivyochipuka katika miaka ya hivi karibuni nchini Kenya. Makala inaangalia jinsi ambavyo hali hii inaweza kuchangia uimarishaji wa lugha ya Kiswahili kwa jumla. Tangu azali na hata enzi ya ukoloni, lugha ya Kiswahili imekuwa zana muhimu ya mawasiliano timilifu sio tu katika ukanda wa Afrika Mashariki bali pia kwa umma mkubwa wa kimataifa. Matumizi ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za binadamu yamekuwa mhimili muhimu wa kukuza na kueneza lugha hii (Tuli, 1985). Katika kizazi cha kisasaleo, harakati za kiuchumi zimejifaragua kutoka biashara ya bidhaa na kujumuisha huduma mbalimbali ikiwemo habari. Kama huduma, habari imekuwa nguzo muhimu ya ufanisi. Dhima ya habari katika maendeleo ya dunia ya kisasaleo imeifanya kuwa huduma ambayo wateja wake wanaongezeka kila uchao. Hii ni hali mojawapo iliyochangia kuchipuka kwa vituo vingi vya redio vinavyoitwa vya Kiswahili ambavyo hutoa matangazo yao kwa Kiswahili. Makala hii inajikita katika kuangalia ufaafu na uamilifu wa majina au anwani na kaulimbiu zenye maneno ya Kiswahili kwa vituo vya redio vilivyoanzishwa na vyombo vya habari katika miaka ya hivi karibuni. Makala inaangalia matumizi ya maneno haya ya Kiswahili kutajia vituo vya redio sawa na mikakati ya kutoa mshawasha kwa wasikilizaji kuonea fahari vituo hivi na kuwateka ili waendelee kuvisikiliza. Kwa namna hii, lugha ya Kiswahili hujitokeza kuwa na uwezo wa kutanguliza, kutambulisha, kutangaza na kuuza vituo hivi kwa umma mkubwa wa wasikilizaji. Kadri wasikilizaji wanavyoendelea kusikiliza na kuchangia mijadala katika vituo hivi ndivyo vituo hivi vinavyoendelea kukubalika kuwa maarufu miongoni mwa wasikilizaji. Vivyo hivyo ndivyo lugha ya Kiswahili inavyoendelea kuimarika, kupanuka na kuenezwa na hivyo kuakisi mustakabali bora wa lugha ya Kiswahili.
1 Makala hii iliwasilishwa kwa mara ya kwanza katika Kongamano la Kiswahili la CHAKITA lililofanyika katika Taasisi ya Maendeleo ya Mtaala wa Elimu (KICD), Nairobi, Oktoba 23-24, 2014.
1.0 Utangulizi
Ijapokuwa kuna nadharia tofauti kuhusu chimbuko na kuenea kwa Kiswahili, wataalam wengi wakiwamo Chiraghdin na Mnyampala (1977) na Chacha (1995) wanaafikiana kuwa lugha hii ina kitovu chake pwani na kuwa ilienea kutoka upwa wa bahari ya Hindi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki. Sengo (1995) anadai kuwa Kiswahili ni kizalia cha lugha asili za Waafrika hususan wakazi wa mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki kabla ya majilio ya wageni. Kwa mujibu wa Whiteley (1969), Chiraghdin na Mnyampala (1977), Mbaabu (1985, 1991a) na Ogechi (2002), miongoni mwa zana muhimu za kuenea huku kwa lugha tangu awali ni utawala wa kikoloni, siasa, elimu, biashara, ndoa, machapisho na vyombo vya habari ambavyo mchango wake umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni kutokana na uwezo wake wa kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja.
Zana hizi zinajitokeza kama sehemu muhimu ya shughuli za binadamu ambazo zimesawiri Kiswahili kama chombo muhimu cha mawasiliano timilifu sio tu katika ukanda wa Afrika Mashariki bali pia kwa umma mkubwa wa kimataifa (Tuli, 1985). Kwa kufanya hivi, lugha hii imefanikisha si mahitaji ya watu binafsi tu bali pia malengo ya makundi na taasisi anuwai. Onyango (2014) anasema kuwa lugha ya Kiswahili inatumiwa kuleta maendeleo ya uchumi nchini Kenya kwa kufanikisha mawasiliano ya kibiashara katika sekta mbalimbali ikiwamo sekta ya huduma za benki. Matumizi ya Kiswahili katika shughuli hizi yamekuwa mhimili muhimu wa makuzi, malezi na maenezi ya lugha hii.
Katika kizazi cha kisasaleo, harakati za kiuchumi zimejifaragua kutoka biashara ya bidhaa na kujumuisha huduma mbalimbali ikiwamo habari. Kama huduma ya habari imekuwa nguzo muhimu ya ufanisi, habari za shughuli za kijamii kama vile sanaa na burudani na zile za kiuchumi kama vile kazi, biashara na uzalishaji huwafikia walengwa wengi kwa haraka zaidi kupitia vyombo vya habari. Hivi ni kusema kuwa dhima ya habari katika maendeleo ya dunia ya kisasaleo imeifanya kuwa huduma ambayo wateja wake wanaongezeka kila uchao.
Hii ni hali mojawapo iliyochangia kuchipuka kwa vituo vingi vya redio vinavyoitwa vya Kiswahili na pia kutangaza kwa lugha ya Kiswahili katika miaka ya hivi karibuni nchini Kenya, hasa baada ya masharti ya utoaji wa leseni ya masafa ya utangazaji kulegezwa mwaka 1999. Maswali tunayojiuliza katika makala hii ni: Je, majina haya ya vituo vya redio yanayosheheni istilahi za Kiswahili yanaathiri vipi usikilizaji wa vituo hivi? Kiswahili kinachotumika kufikisha habari kwa walengwa ni cha kiwango gani? Nini hatima na mustakabali wa lugha ya Kiswahili katika mchakato huu wote? Ni katika kujibu maswali haya ndipo makala hii inatathmini ufaafu wa matumizi ya maneno ya Kiswahili kama anwani na kaulimbiu ya vituo vya redio vilivyochipuka kati ya mwaka 1999 na 2014 na jinsi ambavyo hali hii inaweza kuchangia uimarishaji wa lugha ya Kiswahili kwa jumla. Makala inaangalia matumizi ya maneno ya Kiswahili kutajia vituo vya redio sawa na mikakati ya kutoa mshawasha kwa wasikilizaji kuonea fahari vituo hivi na kuwateka ili waendelee kuvisikiliza. Data za makala hii zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya kusikiliza vituo vya redio, mahojiano na wasikilizaji na watangazaji wa vituo vya redio na pia mtandaoni. Makala imegawanywa katika sehemu sita zinazofuatana kama ifuatavyo: utangulizi, vituo vya redio vyenye anwani za Kiswahili, kaulimbiu za vituo vya redio, matumizi ya lugha katika vituo vya redio, mapendekezo na hitimisho.
2.0 Vituo vya Redio vyenye Anwani za Kiswahili
Kufikia mwaka 1999, vituo vya redio nchini Kenya vilikuwa 10 pekee. Mwaka 2004 idadi hiyo iliongezeka na kufikia 118 (BuzzKenya.com; Communications Authority of Kenya, 2014). Idadi kubwa ya vituo hivi imeongezeka kuanzia mwaka 2000 wakati sekta ya habari na utangazaji ilipowekwa huru kutokana na masharti ya utoaji wa masafa ya kutangazia kulegezwa na hivyo kuwaruhusu wamiliki binafsi kuanzisha vituo vya redio.
Mbali na kutoa matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili, baadhi ya vituo hivi hutoa matangazo yao kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyingine za kiasili. Kati ya vituo 118, vituo 30 vinatumia Kiswahili kama sehemu za anwani za vituo hivyo. Mbinu ya usampulishaji lengwa imetumiwa kuviteua vituo hivyo 30 ambavyo vimetumiwa katika uchanganuzi na maelezo. Vituo hivi ni Redio Maisha (Nairobi), Redio Jambo (Nairobi), Baraka FM (Nairobi), Redio Salaam (Mombasa), Sauti ya Mwananchi FM (Nakuru), Rehema FM (Nairobi), Redio Pamoja (Nairobi), Bahari FM (Mombasa), Jambo FM (Nairobi), Amani FM (Nakuru), Sifa FM (Voi), Redio Umoja (Nairobi), Redio Kisima (Nyamira), Biblia Husema Redio (Nairobi), Injili FM (Kericho), Mambo FM (Nairobi), Pwani FM (Mombasa), Imani FM (Kitale), Sauti ya Rehema Redio (Sayare Radio) (Eldoret), Milele FM (Nairobi), Pilipili FM (Mombasa), Sema Redio (Kericho), Redio Simba (Kampala, Uganda), Redio Waumini (Kasarani, Nairobi), Risala FM (Garissa), Bahasha FM (Nakuru), Hosana FM (Nairobi), Mwangaza FM (Dodoma, Tanzania), Neema FM (Mwanza, Tanzania), na Rock Mambo FM (Tororo, Uganda). Baadhi ya vituo vya redio vya Tanzania na Uganda vimejumuishwa katika makala hii kwa sababu matangazo yake hufika pia Kenya.
Mifano michache ifuatayo inaonyesha jinsi majina haya ya Kiswahili yanayotumiwa kutajia vituo vya redio yanavyoafiki na kuathiri usikilizaji wa vituo hivi.
i) Redio Jambo
Katika kujinasibisha na wasikilizaji, inazingatiwa kuwa msikilizaji yeyote aliye na jambo linalomkera aliwasilishe katika kituo hiki ili litatuliwe. Kituo hiki huwa na kipindi maarufu kinachoitwa ‘Patanisho’ ambapo wasikilizaji walio na jambo linalotatiza mahusiano yao na wengine wanaruhusiwa kupiga simu ili waweze kupatanishwa kutokana na rai au nasaha za watangazaji pamoja na ushauri wa wasikilizaji wengine wanaoruhusiwa kutoa maoni yao kwa kupiga simu moja kwa moja au kutuma ujumbe mfupi kwa nambari ambayo hutolewa. Aidha, wasikilizaji wanahusishwa katika mijadala ya masuala yanayojiri na kuathiri maisha ya kawaida ya wananchi. Hivyo basi, kituo hiki kimeweza kushawishi wananchi kuwa na ujuzi wa mambo mbalimbali yanayohusu sanaa, michezo, mapenzi na siasa kutegemea usikilizaji wa kituo hiki. Yamkini dhana kama hii inaweza kuhusishwa na vituo kama vile Jambo FM, Mambo FM na Rock Mambo FM.
ii) Redio Maisha
Kituo hiki hujaribu kujitambulisha na masuala yanayowakumba wasikilizaji wake katika maisha yao ya kila siku. Kwamba yeyote anayetaka kujua mambo muhimu yanayohusu maisha ya kisasa hana budi kusikiliza kituo hiki. Katika utangazaji wake, kituo hiki kinaangalia maisha kuwa ‘matamu’ na kwamba mada zote zinazofanya maisha kuwa ‘matamu’ kama vile mapenzi, sanaa na michezo hutokana na kusikiliza kituo hiki. Kwa hiyo, wasikilizaji wanakiona kama kitovu cha maisha.
iii) Milele FM
Kituo hiki hulenga kuwapasha habari na kuwaburudisha wasikilizaji wake wakati wote au ‘milele’ kama ambavyo jina lake linavyoonesha. Kituo hiki ni maarufu kwa nyimbo za dini ya Kikristo na kilishinda tuzo ya kituo kinachocheza muziki mzuri zaidi wa kidini nchini Kenya kwa miaka mitatu iliyopita. Mtangazaji aliyetambuliwa kuwa bora zaidi ni Eva Mwalili (Groove Awards, 2014). Hivi ni kusema kuwa kituo hiki kinawahakikishia wasikilizaji wake ‘uzima wa milele’.
iv) Redio Waumini
Kituo hiki kinajihusisha na matangazo, mijadala na uchezaji wa muziki wenye mada za dini ya Kikristo. Hivi ni kusema kuwa waumini wote wanaweza kutoshelezwa haja zao za kiroho wanaposikiliza kituo hiki. Hivyo basi, kituo hiki kinajitokeza kama chombo cha kuwabadilisha watu ili wawe waumini wa dini ya Kikristo. Hii ndiyo hali ambayo aghalabu hujitokeza katika vituo kama vile Baraka FM, Injili FM, Imani FM, Rehema FM, Sauti ya Rehema Redio (Sayare Radio), Hosana FM, Biblia Husema Redio na Neema FM vinavyolenga kutambulishwa kwa waumini kama vituo vinavyohusishwa na mada za kidini.
v) Sauti ya Mwananchi FM
Kituo hiki kinajitokeza kama mtetezi wa mwananchi kwa kuangazia changamoto zinazowakumba. Kinajaribu kuwapa wananchi muda wa kutosha kutoa kauli zao kuhusu masuala yanayowahusu na kuwaathiri moja kwa moja. Maoni ya wananchi yanapewa umuhimu mkubwa na watangazaji wa kituo hiki. Hali inayojitokeza hapa ni kuwa kituo hiki kinajitokeza kama mtetezi wa wasikilizaji (Mahojiano yetu na Wasikilizaji wa Kituo hicho, tarehe10 Oktoba, 2014, Nakuru).
vi) Redio Umoja
Kituo hiki hujinasibisha na kuleta umoja, mshikamano na mtagusano miongoni mwa wasikilizaji wake licha ya maoni ya wasikilizaji hao kutofautiana wakati mwingine. Kwa hiyo, kituo hiki hujaribu kujenga fikra za maafikiano na utangamano miongoni mwa wasikilizaji pamoja na watangazaji wa kituo hiki. Kinawasawiri wasikilizaji kama wamoja. Kituo hiki kinaonekana kuwa na mkabala ulio sawa na kituo cha Redio Pamoja. Kuna madai kwamba baadhi ya idhaa za redio na wanahabari walichangia katika ghasia zilizofuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007/2008 nchini Kenya maarufu kama PEV (Post Election Violence). Inawezekana kwamba kuanzishwa kwa baadhi ya vituo hivi vya redio ni juhudi za wawekezaji kupata faida na pia kuondoa utengano uliopandwa wakati wa ghasia hizo. Kwa hivyo, hizi ni juhudi za kuleta uwiano na utangamano miongoni mwa Wakenya.
vii) Pwani FM
Kituo hiki kimsingi kinatoa matangazo yake kutoka maeneo ya pwani, ingawa pia, kinaangazia pia masuala yanayosheheni taifa zima. Hata hivyo, kituo hiki huelekea kuonekana ‘miliki’ ya wenyeji wa mwambao wa pwani, hasa maeneo ya Mombasa, Kwale na Malindi, ambao ndio hujihusisha nacho zaidi. Hivi ni kusema kuwa wasikilizaji wake wanakionea fahari kubwa kama ilivyo kituo cha Bahari FM.
viii) Redio Kisima
Kama kisima kinachotoa maji safi kwa matumizi ya binadamu, kituo hiki huwa kama kitovu cha habari zote muhimu anazohitaji msikilizaji kuhusu nyanja zote za maisha. Kituo hiki wakati mwingine huangazia masuala nyeti na mada nzito zinazoamsha hisia na kuwakanganya wasikilizaji kwa nia ya kupata suluhu inayokubalika kwa wote. Mada hizo ni pamoja na ndoa, mapenzi, malezi, lishe na imani. Hii ni kwa sababu kituo hiki kina msingi wake katika dini ya Kiadventista.
ix) Sema Redio
Kituo hiki huonekana kutilia mkazo utoaji wa nafasi kwa wasikilizaji wake kusema jambo lolote na kutoa maoni waliyonayo kuhusiana na matukio ya kila siku katika jamii. Mbali na kusemezana wao kwa wao, wasikilizaji husemezana na kujadiliana na watangazaji wa kituo hiki. Hivyo basi, kituo hiki kinaonekana kuthamini maoni na hoja za wasikilizaji wake kuhusu masuala tofauti yanayowashughulisha.
3.0 Kaulimbiu za Vituo vya Redio
Baadhi ya vituo vya redio vinavyotumia Kiswahili kama anwani yake pia huwa na kaulimbiu zilizoandikwa kwa lugha hii. Japo baadhi ya vituo vya redio havina majina ya Kiswahili, vimeshehenezwa na kaulimbiu zinazohusisha lugha ya Kiswahili. Hapa inabidi tuvuke mipaka ya redio 30 zilizotajwa katika sehemu ya 2.0 na kutaja mifano ya redio tatu ambazo hutangaza kwa Kiswahili kote nchini na hutumia kaulimbiu za Kiswahili ili kuonyesha jinsi zinavyoathiri usikilizaji. Redio nyingi kati ya zile 30 zilizotajwa hazitangazi kote nchini. Ifuatayo ni baadhi ya mifano na jinsi inavyoathiri usikilizaji wa vituo vya redio husika.
i) KBC Kiswahili – Redio Taifa
Kituo hiki kinalenga kutoa habari muhimu zinazogusia masuala ya kitaifa. Hivi ni kusema kuwa kituo hiki kilianzishwa kwa ajili ya taifa zima na kuwa wasikilizaji wote wanaweza kukitumia kutoa sauti au maoni yao kuhusu taifa. Kwa namna hii kituo hiki kinahimiza wasikilizaji kukionea fahari na hivyo kuendeleza fikra za utaifa na uzalendo miongoni mwa wasikilizaji kutokana na kuwashirikisha katika shughuli zinazojenga utangamano.
ii) Redio Citizen – Chemchemi ya Ukweli
Jina la kituo hiki inakieleza kuwa kama chanzo na mbubujiko usio na mwisho wa habari za kina na hakika kuhusu nyanja zote za maisha. Ni kana kwamba kituo hiki ndicho kinachopaswa kuaminika kwa usahihi wa habari kwani huenda vingine vimepungukiwa uwezo huo au vinaweza kupotosha ujumbe.
iii) Redio Maisha – Tuko Mbele Pamoja
Tamko hili hujaribu kusisitiza umoja na utangamano kati ya watangazaji na wasikilizaji. Ujumbe unaofikishwa hapa ni kuwa umoja na ushirikiano ndio nguzo ya ufanisi. Kwamba kadri kituo hiki kinavyoendelea kujiimarisha ndivyo wasikilizaji pia watakavyoweza kuendelea na kwamba kituo hiki huweza kufifia iwapo wasikilizaji hawapo. Kwa hiyo, kituo hiki kinajaribu kujihusisha na kujinasibisha na wasikilizaji kama vipande visivyoweza kutenganishwa.
iv) Q FM – Kata Kiu
Q FM (Kiu FM) ni kituo kinachojifananisha na kinywaji baridi kinachoweza kunywewa ili kukata kiu ya mnywaji. Hali ya wasikilizaji kutopata habari za kina inaangaliwa sawa na kuwa na kiu. Hivyo basi, yeyote anayetaka kupata taarifa za kweli na burudani za kutosha hana budi kusikiliza matangazo kutoka katika kituo hiki ili ‘kukata kiu’ yake. Dhana kuu inayotokana na kaulimbiu hii kimsingi huelekea kuoana na ile ya kituo cha Redio Kisima inayojulikana kama ‘Chota unywe’.
v) Milele FM – Wewe ni WetuUjumbe ulio katika kaulimbiu hii ni ule unaomthamini msikilizaji kama sehemu muhimu ya kituo hiki. Dhana inayojitokeza hapa ni hali ya umoja, mshikamano na utambulisho wa kituo hiki na wasikilizaji wake. Hivi ni kusema kuwa maoni au mchango wa wasikilizaji wa kituo hiki ndiyo yanayojenga msingi wa matangazo ya kituo hiki.
Dhana zinazobainika katika anwani za vituo hivi vya redio na kaulimbiu zake zinaviafiki kwa kuwashawishi wasikilizaji kuendelea kuvisikiliza, kuvionea fahari na kujinasibisha navyo. Kwa njia hii, anwani na kaulimbiu hizi hujitokeza kama mbinu muhimu za kutambulisha na kutangaza vituo hivi kwa wasikilizaji wake.
MarejeleoAhmed, S. (2013). “Tungo za Kinahau Zinazotoa Taarifa ya Mpira wa Miguu katika Magazeti ya Kiswahili”, Mulika. Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.
BuzzKenya.com <http://buzzkenya.com/Redio-stations-in-kenya/ 25 Septemba 2016>
Chacha, L. M. (1995). “Chimbuko la Kiswahili”, katika BARAGUMU, Juzuu la 2 Nam. 1&2 kur. 1-7.
Chiraghdin, S. na Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.
Communications Authority of Kenya, June 2014. <http://www.ca.go.ke/ 25 Septemba 2016>
Groove Awards, 2014. <www.grooveawards.co.ke 25 Septemba 2016>
King’ei, K. (2000), “Matatizo ya Matumizi ya Lugha katika Vyombo vya Habari: Mifano kutoka Kenya” katika Swahili Forum VII. 45-56.
King’ei, K. na Musau, P. (2000). Utata wa Kiswahili Sanifu. Nairobi: Didaxis.
Marshad, H. (1993). Kiswahili au Kiingereza nchini Kenya? Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Mbaabu, I. (1985). New Horizons in Kiswahili. Nairobi: Kenya Literature Bureau.
Mbaabu, I. (1991a). Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili. Nairobi: Longman Kenya Ltd.
Mbaabu, I. (1991b). “The Impact of Language Policy on the Development of Kiswahili in Kenya, 1930-1990.” Ph.D Thesis, Howard University.
Mbaabu, I. (1995). Usahihishaji Makosa katika Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers.
Mlacha, S.A.K. (mh) (1995). Kiswahili na Vyombo vya Habari. Dar-es-Salaam: TUKI.
Momanyi, C. (2001). “Matumizi ya Kiswahili katika Njia Panda: Mtazamo wa Kiisimu-Jamii,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.
Momanyi, C. (2009). “The Effect of ‘Sheng’ in the Teaching of Kiswahili in Kenyan Schools,” katika Journal of Pan African Studies, 2(8): 127-138.
Musau, P. M. (2001). “Freeing the Airwaves or Cultural Enslavement: The Case of Media in Kenya,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press. Pp. 36-42.
Ogechi, N. O. (2002). Mbinu za Mawasiliano kwa Kiswahili. Nairobi: Moi University Press.
Onyango, J.O. (2002). AKS 102: Historical Development of Kiswahili. (Bachelors Module). Institute of Open Learning, Kenyatta University.
Onyango, J. O. (2014). “Kiswahili kama Lugha ya Mawasiliano katika Shughuli za Benki: Changamoto za Tafsiri”. Katika Simala, I., Chacha, L. na Osore, M. (wahr). Miaka Hamsini ya Kiswahili Nchini Kenya. Nairobi: Twaweza Communications. 107-112.
Sengo, T. S. Y. (1995). “Hali ya Kutatanisha ya Kiswahili hivi leo Afrika ya Mashariki”, Makala yaliyotolewa katika Kongamano la Nane la Kiswahili, Chuo Kikuu cha Bayreuth, Mei 26-27, 1995.
Tuli, R. S. K. (1985). Chimbuko la Kiswahili, Kukua na Kuenea kwake Afrika Mashariki. Arusha: Utalii Exporters and Publications.
Waihiga, G. (1999). Sarufi Fafanuzi ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers.
Whitely, W. H. (1969). Kiswahili: The Rise of a National Language. London: Methuen.
Mwl Maeda