ETIMOLOJIA YA NENO 'ADUI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'ADUI' (/showthread.php?tid=2456) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'ADUI' - MwlMaeda - 03-15-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'ADUI' Neno *adui* katika lugha Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino [Ngeli: a-/wa- wingi: maadui]* mtu, mnyama au kiumbe chochote kinachofanyia kiumbe kingine uovu; mtu aliye dhidi yako, kitu kibaya unachopambana nacho kwa mfano: magonjwa, njaa, chuki, wivu, ujinga na kadhalika. *Methali* : adui wa mtu ni mtu, adui mpende, adui aangukapo mnyanyue. 2. *Nomino [Ngeli: a-/wa-]* mtu unayekabiliana naye katika mchezo; *mshindani* . Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *adui*( *soma: aduwwun/aduwwan/aduwwin عدو)* ni nomino ya Kiarabu yenye maana ya mtu aliye dhidi yako; hasimu wako, mgomvi wako. Waarabu wana msemo: *aduwwun aaqilun khayrun min swadiiqin jaahilin عدو عاقل خير من صديق جاهل* adui mwerevu ni bora kuliko rafiki mjinga. Katika Qur'aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 168 shetani ametangazwa kuwa adui wa mwanadamu. Imeandikwa: *Walaa Tattabiu Khutwuwaatish Shaytwaani Innahuu Lakum Aduwwum Mubiin. ولا تتبعوا خطوات الشيطان إنه لكم عدو مبين* Wala usifuate nyendo za shetani, hakiki yeye ni adui aliye wazi. Kinachodhihiri ni kuwa neno la Kiarabu *aduwwun/aduwan/aduwwin عدو)* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *adui* maana yake katika lugha yake ya asili - Kiarabu haikubadilika bali iliongezeka maana ya mtu unayekabiliana naye katika mchezo; *mshindani* . *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |