MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 2 - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Watunzi wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=17) +--- Thread: MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 2 (/showthread.php?tid=1407) |
MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 2 - MwlMaeda - 10-29-2021 Bila shaka, baada ya kusoma
mawazo mengi ya Shaaban Robert juu ya maisha ya binadamu, mtu atakuwa na hamu ya kutaka kujua maswali gani yeye mwenyewe alivyoishi. Na pengine atataka kujiuliza maswali kama haya: Je, yeye mwenyewe Shaaban aliishije na jamaa zake? Aliishi kwa kupendana, kusaidiana na kwa usawa wa ujamaa, kama ionekanavyo katika Adili na Nduguze? Hayo ni kuhusu maisha yake na jamaa yake. Lakini je, yeye binafsi aliishi kwa kufanya kazi kwa bidii kadiri ya uwezo wake, na alijitegemea kama awaidhivyo katika Wasifu wa Siti Binti Saad? Je, mtu akiyachunguza maisha yake ataona nini katika uhusiano wa uraia wake nan chi yake? Majibu ya maswali ya namna hii ndiyo nipendayo tuyapekuepekue katika Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Siyo kwamba mimi nataka kukariri au kufupisha maandishi ya kitabu chake, bali natarajia kutoa maoni yangu kuhusu maisha yake, na kuyalinganisha na maoni yake kuhusu maisha ya watu kwa ujumla. Kama ilivyo sheria ya asili, mtu
huzaliwa na kufa. Na katikati ya hayo mambo mawili ndipo penye maisha ya mtu. Mambo mengi yanaweza kutokea katika nafasi hiyo. Napenda kutumia neno hili ‘nafasi’ ili kuleta maana halisi kwamba maisha ya mtu ni nafasi hasa ya kutenda mambo kadha wa kadha. Maisha ya mtu ndiyo nafasi yake, na matendo yote hutegemea nafasi hiyo. Nafasi hii ina ncha, na kwa hivyo huisha. Kwa sababu hii, maisha si kitu cha daima na milele. Yana ukomo wake. Inaelekea kuwa Shaaban Robert
alijivika mawazo haya kichwani mwake. Lakini hapa pana jambo zima: nalo ni kwamba hakukomea tu kuwaza kwamba maadamu maisha ni nafasi ya mtu basi ni lazima mtu ayatumie vema kwa ajili yake binafsi. Marehemu aliona kwamba ingawa mtu ndiye aliyepewa maisha, lakini maisha yenyewe ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Ikiwa basi ‘maisha ya mtu ni msingi wa maendeleo ya nchi’ ndiyo kusema juu ya maisha machafu au mazuri? Maisha ya bidii ya kazi, au ya ulegevu na uvivu? Maisha yenye mipango maalumu, au yale yajiendeayo yenyewe ovyo ovyo tu? Maisha ya kibinafsi au maisha ya ujamaa? Maisha ya marehemu ya miaka
ishirini na sita ya mwanzo hayakuendelezwa katika Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini kwani, kama asemavyo katika utangulizi, hayo yaliandikwa katika insha ambayo haikupigwa chapa na ambayo ilikuwa katika mwandiko wa mkono na kisha haikuwa na nakala. Kwa hivyo basi, katika hiki, mambo hayo hayamo. Baada ya shindano, insha hiyo haikuonekana tena. Hata hivyo, tuna ufununu kwamba hayo hasa yalikuwa maisha ya mwandishi wakati wake wa utoto-alivyopenda kucheza na alivyocheza, alivyokwenda vyuoni na kumbini hadi akawa mtu mzima, akapata kazi na kuoa. Maisha ya kwenda vyuoni na kupata kazi hatimaye ni maisha ya aina ya siku za kisasa. Lakini hakuna mengi ya kuyatolea maoni kwani tumepewa hayo kwa muhtasari tu. Kwa hivyo, tuanzie mwaka wa
ishirini na saba wa maisha yake. Muhtasari nilioutaja awali
haugusiijambo lolote kubwa ambalo Shaaban alilifanya kabla ya miaka hii ishirini na saba. Watu wengi, kama hawajafanya lolote katika miaka yao ishirini na mitano ya kwanza, hakukata tamaa kuwa hawataweza tena kufanya lolote kwa sababu wamekuwa ‘wazee’ ati! Je, Shaaban Robert alijionaje alipokuwa na umri huo? Anasema, ‘Maisha yalikuwa bado mapya na matumaini yake yalikuwa mengi sana.’ Alikuwa mzima wa afya na mwenye furaha moyoni. Anasema, ‘Nilikuwa katika mwanzo tu wa maisha; bado sijafika katikati wala mwisho wake.’ Lakini hakuridhika kwa zile ‘kurasa’ chache za maisha yake ya nyuma kwani hazikuandikwa yoyote yaliyo azizi yawezayo ‘kuwatamanisha wengine kuyanakili’ wala mwenyewe hazikumridhisha kwamba alitarajia maisha yake yawe ni kielelezo kwa wengine na, wawezao, wayanakili. Hakukata tama kwani aliwaza kuwa pengine ubora wa mtu huwezekana kuwa katika wakati ujao. Yaliyopita si ndwele; ganga yajayo. Kwa hivyo alijiandaa kutumia nafasi yake. Shaaban aliamini kuwa ipo bahati
na huwapata watu, lakini haiji tu hivi hivi-sharti mtu ajikongoje kuiendea ndipo akutane nayo, au ainyoshee mkono kujaribu kuishika. Kwa kutokufanya hivi watu wamezichelewesha bahati zao au pengine wamezikosa kabisa. Na bahati haitokei mara kwa mara. Na hata kama ingetokea mara kwa mara maisha ya mtu ni nafasi fupi iliyo na mwisho. Akiwa na mawazo hayo juu ya
bahati, Shaaban akayapata maisha yake mpango maalum na akaweza kuzitandaza fikra zake zote huku ana picha kamili ya nini atakacho. Katika mpango wa maisha yake jambo moja alilitilia mkazo vilivyo: hakutaka utajiri au mamlaka juu ya watu. Ingawa hivi vilileta fahari, lakini kwa wakati ule vitu hivi alivihofu. Msomaji anaweza kukubaliana naye au kumpinga akijiuliza kuwa ile miaka ya 1936 ilikuwa ni enzi gani? Jambo alilotarajia maishani mwake ni ‘jina lililo mbali na madoa katika umaskini na unyonge.’ Kwa hivyo kama jambo hili lilikuwa jepesi au gumu, zuri au baya, la kumpa mtu moyo au uchovu, heri lilinganishwe nay ale mengine mawili kwa kufuata mazingira ya nchi ya Tanganyika siku hizo. Na alitarajia kulipata hilo ‘jina’angalau nusu au hata robo yake. Hebu sasa tumwangalie Shaaban
Robert akiwa mchumba, mume na mfiwa-kwani jambo la ndoa, ingawa si watu wote wanaolitekeleza, ni mojawapo ya miinuko ionekanayo katika maisha ya mtu. ‘Kabla ya kuoa nilitafuta umbo namna yake muda wa miaka kumi!’ Shaaban alikuwa amemtafuta mke ambaye ‘uzuri wake ulikuwa kamili’ na kwa tabia alikuwa mwaminifu na mfano wa kuiga katika nyumba. Mchanganyiko huu wa uzuri wa umbo, pamoja na tabia ndio uliokuwa ‘jembe’ au ‘nyumba’ kwa maongezi ya uchaguzi wa mke. Baada ya kumwoa Amina mwenye sifa
zote hizo mbili, Shaaban alimpenda sana na kumshukuru kwamba alimsaidia katika mambo mengi wakati wa maisha yao pamoja ambayo yeye pekee yangelimshinda kuyatenda. Na mengi waliyatarajia kuyafanya pamoja, Shaaban na Amina, lakini ugonjwa ulimnyakua mapema mkewe mpenzi na akamtangulia mumewe. Bwana Shaaban hakukilalamikia kifo kwani alijua ni lazima kije; alilalamikia kuja kwake mapema hivyo. Akalia machozi kama alivyomlilia marehemu babake na alizipamba dua zake kwa shairi aliloombea marehemu mkewe akubaliwe peponi. Methali yasema ‘akosaye la mama
la mbwa huamwa’. Shaaban alifahamu kuwa mwanawe na binti yake waliyakosa malezi na adili zote za mama yao, ndipo akawapa usia katika tenzi ambazo zilitarajiwa kuwaongoza katika maisha yao. Akatarajia kuwalea watoto wake na kuwafundisha wema wa moyoni. Shaaban hakuwaacha watoto wake wakue tu hivi hivi kama ua mwitu linalotanda ovyo bila kuongozwa. Yeye aliwatunza kama maua ya bustanini. Utenzi wa Hati kwa bintiye na Utenzi
wa Adili kwa mwanawe zilikuwa fimbo au kamba zilizo imara na zilizoongoza kukua kwao na maisha yao. Alikuwa na mengi ya kuwausia kuhusu dunia. Urefu wa kila utenzi ulikuwa beti mia moja. Kwa ufupi alimwandikia bintiye usia wa kumuasa aitunze hiyo hati imsaidie katika dunia ngumu na ulimwengu wenye adha, asiwasaliti watu, awe na matendo mema kwani yote hupaazwa kwa Mungu, na hati hiyo iwe mali na nuru kwake, ashike dini kwani ni mali ya roho, ajifunze elimu awe mtalamu wa kupambanua halali na haramu, nyumba yake iwe nadhifu, taabu zikimkabili awe amejiandaa, nia ya maendeleo aitie moyoni, na asingoje bahati imtendee yote, kwani: ‘watu wengi huchelewa kwa kungoja kutendewa.’ Majivuno hayafai, asishiriki uwongo, masuto si mazuri, awe na ulimi wa kulainisha na ulio mtamu, awe na cheko na tabasamu, usoni awe na haya, awapende wote-wenye vyeo na wanyonge-naawe na adabu kwa baba na mama na walio sawa nao, awe mlezi bora, ajifundishe kukinai, mapato yake yawe halali, na waijenge dunia nzuri na ya furaha-yeye na mumewe. Mtoto wake wa kiume vile vile
‘Maisha bila elimualimpa maagizo ya adili. Kwanza alimfundisha awe mcha Mungu, Muumba mbingu nan chi, wanyama na ndege na samaki, na ajuaye yote kwa ghibu bila kusoma kitabu. Ampe yeyote roho yake ili shetani asiiteke. Pili, amtii mkuu wa Serikali bila ya kinyume. Tatu, awape taadhima baba na mama, awatendee kila jema. Nne, afanye taaluma ya lugha. Tano, ajifunze elimu kwani: Hayafai mwanadamu Sababu mambo magumu Mengi sana mbelee. ‘Milango wazi adimu Kwa asiye na elimu Kwa mwenye nayo gumu Hujifungua wenyewe.’ Sita, akioa mke amshike kwa mapenzi bila makeke, awe na msamaha kwake, ampe heshima kama mama wa watoto wake, awapende watoto wake, awafunze taalimu na adili, awapende sana nduguze kama alivyofanya Adili, apatane na masahibu, kwa rafiki zake awe kitu cha makumbuko akiwapo asiwepo, ajenge matendo mema, awapende watu wote, afiche siri zake ila kwa wachache wapasao, akiweka ahadi kutimiza ajitahidi, atoe msaada kwa wenye kulemewa, asiwe mgomvi, awe na uso wenye tabasamu na wenye furaha, afanye kazi kwa bidii bila uvivu, asahihishe makosa, amwombee dua babake ambaye ni Mwafrika madhubuti. Hakika huo ndio usia wa kuwapa watoto majumbani kabla hawajaenda vyuoni, kwani kuna methali isemayo ‘asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.’ Maagizo kama hayo ni tunu, ngao na mwangaza katika maisha. |