ETIMOLOJIA YA NENO 'JABALI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'JABALI' (/showthread.php?tid=2538) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'JABALI' - MwlMaeda - 05-02-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'JABALI' Neno jabali katika lugha ya Kiswahili ni Nomino [Ngeli: li-/ya-, wingi: majabali] yenye maana zifuatazo: 1. Mwamba mkubwa uliochomoka juu ya ardhi au maji. 2. Mwinuko mkubwa wa jiwe juu ya ardhi. Neno jabali pia ni Nomino [Ngeli: a-/wa-, wingi: majabali] yenye maana zifuatazo: 1. Mtu mwenye umbo kubwa na nguvu nyingi. 2. Mtu aliye gwiji katika jambo. Msemo: Jabali la muziki: bingwa katika masuala ya muziki. Kadhalika, neno jabali ni Nomino [Ngeli: i-/zi] yenye maana ya mshono wa kanzu uliopo kati ya bega moja hadi jingine upande wa mgongoni. Katika lugha ya Kiarabu neno jabali linatokana na neno la Kiarabu jabal (soma: jabalun/jabalan/jabalin جبل) lenye maana zifuatazo: 1. Eneo kubwa la ardhi lililojitokeza juu zaidi ya sehemu nyingine za ardhi; mlima. 2. Mtu thabiti asiyeyumba katika misimamo na maamuzi yake. 3. Nyoka, ibnatul jabali ابنة الجبل. 4. Sauti inayojirudia baada ya mawimbi ya sauti kugonga mahali na kumrudia mzungumzaji aghalabu hutokea pangoni, msituni au kwenye jengo kubwa na tupu; mwangwi . 5. Kundi la watu; umma. 6. Uwanja; uga. 7. Kiongozi wa watu/ukoo. 8. Mwanazuoni. Kinachodhihiri ni kuwa neno jabalun جبل lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno jabali lilibeba maana mpya na kuziacha zile maana za neno hili katika lugha ya Kiarabu. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. RE: ETIMOLOJIA YA NENO 'JABALI' - MwlMlela - 05-04-2022 Safi sana, Uga huu unamaarifa mengi sana |