ETIMOLOJIA YA NENO 'HAYATI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'HAYATI' (/showthread.php?tid=2452) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'HAYATI' - MwlMaeda - 03-09-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'HAYATI' Neno *hayati* katika lugha Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino [Ngeli: a-/wa-]* mtu hai anayeombewa rehema za Mwenyeezi Mungu. 2. *Nomino [Ngeli: a-/wa-]* mtu aliyekwishafariki dunia. *Msemo: si hayati si mamati*: si mzima, si marehemu, hali yake ni mbaya sana, taabani, hajijui, hajitambui. 3. *Nomino [Ngeli: i-/zi-]* uhai, au uzima, 'wakati' au 'enzi' ya kipindi fulani cha mtu aliye hai. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *hayati*( *soma: hayaatun/hayaatan/hayaatin حياة)* ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo: 1. Kukua, maendeleo, kubakia. 2. Manufaa. 3. Katika elimu ya Bailojia *ilmul ahyaai علم الأحياء*: jumla ya vinavyoshuhudiwa kwa wanyama na mimea miongoni mwa sifa bainifu zinazowatofautisha na maada, mfano: kula, kukua, kuzaana na mfano wa hayo. 4. Kipindi kati ya kuzaliwa na kufa; siku na miaka. 5. Kiwango cha maisha. 6. Maisha kwa ujumla, kwa mfano: maisha ya mjini, maisha ya kijijini. 7. Kuendelea kubakia mwanadamu, mnyama na mmea na uzima wake, harakati zake na kukua kwake. Kinachodhihiri ni kuwa neno la Kiarabu *hayaatun/hayaatan/hayaatin حياة)* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *hayati* lilichukua kutoka lugha yake ya asili - Kiarabu maana ya mtu hai na kupewa maana mpya ya mtu aliyekwishafariki. *Tanbihi:* Maana ya neno *hayati* kuwa mtu aliyekwishafariki, yumkini imetokana na imani ya Kiislamu ya kutekeleza maagizo ya Mwenyeezi Mungu ya kutowaita watu wema waliofariki kwa jina la *wafu (maiti)* kwa kuwa wao ni watu hai wanaopewa riziki na Mola wao.(Rejea Qur'aan Tukufu, Sura ya 3 (Surat Aali Imraan, Aya 169 kuwa: " *Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti (wafu). Bali hao ni wahai (watu hai), wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi "* Kadhalika, imani kuwa maiti hurudishiwa roho zao na kuwa na maisha maalumu yaitwayo " *maisha ya Barzakh* " inashadidia dhana ya aliyekufa kuitwa ' *hayati*'. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |