08-27-2021, 06:00 PM
Mwandishi wa Riwaya ya Kiswahili na Suala la Ukweli wa Maisha
J.S. Madumulla
Dokezo
Makala haya yanaanza kwa kutazama kwa ufupi maana ya dhana ya “ukweli wa maisha” kinadharia. Kisha yanaangalia jinsi baadhi ya waandishi wa fasihi ya Kiswahili (hususan riwaya) walivyouakisi ukweli huo wa maisha katika kuyaeleza kisanii matukio ya mazingira yao ya karibu na ya mbali. Suala moja linalozingatiwa ni kujaribu kuona jinsi mwandishi alivyofaulu au kushindwa katika kutoa maudhui aliyokusudia kuyatoa kwa msomaji wake kwa njia ya “ukweli wa maisha” anaousimamia au aliousimamia. Na hatimaye, swali muhimu linalojitokeza ili kujadiliwa ni lile linalohusu “ukweli wa maisha” ambao ungefaa kuzingatiwa na waandishi wetu wa wakati huu. Makala haya yanajiduru katika uwanja wa riwaya tu; kama kuna tanzu nyingine zinazotajwa humu, inakuwa ni kwa kugusia tu. Kisha, mada ya “ukweli wa maisha” ni pana sana. Ingehitaji kurasa nyingi na muda mrefu ili kuijadili kwa utoshelevu. Kwa jinsi hiyo, makala haya yachukuliwe kama ni mchango mdogo katika mada hii, na papo hapo ni kichokozi cha mjadala.
Aristippos: Kwa hiyo, na kapu la takataka nalo ni zuri?
Socrates: Bila shaka; na pia ngao ya dhahabu ina ubaya wake; hasa pale ambapo kapu linafaa kwa kazi yake na ngao haifai kwa kazi yake.
Aristippos: Kwa hiyo basi, unadhani kwamba uzuri na ubaya ni kitu kilekile?
Socrates: Ndiyo, hata wema na uovu ni sawa. Aghalabu ni kwamba kile kitu kifaacho kwa njaa, hakifai kwa homa; na kile kifaacho kwa homa hakifai kwa njaa. Kitu kinachosaidia katika upigaji mbio aghalabu hakifai katika ulingo wa ngumi; na kinachofaa ulingoni huweza kuharibu upigaji mbio. Kila kitu ni chema na kinafaa kutegemea matumizi yake; lakini ni kiovu na kisicho na faida katika uwanja ule ambamo kinaleta uharibifu.1
Xenophon
Kinjeketile: Wao wanataka niseme kuwa maji yalikuwa uwongo. Kwani la uwongo nini hapo?
Kitunda: Maji, yalikuwa kweli? Wewe unaamini? (Kinjcketile anacheka)
Kinjeketile: Unajua kesho watasema nini? Bwana afisa atawaambia watoto – watoto wetu, Kitunda – atawaambia kuwa tuliyofanya sisi makosa. Kupigana ni makosa? Kupigania nchi itakuwa makosa? Anataka na mimi nimsaidie niseme kweli tulikosa. Hapana… Hapana! Sitasema neno hilo. Neno limezaliwa. Watoto wetu watawaambia watoto wao neno hilo. Wajukuu wetu watalisikia. Siku moja neno hilo halitakuwa ndoto, bali ukweli.2
E. Hussein
Kweli hunipa maisha, ya mwangaza wa kandili
Kweli huniadibisha, utu huletwa na kweli
Kweli hunielimisha jinsi ya kuwa kamili
……………………………………………..
Kweli ni sawa na radi, inapotoa kauli
……………………………………………..
Kweli ikifutu neno, haliji mara ya pili.3
Sheikh S. Robert
Kutokana na madondoo hayo maswali yanayojitokeza haraka ni: je, ukweli wa maisha ni nini? Je, ni ule wa kiujumi unaojadili masuala ya ubaya na uzuri, wema na uovu kama Xenophon anavyoonyesha? Au ni ule ukweli wa kisiasa unaojadili masuala ya haki za binadamu, uzalendo na amani kama anavyoonyesha Ebrahim Hussein? Au pengine ni ule ukweli wa kiadilifu (au wa kifalsafa) kama aonyeshavyo Sheikh Shaaban Robert? Ni lengo la makala haya kuijadili mada ya ukweli wa maisha yakitumia mifano kutoka katika riwaya ya Kiswahili. Tunapenda kutazama nafasi ya ukweli wa maisha kama istilahi muhimu ya kiujumi na kinadharia katika fasihi, na umuhimu wake katika historia ya maendeleo ya mwanadamu. Kwa jinsi hiyo tunaweza kubaini wajibu wa mwandishi katika kuusawiri ukweli wa maisha wa mahali alipo na wakati aliomo.
Katika nadharia ya talsafa ya ufahamu (Erkenntnistheorie) sheria ya msmgi ya ukweli iko katika matendo. Matendo (au uzoefu) ni msingi’na lengo la ufahamu (maarifa), na pia ni kigezo cha ukweli. Ndiyo maana wataalamu wengine wamepata kusema kuwa maisha ndiyo huzindua ufahamu,4 na wala si kinyume chake, ijapokuwa ufahamu unaweza kustawisha maisha.
Tunaweza kuugawa ukweli katika mafungu mawili makubwa ambayo yanahusiana sana, kwa sababu fungu la pili hulitegemea lile la kwanza katika kuwako kwake. Fungu la kwanza ni lile tuwezalo kuliita la “ukweli katika hali halisi” – yaani jinsi ukweli unavyojitokeza katika vipengele mbalimbali vya maisha, k.m. dini, siasa, utamaduni, itikadi, sheria, falsafa, n.k. Ukweli huu unafafanuliwa na wanafalsafa kuwa ni ile hali ya (au sifa za) kauli kukubaliana na maudhui ambayo yanaakisiwa na kauli. Fungu la pili la ukweli ni lile la ukweli wa kisanaa. Katika fungu hili ukweli wa maisha wa kisanaa ni istilahi muhimu katika ujumi na nadharia ya fasihi. Husawiri uswanifu wa ubunaji na matukio halisi ambavyo huwasilishwa kwa hadhira (msomaji au msikilizaji) kwa njia ya kisanaa. Aghalabu jambo au tukio linalosawiriwa halipati maana yake halisi kutoka kwa msanii, bali hupata kutoka katika matamanio, malengo, na vipimo maalumu vya jamii ambamo jambo hilo limetokea. Kauli ya kisanaa ina upekee wake; haifuati kanuni za kisayansi za kauli. Katika sanaa ‘ukweli’ katika kauli huweza kuvuka mipaka ya uhalisi. Kwa jinsi hiyo ili kuweza kugundua ukweli uliomo ni sharti kuisoma kazi ya sanaa kwa uangalifu na kuuelewa mfumo wa usawiri wa matukio.
Kiini cha picha au taswira ya kisanaa ni ule uhusiano wa kitu na msanii ambapo kitu kinasimama badala ya tukio na msanii anawakilisha uakisi wa kisanaa wa tukio hilo.
Taswira
“A” huumba ‘ukweli’ wa ‘B’ kutokana na maisha ya watu kwa njia ya kauli za kisanaa. Na kauli ya kisanaa inasemekana kuwa ni kweli ikiwa imeakisi vizuri uhusiano wa mtu na ukweli wa asili na wa kijamii.5 Uakisi sahihi hupata msingi wake katika jumuiko la mambo mawili: ufahamu wa kisanaa wa ukweli, na ubora wa kiujumi wa ukweli. Katika maelezo ya kisanaa, msanii hujihusisha zaidi na jinsi ambavyo jambo lingewezekana kutokea au jinsi ambavyo jambo lingefaa litokee lakini katika hali halisi halikutokea au halijatokea hivyo. Nguvu ya usanii (uakisi wa jambo) hutokana na uzoefu wa mwandishi katika mazingira yake na kiwango cha ufahamu wake. Na umuhimu wa kazi ya sanaa unatokana na jinsi mwandishi alivyohusisha kazi yake na matukio muhimu ya wakati wake.
Hapo juu tumesema kwamba ukweli wa kisanaa na ukweli wa kiujumi kwa pamoja hujenga msingi wa uakisi mzuri. Wajibu wa ujumi katika kazi ya sanaa ni kubainisha masuala muhimu ya kiutu, sifa za utu, masuala ya kuujenga wakati ujao (k.m. amani, njaa, ukame, n.k.) kwa kutumia vigezo vya ujumi vya wakati huo. Ijapokuwa ukweli wa kisanaa huweza kuvuka mipaka ya kauli, lakini mara nyingi maana ya taswira za kisanaa inapaswa ilingane na maana ya matukio katika maisha halisi.
Katika kuchunguza maendeleo ya riwaya za Kiswahili tangu enzi za Shaaban Robert hadi sasa tutabaini kuwa tunajishughulisha na utanzu wa fasihi ambao ni hai, tena uliofungamana imara na nguvu au sheria zinazoidhibiti jamii katika vipengele mbalimbali vya maisha. Hii inadhihirisha kuwa asili yenyewe ya fasihi pamoja na tanzu zake ni tukio la kihistoria, ambamo vipengele vyake vyote vya kazi za kisanaa pamoja na mwenendo wenyewe wa kisanaa na sifa zote za fasihi hubadilika daima. Hii ina maana kuwa fasihi ni mfumo wa kisanaa wenye uhai na ambao unaguswa sana na mabadiliko ya maisha.
Katika majaribio ya awali ya uandishi wa riwaya za Kiswahili tunaweza kuona kuwa ijapokuwa mada inayahusu mazingira ya wakati wa sasa, na hivyo kuonyesha usasa wa wakati na mahali, msanii anatumia mbinu za zamani za kisanaa katika kuusawiri ukweli wa maisha. Majaribio haya ya awali yanajitokeza katika mkondo wa riwaya ya kimaadil – Bildungserzaehlungambayo lengo lake la msingi ni kufundisha maadili ya jamii. Namna msanii anavyofundisha maadili ya jamii tunaipata katika jinsi alivyowachora wahusika wake ambao kwao anausawiri ukweli wa maisha. Na ni mhusika mkuu ndiye anayetumiwa kuufafanua, kuhubiri na kuutetea ukweli huo wa maisha. Mhusika huyu, kwa kiasi kikubwa, ana sifa za kitendi, yaani ana nguvu za ajabu na ujasiri usio wa kawaida; ana sifa za uadilifu na akili zisizo na mpaka; tena ana hamu isiyolegea ya kutimiza lengo alilodhamiria kulitekeleza. Mhusika huyu amechorwa na msanii kwa makusudi mazima ya kuumba mfano bora wa kuigwa na kumfanya awe kielelezo cha ukweli na ukamilifu wa maisha. Hebu tuipitie mifano michache ya riwaya zenye wahusika hawa.
Adili na Nduguze (1952) na Kusadikika (1951) ni mifano mizuri ya riwaya za Shaaban Robert za mkondo wa kimaadili. Adili anayapata majaribu magumu, akishindana na watu na majini, na hatimaye anashinda. Vivyo hivyo katika riwaya ya Kusadikika wale wajumbe sita ambao ni mashahidi wa mhusika mkuu, yaani Karama, wanapita katika majaribu magumu na ya kusikitisha kwa ajili ya uzalendo wao, ijapokuwa wenye mamlaka juu yao hawathamini uzalendo wa wajumbe hawa. Hata hivyo hatimaye wanashinda kwa msaada wa Karama. Je, Shaaban Robert anatumia kigezo gani katika kueleza ukweli wa maisha?
Mhakiki mmoja, E. Bertoncini (1977: 85) aliandika kuwa kazi za sanaa za Shaaban Robert ziliathiriwa na ushairi wa kimaadili wa kame ya kumi na tisa na masimulizi ya jadi. Tukiuchunguza huo ushairi wa karne ya kumi na tisa tutagundua kwamba sehemu yake kubwa ilikuwa ni tenzi ambazo zilikuwa na uhusiano wa karibu sana, au wa moja kwa moja na dini.6 Kigezo cha ukweli wa maisha kilikuwa ni dini. Hivyo ndivyo ilivyo hata katika maandishi ya Shaaban Robert. Wahusika wake wamegawika kati ya wazuri na wabaya. Wazuri ni wazuri (wema) wasio na dosari, na wabaya ni wabaya moja kwa moja; na katika migogoro na mikinzano wazuri wanawashinda wabaya. Ndiyo maana Shaaban Robert alijulikana na baadhi ya wahakiki kama ni “mhubiri mimbarini”. Kwa maneno mengine, ukweli wa maisha katika Shaaban Robert au katika kazi za mkondo wa kimaadili umo katika mhusika adili. Katika kuusawiri ukweli huu, msomaji anashuhudia jinsi Shaaban Robert anavyotumia kwa ufundi ujumi wa uzuri na ubaya na lugha ya busara ili kuziteka hisia za msomaji wake.
Mifano mingine ya riwaya zinazoangukia katika mkondo wa kimaadili ni Mtu ni Utu (G. Mhina, 1971) na riwaya za M.S. Abdulla zenye mhusika mkuu Bwana M(u)sa. Wahusika wa Mtu ni Utu ni wa kiShaaban Robert, yaani ni bapa. Pia wamegawanywa katika uzuri unaoshindana na ubaya, na hatimaye uzuri unashinda. Kwa G. Mhina ukweli wa maisha kwa jamii mpya uko katika mhusika adili anayepigania utu – kwa njia ya kuheshimiana, kupendana, kushirikiana, kusameheana, na kufanya kazi kwa bidii. Mhusika mkuu, Sozi, anajaribu kuishi katika maadili haya na kupingana na uovu. Jinsi uovu unavyosamehewa unadhihirisha falsafa ya kibiblia ya kumsamehe aliyekukosea hata mara saba au sabini. Na katika riwaya za M’.S. Abdulla, ijapokuwa tunashuhudia maendeleo makubwa katika mbinu za uandishi wake kama vile lugha na wahusika (kwamba vimekaribiana sana na maisha ya kila siku), bado wahusika wake (hasa mhusika mkuu) wana dalili ya wahusika wa mkondo wa kimaadili. Bwana (M(u)sa ameumbwa juu ya wahusika wengine kwa kuwa na sifa za ukamilifu katika uneni na utenzi wake, na hivyo kuwa mhusika adili. Kisha karibu wahusika wote wa M.S. Abdulla hawakui; mwenendo wao ni wa mlalo.
Tukiichunguza zaidi riwaya ya mkondo huu wa kimaadili ambayo inauchora ukweli wa maisha kwa kumtumia mhusika adili tunayaona masuala mawili ambayo yanaweza kuitwa ni upungufu wa msingi wa riwaya hii. Kwanza, mhusika huyu adili, ijapokuwa anajitokeza kuwa ni shujaa na mtenzi mkubwa, hana saikolojia wala hisia; na kwa jinsi hiyo kwa kiasi fulani anaonekana kama ni kipaza sauti tu cha matukio ya wakati wake.7 Pili, ni suala la uhusiano kati ya mhusika huyu na wakati. Mhusika huyu – kama alivyo mhusika wa kwenye hadithi ya kifasihisimulizi – ni mhusika wa wakati wote. Kwa msanii wa namna hii ya mhusika, yaarii mhusika adili ambaye ameainishwa kama mhusika mkwezwa, dhana za wakati na ukweli uliokamilika zinaonekana kuwa ni vitu visivyobadilikabadilika. Kwa hiyo mhusika huyu adili anauwakilisha ukweli uliokamilika wa wakati wote.
Kwa upande wa Shaaban Robert ambaye anajitokeza zaidi katika uchoraji wa mhusika wa namna hii, anawapa wahusika wake lugha teule tena sanifu, ambapo waandishi wa baadaye ambao wameandika riwaya ya mkondo huu, hususan waandishi wa riwaya – pendwa,8 wamewapa wahusika wao lugha ya kila siku, ikiwa ni pamoja na ya mitaani. Hii inatokana na kuathiriwa kwa waandisni na mazingira ya wakati wao. Ukweli wa maisha wa Shaaban Robert ulikuwa na mizizi yake katika dini, na hii ndiyo iliyolazimisha utumiaji wa lugha teule. Hali kadhalika usanifu wa lugha inawezekana ulitokana na Shaaban Robert kuwa mmoja katika kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambayo, kwa kipindi fulani, alipata kuwa Mwenyekiti wake. Kama kiongozi wa chombo hicho cha lugha, tena lugha changa, wakati wa ukoloni Shaaban Robert alijiona kuwa ni mtetezi na mdhamini wa lugha hiyo katika kuwaonyesha wengine uwezo na mvuto wake kama chombo cha kitaaluma na cha kisanii.
Kwa ufupi, waandishi wa riwaya ya mkondo wa kimaadili pamoja na kuwa wameyagusia au kuyazungumzia masuala mbalimbali ambayo yameikabili jamii yao na hata kuifunza juu ya maadili yanayotakiwa (yaani ukweli wa maisha unaofaa), lakini wanaonyesha bado upungufu wa namna ya kuyachunguzamasuala ya kijamii na kiasili. Mtazamo wao wa matukio unajikita mno katika mkabala wa kijadi wa ujumi na wa kuangalia ukweli wa maisha.
Mwanzoni mwa miaka ya sabini kuliendelezwa namna nyingine ya kuutazama ukweli wa maisha, hatua fulani ilipigwa, hasa kwa upande wa fani. Hapa tutamchukua E. Kezilahabi na riwaya yake ya Rosa Mistika. Mhakiki mmoja, E. Bertoncini, aliandika kuwa E. Kezilahabi huandika kwa kuguswa juu ya matatizo nyeti ya kisiasa na kijamii yanayotukia kila siku katika Tanzania na katika Afrika ya leo.9 Na kuhusu riwaya ya Rosa Mistika mhakiki huyo anaeleza kuwa ni riwaya iliyopokelewa kwa mchanganyiko wa furaha, mshangao na chuki ambayo ilielekea kwenye fedheha kwa sababu mtunzi aliichagua kama mada yake moja ya maovu ya msingi yanayoishambulia jamii ya wakati huu ya Afrika Mashariki, akaishughulikia waziwazi bila kujizuia.10
Katika nadharia hapo nyuma tumeona kuwa jambo au tukio linalosawiriwa halipati maana na umuhimu wake kutoka kwa msanii bali hutokana na matamanio, malengo na vipimo maalumu (hususa vya kiujumi) vya jamii. Lakini ‘jamii’ hapa ina maana gani? Lini jamii hukutana na kuweza kuyafanyia uamuzi maandishi fulani, licha ya kuwa si jamii nzima yenye uwezo wa kuyasoma maandishi hayo na kuyaelewa? Hata sehemu ya jamii yenye uwezo wa kuyasoma maandishi hayo, si yote inayopendelea kuyasoma. Hatimaye itabainika kuwa ‘jamii’ izungumziwayo hapa ni kijiidadi kidogo tu cha watu kinachopitisha maamuzi juu ya maandishi fulani kwa niabaya jamii. Aghalabu matamanio, malengo na vipimo maalumu vya jamii huamuliwa na kijiidadi kidogo hiki kwa niaba ya jamii. Hivyo basi katika Rosa Mistika vipimo vya kiujumi vilivyotumika kuusawiri ukweli wa maisha havikuafikiana na vile vya ‘kijamii’.
Kezilahabi ndiye aliyeleta mapinduzi ya kwanza ya mhusika katika riwaya ya Kiswahili kwa kumuumba mhusika mwenye saikolojia na hisia. Mhusika huyu, ijapokuwa hakuchorwa vizuri kama yule wa M.S. Abdulla, lakini alionyesha dhahiri mambo mawili juu ya ukweli wa maisha. Kwanza, alibainisha utatu (multiplicity) wa maisha katika mtu ambao ulimwondosha mhusika mkwezwa. Pili, ukweli na wakati havikutulia pamoja. Rosa Mistika aliasi kutii vigezo vya jadi vya ukweli mkamilifu. Na mwishoni mwa riwaya kigezo cha jadi ambacho ni muhimu kupita vyote katika kupima ukweli wa maisha (yaani Mungu) kinapaswa kirudi katika hali halisi ili kiutafute ukweli halisi. Riwaya hii tunaiweka katika hatua za mwanzo za tapo la uhalisia wa kihakiki. Pamoja na kuleta mchango uliotajwa hapo juu na kuibua masuala kadhaa ya kijamii kama vile ya urithi, mimba mashuleni, n.k., bado kiwango cha riwaya hii cha kujadili bado ni cha chini, na matatizo ya jamii hayatafutiwi suluhu.
Katika Rosa Mislika linajitokeza suala moja ambalo linachukuliwa kama ni upungufu mmojawapo wa kisanii kwa Kezilahabi. Hili ni kuhusu jinsi wahusika wake wanavyoamua kuyakwepa matatizo kwa kujiua. Upungufu huu unajitokeza pia katika baadhi ya kazi zake nyingine, k.m., Kichwamaji, Gamba la Nyoka, “Cha Mnyonge Utakitapika Hadharani” na “Mayai Waziri wa Maradhi”. Kujiua hakumalizi matatizo ya jamii, bali pengine humaliza kwa kiasi fulani tu matatizo ya aliyejiua. Baadaye, katika kazi zake nyingine za sanaa, hususan Dunia Uwanja wa Fujo (1974) na Nagona (1987) Kezilahabi analizamia kwa tafakuri suala la ukweli wa maisha. Katika Dunia Uwanja wa Fujo kwa njia ya mhusika Dennis, mwandishi anayaona maisha hivi:
Quote:Zamani niliamini kwamba kila mwanadamu ameumbwa kuja hapa duniani ili apate kufurahia ulimwengu kiasi awezavyo kabla hajafa. Laki ni sasa ninaamini kwamba ‘Dunia Uwanja wa Fujo’. Kila mwanadamu ameumbwa kuja kufanya fujo yake halafu anajiondokea na kupotea. Kuna fujo za aina nyingi. Watu wengine wamefanya fujo kuliko watu wengine. Hao ndio wamejulikana kwa sababu walitumia nguvu. Watu kama kina Napoleon, Juliasi Kaizari, Alekizander, Hitler; wengine wamefanya fujo kwa jina la amani: nao pia wamejulikana, watu kama kina Bwana Yesu, Lincoln, Livingstone, Gaodhi; wengine wamefanya fujo kwa maandishi; fujo waliyoanzisha watu hawa haitakwisha mpaka ulimwengu utakapofutika; watu kama akina Karl Marx, Shakespeare, Plato, Mao; na halafu kuna watu wengine wanaofanya fujo kidogo na kutapakaa kama viwimbi vya maji baada ya kutupa jiwe dogo majini; ni wale tu walio karibu wasikiao mshindo wao, lakini wanatisha zaidi; watu kama kina Mkwawa, Mutesa, Marais mbalimbali ambao hawajatenda makuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya; halafu mwisho kuna watu kama sisi na wengine, hasa wakulima; sisi tunafanya fujo ambayo haipati kujulikana. Tunafanana na mtu mwehu anayelala chini na kupigapiga miguu juu mpaka atakapojifia mikono yake mapajani… Kwa mfano mwalimu atafanya fujo yake darasani halafu atajifia na kikohozi cha chaki; polisi atapiga kelele ‘hoi! hoi’ halafu atajifia na mishipa yake miguuni; mwanamke anayefanya kazi bar atafanya fujo humo kwa kueneza magonjwa na kuvunja nyumba za watu, halafu atajifia.” uk. 92).
Dennis anapoulizwa kwamba mambo haya yote ameyapata wapi anakionyesha kichwa chake kwanza! Lakini waumini wa uyakinifu wa kihistoria wanaoona kuwa maisha ndiyo huzindua ufahamu (being determines consciousness) – kama ilivyodokezwa katika sehemu ya nadharia wangeliona jibu la Dennis kuwa ni kinyume cha mambo. Ndiyo maana mhakiki mwingine wa Kezilahabi, M. Mulokozi (1976:11) alipata kusema juu ya falsafa ya kazi za sanaa za Kezilahabi katika maisha kwamba: “Kwa kuwa mahitimisho yake yanabuniwa kichwani zaidi kuliko kutoka katika mambo ya ukweli wa kijamii, mahitimisho hayo, kwa vyovyote vile, hayaleti matumaini bali yanamwelekeza mtu kwenye kukata tamaa na hali ya upweke”.
Katika kiwango hiki riwaya za Kezilahabi hazikuwa na kazi za tapo la uhakiki wa kihalisia tu, bali zilijipatia sifa nyingine iliyobainisha upekee wa msanii huyu akilinganishwa na waandishi wengine wengi wanaoangukia katika tapo hili ambao wengi wao waliinukia katika miaka ya sabini. Sifa hiyo ni ile inayoziweka kazi za Kezilahabi katika mkondo wa kidhanaishi (existentialism) kutokana na mkabala wake wa ukweli wa maisha ambao msingi wake ni “Cogito ergo sum” (m.y. ‘Nafikiri, kwa hiyo nipo!’)12 Katika sehemu ya nadharia tumeona kuwa matendo (au uzoefu) ni msingi wa ufahamu, tena ni lengo la ufahamu, na hali kadhalika ndicho kigezo cha ukweli. Kwa kukitumia kipengele hiki cha nadharia tutaona kuwa msingi wa kidhanaishi wa kuutazama ukweli wa maisha unawekwa juu chini, chini juu, unakuwa “Nipo’ Kwa hiyo nafikiri.”
Jinsi Kezilahabi alivypendelea na uandishi ndivyo ambavyo ameelekea kujikita zaidi katika mkondo huo wa kidhanaishi akiudadisi ukweli wa maisha kwa namna ya kufikirisha zaidi kuliko hapo awali. Hii inajidhihirisha katika Nagona (1987). Akitumia mtindo wa kihemetiki13 wa kuuangalia ukweli wa maisha, anaona maisha yako katika namna ya duara, na ukweli upo katikati. Katika duara hii watu wanatumia njia (‘fujo’) mbalimbali ili kuufikia ukweli pale katikati. Maisha yanaendelea katika mzunguko huu daima pasipo kuifikia kweli ya katikati, kwani kuifikia kweli pale katikati na kuishika mkononi ndio mwisho wa kufikiri. Mduara wa kihakiki wa kihemetiki wa M. Heidegger14 ndio unaochangia vikubwa katika mtazamo huu wa maisha wa Kezilahabi katika Nagona.
Kwa kifupi, Kezilahabi ni mwandishi aliyejitokeza kuliko waandishi wote katika mkondo huu wa kidhanaishi katika riwaya ya Kiswahili, na kwa kutumia mkondo huo ameyajadili masuala ya kisiasa na ya kijamii yanayoisibu jamii ya wakati huu ya Kitanzania ijapokuwa, kama ilivyodokezwa, suluhu ya matatizo hayo si ya msingi. Kifani na kiujumi katika riwaya zake zilizotangulia alionyesha matukio bila kujali mipaka ya vionjo vya ‘jamii’ akajikuta akigongana na ‘jamii’. Lakini katika Nagona huenda atakwepa mgongano mwingine kutokana na uwezekano wa riwaya hiyo kutokueleweka na ‘jamii’, hasa kwa namna alivyoijenga riwaya yake akitumia visasili vya asili mbalimbali duniani.
Waandishi kadhaa walioandika riwaya zao katika miaka ya sabini wanaangukia katika tapo la uhakiki wa kihalisia, na miaka ya sabim inaweza kuitwa kama ni kipindi cha riwayadhati (serious novel) ya Kiswahili. Baadhi ya waandishi hao ni M.S. Mohammed, Sh. A. Shafi, N. Balisidya, S. Komba, H. Mwakyembe, J. Ngomoi, W. Seme, M. Mvungi, C. Chachage, C. Mung’ong’o, A. Banzi, F. Senkoro, C. Liwenga, n.k. Idadi kubwa ya maandishi haya inajihusisha na ujenzi wa jamii mpya baada ya Azimio la Arusha na siasa ya ujamaa na kujitegemea, pamoja na mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964; na pia kulitazama suala la mkinzano wa kipembuzi kati ya kijiji na mji, kati ya jadi na mamboleo.
Hata hivyo, katika miaka hiyohiyo ya sabini kuna riwaya iliyojitokeza ikiwa imeguswa kiasi kikubwa na itikadi ya kiMarx. Riwaya hii inaona kuwa ukweli wa maisha uko katika usawa na haki, na mambo haya yatapatikana pale ambapo watu wote watakuwa huru na sawa, na pasipokuwepo matabaka wala ukoloni. Kwa hiyo riwaya hiyo imejihusisha na masuala ya ukombozi au kuwapa wananchi mwamko wa kisiasa. Mifano ya riwaya hizo ni Ubeberu Utashindwa (J.K. Kiimbila, 1971), Mzalendo (F. Senkoro, 1975), Kuli (Sh. A. Shafi, 1979), Kabwela (A.J. Saffari, 1978) na Dunia Mti Mkavu (S. A. Mohamed, 1980). Riwaya hii imeainishwa kama ni ya ‘kimapinduzi’. (Neno ‘mapinduzi’ katika muktadha wa kifasihi nimelitumia hapa kwa maana ya mabadiliko ya haraka ya kisiasa, kiuchumi na kifikra katika jamii kwa lengo la kuyaleta mahusiano mapya ya kijamii yanayoleta uhuru, usawa, amani na maendeleo).
Riwaya ya mwisho, yaani Dunia Mti Mkavu, ikijitokeza kwa ubora katika kundi hili, na hasa inavyoyajadili maudhui katika mazingira ya wakati wake kwa jicho la ufahamu wa sheria zinazoyatawala maendeleo na mahusiano ya jamii. Wakati ambapo riwaya kadhaa hazijaonyesha wazi kuwepo kwa matabaka ya kijamii na ukinzani uliopo baina yao, Dunia Mti Mkavu imelishughulikia suala hili vizuri. Sifa nyingine ya kisanii ni jinsi msanii anavyoutazama ukweli wa maisha. Katika jadi ya riwaya nyingi wahusika muhimu wanatokana na umuhimu wa nafasi zao katika jamii tangu mwanzo, au baadaye katika maisha yao. Katika riwaya ya kimapinduzi maendeleo yanamlenga mtu (mfanyakazi) wa kawaida. Mtu huyo anatakiwa azinduliwe na kuendelezwa kwa kufahamishwa nafasi muhimu aliyo nayo katika kuleta maendeleo na mapinduzi ya kijamii. Katika Dunia Mti Mkavu watu wa kawaida wamepewa nafasi ya kuwa na hali ya udadisi katika harakati za kujielewa wenyewe, kuielewa jamii yao, mazingira yao, na mahusiano ya hayo yote. Mtazamo wa ukweli wa maisha wa riwaya hii ni ule wa upembuzi wa kiyakinifu.
Upungufu wa riwaya hii uko hasa katika upande wa fani. Wasanii wake aghalabu wameondokea kuunda risala za kisiasa. S.A. Mohammed katika Dunia Mti Mkavu amejaribu kulikwepa tatizo hili kwa kutumia sana mifano.
Hatimaye kuna hadithi nyingi zilizoandikwa katika miaka ya themanini ambazo tumeziweka chini ya fungu la riwayapendwa kutokana na ukweli kuwa zinasomwa na idadi kubwa ya watu, hasa vijana.15 Maandishi ya namna hii kwa bahati mbaya yamezungumziwa kidogo sana na wahakiki wa fasihi ya Kiswahili kwa sababu yanadhaniwa kuwa hayana umuhimu kama vile riwayadhati. Lakini kwa sababu maandishi haya yanasomwa na wengi, hasa vijana – ambao ni taifa la kesho – hayakosi yawe na jambo fulani linalowavutia na pengine hata kuwaathiri. Je, riwaya hii au maandishi haya yana nafasi gani katika kuakisi ukweli wa maisha? Riwaya hii imejitokeza katika mikondo ya mapenzi na mazingira, uhalifu na upelelezi. Riwaya hii imelaumiwa na wahakiki kuwa ni ya utoro wa ukweli wa maisha kwa sababu inauakisi ‘ukweli’ ambao hauchukuani na mazingira yetu; pia imedhaniwa kuwa inafundisha majangili na wahalifu mbinu mpya katika shughuli zao za kufanya uhalifu.16
Ijapokuwa katika sehemu ya nadharia tumeona kuwa katika ukweli wa kisanaa, ‘ukweli’ wa kauli huweza kuvuka mipaka ya hali halisi, lakini ukweli huo unatakiwa usipingane na matamanio na malengo ya jamii. Katika kazi nyingi za riwayapendwa kiasi cha mwigo kutokana na fasihipendwa ya kigeni pamoja na filamu kimezidi hadi kuweza kumnyima msanii nafasi ya kubuni kazi zenye utajiri wa mawazo yake mwenyewe na ujumi wa jamii yake. Hata hivyo, kuna waandishi wa kutoka katika kundi hili, kama vile Mbunda Msokile, ambao kazi zao hazina budi kutazamwa kwa jicho tofauti kidogo kutokana na jinsi wanavyolishughulikia suala kuu la wakati wetu ambalo ni m’gongano wa kitabaka, wakionyesha mtu wa kawaida anavyoonewa.17 Kwa kuwa riwayapendwa itaendelea kuwa baina yetu kwa muda mrefu ujao kutokana na kupendwa na wengi, pengine wasanii wangenasihiwa wajaribu kuiandika riwayapendwa inayozibomoa kuta zinazouhifadhi utoro wa ukweli wa maisha. Pia wahakiki wangejihusisha nayo zaidi ili kuifahamu vizuri zaidi, na kuona jinsi ya kuisaidia iyafae mazingira yake, kuliko kuishambulia tu au kuisoza pembeni.
Baada ya kuipitia mifano hii michache ya waandishi wa Kiswahili na jinsi wanavyolitazama suala la ukweli wa maisha katika wakati wao, bado swali la msingi linabaki: Je, ni mtazamo upi wa ukweli wa maisha ungefaa kutumiwa na wasanii wetu? Swali hili linastahili kujibiwa na wakati. kwa maana, kadiri wakati unavyozidi kusonga mbele ndivyo uga wa uelekeobinafsi (subjectivism) unavyozidi kupungua, na ule wa uhalisi (objectivism) kuzidi kupanuka kutokana na mabadiliko ya mahusiano ya kijamii na kiasili. Na ikiwa kauli hii ni sahihi maana yake ni kwamba mitazamo ya ukweli wa maisha itazidi kujichuja kufuatana na wakati wa historia hadi hapo mtazamo bora zaidi utakapofikiwa (huenda kwa waumini wa dini mbalimbali ni siku ya kiama, na kwa waMarx ni siku ukomunisti utakapopatikana). Kwa wakati huu mahusiano ya kijamii yanadhihirisha ongezeko la mapambano ya kitabaka kati ya walionacho na wasionacho, kati ya watawala na watawaliwa wanaokandamizwa na kuonewa; kuna ongezeko la harakati za kupigania ustawi wa jamii kwa njia ya mapinduzi ya kisayansi na kiteknolojia, harakati za kupiga vita njaa, umaskini na ujinga, na pia kusisitiza suala la amani na maendeleo ya binadamu. Riwaya inayostahili ya wakati huu ni ile inayousawiri na kuupigania ukweli huu wa maisha.
Hata hivyo, pamoja na kuwa waandishi wa Kiswahili hawajaziandikia mada hizi kwa upana wa kutosha, lakini ni suala la wakati tu, kwani wanazidi kuandika. Lakini vile vile si lengo la waandishi kujiandikia wenyewe au kuwaandikia wahakiki ili kazi zao zihakikiwe, bali lengo lao kuu ni kuwaandikia wasomaji ili kuwasiliana nao juu ya maisha kwa njia maalumu ya kiujumi: kwa kufurahisha, kusikitisha au yote mawili kwa pamoja. Bila msomaji, waandishi na hata wahakiki wanafanya kazi bure; na majadiliano haya juu ya ukweli wa maisha katika riwaya au fasihi yanakuwa ni kupoteza muda tu. Kwa bahati mbaya hutokea kwamba wale ambao wangetakiwa kusoma kazi hizi zaidi ili wajifunze zaidi juu yao wenyewe na shughuli zao na uhusiano wao na jamii, n.k., hawajajenga bado hamu na tabia ya kuzisoma kazi za fasihi. Hivyo uandishi unakuwa kama ni shughuli ya wasanii kwa ajili ya mashule na vyuo tu. Na kwa jinsi hiyo nafasi ya msanii na umuhimu wake bado havijapata uzito unaostahili katika jamii yetu.
Kumbe riwaya nzuri au kazi nzuri ya fasihi ni mfano wa ‘nadharia’ zinazosubiri kutekelezwa; nadharia ambazo zimetayarishwa na waandishi baada ya kuyachunguza mazingira yao kwa makini, wakayasawiri matukio kwa kuyakosoa au kupendekeza njia ambazo zingeyafanya maisha ya jamii yawe bora zaidi, na pia kuifanya dunia isiwe ni ‘uwanja wa fujo’, bali uwanja wa mapatano, furaha, amani na maendeleo. Huenda upana huu wa mada utamfanya mtu ajiulize ni kwa vipi riwaya ya Kitanzania inayotumia Kiswahili itajitanua namna hiyo katika majukumu yake. Jibu ni kwamba siku hadi siku Kiswahili kinazidi kupata nyanja mpya na hadhi mpya za utumishi wake. Watu wengi walioko nje ya dunia ya Kiswahili wanazidi kujifunza Kiswahili na kuweza kusoma kazi za wasanii wetu. Kwa njia hii kazi zinazowavutia zinaweza kufasiriwa katika lugha zao kama baadhi ya kazi zilivyoanza au kwisha kufasiriwa tayari.18
Marejeo na Maelezo
1. Dondoo kutoka katika kitabu kilichohaririwa na J. Krueger (1983) Aesthetik der Antike. Aufbau-Verlag, Berlin und Weimar, uk. 28.
2. E. Hussein (1969) Kinjeketile. OUP, Nairobi, uk. 49.
3. Shaaban Robert (1968) Kielelezo cha Fasili. Nelson, Nairobi uk. 93 – 4.
4. Buhr, M. na Kosing, A (1982) Kleines Woerterbuch der Marxistisch – Leninistischen Philosophie. Dietz Verlag, Berlin, uk. 203 – 5.
5. KulturPolitisches Woerterbuch (1978) Dietz-Verlag, Berlin, uk. 751 – 6. Rejea “Kuenstlerisher Wahrheit”.
6. E. Bertoncini (1977) “Two Contemporary Swahili Writers…” katika The East African Experience, Frankfurt a.m. uk. 88.
7. J. Madumulla (1982) “Maendeleo ya Wahusika katika Riwaya ya Kiswahili,” Makala hayajachapishwa. Chuo Kikuu Dar es Salaam.
8. Riwayapendwa imejadiliwa kwa kirefu katika makala yaitwayo “Riwaya ya Kiswahili (Tanzania) katika miaka ya Themanini” yaliyoandikwa na J. Madumulla (1987) na huenda yakatoka katika Lugha Yetu.
9. E. Bertoncini, m.y.k., uk. 87.
10. k.h.j., uk. 87.
11. M. Mulokozi (1976) “Development of Kiswahili Literature,” katika: Daily News Supplement, DSM, 21.7.1976, uk. 6, 11 & 18.
12. Wanadhanaisni wana namna kadhaa za kuieleza falsafa yao, hii ikiwa ni namna yao mojawapo, wakiwa na lengo la kusisitiza kwamba wazo ndilo huja kwanza kuliko uzoefu (au tendo). Soma Kleines Woerterbuch der Philosophie chini ya “Materialismus.”
13. Neno hili “hemetiki” hnatokana na neno la Kiingereza hermeneutics linalosimamia mbinu mojawapo ya kisanaa ya kuelewa maana na kutambua mpango wa maandishi ambapo vipimo muhimu vya kiitikadi vya wakati ‘fulani’ vimetumika. Mbinu hii ilianza kupata nguvu katika dini, hasa namna ya kufafanua Biblia, tangu karne ya 16 hivi.
14. Kwa habari zaidi soma Senkoro, F.E.M.K. (1987) “Nadhana ya Fasihi na Fasihi ya Kiswahili ya Majaribio” (Makala hayajachapishwa), au D.C.
Hov (1978) The Critical Circle, UCP. London. 15. J. Madumulla (1987) “Riwaya ya Kiswahili (Tanzania) katika Miaka ya themanini,” m.y.k.
16. P. Mhando na N. Balisidya (1976) Fasihi na Sanaa za Maonyesho, TPH, uk. 70. Pia Madumulla (1987) k.h.j. uk. 7.
17. Soma M. Msokile (1981) Nitakuja kwa Siri, DUP, Dar es Salaam.
18. Mifano ya vitabu vinavyofasiriwa au viliyyofasiriwa ni Myombekere na Bugonoka, Kusadikika, Gamba la Nyoka, Dunia Uwanja wa Fujo, na baadhi ya vitabu vya S.A. Mohamed.
Mwl Maeda