ETIMOLOJIA YA NENO 'ALASIRI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'ALASIRI' (/showthread.php?tid=2516) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'ALASIRI' - MwlMaeda - 04-19-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'ALASIRI' Neno *alasiri* katika lugha ya Kiswahili ni *Nomino [Ngeli: i-/zi-]* yenye maana zifuatazo: 1. Kipindi cha siku kati ya saa tisa mchana hadi saa kumi na moja na nusu jioni. (Kamusi ya Karne ya 21, imesajili alasiri ni muda baina ya saa nane jioni na saa Kumi na moja jioni.) 2. Kipindi cha Swala ya Waislamu baina ya saa tisa na kumi na mbili jioni. Katika lugha ya Kiarabu neno *alasiri* linatokana na neno la Kiarabu *al-aswru (soma: al-aswru/al-aswra/al-aswri العصر)* lenye maana zifuatazo: 1. Kipindi kinachonasibishwa na mtu fulani, dola fulani na mfano wa hayo. *Aswru Shaikhi Ali Hasan Mwinyi عصر الشيخ علي حسن مويني* zama za Mzee Ali Hasan Mwinyi. 2. Wakati kivuli cha kitu kinapokuwa mfano wake au zaidi; *wakati wa Swala ya Alasiri.* Kinachodhihiri ni kuwa neno *al-aswru العصر* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *alasiri* maana yake ya msingi katika lugha ya asili - Kiarabu inayohusu muda wa Swala ya Alasiri haikubadilika na maana ya jumla ya wakati unaonasibishwa na mtu fulani au dola fulani iliachwa. *TANBIHI:* Kutumia saa kubaini wakati wa Swala ya Alasiri si kipimo sahihi na maana hiyo itahusika tu na nchi/maeneo ambayo muda uliyotajwa unaafikiana na muda wa Swala ya Alasiri si kinyume chake. Kipimo sahihi ni kuwa wakati wa Swala ya Alasiri ni pale kivuli kinapokuwa mfano kitu husika hadi kivuli kinapokuwa mara mbili ya mfano wa kitu husika. Mwisho wa wakati wa Swala ya Alasiri ni kuzama Jua na huo ni mwanzo wa wakati wa Swala ya Magharibi. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |