ETIMOLOJIA YA NENO 'MBASHARA/MUBASHARA' NA 'MUBASHIRI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'MBASHARA/MUBASHARA' NA 'MUBASHIRI' (/showthread.php?tid=2392) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'MBASHARA/MUBASHARA' NA 'MUBASHIRI' - MwlMaeda - 02-08-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'MBASHARA/MUBASHARA' NA 'MUBASHIRI' Neno *mbashara* katika lugha ya Kiswahili ni *kivumishi* chenye maana ya kinachorushwa hewani moja kwa moja na kusikika na kuonwa wakati huohuo aghalabu kupitia matangazo ya redio na televisheni. Mfano: Kipindi mbashara cha televisheni kitarushwa saa moja kamili usiku. Katika lugha ya Kiarabu, neno linalofanana na hili kimuundo ni neno la Kiarabu *mubaashara* *( *soma: mubaasharatun/mubaasharatan/mubaasharatin مباشرة)* tendo-jina ( *masw-dar مصدر* ) litokanalo na kitenzi cha Kiarabu *baashara باشر* chenye maana zifuatazo: 1. Ameanza jambo au shughuli yeye mwenyewe bila ya kumtegemea mwengine. 2. Amedhihiri. 3. Amewahi kufanya tendo fulani; mara moja. Neno *mubashiri* (Soma: *mubaashirun/mubaashiran/mubaashirin مباشر*) katika lugha ya Kiarabu ni jina la mtendaji ( *faailun فاعل* ) wa *kitenzi* cha Kiarabu *baashara باشر* lenye maana zifuatazo: 1. Kitu kinachotokea bila ya kusaidiwa na kitu kingine: *sababun mubaashir سبب مباشر* sababu ya moja kwa moja. 2. Amezungumza kwa kutumia data/nyaraka rasmi. 3. Matangazo ya moja kwa moja ya redio na televisheni *bath-thun mubaashir بث مباشر.* 4. Uhusiano wa moja kwa moja usiokuwa na mtu wa kati. *Alaaqatun mubaashiratun علاقة مباشرة.* 5. Kodi isiyo ya moja kwa moja *dhwaribatun ghayru mubaashiratin ضريبة غير مباشرة* kama kodi inayopatikana kutokana na mauzo ya stampu. Kinachodhihiri ni kuwa Waswahili wamelichukua neno la Kiarabu *mubaasharatun مباشرة* wakalitohowa kuwa *mbashara* na kulipa maana ya neno la Kiarabu *mubaashirun/mubaashiran/mubaashirin مباشر* ambalo moja ya maana zake ni matangazo ya moja kwa moja aghalabu kupitia redio na televisheni. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |