VYOMBO VYA HABARI NA MATUMIZI YASIYO SAHIHI YA LUGHA NA ATHARI ZAKE KWA WASIKILIZAJI WAKE
- UTANGULIZI
Andiko hili ni maalumu kwa watu wa habari hapa nchini pamoja na watanzania wote na watumiaji wa lugha ya Kiswahili kama lugha muhimu ya mawasiliano Tanzania. Lengo la andiko hili ni kujaribu kuonesha jinsi gani kupitia habari, upo ukiukwaji mkubwa wa matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili, na jinsi ambavyo makosa kama hayo yanavyorudisha nyuma maendeleo na ukuaji wa lugha yetu adhimu ya Kiswahili ambayo ni hazina kubwa kwa urithi na utajiri wa nchi hii.
1.1 LUGHA
Kabla ya kuzama ndani ya kiini cha andiko hili, ni vema tukapata fasili ya lugha. Wataalamu wengi wa sayansi ya lugha(isimu ya lugha) wanakubaliana kuwa lugha ni, “mfumo wa sauti nasibu ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao (Massamba et al,2012:1 na Malenya, 2012:14). Aidha, dhumuni kubwa la lugha chombo muhimu cha mawasiliano na kiashirio kiashirio kikuu cha uhimara wa kisaikolojia na afya ya mihimili ya kijamii kama vile familia, makundi ya watu katika jamii au mahala pa kazi. . . Hivyo basi, lugha ni utaratibu halisi kwa kila maelewano kwa kuzingatia maana na matumizi ya wanajamii na utamaduni wao. Lugha inapokosa kueleweka ndipo mawasiliano huzua utata na makusudiao mengi kwenda mrama kwa kukosa mwelekeo maalum. Ni muhimu kwa mwanajamii yeyote anayetoa ujumbe kuzingatia lugha mwafaka inayoeleweka ili kuondoa mapungufu ya kutoelewana na kupotosha ujumbe uliolengwa (Malenya, 2012:14).
Kwa matiki hii tunaweza kung’amua kuwa dhumuni kubwa la lugha ni kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wanajamii wanaotumia lugha hiyo. Na urahisi huo wa mawasiliano, ni kupitia matumizi mema ya lugha fasaha na lugha sanifu. Waaidha, matumizi mabaya ya lugha yoyote ile husababisha ugumu wa mawasiliano na kutoelewana miongoni mwa wahusika wa lugha maalumu. Kupuuzia kanuni za lugha ama kwa kutojua au kwa makusudi, ni nyenzo rahisi ya kuelekea kuiharibu lugha na kuleta mikanganyiko miongoni mwa wanajamii hasa kwa kukosa kupata ujumbe mahususi uliolengwa na kufanya hivyo ni kuharibu mawasiliano kwa kutokuelewana.
1.2 LUGHA YA KISWAHILI
Katika jamii zetu za Tanzania, lugha inayotumika kwa kiasi kikubwa ili kurahisisha mawasiliano kwa taifa ni lugha ya Kiswahili, ambayo ndio lugha mama au lugha ya taifa kwa Tanzania. Lugha ya Kiswahili, ni lugha inayoongelewa zaidi afrika mashariki; yaani, kwa maneno mengine tunasema kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha ya afrika mashariki, ikizungumzwa katika nchi zote za ukanda wa afrika mashariki zote. Aidha, kwa mujibu wa utafiti juu ya lugha hii, inasadikika kuwa idadi ya waongeaji wa lugha hii inakadiriwa kufika zaidi ya milioni 60.[1] Lugha hii ndiyo itumikayo katika shughuli zote za mawasiliano, ikiwa ni lugha ya taifa nchini Tanzania na Kenya, na lugha rasmi itumikayo katika shughuli za kiserikali maofisini. Kwa hiyo, unapoongea Kiswahili, hakika unaonge utamaduni wa mtu wa afrika mashariki, kwani lugha ndio kiashiria kikubwa cha utamaduni husika. Lugha ya Kiswahili inazo sifa zote za lugha kama zilivyo lugha zingine ulimwenguni. Hivyo basi, kutokana na dhumuni la makala hii, lugha ya Kiswahili imekuwa ikikumbana na vizingiti mbalimbali vinavyoirudisha nyuma katika maendeleo. Na watanzania wenyewe ndio hao hao wanaochangia katika kuiharibu lugha hiii.
1.2.1 MAKOSA YANAYOFANYWA KATIKA TAALUMA YA HABARI
YENYE KUTATIZA MAENDEEO YA KISWAHILI.
Lugha ya Kiswahili imekumbwa na misukosuko mingi, na baadhi ya misukosuko hiyo ni ile ambayo inajaribu kurudisha nyuma maendeleo yake. Sehemu moja wapo ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya Kiswahili ni katika tasnia ya habari au taaluma ya habari, kupitia vyombo vyake, waandishi na watangazaji wa habari. Makosa hayo ya lugha yanayofanyika katika uga wa habari, yanaathiri kwa kiasi kikubwa utaratibu mzima wa lugha, kwani wasilikizaji wa vyombo vya habari wanaathirika na makosa hayo kwa kuyaendeleza katika matumizi ya mawasiliano, wakijua ni sahihi kwa kuwa neno au jambo lolote linalotolewa kupitia vyombo vya habari huwa ni sahihi. Kwa hiyo, wananchi wana imani sana na vyombo vya habari na hivyo makosa yoyote yale yanayofanywa katika tasnia ya habari ni rahisi kuenea na kuathiri ukweli au utaratibu wa jambo husika kama lugha ya Kiswahili. Yafuatayo ni baadhi ya makosa yanayofanyika mara kwa mara katika taaluma ya habari hapa Tanzania yanayoharibu lugha ya Kiswahili:
Makosa ya kisarufi
Sarufi ni utaratibu maalumu wa lugha husika. Utaratibu huu ni kanuni, sheria au kaida nyingine zinazotawala mfumo mzima wa lugha ili iweze kukubalika na kueleweka katika matumizi ya lugha hiyo kwa wanajamii. Hivyo tunapoongea sarufi ya lugha moja kwa moja tunalenga utaratibu maalumu wa lugha Fulani. Kama zilivyo lugha nyingine, Kiswahili kina utaratibu wake pia, yaani sarufi ya Kiswahili, ambayo inafanya lugha hii kuwa katika utaarabu wake.
Katika matumizi ya lugha, wadau wengi wa habari hasa waandishi, wa habari, watangazajia, na wahariri wa habari, wamekuwa wakifanya makosa ya kisarufi ya mara kwa mara katika habari wanazoandika na kuzichapisha kama zilivyo. Habari za magazetini, kwenye mitandao, runinga, hata zile zinazosikika redioni, hujaaa makosa mengi ya kisarufi. Makosa hayo ni kama kuchanganya au kuhazima sarufi ya lugha za kigeni kama kiingereza na kuitumia katika Kiswahili; mathali, mtangazajia katika kujitambulisha anaweza kusema “yangu majina” badala ya jina langu; “yangu matumaini” badala ya matumaini yangu. “Yangu Majina” ni sarufi ya Kiingereza sio ya Kiswahili, halafu katika Kiswahili hatuna dhana ya majina; majina’ kwa mtu mmoja, bali tuna jina. Katika utaratibu sahihi wa Kiswahili, jina/nomino hutangulia kivumishi na kivumishi hufuata kwani kivumishi hufanya kazi ya kutoa sifa kwa jina, ila kwa kiingerza utaratibu ni tofauti kwani kivumishi huweza kutangulia nomimo – mfano: my name (jina langu), beautiful lady( binti mrembo), strong man (mtu shupavu) n.k. Katika mifano hii, tungo za Kiswahili kwenye mabano ndio muundo sahihi kisarufi wa Kiswahili lakini kiingereza ni tofauti kwani katika kiingerza kivumishi hutangulia nomino katika mazungumzo au maandishi. Vilevile kutofuata kanuni za lugha ya Kiswahili imekuwa ni jambo la kawaida kwa wanahabari. Imekuwepo kasumba kwa baadhi ya watangazaji na waandishi wa habari hapa nchini kusema au kuandika neno “jumbe” wakiwa na dhana ya wingi wa ‘ujumbe’. Hakika katika taaluma ya sarufi ya Kiswahili hatuna wingi “jumbe” kwa maana ya ujumbe.
Kubuni maneno ambayo hayana ithibati ya matumizi na kuyatumia katika lugha pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya maneno katika kugha.
Kosa hili limeshika kasi sana katika maisha ya sasa ya vijana na uga mzima wa habari. Katika mitandao ya kijamii, redio, runinga na magazetini yamekuwepo matumizi ya maneno ya kubuni na yamezoeleka ni ya kawaida kumbe sio. Pamoja na hayo yapo matumizi ya maneno ambayo sio sahihi kwa maana yake halisi. Mfano kuna maneno kama “tiririka au funguka” – hutumika kumaanisha mtu kujieleza au kutoa ya moyoni( kwa matumizi ya sasa); matumizi ya maneno hayo sio sahihi katika mantiki yake ya msingi maneno haya kwa Kiswahili. Pia kuna “ngoma” kwa maana ya wimbo/muziki n.k.
Kosa la kuchanganya lugha mbili au zaidi (Kiswahili na Kiingereza).
Lugha yetu ya Kiswahili imekumbwa na wimbi hili zito la baadhi ya watu wengi kuchanganya lugha ya Kiswahili na lugha za kigeni. Katika uga wa habari jambo hili siku hizi ni la kawaida. Ipo misemo, maneno ya kiingereza na lugha nyingine, ambayo hutumika kama maneno ya Kiswahili. Magazeti mengi na makala huandika habari kwa kuchanganya maneno ya lugha mbili tofauti. Mfano, “wikiendi/wikendi (mwisho wa wiki); wachezaji walikuwa kambini wakifanya training ya viungo; habari zilizotufikia katika newsroom (chumba cha habari), reporter wetu(mtoa habari wetu); time imekata(muda umeisha) n.k”. Katika gazeti la mwana sporti namba 1217 la tarehe 3 hadi 6, mwaka 2012, ukurasa wa 18, kuna kichwa cha habari kimeandikwa hivi, ‘First Eleven ya waliofunga mabao mengi’. Hivyo basi kuchanganya lugha sio taratibu sahihi katika kuhimarisha lugha.
Kosa la kudharau lugha ya Kiswahili.
Baada ya vijana wengi kwenda shule na kusoma elimu ya magharibi, hasa pale wanapopata kujifunza lugha mbili zaidi wamejengewa na kujijengea dhana potofu kuwa Kiswahili ni lugha changa; si lugha ya maendeleo; haina msamiati wa kutosha; si lugha ya kimataifa, wala sio lugha ya kisomi nakadhalika. Dhana hii mbovu imeenea sana kwa kizazi cha sasa hadi kuwaadhiri wadau wa habari na wasilikizaji wake. Ukosefu huu wa fikra unadidimiza kabisa juhudi za kukuza lugha yetu adhimu.
Ni kupitia makosa haya madogo madogo lugha yetu ya Kiswahili inakumbana na vizingiti vya kuiendeleza na kupoteza fursa murua za kulitangaza taifa letu na utamaduni wetu kama kitambulisho chetu ulimwenguni.
1.2.2 SABABU ZINAZOLETA MAKOSA HAYA
Baada ya kutalii baadhi ya makosa machache ambayo yanafanywa kupitia uga wa habari katika juhudi za kuikuza lugha yetu, sasa makosa haya yanasababishwa na baadhi ya sababu zifuatazo:
Kutokuwa na elimu juu ya taaluma ya lugha
Lugha yoyote ile ikifanyiwa utafiti na wataalamu wa isimu na historia kisayansi huweza kuwa taaluma kama taaluma nyigine, na taaluma hiyo ni kama fasihi ya lugha; sarufi/isimu ya lugha. Lugha ya Kiswahili ni taaluma kama taaluma zingine ulimwenguni hasa kupitia fasihi ya Kiswahili au isimu/sarufi ya Kiswahili. Taaluma hii hufundishwa shuleni na vyuoni. Lakini wasomi wengi wamekuwa na dhana mbovu ya kudharau kuisoma lugha hii ajwadi ya Kiswahili, jambo ambalo linasababisha watu wengi kutojua utaratibu na kanuni zake hadi kupelekea kufanya makosa ya hapa na pale. Hii ni pamoja na wahusika wa habari kuwa miongoni mwa watu wanaoharibu Kiswahili kwa kutokuwa na uweredi katika lugha hii.
Ukosefu wa elimu ya ukombozi wa fikra
Katika vichwa vya watanzania wengi, bado kuna chembechembe za fikra za kikoloni hasa pale ifikapo katika kuthamini mambo yaliyo yetu. Kumekuwepo kasumba ya kudharau asili yetu na kukuza ya wazungu. Hivyo fikra hizo za kikoloni bado hajizamkomboa mtanzania, na kuharibu au kufifisha lugha hasa kupitia vyombo vya habari.
Ulimbukeni wa utandawazi
Baada ya utandawazi kushika hatamu karne ya 21, watanzania tumekuwa waathirika wakubwa wa utandawazi hasa pale tunapodhani kuwa mambo yetu ni ya kale na hayana nafasi tena katika maisha ya sasa. Athari hii imepelekea watu kuwa kuchanganya lugha ndio utandawazi au kusoma lugha za watu na kuzitumia katika utamaduni wetu ndio utandawazi. Suala hili linadidimiza zaidi lugha ya Kiswahili hasa pale tunapokosa kuelewa uhasili wa baadhi ya maeno yatu hasa kwa kukuza na kutukuza maneno ya lugha zingine. Vyombo vya habari hasa kupitia mawakala wake wamekuwa waathirika wakubwa wa jambo hili.
Uzembe wa kusoma msamiati katika kamusi na kuutumia katika mazungumzo ya kila siku
Kutotumia msamiati au kutokusoma kamusi za Kiswahili, limekuwa jambo linalodidimiza Kiswahili has pale ambapo mzungumzaji anapungukiwa msamiati wa Kiswahili na kuamua kutumia au kuchanganya au kuhazima maneno kutoka lugha za kigeni. Kuchanganya lugha ni ukosefu wa utajiri wa msamiati. Vyombo vya habari na wanahabari, hakika hili hawalikwepi kwani wao wamekuwa mstari wa mbele kuchanganya lugha mbili au tofauti kwa wakati mmoja; zaidi wanachanganya lugha za kigeni kuliko Kiswahili na lugha zetu mama. Na hii ni kwa kuwa wanahabari wengi hawana tabia ya kusoma kamusi za Kiswahili na kufanyia utafiti maneno ya Kiswahili na kuwa na uhaba wa msamiati wa Kiswahili.
Ukaidi wa kanuni za lugha ya Kiswahili pamoja na dharau kwa baadhi ya wanahabari
Waandishi wengi wa habari wa Tanzania hasa vijana wanao ukaidi mkubwa na dharau kuhusu kufuata kanuni na taratibu za lugha ya Kiswahili. Mfano, mimi nimekuwa miongoni mwa watu wanaochukiwa na pengine kudharauliwa hasa pale ninapojaribu kuwakosoa baadhi ya watu wa habari kupitia mitandaoni kuhusu kuharibu taratibu za lugha. Mwandishi au mtangazajia anayeambiwa hivyo huchukulia kuwa yule anayemrekebisha hana hadhi yoyote ya kumrekebisha yeye na pengine huona kuwa kutofuata taratibu za lugha ya Kiswahili haina maana yoyote kwake.
Kukosa umakini katika kuandika na kuhariri matini za lugha ya Kiswahili kwa watu wa habari
Makala nyingi katika habari au mitandaoni zina makosa mengi ya uandishi na matini nyingi zina makosa mengi ya kisarufi na makosa ya kimantiki; kukosea herufi na uchaguzi usio sahihi wa maneno. Hii huchangia sana wasomaji kuchukulia kuwa makosa yale ni sahihi na hivyo wao kuendeleza makosa hao katika mawasiliano. Kinyume na taratibu.
Hivyo basi, ni kwa sababu hizi baadhi ambazo zimebainika ambapo Kiswahili kinashindwa kushamiri kwa kasi kama yalivyo matarajio yetu.
1.2.3 HITIMISHO NA MAPENDEKEZO
Lugha ya Kiswahili ni lugha yenye sifa zote na inayokidhi mawasiliano miongoni mwa watumiaji wake kama zilivyo lugha nyinginezao hapa ulimwenguni, hivyo inapaswa iheshimike na ithaminiwe sawa kama lugha nyingine. Na kufanya hivyo, upendo katika lugha hii utakuwepo na kuitangaza lugha hii kimataifa. Sanjali na hili, ni jukumu letu sisi sote watanzania kuifuatilia na kuisoma lugha hii kwa undani ili tuweze kuwa wamaizi kwa undani wake na kupunguza makosa madogo madogo yanayosababisha lugha hii kutoendelea.
Tasnia ya habari, ni sehemu muhimu katika kuleta mchango na maendeleo makubwa katika jamii, na hivyo basi kupitia dhamana hii, vilevile wanahabari wanayo nafasi kubwa kuithamini, kuipenda, kuisoma na kuiendeleza lugha ya Kiswahili katika kutoa taarifa na babari katika jamii husika. Hii itaenda sambamba endapo wanahabari watafunguka macho na kuona umuhimu wa kusoma Kiswahili kama taaluma ya kumwezesha mtu kupata cheti kama mwanatabari. Makosa ya kisarufi, kuchanganya lugha, na mengineneyo hayataonekana katika matini mbalimbali za habari huku wahariri wakitakiwa kuwa ni wenye ujuzi wa lugha hii.
Kupitia juhudi hizi, hakika, watanzania wote tukishirikiana tunaweza kuiendeleza lugha yetu murua ya Kiswahili na kuitangaza kimataifa.
Na: Mushumbwa Alcheraus
Mdau wa lugha ya Kiswahili.
Tazama kitabu cha Massamba na wenzake, SAMIKISA, (2012:2-3).
Mwl Maeda