MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
NADHARIA YA UPOKEZI (MWITIKO WA MSOMAJI)

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
NADHARIA YA UPOKEZI (MWITIKO WA MSOMAJI)
#1
MAANA YA NADHARIA
(Williady, 2013), Nadharia ni maelezo yakinifu kuhusu kitu, tajiriba, mahalifa au upumbavu na mafanikio au maangamizi yanayochomoza katika jamii. Hivyo nadharia hufungamana na mambo mbalimbali ya jamii kama vile mbinu, maarifa, tasinifu, mikabala na mienendo mbalimbali ya jamii.
1. NADHARIA YA UPOKEZI (MWITIKO WA MSOMAJI)
Nadharia ya Upokezi (mwitiko wa msomaji) ambayo husisitiza nguvu ya msomaji. Nadharia ya Upokezi (Reception Theory) iliasisiwa na wahakiki wa waasisi wa Kijerumani mwishoni  mwa miaka ya 1960.Miongoni mwa waasisi wa nadharia hii ni Robert C. Holub,Hans Robert  Jauss na Wolfagang Isser.Katika kitabu chake Reception Theory (1984), Holub anaelezea nadharia ya Upokezi  kuwa ni Mabadiko ya jumla ya umakinikiaji kutoka kwa mwandishi na kazi yake kwenda kwa matini na msomaji”
Nadharia ya upokezi inaakisi mabadiliko ya mbinu katika historia ya fasihi na ilizingatiwa kama jibu kwa jamii,wanazuoni na maendeleo ya fasihi huko Uerumani Magharibi  mwishoni mwa miaka ya 1960.Kwa mujibu wa Holub, nadharia ya Upokezi ulikuwa ni njia ya Kimapnduzi kwa wahakiki wa kisasa.
Waitifaki wa nadharia hii wanashiilia msimamo kuwa kazi ya fasihi hupata maana baada ya matini na msomaji kuadhiriana.Msomaji au mpokeaji ndiye huipa maana kazi ya fasih.
Kwani huiona na kuilinganisha na uzoefu wake wa maisha. Kielelezo hiki kipya cha uhakiki hutilia maanani dhima ya msomaji.Hans Robert Jauss katika makala yake “The change in the Paradigm of Literary Scholarship” (1926) ambaye anachukuliwa kama mmoja wa mihimili ya nadharia hii ya Upokezi anaelezea umuhimu wa kuielezea kazi ya Fasihi.Isser anaiona kazi ya Fasihi kama kitu au tukio lililo nje ya muktadha na historia.
Anasema kuwa ili kazi ya fasihi ieleweke ni lazima ushiriki  wa msomaji uoane au upatane na maana inayojitokeza katika kazi ya Fasihi.
Kwa hiyo basi , nadharia ya Upokezi hufasili Fasihi kama mchakato wa namna msomaji na wanavyoathiriana.Uzoefu wa maisha wa msomaji unaweza kutoa tafsiri tofauti kwa kazi ya fasihi kutoka msomaji mmoja na mwingine.
2.NADHARIA YA  ONTOLOJIA YA KIBANTU.
Nadharia ya Ontolojia ya Kibantu. Kuna wataalamu mbalimbali waliozungumzia nadharia hii. Kwa jumla, wataalamu hawa wameeleza maana ya Ontolojia kuwa ni mtazamo unaohusu kuwepo kwa kitu katika dunia na kuangalia vitu katika uhasilia wake (Nicholaus 2011).
Ontolojia inaweza kutazamwa kwa namna tatu: kama taaluma, kama falsafa na kama nadharia. Hivyo kwa kuwa utafiti huu ulichunguza “Mabadiliko ya kiuandishi kutoka kanuni za Ki-Aristotle kwenda kanuni za jadi ya Ki-Afrika”, kipengele cha Ontolojia ya Kibantu kinachoweza kutumika katika kazi za fasihi, tuliona ni vyema kutumia Ontolojia kama nadharia katika utafiti huu, kwani imewezesha utafiti huu kufikia malengo yake, pia ilihusiana na mada iliyoshugulikiwa.
Kimsingi kuna mitazamo minne kuhusu Ontolojia ya Kibantu. Mitazamo hiyo ni, ule wa falsafa ya kisiasa (Itikadi ya kisiasa), mtazamo au falsafa ya Kihikimati (Sagacty), wanafalsafa waliojikita katika kurekodi imani katika utamaduni wa mwafrika (Ethnofilosofia), na falsafa ya Kiuweledi.
Wanaitikadi wa kisiasa walichunguza masuala ya undugu wa kifamilia, ujamaa na kujitegemea ndani ya Afrika. Wanasiasa hao ni Julius Nyerere, Leopold Senghor na Kwame Nkurumah. Lengo lao lilikuwa ni kutaka kutafuta uhuru wa kweli kwa waafrika ili kurudisha heshima kwa mwafrika kama ingewezekana.
Mtazamo wa Kihikimati umejikita katika masuala ya uhuru, hekima na desturi za watu. Waanzilishi wa mtazamo huu wameshawishika kwamba falsafa ya kiafrika haiangalii vitu vyote vinavyohusu kazi. Lengo lao walitaka kuonesha kwamba ujinga sio hali ya kifalsafa na ujinga upo kwa kila jamii, ujinga wa mwenzako waweza kuwa uhuru kwake. Waanzilishi wa falsafa hii ni Odera H. Oruka na Marcel Griaule’s.Marcel Griaule’s alifanya mazungumzo na Oyotemmeli kiongozi wa kabila la Wadogoni na matokeo yake walipata falsafa ya kidini ya wadogoni.
Ethnofilosofia hujishughulisha na ukusanyaji wa mitazamo ya kiulimwengu kutoka katika tamaduni mbalimbali za waafrika. Hii imejikita katika masuala ya imani, masimulizi na misemo ya watu. Muunganiko huo umeunganishwa na Paulin Hountondji.  Wengine waliojihusisha na falsafa ya kiafrika katika mtazamo huu ni Placid Tempels, Leopald Senghor, John Mbiti na Alex Kagame. Hivyo, mtazamo huu umejikita zaidi katika masuala ya mila, desturi na imani za jamii.
Falsafa ya Kiuweledi imejikita katika uchambuzi na ufafanuzi wa ukweli. Zaidi inajihusisha na uhakiki, na hoja ndizo sifa za msingi kwao. Waanzilishi wa falsafa hii ni Paulina Hountondji, Kwasi Waredu, Odera Oruka na Peter Bodunrin. Wanasema kuwa falsafa ya kibantu kwa sasa inaitwa Metafilosofia, na imejikita katika kuangalia maudhui ya msingi. Wao wanahoji kwamba falsafa ya Afrika ni ipi?
Roberto (1996) anasema Ontolojiani nadharia inayohusu kuwapo, yaani ni nadharia inayoangalia yaliyokuwepo na yale ambayo hayakuwepo, halisi na yasiyo halisi, tegemezi na vinavyojitegemea.
Parrinder (1969) anasema kuwa nadharia ya kibantu inahusisha mwafrika na imani yake. Hujumuisha maisha, mazingira pamoja na fikra zake. Pia anasema kuwa mawazo ya mwafrika hujengwa katika misingi ya nguvu mbalimbali ambazoni Mungu, binadamu, wanyama, mimea na kadhalika.
Wataalamu wengine waliozungumzia nadharia ya Ontolojioa ni: Husserl (1913), Tugendhat (1928), Wolff (1928), Gruber’s (1993), Bolzano (1996), Guariono (1998), Wamitila (2008) na Cocchiarella (2007).
Kwa jumla, wataalamu hawa wameeleza mengi juu ya nadharia hii, jambo lililosisitizwa sanana wataalamu wengi waliojadili nadharia hii ni kuhusu uchaguzi wa Ontolojia nzuri na namna ya kutumia nadharia hii. Wanasema Ontolojia nzuri ni ile inayohusisha njia za Kisayansi na kutupatia njia chache na rahisi ambazo zitaelezea mambo mbalimbali katika ulimwengu. Pia nadharia hii inatukuza sana Ubantu na kumuona mwafrika kama kiumbe bora mwenye uwezo wa kubuni na kusimamia mambo yake kwa usahihi. Mbali na kutumia Ubantu (U-Afrika), nadharia hii inaeleza mambo kadhaa ambayo ni sehemu ya ufahari kwa waafrika, mambo hayo ni pamoja na dhana ya familia pana, kuamini uzazi kuwa ndio njia ya uzima wa milele, yenye kuhashiria umuhimu wa binadamu, na Ugumba ni laana na utupu kwa binadamu, kuabudu katika Mungu na miungu na kuheshimu Wahenga. Pia huhusisha na imani kuhusu uchawi, na sihiri, na ndani yake kuna masuala ya uganga. Pia umri kwa waafrika una nafasi kubwa sana katika jamii na unabeba hekima za mtu.
3.UJUMI (AESTHETICS)

Ujumi ni nini?
Ujumi ni tawi la falsafa linaloshughulika na uzuri, ubaya, ladha, n.k.
 AU
Ujumi ni elimu ya sheria na kanuni za sanaa.
Neno ujumi kwa kiingereza linajulikana kama “Aesthetics”. Neno hili limetoholewa kutoka katika lugha ya kigiriki “Ais  –  thesis”, likiwa na maana ya “Hisia” (Feelings), hasa hisia za akilini (Mental perception).
Alexander Gottlieb Baumgarten (mjerumani) ni miongoni mwa wanafalsafa yalioshungulikia kwa kina juu ya falsafa hii ya Ujumi. Baumgarten alidokoa baadhi ya mawazo fasaha kutoka kwa Leibniz. Leibniz alizungumzia mambo makubwa mawili amabayo ni LOGOS na ETHOS.

 
LOGOS, ni mantiki itokanayo na neno la maharifa au sababu ipelekeayo uwelewa mpya au kuyachekecha mawazo makuukuu na kupata neno lenye kuchukua mkondo mpya.
 
ETHOS, ni desturi ama mguso, tabia ama kaida Fulani ndani ya jamii ambazo hufanya matakwa yahusuyo jamii Fulani tu.
 
Baumgarten, alikiendeleza kipengele cha mguso na hisia na neno “Aesthetics” likaanzishwa.
 
Kabla falsafa mpya ya Aesthetics haijachukua kasi yake, hapo awali masuala ya hisia yaliwekwa chini ya nadharia ya hisia za akili (mental perception). Dhana ya ujumi ilitoka kwenye nadharia ya hisia za akili katika karne ya 18 na kuitwa “Falsafa ya uzuri” au “Falsafa ya sanaa” au yote mawili kwa pamoja.  Baadaye ujumi uliachana na falsafa na kuwa tawi linalojitegemea la elimu.
 

Kabla ya Baumgarten, ushairi na sanaa kwa ujumla ilijadiliwa kitaalamu katika kapumoja. Hii inamaana kwamba ushairi haukutofautishwa na muziki au uchoraji ama ususi, vyote vilielezwa kwa pamoja.
Baumgarten akaigawa dhana hii katika maeneo mawili ambayo ni uzuri na sanaa.

1.       UZURI (The good or the truth).

Uzuri ni ukamilifu wa hisia za akili unaoleta kulitazama jambo au mambo Fulani katika mtazamo chanya, haijalishi, kwani mwingine anaweza kulichukulia jambo hilo kimtazamo hasi lakini mtazamo wake hauondoi uzuri wa chanya kwa atazamaye chanya.

2.       SANAA

Sanaa ni ufundi wa kuunda jambo. Twaweza kuueleza uzuri kupitia sanaa. Sanaa yaweza kuupambanua uzuri kwa viwango vya juu zaidi kuliko jambo lolote lile.

4. NADHARIA YA UFEMINISTI ( Mtazamo wa kike)
(Williady, 2015) Nadharia hii inahistoria ndefu duniani, ikimaanisha ni moja ya nadharia zilizopata kutokea miongo mingi iliyopita. chanzo cha kuibuka kwa nadharia hii ni vuguvugu la kutaka kufuta kabisa uonevu wa mwanaume kwa mwanamk. nadharia hii inadai kuwa chimbuko lauonevu na ukandamizaji unaofanywa na wanaume kwa wanawake ni uroho wa mwanaume katika kumtawala mwanamke. Kwaufupi, ajaenda kuu ya ufeministi na mafeministi ni kumaliza kabisa utawala wa mwanaume kwa mwanamke.
moja ya wadau waliochangia sana kuendelea kwa nadharia hii kwa kasi ni Adrew Dworkin. Mwaka 1976, akiwa katika mji mkuu wa Uingereza, London, alitoa mapendekezo makali katika kukomesha utawala wa mwanaume kwa mwanamke, Dworkin anasema: Ili kufanikisha, tunahitaji kubomoa kabisa muundo wa mihimili ya utamaduni wa jamii kama vile sanaa, kanisa, sheria, kaya zinazodhibitiwa na baba, jamii na taswira zote za asasi, mila, desturi ambazo zinamwona mwanamke kuwa mtu ovyo.
WATAALAMU MBALIMBALI WALIVYOZUNGUMZIA MAANA YA UFEMINISTI
Nadharia ya Ufeministi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama vile:
Wamitila (2003:253), hii ni nadharia ambayo imewekewa msingi na msukumo mkubwa pamoja na nia ya kupigania ukombozi wa mwanamke kutokana na pingu za kiutamaduni, kidini, kijamii, kisiasa na kiuchumi. Hii ni nadharia ambayo inasaili na kudadisi itikadi ya kiume ambayo imekuwepo katika jamii kwa kipindi kirefu. Kudadisi pia fasiri za kiume za fasihi pamoja na mikabala ya kiubabedume.
Ntarangwi (2004:45), ni nadharia ambayo inajaribu kukiuka mitazamo ya kiume ambayo yaelekea inatumiwa sana katika jamii.
Mukobwa M. nadharia ya ufeministi imetokana na mkondo na harakati za kutetea haki za wanawake ulimwenguni na imejikita katika imani ya usawa wa kijinsia, kijamii, kisiasa na kiuchumi.
(Williady, 2015) Ninadharia iliyojaribu kuvunja mwiko wa mfumo dume hapa dunia kwa kuanzisha mapambano ya usawa wa kijinsia, bilashaka majaribio haya bado hayajafanikiwa.
Kwa jumla, nadharia ya ufeministi ni nadharia iliyojikita katika kupinga ukandamizaji wa mwanamke katika jamii hususan katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni.
KUIBUKA KWA UFEMINISTI NA HARAKATI ZA KUIENDELEZA NADHARIA HII
Uhakiki wa kifeministi ulishika kasi miaka ya 1960 na kuendelea kukua na kuishia kuwa muhimu katika miaka ya hivi karibuni. Zipo kazi kadhaa zilizoandikwa kabla na kulimulika suala hili kwa namna moja ama nyingine. Kazi kuu mbili zinazorejelewa hapa ni A Room of One’s Own ya Virginia Woolf na A virdiction of the Right of women ya Mery Wollsto Necraft.
Hata hivyo, kazi iliyoishia kuwa na mchango mkubwa katika kuuweka msingi wa uhakiki wa ufeministi ni kazi maarufu ya mwandishi wa Kifaransa, Simone de Beauvoir iitwayo, The Second sex, 1952 katika kitabu hiki, mwandishi huyu anachukuwa mkabala wa kiharakati kwa kushambulia na kukosoa baadhi ya asasi zinazochangia katika kumdhalilisha au kumdunisha mwanamke. Asasi kuu anazozishambulia ni ndoa, dini na utamaduni.
Nadharia ya ufeministi ilichimbuka huko Marekani katika harakati za kukomesha biashara ya utumwa mwaka 1830. Wanawake wakaanzisha harakati za kupigania haki za mwanamke.
Wamitila (2006:160-161) na Ntarangwi (2004:52-56) wamebainisha malengo mbalimbali ya ufeministi.
Ni kweli kwamba kuna baadhi ya malengo ya ufeministi yanakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika lakini baadhi ya malengo hayo yanasawiri maisha halisi ya mwanamke wa kiafrika kama ifuatavyo:
Kubainisha umuhimu wa mwanamke, kutokana na mwanamke kukulia katika jamii zenye mfumodume. Umuhimu wake haukuonekana, ndiyo maana ikaanzishwa nadharia ya ufeministi ambayo yenyewe iligundua umuhimu wa mwanamke katika jamii. Umuhimu wake upo katika Nyanja zote za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Mfano, katika nyanja ya kisiasa mwanamke anaweza kuwa kiongozi bora na mwenye ushauri. Hili linajidhihirisha katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Bâ (1994). Mwandishi anathibitisha hili anaposema:
“Tunayo karibu miaka ishirini ya uhuru! Lini tutampata mwanamke wa kwanza awe waziri atakaye husishwa na maamuzi yatakayoongoza nchi yetu huko tuendako? Kumbe nguvu walizonazo wakina mama, uwezo wao wa kupambana, na kujihusisha kwao bila kutegemea kupata faida yoyote ni mambo ambayo hayahitaji tena kuthibitishwa. Wanawake wamewainua wanaume wengi kwenye ngazi za juu.” (uk.82)
Katika nyanja ya kijamii, mwanamke ni mlezi wa familia. Mfano, Ramatulayi anailea familia yake kwani ameweza kulipa bili ya maji, umeme bila hata kumtegemea mwanaume. Mfano, mwandishi anasema:
“Licha ya mzigo niliokuwa nao tangu zamani, nikaubeba na ule uliokuwa wa Modu. Ununuzi wa vyakula muhimu ulinishughulisha kila mwisho wa mwezi. Nilihakikisha kwamba sikuwa na upungufu wa nyanya au mafuta, viazi mviringo na vitunguu wakati ambapo vyakula hivi viliadimika sokoni… Nilikuwa mwangalifu kuzilipa bili za maji na umeme pindi zilipofika.” (uk.69)
Lengo hili la ufeministi linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwa kuwa mwanamke wa Kiafrika anaonekana hana umuhimu katika jamii, pia anaonekana kuwa dhaifu ambaye hawezi kuiendesha familia yake bila msaada wa mwanaume hii ni kutokana na jamii nyingi kuendeshwa na mfumodume.
Kuorodhesha kuwa kihistoria wanawake wamekuwa ni tegemezi na wasaidizi wa wanaume, ni kweli kihistoria wanawake wamekuwa wategemezi na wasaidizi wa wanaume. Mfano katika tamthiliya ya Nguzo Mama iliyoandikwa na Penina Muhando (2007) tunaona mhusika BI MOJA alivyokuwa akimtegemea mume wake na kutaka anunuliwe kanga. Mwandishi anasema:
“BI MOJA: (kwa Shaabani): Kama ulijua kufika sasa hivi nipe hela ya kanga bwana meli meli hii hainikosi leo utanipa hela hizo kanga nikakate. Mwezi wa tatu huu kanga sizijui.
Shaabani: Nimekuambia mimi hela sina. Sasa unataka nikaibe?”(uk.31-32)
 Ni kweli kwamba mwanamke wa kiafrika amekuwa tegemezi katika jamii, kwani humtegemea mwanaume katika mambo mbalimbali ya kifamilia. Kwa mfano kutafuta au kununua mahitaji ya nyumbani kama vile chakula, mavazi yake na watoto wake au kulea watoto wake.
Kuondoa ukandamizaji wa mwanamke kutokana na pingu za kiutamaduni, kijamii, kidini, kisiasa na kiuchumi. Jamii nyingi za Kiafrika zimejengeka katika mfumodume, hivyo basi jamii zinamkandamiza mwanamke kutokana na pingu hizo. Katika kulithibitisha hili waandishi wa kazi za fasihi nao hawakuwa nyuma kulizungumzia katika kazi zao na lengo ni kuondoa mfumodume uliojengeka muda mrefu katika jamii.
Kwa upande wa kiutamaduni mwanamke ameonekana kukandamizwa kwa kuonekana hana mamlaka hata ya kurithi mali za mumewe au zake mwenyewe, badala yake hata akifiwa na mumuwe anapigwa, anafukuzwa na kudhalilishwa. Penina Muhando anayathibitisha haya katika tamthiliya yake ya Nguzo Mama kwa kumtumia BI SABA pale anaposema:
            “Akalia Bi Saba tena akalia
            Hana wa kumsaidia
            Mumewe kafa nduguze wakaja juu
            Pesa wamechukua senti tano haikubaki
Vyombo na nguo zote wakagawana
            Roho ilimpasuka Bi Saba kuwaona hao ndugu
            Walivyogombania mali wasiyoichuma…
Sasa juu ya yote haya wamerudi kufagia
Hata ufagio wamebeba
            Na lawama kumtupia eti pesa kazificha.” (uk.39)
Pia mwanamke anaonekana anajishughulisha na kazi mbalimbali za kujiletea maendeleo yake binafsi lakini anarudishwa nyuma kwa kukandamizwa na mwanaume. Penina Muhando anayathibitisha haya kwa kumtumia BI PILI ambaye alikuwa anapika pombe ili kujikwamua katika hali ngumu ya maisha lakini mumewe SUDI alizichukua hela zote alizokuwa alizozipata. Kwa mfano, mwandishi anasema:
            “BI MSIMULIZI: Upishi wa pombe balaa ulimzushia
                                    Visa na mikasa Bi pili havikumuishia
                                    Pesa alizipata kutokana na hiyo pombe
                                    Lakini visa vya pombe hiyo pesa hazikufidia”
            SUDI:              (kwa Bi Pili) Nani kalewa? Umeninywesha wewe?
                                    Wee!hawara zako ndiyo wamekutia jeuri unaninyima pesa.
                                    Toa pesa sasa hivi (Anampiga) Bi Pili anakimbia huku akilia.”          (uk.16)
Vilevile, mwanamke alikuwa anakandamizwa kwa kulazimishwa kurithiwa na kaka au ndugu wa mume pindi anapofiwa na mumewe. Mwandishi analithibitisha hili katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii pale anaposema:           
            “Tamsiri, zitapike hizo ndoto zako za kutaka kuniposa.
            Umeshakaa nazo kwa siku arobaini. Kamwe sitokuwa mkeo.”(uk.81)
Kwa upande wa kisiasa, mwanamke amekuwa akikandamizwa kwa kuonekana hawezi kuwa kiongozi bora wa kuiongoza nchi ndio maana hata nafasi za wanawake zilikuwa chache huko bungeni. Katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Bâ mwandishi anayadhihirisha haya kwa kumtumia Ramatoulayi ambaye akilalamika kuhusu ukandamizwaji wa wanawake huko bungeni pale anaposema:
“Wanawake wanne, Dauda, wanne miongoni mwa wabunge mia moja uwiano gani huu wa kimzaha! Wala hakuna uwakilishaji wa kimkoa” (uk.81)
Kwa upande wa kijamii, mwanamke amekuwa akikandamizwa kwa kupigwa na mumewe bila sababu zozote za msingi. Hili linajidhihirisha katika riwaya ya Rosa Mistika iliyoandikwa na Euphrase Kezilahabi (1988) kwa kumtumia mhusika Zakaria ambaye alikuwa anampiga mkewe bila sababu. Mwandishi anasema:
“Regina tangu aolewe hakuwa na raha! Alikuwa akisumbuliwa na kuteswa na mumewe kwa kosa lisilokuwa lake. Katika kijiji chote cha Namagondo hapakuwa na mwanamke aliyekuwa akipigwa karibu kila juma kama Regina. Wanawake wengi kijijini walijiuliza kwa nini hakutaka kumuacha bwana wake. wengine walimuonea huruma, wengi lakini walimuona mjinga.” (uk.3)
Pi, mwanamke alikuwa anakandamizwa kwa kuonekana kuwa yeye ndiye mwenye majukumu ya malezi, kwa hiyo hata watoto wakiharibika anayelaumiwa ni mwanamke. Euphrase Kezilahabi analithibitisha hilo pale anaposema:
“Lete hiyo barua iko wapi? Pamoja na shilingi ulizopewa unafikiri sisi hapa maskini. Rosa alipigwa tena na tena. Makofi yalikwenda mfululizo hata damu zikamtoka puani na mdomoni. Baba nihurumie sitarudia tena… Zakaria hakujali alichukua fimbo na kuongozana na bintiye mpaka chumba cha watoto hali akinguluma lazima unioneshe barua hiyo unataka kuniletea umalaya wa mama yako hapa.” (Uk.7)
Vilevile, mtoto wa kike alikuwa anaonekana hana thamani katika jamii, na watoto wa kiume ndio waliopewa kipaumbele. Euphrase Kezilahabi anathibitisha haya katika riwaya ya Rosa Mistika kwa kumtumia Zakaria ambaye kabla ya kumpata mtoto wa kiume alikuwa anamnyanyasa sana mke wake lakini baada ya kujifungua mtoto wa kiume manyanyaso yaliisha na alimpenda sana mkewe. Mwandishi anasema:
“Zakaria alirudi nyumbani siku hiyo. Alikuwa amekwisha pata habari hizo njiani. Alimbeba mtoto. Alimpa pongezi mke wake. Regina sasa mji huu umekuwa wako. Asante Regina alijibu akitabasamu, alijiona anauwezo wa kuzungumza.” (uk.24)
Lengo hili linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwani mwanamke hatakiwi kurithi mali yoyote pindi wazazi wake wanapofariki au mumewe anapofariki. Pia mwanamke kushindwa kupewa nafasi ya kutoa maamuzi yoyote katika masuala ya kiukoo. Kwa upande wa dini mwanamke anakandamizwa na kuonekana dhaifu hivyo kutokuwa na nafasi ya kuongoza waamini. Mfano, dini ya Kiislamu na baadhi ya madhehebu ya Kikristo.
Lengo lingine ni kuzitambua na kuzibainisha dhamira kuu katika kazi zilizoandikwa na wanawake. Dhamira kuu ni dhamira inayomsukuma mwandishi katika kuandika kazi ya fasihi. Baadhi ya waandishi wanawake wameonesha dhamira kuu katika kazi zao kama ifuatavyo:
Nguzo Mama iliyoandikwa na Penina Muhando (2007) imebeba dhamira kuu ambayo ni ukombozi wa mwanamke. Ukombozi huo upo katika nyanja mbalimbali kama vile kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Mfano, mwandishi ameonesha wanawake wanavyojishughulisha katika kuinua uchumi wao, kwani walikuwa wakiuza vitambaa na kupika pombe. Mwandishi anathibitisha haya kwa kusema:
“BI TANO: Yaani mnasema mimi mvivu siyo nimezunguka mji mzima na zigo hilo halafu mnaniambia mimi mvivu. Nawaambia watu hawataki kununua au mnataka niwagawie bure.”
BI NANE: Lakini kwa nini wakatae kununua hivi, mbona vile vya mwanzo walivinunua? (uk.16).
Vilevile, Katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Bâ (1994) suala la ukombozi wa mwanamke limejitokeza kama dhamira kuu. Ukombozi huu umejikita katika nyanja za kisiasa, kiutamaduni, kijamii na kiuchumi.
Mfano, katika nyanja ya kijamii, mwandishi ameonesha jinsi ya kumkomboa mwanamke kielimu, pale anaposema:
“…Shangazi Nabu anampeleka Nabu mdogo katika shule ya Kifaransa huko. Huko Nabu alijifunza aina mbalimbali za mapishi, matumizi ya pasi na zana za kutumia na kumenyea…” (uk.39)
Lengo hili linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwa kuwa tangu mwanzo wanawake walikuwa hawaruhusiwi kuwa viongozi, badala yake wanaume ndio waliochukuwa jukumu hilo la uongozi katika jamii. Pia, wanawake hawakuruhusiwa kupata elimu wakitegemezwa katika majukumu ya nyumbani na kuandaliwa kwenda kuolewa na kuja kuwa walezi wa familia.
Kuichunguza historia ya kifasihi ya jadi ya kike na kuwamulika waandishi wa kike waliotambua hali za wanawake na ambao wanaweza kuchukuliwa kama vielelezo kwa wasomaji wao. Hapo awali kazi mbalimbali za kifasihi za jadi za kike zilielezwa na waandishi wa kiume. Lakini nadharia hii imemulika waandishi wa kike wanaotambua hali mbalimbali na wameamua kuandika kazi mbalimbali ambazo zinaelezea matatizo ya wanawake. Mfano, katika tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi anaelezea jinsi wanawake wanavyonyanyaswa na kuachiwa majukumu ya kulea familia, kuchukuliwa mali zilizoachwa na waume zao baada ya kufariki. Mfano, mwandishi anasema:
“…Haa! Shemeji mmerudi kuchukua hata kitanda! Hata sufuria! Nitalala wapi na nitapikia wapi jamani!” (uk.39)
SUDI: Haya nipe pesa ulizokwisha kupata.
BI PILI: Hee! Kwa nini nikupe?
            SUDI: Leta pesa upesi kabla sijakukong’ota.” (uk.13)
Mariama Bâ naye ni kielelezo kwani ameelezea matatizo mbalimbali yanayowakumba wanawake na namna wanavyokabiliana na matatizo hayo. Mfano mwandishi anasema:
“… Ramatulayi, Acha nisikilize mimi zaidi; Redio ya Kankan ilinifahamisha kwamba ulikataa kuolewa na Tamsiri. Ni kweli? Ndio.”  (uk.87)
 Mwandishi anaonesha jinsi mhusika Ramatulayi alivyojitambua na kukataa kurithiwa na Tamsiri, pia anamkataa Dauda ambaye alitaka kumrithi baada ya kufiwa na mume wake.
Kupitia lengo hili tunaona wanaufeministi wameongelea kuhusu wanawake tu ambao ni vielelezo katika kazi za fasihi, lakini wapo wanaume ambao wamezungumzia masuala mbalimbali yanayowahusu wanawake. Mfano, Shaaban Robert aliyeandika Wasifu wa Siti Binti Saad.
Kudhihirisha kuwa kuna sifa fulani za kike na uzoefu fulani wa kike katika uwazaji, hisia, kutathmini, kujiangalia na kuuangalia ulimwengu wao wa nje. Uzoefu fulani wa kike unajitokeza katika uwazaji na jinsi wanavyousawiri uhalisi. Kazi ambazo zinamsawiri mwanamke kwa njia chanya, mfano ni riwaya ya Kiwasifu ya Shaaban Robert Wasifu wa Siti Binti Saad.  Kuna mashairi kadhaa aliyoyatunga mwandishi ambayo yanaendeleza suala hili la uchanya wa wanawake katika jamii. Mfano wa usawiri wa wahusika linathibitishwa pale mwandishi anaposema:
            “Siti binti Saad,
Ulikuwa mtu lini,
Ulitoka shamba,
Na kaniki mbili chini,
Kama si sauti,
Ungekula nini?” (uk.22)
Hisia: mfano, katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii kupitia mhusika Daba alivyomwambia mama yake kuhusu Benetuu. Mwandishi anasema:
“Hasira ya Daba iliongezeka zaidi jinsi alivyozidi kuichambua hali ilivyokuwa. “Mama! Vunja ndoa yako! Achana naye mtu huyu hajatuheshimu, si wewe wala si mimi… sitaki kukuona unagombania mwanaume na mwanamke mwenye umri sawa na mimi.” (uk.52)
Lengo hili la wanaufeministi, linaendana na hali halisi ya wanawake wa Kiafrika, kwa kuwa mawazo ya mwanamke jinsi anavyojiwazia yeye mwenyewe au kuwawazia wanawake wenzake hutofautiana . vilevile, hisia za mwanamke zinaweza kudhihirika katika maandishi na kuonesha jinsi wanavyowaza katika hali ya kawaida.
HITIMISHO
Lengo la nadharia ya ufeministi lilikuwa ni kuondoa unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa mwanamke. Hivyo basi, malengo ya ufeministi yalijikita katika kumnasua mwanamke kutoka katika pingu za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii. Malengo haya ndiyo yanayoleta ukinzani wa maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika. Hali hii imeleta mabadiliko katika maisha ya wanawake wa kiafrika, kama vile kutaka haki ya elimu, kumiliki mali, kurithi mali, kutaka nafasi za uongozi, pia kuwa na maamuzi ya kifamilia au kiukoo, katika kupingana na pingu za maisha.
Nadharia ya Uhemenitiki
Uhemenitiki ni taaluma inayohusiana na uelewaji na kutafsiri matini. Chimbuko la nadharia hii ni katika uchambuzi wa falsafa katika matini za kidini, hususani dini ya Kikristo. Waasisi wanaohusishwa na chimbuko la nadharia hii ni kama vile Friedrich Schleiermacher (1768-1834),Wilhem Dilthey (1833-1911) na Martin Heidegger (1889-1976).
 
 Msingi mkubwa wa nadharia ya Uhemenitiki ni imani ya kwamba matendo ya binadamu yanaathiriwa kwa njia  mbalimbali na asasi tofauti zilizoko katika mazingira yake. Msingi huo unatupeleka katika dhana ya kuibua umuhimu wa kuelewa njia au mbinu za uelewaji wa maana za matini. Madai ya msingi ya nadharia ya Uhemenitiki yanahusisha dhana mbalimbali kama vile duara la kihemenitiki, utukuzaji pamoja na ile ya ufufuaji wa kisarufi, kisaikolojia na kimuktadha (Senkoro, 1987; Wamitila, 2002 katika Ponera, 2010).
 
Akizungumzia suala la Mviringo au Duara la Kihemenitiki, Senkoro (1989:9) anasema:
“…katika usomaji kuna mviringo wa kihemenitikiambao humfanya msomaji aende mbele na nyuma, kushoto na kulia mwa yale yaongelewayo katika kaziya fasihi.Hadhira huwa wanabashiri na kuhusisha mambowanayoyapitia maishani mwao”.


Kulingana na nadharia hii ya Uhemenitiki huwa kuna ugumu wa kuwepo kwa uwiano kati ya malengo na maana asilia ya mtunzi dhidi ya uelewaji wa maana aipatayo msomaji. Uelewaji wa maana kwa msomaji huhusisha kuyajua mambo mbalimbali yaliyomzunguka mtunzi wakati au kabla ya kuitunga kazi husika. Ni vigumu kuelewa malengo na maana asilia ya mtunzi iwapo msomaji au mhakiki hatahusisha mambo hayo. Kwa kufanya hivyo, ndipo msomaji atakuwa amelitalii duara la kihemenitiki. (Ponera, 2010).

 
Dhana ya Utukuzaji  katika nadharia ya Uhemenitiki inamaanisha jumla ya makisio mbalimbali ambayo msomaji au mhakiki wa kazi ya fasihi huwa nayo punde aishikapo kazi yoyote ya kifasihi. Makisio hayo  hujengwa akilini mwa msomaji kulingana na misingi mbalimbali kama vile anwani yake (jina na picha ya kitabu), kiwango cha usomi, utamaduni, upeo wa uelewa, pamoja na ulinganisho wa kazi zozote zilizotungwa na watunzi wengine zinazofanana na hiyo (Wamitila, 2002).
 
Wamitila (2002:193) anafafanua kuwa dhana ya Ufufuaji, hususani ule wa kisaikilojia iliasisiwa na Dilthey (1833-1911).  Alisisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa msomaji au mhakiki kufufua muktadha asilia wa kazi inayohusika na kujaribu kujiweka katika muktadha huo ili aweze kuipata maana asilia ya matini. Kwa mujibu wa mawazo yake, kazi mbalimbali za kifasihi zinaweza kuwa na maana mbalimbali kwa wasomaji mbalimbali. Aidha, dhana ya ufufuaji inasisitiza kuwa ili kuielewa na kuitafsiri maana ya matini lazima msomaji au mhakiki azame katika kuuelewa mtindo. Hapa neno ‘mtindo’ limetumika kumaanisha muktadha wote wa mfumo wa maneno na sentensi zilizotumika katika matini.
 

 
Dhana hizi zinazobeba madai ya msingi ya nadharia ya Uhemenitiki zinahusiana kwa kiasi kikubwa. Gadamer (1960) ambaye amenukuliwa na Senkoro, (1987:7) anasema:
 
 “Taaluma ya Uhemenitiki hujihusisha na utafutaji wa maana ya kazi ya fasihi
                kwa kuuliza maswali muhimu manne:
                i. Ni nini maana ya fasihi?
                ii. Je, maana hii inahusianaje na kusudi la mwandishi?
                iii. Je, tunaweza kuzielewa kazi za fasihi za tamaduni na historia tofauti na zetu?
                iv. Je, ni rahisi kupata uelewaji wa ndani wa kazi ya fasihi au huu hutegemea
                      mazingira na historia ya hadhira ihusikayo?”.

Kuyajibu maswali haya kulihusisha kwa pamoja dhana za Duara la Kihemenitiki, Ufufuaji na Utukuzaji ambazo zinaunda madai ya msingi ya nadharia hii. Misingi ya nadharia hii ilitumika katika kuendesha utafiti uliofanywa unaohusu vipengele vya msingi vya kiufafanuzi. Misingi hiyo ni ile iliyomo katika dhana tatu muhimu zilizomo katika nadharia hii ambazo ni Duara la Kihemenitiki, Ufufuaji na Utukuzaji.

 
Hivyo, taswira zinazojitokeza katika ushairi wa Kaluta Amri Abedi zilichunguzwa kwa kuhusianishwa na vipengele vingine vya kimaisha kama vile matukio ya kihistoria yaliyojiri kabla au wakati wa utunzi, tabia na mwenendo halisi wa Sheikh Kaluta Amri Abedi mwenyewe, hali halisi ya maisha tangu kipindi cha baada ya kazi husika kutungwa hadi sasa, na jiografia ya alipokuwa mtunzi (duara la Kihemenitiki). Aidha, uchunguzi ulihusisha fikra binafsi za mtafiti kuhusiana na lugha na taswira mbalimbali zijitokezazo katika Diwani ya Amri (Utukuzaji). Vilevile uchambuzi wa data ulizingatia mtindo mahsusi ambao Kaluta Amri Abedi aliutumia katika utunzi kwa kuulinganisha na matumizi ya lugha ya wakati huo (Ufufuaji).
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)