Warusi walianza kuifahamu lugha ya Kiswahili mwanzoni mwa karne ya 19, lakini uchunguzi kamili wa lugha ya Kiswahili na lugha zingine za Kiafrika ulianza nchini Urusi baada ya mapinduzi ya Oktoba 1917. Kiswahili ni lugha ya kwanza ya Kiafrika iliyokuwa ikifundishwa nchini humo.
Uteuzi wa lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya mafunzo ulitegemea maana na umuhimu wa lugha hii. Kiswahili kilienea sana katika nchi za Afrika Mashariki na kutumiwa na makabila mengi tangu zamani. Idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili ilikuwa kubwa zaidi kuliko lugha nyingine za Kiafrika. Uchunguzi wa kinadharia wa Kiswahili ulianza kuendelezwa nchini Urusi katika miaka ya 1930. Mnamo mwaka 1933, Warusi walianza kujifunza Kiswahili. Mmoja wa waalimu wao alikuwa Jomo Kenyatta, Raisi wa kwanza wa Kenya ambaye wakati huo alikuwa anasomea siasa huko Moscow.
Mwaka 1934, kulianzishwa idara ya lugha za Kiafrika katika chuo Kikuu cha Leningrand na kukubaliwa kwa kundi la kwanza la vijana wanafunzi waliojifunza lugha hizi, hasa Kiswahili. Vilevile lilifanyika kongamano la kwanza la elimu nchini Urusi, yaani kongamano la wanataaluma Warusi waliojishughulisha na utafiti wa lugha za Kiafrika. Kongamano hilo liliwashirikisha wanaisimu wa Leningrand na wa Moscw.
Ni katika kongamano hili, wanataaluma waliidhinisha mpango wa kazi za uchunguzi wa lugha za Kiafrika. Miongoni mwa kazi hizo, zilikuwemo Kamusi za istilahi za kiuchumi na za kijamii za lugha zifuatazo: Kihausa (Yushmanov), Kizulu na Kihosa (Snegiryov), Kisotho (Olderoge) na Kiswahili (Danilov). Zaidi ya hayo, wataalamu hawa walipanga kutunga sarufi ya lugha ya Kiswahili na ya Kizulu.
Siku hizi, lugha ya Kiswahili inafundishwa na kuchunguzwa kwenye baadhi ya vyuo vikuu na taasisi za nchi ya Urusi: Taasisi ya nchi ya Asia na Afrika iliyoko chini ya Chuo Kikuu cha Moscow kwa jina la Lomonoscov (tangu mwaka 1960), Kitivo cha Mashariki cha Chuo Kikuu cha Petersburg (tangu mwaka 1934), Taasisi ya uhusiano wa kimataifa (tangu mwaka 1957) na Chuo Kikuu cha Urafiki baina ya mataifa kwa jina la Patrice Lumumba (tangu mwaka 1961). Academia ya kisayansi ya Urusi inajishughulisha vilevile na utafiti wa Kiswahili. Katika taasisi ya isimu kuna idara ya lugha za Kiafrika.
Zaidi ya miaka 70, uchunguzi wa lugha ya Kiswahili pamoja na lugha nyingine za Kibantu uliendelezwa kwa nguvu zaidi. Vilitungwa vitabu vya sarufi ya Kiswahili kikilinganishwa na lugha nyingine za Kibantu. Kwa mfano Lugha ya Kiswahili (E. Miachina), Sarufi ya Kinadharia ya Kiswahili (N. gromov na N. Okhotina), Aina za Maneno katika Lugha za Kibantu na Misingi ya Kuzifafanua (N. Gromov). Kulitolewa makala nyingi zinazohusu mfumo wa kisarufi wa Kiswahili, mnyambuliko wake, utaratibu wa kifonetiki, n.k. Hivyo, wanataaluma wa Kirusi wanachunguza lugha ya Kiswahili katika vipengele vyake pamoja na nyanja zake zote (Fasihi na sarufi).
Walimu wa lugha ya Kiswahili nchini Urusi wametunga vitabu vya masomo kwa ajili ya kufundishia wanafunzi vitabu vya kiada, vya ziada, matini, n.k. vinavyowezesha kufanya ufundishaji uwe bora zaidi. Vilevile kamusi za aina mbili: Kamusi ya Kiswahili-Kirusi na Kirusi – Kiswahili zimechapishwa. Kamusi ya kwanza ya Kirusi – Kiswahili ilitolewa mwaka 1961. Mwaka 1987, ilichapishwa kamusi mpya na mwaka 1996, ilitolewa kamusi kubwa ya kwanza ya Kirusi – Kiswahili yenye zaidi ya maneno 30,000. Nyongeza ya kamusi hiyo ni “Sarufi linganishi ya lugha ya Kirusi na lugha ya Kiswahili”
Aidha, vitabu vya tafsiri vimesaidia sana kukuza na kueneza Kiswahili nchini Urusi. Maandishi ya Kirusi yalianza kutafsiriwa kwenda lugha nyingine miaka ya sabini. Baadhi ya vitabu vya Kirusi vilivyotafsiriwa kwa Kiswahili ni Mama (1980), Tabia ya Mrusi (1964), Ajali ya Mwanaume (1962), Watabakia Vijana Milele (1963) na nyinginezo. Wafasiri wa vitabu hivyo walikuwa Waswahili waliokuwa wakiishi Moscow, wakisomea taaluma fulani, au kufanya kazi redioni. Baadaye, Warusi waliojifunza Kiswahili na kukimudu kikamilifu walishiriki katika kazi hiyo ya kutafsiri.
Fasihi ya Kiswahili ilitafsiriwa pia katika Kirusi. Vitabu vilivyotafsiriwa sana ni vya Shaaban Robert. Vitabu vyake vilivyotafsiriwa katika Kirusi ni: Kusadikika, Adili na Nduguze, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, Wasifu wa Siti Binti Saad, Siku ya Watenzi Wote, Utubora Mkulima, mashairi yake mengineyo. Waliotafsiri walikuwa ni Warusi waliojifunza Kiswahili. Maandishi hayo yalitolewa katika vitabu viwili: kimoja kilichoitwa Maisha Yangu kilitolewa mwaka 1969, kwa idadi ya nakala 50,000 na kingine ni Maandishi Yaliyoteuliwa kilitolewa mwaka 1981, kwa idadi ya nakala 30,000. Hivyo wasomi Warusi walipata nafasi nzuri ya kujua kazi hizo za Fasihi ya mwandishi maarufu wa Kiswahili inayoakisi upeo wa juu wa usanifu na utajiri wa lugha ya Kiswahili.
Baada ya Urusi kusambaratika, shughuli zote za fatsiri zimesimamishwa pamoja na kufungwa kwa asasi zote zilizoshughulikia lugha na Fasihi ya Kiswahili. Kutokana na hali hii, shughuli za ukuzaji wa Kiswahili nchini humo zinaenda kwa kusuasua. Wataalamu wa Kirusi wanaojishughulisha na Kiswahili wanakosa uhusiano na asasi za lugha ya Kiswahili zilizoko Afrika ya Mashariki hali hii hukwamisha maendeleo ya Kiswahili nchini humo.