12-27-2021, 10:29 AM
CHIMBUKO LA TAMTHILIYA NA HISTORIA FUPI YA TAMTHILIYA YA KISWAHILI
Kabla ya mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki kuingiliwa na athari za kigeni zilizotoka ng’ambo, fasihi ya Kiswahili, kama fasihi nyinginezo za kiafrika, ilikuwa ni ya kusimuliwa tu (pasi na kuandikwa) na ilikuwa na tanzu kama vile ngano, sanaa za maonyesho, vitendawili, methali na kadhalika. Utanzu wa tamthiliya haukuwa na taswira kama iliyokuwanayo sasa, bali palikuwa na maigizo ambayo yalitolewa mbele ya hadhira kwa minajili ya kuongoa na kufundisha maadili au hata kutoa sifa kwa vitendo mwafaka vya wanajamii husika. Baada ya majilio ya wageni (Waarabu na Wakoloni) maonyesho haya yalianza kubadilika kwa kuingizwa katika maandishi na kuiga mitindo ya kimagharibi ili kuchukua mkondo wa tamthilia kwa jumla.
Kihistoria, tamthiliya ilianza kwa kutongoa maudhui ya kidini ambayo aghalabu yalikuwa ni uteuzi wa visa fulani kutoka katika Bibilia Takatifu ili kutoa funzo fulani. Pindi mabadiliko yalipoendelea kutokea katika maisha ya mwanadamu, hali hii ilibadilika hadi kuingia katika tamthiliya zilizozingatia maudhui mengine kama vile vichekesho na tanzia. Peck na Coyle (1984:75), wanashadidia maoni haya kwa kusema kuwa katika drama ya Kigiriki, wahusika walikabiliana na matatizo yaliyohusu uhusiano kati ya binadamu na miungu au Mungu. Katika karne ya kumi na sita (16) hata hivyo msisitizo ulitoka katika dini na kuingiza masuala ya kijamii, hivyo tamthiliya zikaanza kuzingatia maadili ya kijamii na kisiasa.
Katika Kiswahili, tamthiliya ya kwanza kabisa kutungwa na mwafrikanakuchapishwani ile ya Henry Kuria (1957) kwa kichwa cha Nakupenda Lakini, ambayo ilitungwa katika enzi ya ukoloni, tamthiiya hii iliigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1954 huko Kenya. Maudhui yake sawa na tungo nyingine nyingi za wakati huo, yaliegemea zaidi upande wa kufurahisha. Huu ni mchezo wa kuigiza unaotongoa maisha ya kijamii, lakini maudhui yake si mazito na hayazingatii hali ya jamii kujisaka na kujitafiti.
Henry Kuria, Kimani Nyoike, Gerishon Ngugi na B.M Karutu ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo wa Graham Hyslop waliokuwa wakisoma katika shule ya Alliance High School. Hyslop ni mwingereza aliyekuwa katika utumishi wa serikali ya kikoloni nchini Kenya. Hyslop alianzisha kikundi cha maigizo kwa ajili ya askari waliopigana katika vita ya pili ya dunia, miaka ya 1950 alianza kutunga michezo ambayo iliigizwa na kikundi chake. Michezo yake ya mwanzo katika lugha ya Kiswahili ni Afadhali Mchawi (1957), naMgeni Karibu (1957). Inasemekana kuwa Mwingereza huyu (Graham Hyslop) ndiye mtu wa kwanza kuleta tamthiliya kwa lugha ya Kiswahili yenye kufuata kanuni zote za Ki-Arstotle. Mbali na Henry Kuria, wanafunzi wengine wa Hyslop walioandika tamthiliya kwa Kiswahili ni Kimani Nyoike aliyeandika tamthiliya ya Maisha ni Nini mwaka 1955, B.M Karutu Atakiwa Polisi mwaka 1957 na Gerishoni Ngugi Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi mwaka 1961.
Mulokozi (1996), anadai kuwa kabla ya Graham Hyslop kuchapisha tamthiliya zake tayari kulikuwa na tathiliya za Kiswahili zilizoandikwa kwanza kabla ya kuigizwa jukwaani. Katika kutetea hoja yake Mulokozi anamtaja C. Frank na tamthiliya yake ya Imekwisha iliyochapishwa mwaka 1951, vilevile anadai kuwa tamthiliya nyingi katika kipindi hiki zilizugumzia masuala ya kidini, ziliandikwa na kuigizwa tu mashuleni na makanisani, lakini hazikuchapishwa vitabuni. Mtaala huyu wa fasihi ya Kiswahili anahitimisha hoja yake hii kwa kusema kuwa hadi tulipopata Uhuru, tamthiliya zote za Kiswahili zilizochapishwa ilikuwa zimeandikwa na Wakenya. Madai haya yanaugwa mkono na mtafiti wa utafiti huu.
Kipindi cha Uhuru,Coyle (1984), anadai kuwa, kabla ya miaka ya 1970, tamthiliya za Kiswahili zilikuwa chache sana, na nyingi kati ya chache hizo zilikuwa ni tamthiliya tafsiri, kwa mfano Mfalme Edipode, Mabepari wa Venisi, Julias Kaizari na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Tamthiliya hizi zilitungwa kwa kufuata kanuni za Ki-Aristotle na zilikuwa katika mtindo wa kishairi, nyingine zilizotungwa katika hali ya mazungumzo.
Mulokozi (1996), anaeleza kuwa tamthiliya ya Kizungu na zile za vichekesho ziliendelea kuandikwa na kuigizwa majukwaani. Tamthiliyaandishi ya Kiswahili ilishika kasi sana kipindi hiki, Ebrahim Hussein na Penina Muhando waliongoza katika uandishi wa Tamthiliya ya Kiswahili kwa wakati huu. Tamthiliya za kipindi hiki zilikuwa zikizungumzia masuala mbalimbali kama vile Migongano ya Kitamaduni ( mfano ‘Wakati Ukuta na Kwenya Ukingo wa Thim’), Matatizo ya Kijamii (mfano ‘Lina Ubani, Mke Mwenza, Hatia’), Dini (mfano ‘Aliyeonja Pepo, Maalim, Mukwava wa Uhehe), Ukombozi na Utaifa (mfano ‘Mkwawa Mhinya, Johari Ndogo, Kinjekitile, Tone la Mwisho, Harakati za Ukombozi’), Ujenzi wa jamii mpya (mfano, ‘Kijiji Chetu, Nuru Mpya, Giza Limeingia, Mashetani, Mwanzo wa Tufani, Kilio cha Haki), Uake na matatizo ya Kijamii (mfano, ‘Nguzo Mama, Ngozi, Machozi ya Mwanamke), Falsafa ya Maisha (mfano, ‘Kinjeketile, Kwenya Ukingo wa Thim) na Uchawi, Uganga na Itikadi za Jadi (mfano, ‘Njia panda (muhanika), Ngoma ya Ngw’anamalundi, Kinjeketile na Mafarakano).
NANI MUASISI WA KUTUMIA KANUNI ZA KI – AFRIKA KATIKA TAMTHILIYA YA KISWAHILI?
Hoja hii ya nani mwanzilishi wa fasihi ya kiswahili ya kimajaribio katika uwanja wa tamthiliya ilianza kujitokeza katika miaka ya 1980 ki mabishano. Wahakiki wa mwanzo kabisa katika fasihi ya Kiswahili kama wakina Nkwera walianza kuizungumzia hoja hii mwishoni mwa miaka ya 1970 pasipo mabishano.
Miaka ya 1980 na kuendelea ilikuwa ni miaka iliyowapambanisha mafahari wawili katika uandishi wa tamthiliya ya kiswahili, Ebrahim Hussein na Penina Muhando walitawala fikra, majukwaa, mijadala na makabrasha ya wahakiki wa kazi za kifasihi.
Baadhi ya mawazo ya wahakiki nguli juu ya“nani muasisi katika matumizi ya kanuni za ki-afrika katika tamthiliya ya Kiswahili?”
Nkwera (1977), anachambua kazi mbalimbali za Ebrahim Hussein na Penina Muhando. Katika kujadili maendelao ya kazi za sanaa za Ebrahim Hussein, muhakiki huyu anamtaja Bretch, mwandishi hodari na wa pekee wa michezo ya kuigiza ya kimashariki. Nkwera anaanza kwa kusema:
“Hapo mwanzo Ebrahim Hussein aliathiriwa sana na Bretch katika utunzi wake. Lakini kadri alivyoendelea kustawi katika uandishi wake wa sanaa za maonyesho Ebrahim Hussein alianza taratibu kuchanganya jadi za kiafrika kama vile masimulizi, utambaji, mianzo pamoja na miisho ya kifomula katika uandishi wake. Hivyo Hussein ndiye mwandishi wa mwanzo kabisa aliyeanza kuzikiuka taratibu za kiuandishi katika tamthiliya zilizofuata kanuni za ki-aristotle kwa kuingiza ujadi wa ki-afrika katika kazi zake”.
Mhakiki huyu anahitimisha hoja yake hii kwa kujenga mazingira yanayoonyesha kuwa mwanzilishi wa fasihi ya kiswahili ya kimajaribio katika tanzu ya tamthiliya ya kiswahili ni Ebrahim Hussein, kwani ndiye mwandishi wa mwanzo kabisa aliyeanza kuzikiuka taratibu za kiuandishi katika tamthiliya zilizofuata kanuni za ki-aristotle. Nkwera ana hitimisha kwa kuchambua tamthiliya ya Mashetani ya Ebrahimu Hussein na Pambo ya Penina Muhando. Nkwera anasema:
“Pambo ni mchezo wa hali ya juu kimuundo. Hapana shaka yo yote kwamba Penina Mlama (hapo awali alijulikana kwa jina la Penina Muhando) ameathiriwa na Ebrahim Hussein kama Ebrahim Hussein alivyoathiriwa sana na Bretcht, mwandishi hodari na wa pekee wa michezo ya kuigiza ya Kimashariki. Nkwera anasisitiza kuwa kwa mtu aliyesoma Mashetani (OUP) hatasita kusema kuwa Mama Mlama kaathiriwa na Ebrahim Hussein katika uandishi wake. Jambo hili liwe ni kweli ama sivyo, Si jambo la msingi bali la maana zaidi nikufahamu tu kwamba waandishi hawa wawili wamejitokeza kuwa mafundi na mabingwa wa kuandika michezo ya kuigiza katika fasihi ya Kiswahili na ile ya kimajaribio”.
King’ei (1987), anamtaja Ebrahim Hussein kama mwandishi wa sanaa ya maigizo aliyefanikiwa katika kuchanganya mbinu za masimulizi ya mapokeo ya fasihi simulizi kama vile ngano na vitendawili, na ufundi wa fasihi andishi ambao ameutumia kutungia hadithi hizi kwa muundo wa maigizo jukwaani. King’ei anaitaja tamthiliya ya Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi ya Ebrahim Hussein kuwa mfano wa tamthiliya iliyoathiriwa sana na kumbo ya fasihi simulizi.
Wafula (1999), anautaja mwaka 1971 kuwa ni mwaka wa mabadiliko makubwa katika tasnia ya tamthiliya ya Kiswahili. Mhakiki huyu anamtaja E. N. Hussein na tamthiliya yake ya Mashetani, kuwa ni moja kati ya tamthiliya za mwanzo kabisa katika harakati za utumiaji wa kanuni za kijadi ndani ya kazi za kifasihi. Wafura anasema:
“Hussein alijitokeza tena uwanjani, akathibitisha ameidhibiti bahari ya tamthiliya kwa kutoa Mashetani. Tamthiliya ya Mashetani iliweka tarehe mpya katika utungaji wa mchezo wa kuigiza katika lugha ya Kiswahili. Tamthiliya hii ilionyesha kwa mafanikio makubwa, jinsi mapokeo ya kiafrika yanavyoweza kutumika pamoja na mbinu za kisasa kufanikisha malengo ya kijukwaa”.
Katika kutafuta udhibitisho kwa waandishi wenyewe wanaozungumziwa mvutano huu, utafiti huu ulifanya mahojiano na mama Penina Muhando kutaka kujua mambo kadhaa juu ya suala hili. Mwanafasihi huyu mashuhuri alilizungumzia suala hili kwa ufupi sana. Mama Muhando alisema:
“Vuguvugu la mabadiliko nchini Tanzania lilianza mwishoni mwa miaka ya 1970, katika kipindi hiki wasomi wengi wa kiafrika walianza kupinga taratibu za kimaisha zenye umagharibi (taratibu za watu wa Ulaya). Wasomi hawa waliutaja waziwazi ukoloni kama sababu kubwa iliyopelekea kuharibika kwa utamaduni wa kiafrika. Baadhi ya waafrika walianza kubadili majina yao yenye asili ya ukristo ama uislamu kwenda. Kipindi hicho tukiwa wasomi na wanaharakati vijana tuliadhimia kuleta mabadiliko kwenye sanaa ya kiafrika kwa kuzitumia kanuni za kiafrika hasa katika sanaa za maonyesho, ndipo sasa kanuni za jadi ya ki-afrika kama masimulizi, utambaji, mianzo na miisho ya kifomula zilianza kutumiwa na waaandishi. Ukweli ni kwamba katika kipindi hiki cha vuguvugu la mabadiliko Ebrahim Hussein alikuwa tayari ameanza kuugua maradhi yanayomsumbua hadi sasa, hivyo hakushiriki sana katika vuguvugu la mabadiliko haya”.
Muhando (2013);
“Mimi na wasanii wenzangu kipindi hicho tulitunga michezo mingi na kwenda kuicheza katika maeneo mbalimbali “live”, tuliandika michezo mingi sana yenye kanuni za kijadi na mingi kati ya michezo hiyo haijachapishwa na kwasababu kilikuwa ni kikundi michezo mingine sijui hata ilipo. Na unapozungumzia mageuzi ama mabadiliko katika tasnia hii ya sanaa za maonyesho usitazame kazi zilizoandikwa tu vitabuni na kuwekwa ujadi ndani yake, lengo la mabadiliko yetu kipindi hicho ni kuhakikisha kuwa sanaa za jukwaani zinaigizwa katika maeneo husika ya wanajamii na kuleta mwamko wa kimaendeleo zinakuwa na nguvu kuliko zile zinazoandikwa na kuishia kwenye vitabuni tu”.
Maelezo ya Muhando yanaonyesha mwelekeo kuwa yeye pamoja na wasanii wenzake kipindi hicho ndio walikuwa waanzilishi wa kutumia kanuni za jadi ya ki-afrika katika tamthiliya za kiswahili.
(Williady, 2013) katika Utafiti wake, anaunga mkono mawazo ya Nkwera (1977), King’ei (1987), Wafula (1999), Sengo (1977), yanayodai kuwa mwasisi wa kutumia kanuni hizi katika tamthiliya za Kiswahili ni Ebrahim Hussein. Uungaji mkono huu umetokana na sababu moja kubwa. Mwaka 1971, Ebrahim Hussein alichapisha tamthiliya yake inayoitwa Mashetani, kama wasemavyo wahahiki kuwa Mchezo huu wa Mashetaniumekaa kishetani shetani ili msomaji au mtazamaji auelewe vizuri inampasa ajigeuze shetani katika ulimwengu wa chukulizi za kifasihi, ndipo atapata kuuelewa. Mwaka 1975, takribani miaka 4 baadaye tangu kuchapishwa kwa mchezo wa Mashetani, Penina Muhando alichapisha tamthiliya yake inayoitwa Pambo, ama hakika Pambo ni mchezo wa kiwendawazimu wendawazimu, ili msomaji auwelewe vizuri inampasa kujitia katika wendawazimu wa kifasihi. Hakuna tofauti kubwa kati ya michezo hii miwili ya Mashetani na Pambo, inaonekana Penina Muhando alichota baadhi ya misingi ya Hussein katika uandishi wake. Haitoshi, mwaka 1976, Ebrahim Hussein alichapisha michezo yake miwili aliyoiweka katika kijitabu kimoja, Jogoo kijijini na Ngao ya jadi. Michezo hii imeandikwa kwa utaratibu wa fasihi simulizi, kuna ngano, watambaji, hadhira na kuna kuanza na kukamilisha kazi ya fasihi kikanuni (mianzo na miisho ya kifomula). Mwaka (1984), miaka takribani nane (8) baadaye Penina Muhando alichapisha tamthiliya yake inayoitwa Lina Ubani, tamhiliya hii inaonekana kuwa na sifa sawa na zile za Jogoo kijijini na Ngao ya jadi. Kwa hoja hii utafiti huu unaunga mkono mawazo ya Nkwera na wenzake kuwa mwasisi wa michezo yenye kukiuka taratibu za ki-aristotle na kufuata taratibu za jadi ya ki-afrika ni Ebrahim Hussin. Kauli hii ya kumtaja Ebrahim Hussein kuwa ndiye mwasisi wa tamthiliya hizi za kimajaribio haitoi ukweli kuwa Penina Muhando naye anaumuhimu mkubwa sana katika tamthiliya ya Kiswahili.
Mwl Maeda