ETIMOLOJIA YA MANENO ' REHEMA' na 'BARAKA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO ' REHEMA' na 'BARAKA' (/showthread.php?tid=2549) |
ETIMOLOJIA YA MANENO ' REHEMA' na 'BARAKA' - MwlMaeda - 05-09-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' REHEMA' na 'BARAKA' Neno *rehema* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: i-/zi-]* yenye maana zifuatazo: 1. Neema, heri au baraka anazopata mtu kutoka kwa Mungu. 2. Huruma; moyo wa huruma. *Mfano:* Kupona katika ajali ile ni kwa rehema za Mungu tu. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *rehema* limetokana na neno la Kiarabu *rahma* (soma: *rahmatun/rahmatan/rahmatin رحمة* ) lenye maana zifuatazo: 1. Heri na neema. 2. Msamaha. 3. Upole na huruma. 4. Moyo wa huruma. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *rahmatun/rahmatan/rahmatin رحمة*) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *rehema* maana yake katika Kiarabu haikubadilika bali iliongezwa maana mpya ya *baraka* neno ambalo katika Kiarabu linajitegemea Kisemantiki. Neno *baraka* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino [Ngeli: i-/zi-]* jumla ya mambo yote mazuri katika maisha ya mtu. 2. *Nomino [Ngeli: a-/wa-]* jina la mtu aghalabu mwanamume lenye maana ya ulinzi na upendeleo wa Mungu kwa mtu katika mambo yote. Neno hili *baraka* (soma: *barakatun/barakatan/barakatin بركة* ) katika lugha ya Kiarabu lina maana zifuatazo: 1. Maendeleo, kukua na ustawi. 2. Nyongeza, ziada. 3. Furaha, uchangamfu, starehe. 4. *Habasoda* ; aina ya mbegu zenye rangi nyeusi kama vile za vitunguu ambazo hutibu maradhi mbalimbali, *habbatul barakah حبة البركة* mbegu za baraka. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili *baraka*(soma: *barakatun/barakatan/barakatin بركة*) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *baraka* lilichukua maana mpya ya *jumla ya mambo yote mazuri katika maisha ya mtu* na pia jina la mtu aghalabu mwanaume lenye maana ya *ulinzi na upendeleo wa Mungu kwa mtu katika mambo yote.* *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |