ETIMOLOJIA YA NENO 'MSHAHARA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'MSHAHARA' (/showthread.php?tid=2510) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'MSHAHARA' - MwlMaeda - 04-13-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'MSHAHARA' Neno *mshahara* katika lugha ya Kiswahili ni *Nomino [Ngeli: u-/i-, wingi: mishahara]* yenye maana zifuatazo: 1. Malipo ya mwezi anayopewa mwajiriwa kwa kazi aliyofanya. 2. Ujira anaolipwa mtu na mwajiri wake kila baada ya kipindi fulani kwa kazi aliyotumikia. Katika lugha ya Kiarabu neno *mshahara* linatokana na neno la Kiarabu *shahru (soma: shahrun/shahran/shahrin شهر)* lenye maana zifuatazo: 1. Mwezi, sehemu moja ya sehemu kumi na mbili za Kalenda ya mwaka unaozingatia mzunguko wa Mwezi *As-Sanatul Qamariyyatu السنة القمرية* au mwaka unaozingatia mzunguko wa Jua *As-Sanatush Shamsiyyatu السنة الشمسية*. 2. Mwezi Mwandamo. 3. Ulimwengu. Kinachodhihiri ni kuwa neno *shahrun شهر* lilipoingia katika Kiswahili lilitamkwa *shahara* kisha likaingia katika ngeli ya *m-/mi* - na kupatikana neno *mshahara* lililochukua maana mpya ya *ujira anaolipwa mtu na mwajiriwa wake kwa kazi aliyoifanya katika kipindi maalumu.* *TANBIHI* : Maneno ya Kiarabu yenye maana ya ujira anaolipwa mtu na mwajiri wake mwishoni mwa mwezi ni *raatibun shahriyyun راتب شهري* mshahara wa mwezi au *badalun shahriyyun بدل شهري* posho ya mwezi. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |