FASIHI YA KISWAHILI NI IPI? - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi kwa ujumla (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=73) +--- Thread: FASIHI YA KISWAHILI NI IPI? (/showthread.php?tid=1371) |
FASIHI YA KISWAHILI NI IPI? - MwlMaeda - 10-25-2021 FASIHI YA KISWAHILI NI IPI?
Kabla ya kueleza maana ya fasihi ya Kiswahili ni muhimu kujadili msingi wa kuibuka kwa hoja au mjadala huu. Mjadala huu unaweza kutazamwa kwa kuzingatia kuibuka kwa hoja mbili muhimu kwa nyakati mbili tofauti. Katika kipindi cha kwanza, hoja ya msingi ilikuwa ni katika kujibu swali la Waswahili ni kina nani hasa? Baadhi ya wataalamu walisema kuwa Waswahili ni kabila mahususi linalopatikana katika pwani ya Afrika Mashariki. Hivyo basi, kama kuna kabila la Waswahili hivyo basi, fasihi ya Kiswahili ni fasihi inayohusu kabila hili. Kundi jingine ni lile ambalo lilikiona Kiswahili kuwa kama sawa na Kitanzania. Hawa wataalamu walipinga
madai ya kukiona Kiswahili kuwa kama kabila hivyo basi wakakipatia Kiswahili mipaka
ya kitaifa. Hii ilitokana na ukweli kwamba Tanzania ilikuwa imetangaza rasmi kuwa Kiswahili kitakuwa ni mojawapo ya lugha zake rasmi na ndiyo itakayokuwa lugha ya taifa. Kwa muktadha huu, fasihi ya Kiswahili inatazamwa katika mipaka ya Kitanzania kutokana na fasihi ya Kiswahili kupatikana kutokana na fasihi za makabila mbalimbali mapana ya Kiswahili zaidi ya mipaka ya kitaifa. Lugha ya Kiswahili kwa muda mrefu imetumika nje ya mipaka ya Tanzania. Hii ina maana kwamba imezungumzwa na watu ambao si Watanzania. Kundi linguine ni la wataalamu walioitazama
lugha ya Kiswahili kama iliyovuka mipaka ya Afrika Mashariki. Katika kundi hili lugha ya Kiswahili inatazamwa kama lugha ya kimataifa nan i lugha ya kila mmoja. Katika mazingira kama haya fasihi ya Kiswahili ilifungamanishwa na lugha yenyewe ya Kiswahili bila kuifungamanisha na jamii mahususi. Kipindi cha pili kinahusiana na
hoja inayohusiana na mjadala wa fasihi ya Kiafrika ni ipi? Je, mtu anapotumia lugha ya Kiingereza, kwa mfano hiyo fasihi, itaitwa bado kuwa ni fasihi ya Kiafrika? Kuna mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wataalamu wa Fasihi ya Kiafrika juu ya suala hili. Kuna baadhi wanasisitiza kuwa haiwezekani ukatumia lugha ya Kiingereza au Kifaransa nab ado ukaitazama kuwa hii ni fasihi ya Kiafrika. Wanasisitiza umuhimu wa kutumia lugha za Kiafrika. Wataalamu hawa wanaenda mbali zaidi na kuuliza je, kwa mfano, mtu akiandika kazi ya fasihi kwa kutumia lugha mojawapo ya Kiafrika, lakini kazi hiyo ikibeba utamaduni wa Kiingereza, itaitwa kuwa hiyo ni fasihi ya Kiingereza? Mawazo kama haya, yamesababisha leo istilahi kama vile “Literature in Englisha,” ikiwa na maana kwamba Fasihi katika Kiingereza. Hii ikimaanisha kwamba fasihi husika haimaanishi kuwa ni ya Kiingereza bali ni fasihi nyingine yoyote inayopatikana katika lugha ya Kiingereza. Hoja za kundi hili zina faida na
hasara zake katika ustawi wa Fasihi ya Kiswahili na lugha ya Kiswahili kwa ujumla. Faida kuu katika hoja hii ni pamoja na kuhamasisha watu wajivunie Uafrika wao pamoja na utamaduni wao. Kwa kufanya hivyo, hadhi ya Kiswahili miongoni mwa Waafrika itazidi kuongezeka, na watu watafurahia Uafrika wao, pamoja na utamaduni wao, ikiwa ni pamoja na lugha ya Kiswahili na fasihi yake. Hasara kubwa kwa mwelekeo huu, ni pamoja na kupitia upya kazi mbalimbali ambazo kwa muda mrefu zimetambulika kuwa ni kazi za fasihi ya Kiswahili, lakini kumbe kiasili zimetoka katika makabila mbalimbali au nyingine zimetoka katika mataifa mengine na kuingia katika fasihi ya Kiswahili, kwa njia ya tafsiri. Kabla ya kutoa maoni ya nini
kifanyike, ni muhimu kutalii hoja za wataalamu wanaoona hakuna haja ya kuachana na lugha za kigeni. Wataalamu hawa wanasisitiza kuwa wanaweza kuanndika katika lugha za kigeni kama vile Kiingereza, Kifaransa na Kireno na bado kazi husika zikabaki kuwa za Fasihi ya Kiafrika. Wametoa hoja nyingi za sababu ya ugumu wa kuachana na lugha hizi za kigeni. Sababu hizi ni pamoja na suala la mazoea (hii ndio lugha waliyoizoea kuitumia katika uandishi). Pia suala la gharama nalo linatajwa katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa kuachana na lugha hizo za kigeni. Jambo linguine ni idadi kubwa ya wasomaji katika jamii zao wenye umilisi katika lugha hizo ambao wataathirika pale lugha husika zitakapoachwa. Jambo la msingi linalosisitizwa
na watu hawa ni katika kuzingatia utamaduni wa Kiafrika katika kazi hizo za fasihi. Hii inamaana kwamba kazi hizi ni lazima zijibainishe na Uafrika. Hoja hii ina mashiko hata kwa maendeleo ya fasihi ya Kiswahili na Kiswahili kwa ujumla. Faida ya hoja hii ni kutokana na kutambua zaidi suala la utamaduni na ujumi wa watu wa jamii husika kujitokeza katika kazi husika ya fasihi. Kwa mantiki hiyo, hata fasihi ya Kiswahili kwa namna ilivyosasa inazingatia hoja za mtazamo huu. Fasihi ya Kiswahili imenufaika kwa muda mrefu kutoka katika fasihi simulizi ya jamii mbalimbali za Kibantu Afrika Mashariki na nje ya Afrika Mashariki. Pia imenufaika kutoka katika fasihi simulizi za jamii nyingine mbalimbali za Kiafrika na hata nyingine ambazo si za Kiafrika. Fasihi ya Kiswahili pia imenufaika kutoka katika fasihi andishi za mataifa mengine kwa njia ya tafsiri ya kazi mbalimbali za fasihi zilizo katika lugha nyingine. Faida nyingine ya mtazamo huu ni
pamoja na kuendelea kutoa fursa ya fasihi ya Kiswahili kuendelea kutafsiriwa katika lugha za mataifa mbalimbali. Pamoja na hivyo, kwa upande mwingine, fasihi ya Kiswahili nayo inaendelea kunufaika kutoka katika fasihi za jamii mbalimbali. Pamoja na faida hizi, ni muhimu kuhakikisha kuwa kazi iliyotafsiriwa au nyingine yoyote ambayo imeandikwa kwa Kiswahili ni lazima izingatie masuala ya kijamii na kiutamaduni ya jamii pana ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili. Wallace, K.M (2017) Misingi ya Ufundishaji na Ujifunzaji wa Fasihi Karne ya 21. Heko Publishers Ltd. Dar es
Salaam. |