SHAIRI: DUNIA MWENDO WA NGISI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: DUNIA MWENDO WA NGISI (/showthread.php?tid=820) |
SHAIRI: DUNIA MWENDO WA NGISI - MwlMaeda - 08-10-2021 DUNIA MWENDO WA NGISI Nisikilize Kidawa, ewe mwanangu mpendwa Neno langu nakugawa, kwako liwe la kupandwa Mwana nikuweke sawa, kesho usijekupindwa Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa. Kidawa wangu sikia, neno langu ulishike Babayo nakuambia, nataka uhamasike Ungali waibukia, sitaki uhasirike Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Tulikulea kwa dhiki, mamiyo kesha kwambia Mengi hayahesabiki, ambayo tumepitiya Ila kunena mithaki, yote tumevumilia Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Ungali mkangaichi, maoziyo yana kiwi Ila hauchi hauchi, kesho yatapata kawi Daima mficha uchi, uzazini huwa hawi Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Macho utapofumbua, uitazame dunia Mtima utachanua, uhamu kuchapukia Mwanangu hili tambua, babayo nashadidia Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Ina vingi vipendezi, vya hadhi na shani yake Isoisha uchombezi, hutaki hadi utake Mwana nakupa hirizi, ujikingie makeke Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Dunia tambara bovu, ukivuta utachana Itakutia makovu, ukichezeya ujana Ufumbate utulivu, kuepuka kuzozana Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Dunia nzito tambua, endapo huna akili Yaweza kukuumbua, nakukutia thakili Leo ninakuzindua, tafakari kulihali Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Dunia ni mduwara, huzunguka kama pia Kwa idhini na kudura,hujirudia Usitende kwa hasira, keshoye ukajutia Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Dunia ni mapishano, Leo mbele kesho nyuma Kuishi ni mapambano, kusotaka uadhama Kushinda kwenye pigano, mtegemee Karima Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Dunia ni maabara, jaribu hili na lile Yatende kwa tahadhara, uepuke mizingile Ujitoapo kafara, dunia ni ile ile Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Dunia ni darubini, kwayo mwana jiakisi Uishi kwa kubaini, na kuheshimu mapisi Wenzako usiwahini, kwa tendo au kwa tusi Dunia mwendo wa ngisi, isikuteke Kidawa Adamu Djibril Jibril Adam Abu sanaya |