UFUNDISHAJI WA LUGHA YA PILI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Chuo (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=3) +---- Forum: Stashahada/Cheti (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=21) +----- Forum: Nukuu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=25) +----- Thread: UFUNDISHAJI WA LUGHA YA PILI (/showthread.php?tid=1173) |
UFUNDISHAJI WA LUGHA YA PILI - MwlMaeda - 09-06-2021 Utangulizi Kuna mikabala/ mikondo mbalimbali katika historia ya ufundishaji wa lugha ya pili ambayo imewahi kutumiwa. Baadhi ya mikabala hiyo, mpaka sasa imeendelea kuathiri ufundishaji wa lugha ya pili. Ujuzi wa mikabala hiyo ni jambo muhimu kwa mwalimu wa Kiswahili kwa sababu unaweza kumsaidia kupata fununu kuhusu asili ya mbinu tofauti tofauti zinazotumiwa kufundisha lugha ya pili. Hapo awali mbinu hizi zililenga hasa ufundishaji wa lugha ya Kingereza kama lugha ya pili. Hata hivyo, baadhi ya mambo ambayo hupendekezwa katika mbinu hizo yanaweza kumsaidia mwalimu ambaye anajishughulisha na ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya pili.
Madhumuni Ya Somo
Kufikia mwisho wa somo hili utaweza kutoa mifano ya mbinu za kufundishia lugha na kueleza jinsi kila mojawapo ya mbinu hizo inaweza kutumiwa katika ufundishaji wa Kiswahili.
Mbinu Ya Kimapokeo
Hii ni mbinu ambayo hapo awali ilitumika kama njia ya kufundishia lugha za kijadi kama vile Kiyonani na Kilatini. Ilitawala ufundishaji wa lugha za kizungu na kigeni kati ya miaka 1840 na 1940. Lengo kuu la mbinu hii ni kufanikisha ufahamu wa sarufi pamoja na uwezo wa kuandikia kwa usahihi katika lugha inayolengwa. Pia inalenga kuwezesha mwanafunzi kuwa na upeo mpana wa msamiati unaotumika sana katika lugha ya uandishi katika lugha husika, ili hatimaye aweze kuthamini umuhimu pamoja na thamani ya nakala zinazohusika.
Katika mazingira ya darasani, mwalimu anatazamiwa kutekeleza malengo haya kwa kushirikisha wanafunzi katika kazi ya kutafsiri mara kwa mara kutoka lugha zao hadi katika lugha inayofunzwa. Kabla ya kutafsiri, wanafunzi wanapaswa kwanza kijifunza maneno ya lugha inayolengwa ili waweze kutafsiri katika lugha mpya. Pamoja na hayo, wanafunzi wanapewa maelezo marefu kuhusu sheria za kisarufi. Kisha wanapewa zoezi la kutunga sentensi ili kubainisha ufahamu wao wa sheria hizo. Uwezo wa mwanafunzi katika kutafsiri huwa ndicho kigezo muhimu kinachotumiwa kama chombo cha kupima ustadi wake katika kipengele cha sarufi na msamiati.
Udhaifu hasa wa mbinu hii ni kwamba haitilii mkazo juu ya matamshi sahihi pamoja na stadi za kimawasiliano. Inasisitiza sana ujuzi wa sheria za kisarufi bila kupatia wanafunzi nafasi ya kutosha kujieleza kutokana na nafsi zao. Matokeo ya kujishughulisha sana na ufundishaji wa kanuni na vighairi ni kwamba waalimu huishia kwa kufundisha wanafunzi lugha ya ulimwengu wa vitabu, lugha isiyokuwa na uhai, na ambayo mara nyingi haina manufaa katika ufanikishaji wa mawasiliano ya kawaida.
Utumiaji wa mbinu hii unalifanya somo la lugha kukosa ubunifu unaotakikana. Wanafunzi hawapati nafasi ya kutumia lugha kama chombo wanachoweza kukitegemea kutekeleza mahitaji yao ya kimawasiliano. Shughuli ya kujifunza lugha inageuka kuwa zoezi la kukariri maneno chungu nzima na kanuni kemkem za kisarufi. Hakuna hakikisho kwamba baada ya kukariri maneno na kanuni wanafunzi watakuwa na uwezo wa kutumia kanuni na maneno vilivyokaririwa katika mawasiliano ya nje ya darasa. Shughuli ya kufundisha na kujifunza lugha inakuwa kama zoezi la kuchemsha bongo tu.
Mbinu Ya Moja Kwa Moja
Hali ya kutoridhika na mbinu ya kimapokeo ni miongoni mwa mambo ambayo yalichangia kuibuka kwa mbinu ya moja kwa moja. Iliibuka katika karne ya 19 kuchukua mahali pa mbinu ya kimapokeo. Wanaopendelea mbinu hii hushikilia kwamba njia mwafaka ya kujifunza lugha ya pili ni kukabiliana nayo moja kwa moja na kuitumia kama vile mtoto mdogo anavyofanya anapojifunza lugha ya mama. Kulingana na mbinu hii ni marufuku kutumia lugha ya wanafunzi au lugha nyingine yo yote ile.
Mbinu hii husisitiza umilisi wa lugha bila tafsiri wala maelezo rasmi juu ya sheria za kisarufi. Wanafunzi wanatakiwa kijifunza lugha kwa kushirikishwa kikamilifu kama wahusika watendaji katika matumizi tofauti tofauti ya lugha. Inasisitizwa kwamba ikiwa maana inaweza kuwasilishwa moja kwa moja kwa kushirikisha maono au vitendo hakuna haja ya kutafsiri.
Kwa upande wa sarufi, mbinu hii inashikilia kwamba njia bora ya kuendeleza ufahamu wake ni kutokana na uzoefu wa kutumia mara kwa mara lugha inayohusika. Mwanafunzi akipewa fursa ya kutosha kukumbana na matumizi ya lugha, itakuwa rahisi kwake kutambua na kujifunza sheria zinazotawala sarufi ya lugha hiyo. Mbinu hii inasisitiza haja ya kutoa nafasi kwa mwanafunzi ya kujifunza lugha kama vile mtoto anavyojifunza lugha yake ya kwanza. Mtoto anajifunza na kuimudu lugha kwa kukumbana nayo moja kwa moja katika mkutadha maalum wa mawasiliano.
Hakuna mtu anayemfafanulia kanuni za kisarufi za lugha yake. Hata hivyo anazing’amua kanuni hizo yeye mwenyewe baada ya kushuhudia matumizi yake katika vielelezo vya sentensi. Huwa anajifunza lugha ya jamii yake katika mazingira yanayoshirikisha vitendo na maono. Ushirikishaji wa maono na vitendo unachangia kujenga hali ambayo husaidia mtoto kukisia maana ya kile kinachosemwa. Anajifunza lugha ya jamii yake kwa kusikiliza kwanza na baadaye kuigiza yale anayosikiza.
Kwa mujibu wa mbinu hii mwalimu anapofundisha lugha ya pili anashauriwa kutotegemea tafsiri. Anashauriwa vile vile kutofundisha moja kwa moja sheria za kisarufi. Ana wajibu wa kuambatanisha ufundishaji wake na vitendo, uigizaji na mazungumzo. Lakini ikiwa mwalimu hana budi kufundisha sarufi, inafaa ufundishaji wa sarufi uzingatie kiwango cha matumizi ya lugha huko mkazo ukitiliwa juu ya madondoo ya kisarufi yanayotumika sana sana hasa katika mazungumzo.
Kwa mujibu wa mbinu hii, dhima ya mwalimu ni kupanga na kufanikisha utumizi wa lugha badala ya kujishughulisha na ufafanuzi pamoja na uchambuzi wa kanuni za kisarufi. Ili mwalimu aweze kufaulu kutumia mbinu hii anapaswa kuwa na ujuzi wa kiwango cha hali ya juu katika lugha anayofundisha. Ni lazima pia awe na ubunifu wa kumwezesha kuwasilisha maana bila kutumia lugha nyingine yo yote zaidi ya ile ambayo anafundisha. Anatarajiwa pia kujitahidi kujenga mazingira ya kufundishia ambayo yanakaribia kufanana yale ya lugha ya kwanza. Mazingira hayo yanatarajiwa kufanikisha ufahamu wa lugha kupitia mazoezi ya kusikiliza pamoja na mazungumzo. Lazima yawe mazingira ambayo yanaweza kuchangia katika kuhamasisha mwanafunzi kutaka kujifunza lugha inayohusika.
Kwa kawaida mtoto anapojifunza lugha yake ya kwanza anakuwa na hamu ya kujifunza lugha hiyo ili aweze kutangamana na jamii ya watu wanaomzunguka. Jamii hiyo pia humsaidia kuendelea kwa kumtia shime. Pamoja na hayo mtoto huwa na muda mwingi wa kusikia na kutumia lugha hiyo. Lugha inakuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.
Mbinu Ya Uzungumzi
Mbinu hii ilizuka na kukita mizizi katika miaka ya 1950 kutokana na mwamko mpya nchini Amerika wa kujishughulisha na ufunzaji wa lugha za kigeni. Tukio muhimu ambalo lilichangia pakubwa kuamsha ari ya Wamerika katika lugha za kigeni ilitokea mnamo mwaka wa 1957. Mwaka huo Warusi walifaulu kupeleka chombo chao (sputnik) angani. Jambo hili lilikuwa changamoto kubwa kwa taifa la Amerika. Kufuatia tukio hilo, serikali ya Amerika iliamua kujishughulisha kikamilifu katika ufundishaji wa lugha za kigeni ili isiachwe nyuma katika maendeleo ya kisayansi. Jambo ambalo linapewa kipaumbele katika mbinu hii ni ufasaha wa kuzungumza.
Ufasaha unaotarajiwa unahusu matamshi bora, sarufi, pamoja na uwezo wa kuitikia upesi na kwa urahisi katika hali tofauti zinazohusisha utumizi wa lugha katika mazungumzo.
Ufahamu sikizi, matamshi, sarufi na msamiati vinapofundishwa huwa kama njia mojawapo ya kufanikisha ufasaha wa kuzungumza. Vilevile wanafunzi wanaposhirikishwa katika kuandika na kusoma mambo haya yanaambatanishwa na ustadi wa kutumia lugha ya mazungumzo. Kulingana na mbinu hii, stadi za lugha zinastahili kufundishwa kwa kuzingatia mfuatano huu: Kusikiliza, Kuongea, Kusoma na Kuandika.
Katika hatua za mwanzo mwanzo, kusoma na kuandika vinachukuliwa tu kama mambo ambayo yanaweza kuchangia kuimarisha ustadi wa kusikiliza na kuongea.
Vinatiliwa mkazo zaidi katika viwango vya juu wakati ambapo wanafunzi wana uzoefu unaofaa ili kuweza kukabiliana na mitindo zaidi ya lugha ya kimaandishi. Madondoo ya lugha yanapofundishwa kwa kutumia mbinu hii huwa yanawasilishwa kupitia mjadala ambao ni chombo muhimu cha kutoa mkutadha wa kufundishia kile kinacholengwa. Zaidi ya kushiriki katika mjadala, wanafunzi huwa wanatakiwa, mara kwa mara, kukariri vielelezo vya sentensi.
Mbinu Ya Mawasiliano
Msingi wa mbinu hii ni imani kwamba kazi kuu ya lugha ni kufanikisha maingiliano pamoja na mawasiliano katika jamii. Lugha ni chombo ambacho kinamwezesha binadamu kushirikiana na watu wengine na pia kutekeleza mahitaji ya maisha yake. Kwa hivyo, kulingana na waasisi wa mbinu hii, lengo kuu la kufundisha lugha ni kuwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuwasiliana akitumia lugha inayohusika.
Njia moja ya kuhakikisha kuwa mwanafunzi anakuwa na uwezo wa kuwasiliana ni, kwanza, kumpa fursa ya kushiriki kama mhusika mpokezi. Mwanafunzi anapata fursa ya kupanua upeo wake wa lugha kupitia kusikiliza na kusoma. Baada ya kushiriki katika matumizi ya lugha akiwa mhusika mpokezi mwanafunzi anashirikishwa kama mhusika mwanzilishi wa mawasiliano. Kulingana na waasisi wa mbinu ya mawasiliano, lugha ambayo ni ya maana / manufaa kwa wanafunzi inatilia nguvu juhudi za kujifunza. Kwa hivyo ni muhimu kwa walimu kuhakikisha kwamba wanapochagua kazi ya wanafunzi wanatilia maanani uwezo wa kazi hiyo wa kuwashirikisha katika matumizi ya lugha yenye maana na uhalisi.
Kwa kawaida, mawasiliano hufanyika katika mazingira ya watu wakiwa katika vikundi. Pia, aghalabu, mawasiliano huchukua mkondo wa mazungumzo (conversation) na majidiliano (discussion). Wakizingatia ukweli huu, wanaounga mkono mbinu ya kimawasiliano wanapendekeza kugawanya wanafunzi katika vikundi vidogo vidogo. Hii ni njia bora ya kuendeleza uwezo wa wanafunzi wa kuwasiliana kwa kutumia lugha inayofundishwa. Wakiwa katika vikundi vya watu wachache, wanafunzi wanakuwa na fursa bora ya kutumia lugha halisi. Pia wanapata nafasi ya kujieleza kwa ufasaha bila wasiwasi. Ustadi katika kusoma na kuandika unaweza kukuzwa kutokana na msingi imara wa kutumia lugha kwa uhalisi.
Je jukumu hasa la mwalimu ni nini? Kwa mujibu wa waasisi wa mbinu hii, jukumu la mwalimu ni kuhamasisha wanafunzi na kutoa kwao nafasi ya kujieleza katika lugha inayohusika. Ana wajibu wa kuhamasisha wanafunzi kutumia lugha kwa njia mbalimbali. Anapaswa pia kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata fursa ya kujieleza.
Pamoja na hayo, mwalimu ana wajibu kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaelewa vizuri kwa nini wanafundishwa kile wanachofundishwa. Hivi ndivyo watakavyoweza kushiriki kwa njia ya maana na manufaa kwao. Vilevile ni lazima mwalimu ahakikishe kuwa wanafunzi wake wanahusika zaidi kuliko vile anavyohusika mwenyewe.
Aidha, mwalimu anashauriwa kushirikisha wanafunzi katika vitendo ambavyo vinaweza kuwalazimisha kuwasiliana kwa kutumia lugha inayofaa kulingana na mkutadha. Kwa maneno mengine, mwalimu anapaswa kubuni hali na mazingira ambamowanafunzi hawawezi kukidhi mahitaji na matarajio yao bila kuwasiliana. Wakijikuta katika mazingira ya namna hii hawatakuwa na budi kutafuta ufumbuzi kwa kutumia lugha. Kwa ufupi, mwalimu anaweza kusaidia kuendeleza uwezo wa wanafunzi wa kuwasiliana wakitumia lugha kwa kuzingatia mfuatano wa hatua zifuatazo:
Katika hatua ya mapokezi wanafunzi wanashiriki kama wahusika wapokezi. Kazi yao katika hatua hii ni kupokea ujumbe unaowasilishwa na watu wengine na kupata maana ya ujunbe unaowasilishwa. Wanaweza kutekeleza jambo hili kupitia zoezi la kusikiliza au kusoma. Zoezi la kusikiliza husaidia wanafunzi kupata nafasi ya kupanua upeo wa lugha. Kupitia zoezi hili wanaweza kujifunza msamiati mpya na miundo mbalimbali ya kisarufi. Vilevile wanafunzi wanaimarisha ujuzi wao wa yale ambayo wamejifunza tayari.
Kwa upande mwingine, katika hatua ya ufafanuzi (maelezo) mwalimu anaweza kudondoa madondoo fulani ya lugha ambayo wanafunzi wamewahi kukumbana nayo, katika zoezi la kusikia na kusoma. Kisha anatoa maelezo kuhusu madondoo hayo ili wanafunzi wayatilie maanani zaidi kuliko mengine kwa wakati huo. Baada ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafahamu kiini cha somo mwalimu anawapa wanafunzi nafasi ya kujaribu kutumia madondoo hayo katika vielelezo vya sentensi wakizingatia maagizo yaliyotolewa.
Katika hatua ya mawasiliano huru wanafunzi wanapata fursa zaidi ya kujieleza bila kufuata maagizo ya mwalimu. Wanaweza kujieleza kwa njia halisi kulingana na mahitaji ya mawasiliano katika mkutadha unaohusika. Wanafunzi watateua lugha kulingana na hali halisi inayowakabili wakati huo. Mawasiliano huru huwapa wanafunzi fursa ya kutambua kuwa lugha siyo somo ambalo linajikita katika mipaka ya mazingira ya darasani tu, lakini pia ni chombo cha mawasiliano nje ya mipaka ya darasa.
Mawasiliano huria huwapa wanafunzi nafasi ya kutumia lugha kwa njia ya ubunifu katika miktadha tofauti tofauti ya kijamii. Wanatumia lugha bila usimamizi wa mwalimu, lakini kulingana na hali halisi katika mazingira ya mawasiliano. Huwa wajitegemea wao wenyewe. Kadiri wanavyoshiriki katika mikutadha tofauti ya mawasiliano na kushuhudia jinsi lugha inavyotumiwa, ndivyo wanavyoendelea kukuza na kuimarisha uwezo wao wa kimawasiliano (communicative competence). Uwezo huu ni muhimu kwa mwanafunzi kwa sababu akiwa nao anaweza kufasiri lugha kwa njia iliyo sahihi akizingatia mkutadha unaohusika. Na akifanya hivyo anaweza kuitikia kama inavyotarajiwa. Kwa mfano mwalimu akiingia darasani ambamo mna joto jingi na agundue kuwa madirisha yamefungwa, anaweza akasema: Mbona joto limezidi sana humu ndani. Mwanafunzi mwenye uwezo wa kimawasiliano atatambua kuwa mwalimu angetaka madirisha yafunguliwe, na ataitikia kwa kuyafungua. Yule asiyekuwa na uwezo huo atachukulia usemi wa mwalimu kama kauli ya kawaida tu.
Msingi wa Mbinu ya Kimawasiliano
Asili ya mbinu ya kimawasiliano ni imani inayoshikilia kwamba:
(a) Lugha ni mfumo wa kueleza maana.
(b) Jukumu kuu la lugha ni kufanikisha maingiliano na mawasiliano baina ya watu.
© Shughuli ambazo zinachangia kufanikisha ufahamu wa lugha ni zile ambazo zinatoa kwa wanafunzi nafasi ya kushiriki katika mawasiliano halisi (real communication).
(d) Vitendo vinavyohusisha matumizi ya lugha ili kutekeleza shughuli za maana (meaningful tasks) husaidia kufanikisha ujuzi wa lugha.
(e) Lugha yenye maana kwa wanafunzi inaimarisha hali ya kujifunza.
(f) Mawasiliano hufanyika ikiwa wale wanaohusika wana hamu (motisha) ya
kuwasiliana.
|