SHAIRI: NI HERI NINGEKUROGA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: NI HERI NINGEKUROGA (/showthread.php?tid=834) |
SHAIRI: NI HERI NINGEKUROGA - MwlMaeda - 08-13-2021 NI HERI NINGEKUROGA Mara ngapi nakuonya, uwe wangu peke yangu, Haya uliyoyafanya, yamenitia uchungu, Vile nilivyokuonya, ni bure maneno yangu, Kwa haya uliyofanya, ni heri ningekuroga. Sikuthubutu limbwata, moyo wako kuushika, Niliepuka matata, usije ukawehuka, Leo haya kunipata, na mimi nimegutuka, Kwa haya uliyofanya, ni heri ningekuroga. Mara kadha niliwaza, nende kwa Kalumanzila, Mawazo nikapuuza, chanzo cha haya madhila, Sasa kimetua kiza, siwezi tena kulala, Kwa haya uliyofanya, ni heri ningekuroga. Sasa mbali umekwenda, kurudi umekaidi, Ili unitoe chonda, utimize makusudi, Nimebakia kukonda, pamwe na zangu juhudi, Kwa haya uliyofanya, ni heri ningekuroga. Yako simu ninapiga, haupokei mwendani, Nimebaki kichwa boga, sijui nifanye nini, Au chupa ningesaga, nitoweke duniani, Kwa haya uliyofanya, ni heri ningekuroga. Nakumbuka ile juzi, na ulivyonitukana, Umezidi siku hizi, tena mapenzi hakuna, Nalia sitokwi chozi, ninabaki kujikuna, Kwa haya uliyofanya, ni heri ningekuroga. Beti chache nasimama, sili ugali kushiba, Unionee huruma, uchungu unanikaba, Kwa raha imegoma, zimepita siku saba, Kwa haya uliyofanya, ni heri ningekuroga. Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 RE: SHAIRI: NI HERI NINGEKUROGA - MwlMaeda - 08-14-2021 Kunywa maji yatulie,tumlani ibilisi Mie sipendi ulie,ichomwe yako nafusi Filieda nisikie,penzi letu sijepesi Umeniroga kitambo,si mizizi ni mahaba Hakufiki Balkisi,mrembo wazama zile Wote nawaona ngisi,sitamani nende kule Ukutoke wasiwasi,wadharau misukule Umeniroga kitambo,si mizizi ni mahaba Sikuisikia simu,ulipopiga mwandani Usikupate wazimu,nilikuwepo bafuni Usifanye ninywe sumu,roho niweke rehani Umeniroga kitambo,si mizizi ni mahaba Upesi ninarejea,ziara ninakatisha Naja hima kukulea,maneno yamenitisha Moyo wangu waelea,imenihama bashasha Umeniroga kitambo,si mizizi ni mahaba Abdul Ndembo Mburahati Sekondari |