MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
SIKU 100 ZA MHESHIMIWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN NA MCHANGO WAKE KATIKA KISWAHILI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SIKU 100 ZA MHESHIMIWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN NA MCHANGO WAKE KATIKA KISWAHILI
#1
SIKU 100 ZA MHESHIMIWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN NA MCHANGO WAKE KATIKA MAENDELEO YA KISWAHILI UCHAMBUZI WA MASUALA 11 MUHIMU YAHUSUYO LUGHA ADHIMU NA AUSHI YA KISWAHILI

Anaandika PhD Dkt.Ahmad Sovu

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi iendelee.

Tunaendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuazima pumzi yake. Amina.

Wapenzi wasomaji wa makala zetu mnamo tarehe 19/03/2021 Rais wetu Mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Rais wa awamu ya 6 kufuatia kutawafu kwa Rais wa awamu ya 5 Dkt.John Pombe Magufuli tarehe 17/03/2021.

Mheshimiwa Rais Samia ametimiza siku 100 ambako kilele chake kitakuwa siku ya Jumatatu.

Makala haya yamekusudia kuonesha mchango wa Rais Samia na serikali yake kwa kipindi cha siku 100 kuhusu lugha ya Kiswahili.

1 Historia fupi kwa nini siku 100?

Ili kujenga ufahamu wa pamoja, tupitie historia fupi ya siku 100 katika nchi mbalimbali kama ilivyofafanuliwa katika makala ya Ndugu Abbas Mwalimu-Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia ambaye yeye amezungumzia siku 100 za Rais Samia kwa mnasaba au kwa jicho la Diplomasia.

Anafafanua na tuna mnukuu hapa:

Kimsingi asili ya siku 100 zilianza kutazamwa kuanzia mwaka 1933 wakati huo Rais Franklin Delano Roosevelt  alipoapishwa kuwa Rais wa 32 wa Marekani tarehe 4 Machi, 1933 katika kipindi ambacho kulikuwa na mdororo mkubwa wa uchumi nchini  Marekani na duniani kwa ujumla

Rais Roosevelt alifanya mabadiliko makubwa na ya haraka ya kisera katika mfumo wa uchumi na jamii ili kukabiliana na hali hiyo ya mdororo

Rais Roosevelt alihakikisha ndani ya miezi mitatu ya mwanzo Serikali yake inapeleka miswada mingi ya mabadiliko ya sheria mbalimbali Bunge la Congress ili kupambana na mdororo huo

Serikali ya Rais Roosevelt ilifanikiwa kuidhinisha miswada 76 iliyolenga kukabiliana na mdororo  kuwa sheria ndani ya siku 100 na hivyo kuchukuliwa kama mafanikio katika kipindi kifupi cha kuwepo madarakani.

Rais Roosevelt maarufu kama FDR alijiwekea utaratibu wa kuzungumza na wananchi moja kwa moja kupitia redio na kuwaeleza namna alivyokuwa akikabiliana na tatizo hilo na hivyo kuondoa wasiwasi kwa wananchi

Tangu kufariki kwake tarehe 12 Aprili, 1945 siku 100 zimekuwa zikichukuliwa kama kipimo cha namna gani Rais wa Marekani atakabiliana na changamoto zilizojitokeza kwa wakati huo na namna gani ataonesha mwanga wa mafanikio

Utaratibu huu umerithiwa na nchi nyingi duniani ikiwamo Tanzania ambapo hadi Jumatatu itakuwa kilele cha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza siku hizo

Baada ya kupata ufahamu huo. Ufuatao ni mchango wa Rais Samia na serikali yake katika maendeleo ya Kiswahili kama ifuatavyo:

2 Katika Elimu

Katika hotuba yake baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na viongozi mbalimbali wa serikali aliwataka viongozi wanaosimamia sekta ya elimu kutafakari juu ya kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika elimu. Alisema:

...Lakini pamoja na kuangalia suala zima la Historia yetu na kutumia lugha yetu ya Kiswahili kwenye elimu, sasa hivi eeeh nchi za Kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki Kiswahili ni somo katika selabasi zao. Lakini na sie wenye Kiswahili bado ni somo kwenye selabasi yetu. Sasa tunavyosema tunakuza Kiswahili...sijui liangalieni vizuri. Ni mawazo kutoka kwangu liangalieni vizuri...msije mkasema Rais kasema nasema tuliangalie

Ukitazama maelezo haya ni dhahiri Mheshimiwa Rais aliwataka wadau wa elimu na viongozi wanaosimamia masuala ya elimu kuwa na tafakuri juu ya matumizi ya Kiswahili katika elimu.
Hatua hii kwa namna moja ni kama imeanza kuchukuliwa hatua. Ambapo hivi karibuni tumeshuhudia taasisi ya elimu ikifanya mijadala na wadau kuhusu mifumo bora uendeshaji wa elimu nchini. Wadau wa Kiswahili na wataalamu wengine bila shaka wametoa na wanaendelea kutoa maoni yao juu ya Kiswahili kutumika kufundishia.

3. Kuwatia moyo Wabunge wa Kenya kuhusu matumizi ya Kiswahili
Mnamo tarehe 05/05/2021 alilihutubia Bunge la Kenya. Katika hotuba yake pamoja na mambo mengine aliwaeleza Wabunge hao kuwa yeye ni mfuatiliaji mzuri sana wa Bunge hilo. Katika ufuatiliaji wake hufurahishwa sana na matumizi ya Kiswahili cha Kenya ambacho kina vionjo mbalimbali. Anasema:

Kiswahili chenu kina vionjo vingi, kuna vionjo vingi ambavyo peke yake ni burudani tosha kusikiliza(vicheko) anaendelea kusema:

nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Spika anavyoshindwa kutaja namba za miaka (vicheko) kwa Kiswahili lakini inafurahisha kwamba mliishatunga kanuni za Bunge na mkamualika Mheshimiwa Job Ndugai kuja kuzindua kanuni zile tarehe 31 Oktoba 2019. Hii inatia moyo kuwa tuko pamoja  na kweli mnataka kutumia Kiswahili lakini hatua kwa hatua...Rai yangu kwenu ni kuwaomba msaidie kuleta uhusiano wetu

Maelezo haya ya Mheshimiwa Rais Samia  yanatia moyo Wakenya na kuzidi kuzungumza Kiswahili zaidi na kwamba kukifahamu ni hatua kwa hatua.

Ziara ya Mheshimiwa Rais pamoja na masuala mengine muhimu ya kitaifa bado hakuacha kuhimiza matumizi ya Kiswahili.

4 katika uga wa sheria

Katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 27/Mei/2021 Mheshimiwa Profesa Paramagamba Kabudi, waziri wa sheria na katiba alipokutana na  wakurugenzi wa Idara na vitengo vya sheria na Wizara zote za serikali mjini Dodoma.
Pamoja na mambo mengine kikao kililenga kufanya tathimini ya zoezi la kutafsiri sheria mbalimbali mbalimbali katika lugha ya Kiswahili. Mheshimiwa Kabudi alisema:

Maamuzi yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano na sita ya kutumia Kiswahili kwenye sekta ya sheria si kwamba Watanzania hawajui Kiingereza, isipokuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa letu, ni utambulisho wa Taifa letu na ni utambulisho wa utu wetu

Maelezo haya ya Prof.Kabudi yanaonesha namna Rais Samia Suluhu kazi imeendelea katika suala la matumizi ya lugha kwenye uga wa sheria na mahakama.

Katika  hatua nyingine, Mheshimiwa Geofrey Pinda naibu Waziri wa sheria na katiba, katika mkutano wa wadau kujadili mchango wa matumizi ya Kiswahili katika upatikanaji haki kwa wananchi. Alisema:

...na sasa tumeamua kwa makusudi mahakama na Baraza la ardhi yote lazima yatumie Kiswahili katika kutatua migogoro ile ambayo ilikuwapo katika jamii...

Mheshimiwa Pinda alisisitiza kuwa matumizi ya Kiswahili katika uga wa sheria na mahakama kuwa ndio tunarudi kwenye Uhuru wa kweli.
Hapa tunaona namna ndani ya siku hizi 100 za Mheshimiwa Rais Samia  zinaendeleza kazi ya kukuza na kuendeleza Kiswahili katika uga wa sheria na mahakama.

5 Kiswahili chazidi kupaa katika Jumuiya ya SADC na Umoja wa Afrika

Ndani ya siku 100 za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Kiswahili  kimezidi kukua na kutamalaki katika anga za kimataifa. Kupitia kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje Mheshimiwa Balozi Leberata Mulamula, katika siku ya Umoja wa Afrika (Africa Day) kwenye kikao na mabalozi  alisema:

Lugha ya Kiswahili yachaguliwa kuwa lugha rasmi katika mikutano ya umoja wa nchi za Afrika

Mheshimiwa Balozi Mulamula alisisitiza kuwa Kiswahili ni lugha inayotumika katika anga hizo ukilinganisha na lugha nyingine za Kiafrika.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa waziri wa fedha na uchumi Daktari Mwigulu Nchemba kwa niaba ya nchi alitetea kwa hoja kuntu matumizi ya kuboreshwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) badala ya kufutwa kama ilivyokuwa imependekezwa na Mtaalamu mshauri.

  Mheshimiwa Mwigulu alisema:

Tunatetea Kiswahili kama kielelezo cha Afrika Mashariki na tume hii ambayo imesimamia hicho Kiswahili. Tunaiona ni taasisi muhimu sana ambayo baadae inatakiwa hata iweze kuunganisha hizi nchi zetu, yaani Kiswahili kiweze kufika kwenye kila taasisi zingine pamoja na huko kwenye Idara za elimu ambayo tunasema...

Hapa inadhihirika  namna ambavyo wateule wa Mheshimiwa Rais Samia wakisimama imara katika kupigania Matumizi ya Kiswahili na utamaduni wetu.

Hii ni kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia  mwenyewe pale alipolihutubia Bunge
la 12 tarehe 22 Aprili, 2021 alisisitiza:

Jambo la kwanza na muhimu kabisa tutakalolipa kipaumbele kwenye miaka hii mitano ni kuendelea kulinda na KUDUMISHA TUNU ZA TAIFA letu, yaani Amani, Umoja na Mshikamano, Uhuru wa nchi yetu, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wetu. Kama mnavyofahamu, amani na umoja ni msingi mkuu wa maendeleo katika Taifa lolote. Hivyo basi, nawasihi sana Watanzania wenzangu
tushirikiane kwa pamoja katika kulinda tunu hizi

Moja ya tunu zetu kama Taifa  ni lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

6 Kuongeza vifaa vya Kisasa vya mafunzo ya ukalimani kwa vitendo na matumizi ya TEHAMA katika ukuzaji wa Kiswahili

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kupitia Naibu Waziri wa Habar, sanaa na michezo, , Mheshimiwa Pauline Gekul alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Singida Mjini Mheshimiwa Mussa Simai alilotaka kujua mpango wa serikali kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa ya kimataifa ili kuendelea kukuza utamaduni wetu duniani.

Mheshimiwa Gekul alijibu:
Tayari tunao Mpango wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kupitia Balozi zetu nje ya nchi na serikali imeboresha na kuimarisha mafunzo ya stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni. Pamoja na kutoa machapisho ya Kiswahili rahisi kwa wataalamu wetu

Majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri yalikuja kudhihirishwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara hiyo Ndugu Mheshimiwa Innocent Bashungwa.
Ambapo Mheshimiwa Waziri alisisitiza jambo hili litakwenda sanjari na uongezaji wa vituo vya Kiswahili katika Balozi mbalimbali za Tanzania zilizoko katika nchi mbalimbali duniani.

Katika hili napenda pia kumpa Kongole sana Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini Mheshimiwa Batilda Swila na Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini China Mheshimiwa Balozi Mbelwa Kairuki na pia ubalozi Qatar kwa mchango wao katika kueneza Kiswahili katika Balozi zao. ?? ndani ya siku hizi 100  ubalozi wa Korea kusini ulifanya Kongamano kubwa la mtandaoni la Kiswahili ambalo lilikuwa zuri sana na lilijumuisha wapenzi wa Kiswahili kutoka pande zote za dunia. Katika Kongamano hili tulishuhudia vijana Wa Kikorea wakiimba nyimbo za uzalendo za Tanzania. Kongoleni sana Mabalozi wetu.

7 Kiswahili chapenya kuwa lugha ya ADPA

Katika kipindi cha siku 100 za Mheshimiwa Rais Samia Kiswahili kimebahatikiwa kupenya na kuwa lugha katika Jumuiya hiyo ya wachimba Almasi Afrika, yaani African Diamond Producers Association ambayo ina jumla ya nchi wanachama 19.

Alipokuwa akizungumza na wanahabari mnamo tarehe 8/4/2021 Waziri wa Madini Mheshimiwa Doto Biteko alisema:

la pili tumekubaliana kwamba, Kiswahili na chenyewe iwe moja ya lugha za mawasiliano katika umoja wetu wa ADPA. Kabla ya leo (yaani siku hiyo) lugha zilizokuwa zinatumika kwenye ADPA ni Kiingereza, Kifaransa pamoja na Kireno leo tumeongeza lugha ya Kiswahili na chenyewe kiweze kutumika katika umoja wa nchi zinazozalisha Almasi hapa Afrika

Kwa lugha ya vijana niliyoisikia hivi karibuni wanasema Mama anaendelea kuupiga mwingi katika lugha ya Kiswahili??

8 Kuongeza msamiati wa kilahaja katika lugha ya Kiswahili

Ndani ya siku hizi 100 za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani alitumia Kiswahili cha lahaja ya kikae (Kimakunduchi) katika hotuba yake alipokuwa anaongea na viongozi wa dini jijini Dodoma mnamo tarehe 18/4/2021. Mheshimiwa Rais alisema:

...Inasikitisha sana kwamba watu wanapiga ngoma mitandaoni lakini ngoma ile inachezwa Bungeni na inachezwa kwa kudemka vizuri sana, mnademka vizuri sana...kulinganisha watu na sio ajenda za kitaifa...

Mheshimiwa Rais Samia anatumia neno demka ambalo maana yake ni kucheza ngoma kwa madaha, matao au maringo  alitumia neno hili pale alipokuwa akiwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kujikita kwenye mijadala yenye afya na tija kwa Taifa.
Mheshimiwa Rais Samia anatutambulishia msamiati mpya masikioni mwa Watanzania wengi na sasa tunaanza kuufahamu na kuutumia katika miktadha mbalimbali ya matumizi.

9 Matumizi ya misemo na kaulimbiu mbalimbali ya Kiswahili

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ndani ya siku hizi 100 za utawala wake mbali ya kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha na usanifu, amekuwa akiunda na kutumia misemo mbalimbali ya Kiswahili ambayo husaidia kunogesha hotuba zake na kuhakikisha malengo aliyoyakusudia yanafikiwa.

Tutazame kwa muhtasari misemo hiyo na uchambuzi wake mfupi.

i) Kazi iendelee
Kaulimbiu ya kazi iendelee mwandishi wa makala haya aliwahi kuifafanua kwa kina katika moja ya makala zake zilizohusu hotuba ya Mheshimiwa Rais Samia aliyoitoa Bungeni. Kwa ambao hawakupata nafasi ya kusoma makala hayo nawasihi waisome kwani imeeleza kwa muhtasari namna falsafa hiyo inavyoweka msingi wa namna utawala wake utakavyokuwa.

Kwa ufupi sana falsafa ya kazi iendelee inahimiza na kutaka Watanzania waendelee kuchapa kazi. Kumbuka Mheshimiwa Rais Samia amechukua nafasi ya hayati Magufuli ambaye kaulimbiu yake ilikuwa ni hapa kazi tu ndani ya siku 100 mama Samia anatupatia kaulimbiu mpya inayochagiza kuendeleza mambo yote mazuri ya hayati JPM na kuhimiza kazi iendelee.

ii) Aitambulisha salamu mpya

Mheshimiwa Rais Samia katika kuichagiza kaulimbiu ya kazi iendelee anaitambulisha salamu mpya ya Kiswahili pale aliposema:

leo nina salamu mpya nikisema nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnatakiwa kujibu kazi iendelee

Salamu hii ya Kiswahili imekuwa adhimu inayotumiwa katika hafla mbalimbali za serikali na hata za kijamii.
Mwandishi Majid Mswahili katika makala yake inayohusu Falsafa katika salamu hii alisema:
salamu hii ni zaidi ya salamu kwani inaondoa tofauti zetu za makabila, rangi, dini na hata umaeneo
Hivi ndivyo ambavyo Kiswahili kinavyoweza kutumika kuimarisha umoja, mshikamano na mwenendo bora wa Taifa.

iii) Zege halilali

Msemo mwingine aloutumia Mheshimiwa Rais Samia ni msemo huu wa zege halilali. Msemo huu ni maarufu sana katika shughuli za ujenzi. Katika shughuli za ujenzi mafundi waashi wanapokoroga zege iwe kwa mashine au kwa mikono shurti lile zege limwagwe wakati huohuo, vinginevyo likiachwa litaganda na halitakuwa na maana wala tija.

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatumia lugha ya zege halilali kwa lengo la kuhimiza kaulimbiu yake kuwa kazi lazima ziendeleee na hakuna kulala.
Hivi ndivyo ambavyo, unawaona wateule mbalimbali wa Mheshimiwa Rais wakiendeleza kazi hizo ndani ya siku hizi 100.

iv. ukinizingua nitakuzingua

Mheshimiwa Rais Samia ametumia msemo huu unatumiwa zaidi na rika la vijana. Alibainisha wazi kuwa msemo huu hutumiwa zaidi na Mheshimiwa Waziri kijana na machachari Mheshimiwa Juma Aweso anapotekeleza majukumu yake. Katika kile ambacho ni kuitazama hadhira yake kuwa ni ya viongozi. Wengi katika viongozi hao ni vijana anatumia msemo huu ambao unasadifu muktadha huo pale aliposema:

Wewe ni kijana na mimi ni Mama, ukinizingua na mini nakuzingua

Zingua kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili ni kubabaisha mtu, sumbua mtu au kutesa. Mheshimiwa Rais Samia anawasisitiza viongozi wake kuwa wakimbabaisha naye atawababaisha japo ni Mama. Haya yanadhihirika ndani ya siku 100 ambapo baadhi ya viongozi waliomzingua Mama tayari kishawazingua.

v) Nyumba uliyoizoea kuihama ina tabu

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika mkutano Mkuu maalumu wa Chama cha Mapinduzi Dodoma, alitumia msemo huu katika kushadidia kauli za Ndugu Lazaro Nyalandu alipokuwa akifafanua namna alivyoishi kwa tabu katika Chama alichokuwa amehamia cha CHADEMA  huko awali kabla ya kurudi nyumbani CCM.
Mheshimiwa Rais Samia alisema:

Kule Zanzibar kuna mshairi aliimba nyumba uliyoizoea kuihama ina tabu (shangwe). Ni kazi kweli kuihama nyumba uliyoizoea...na wanaume wanajua hilo...

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu anaitumia lugha katika muktadha mwafaka kabisa. Wimbo aliounukuu kipande hiko unaitwa Dunia ina fisadi ni katika  taarabu asilia. Ambapo unaanza katika beti hiyo wale walionikamia nawaambia waziwazi x2...nyumba uliyoizoea kuihama ina kazi
Maudhui ya shairi hili ni mapana lakini katika makala haya hatujakusudia kulidadavua kwa kina. Msisitizo wetu ni kuonesha ndani ya siku hizi 100 anavyotumia lugha ya Kiswahili katika muktadha sahihi na kushajiisha suala alilolikusudia.

10 Kuendelea kutumia Kiswahili katika hafla mbalimbali za serikali

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu mbali ya umahiri na ulumbi wa kulumba Kiswahili alioruzukiwa na Mola, ndani ya siku 100 za utawala wake ameendelea kutumia lugha ya Kiswahili katika hotuba zake. Amefanya hivyo akiwa ndani ya nchi na hata nje ya nchi, awe na ugeni wa ndani au wa nje haya ni maendeleo makubwa sana kwa lugha yetu ya Kiswahili.

Huyu ndiye Mama Samia Suluhu Hassan ambaye hata kabla ya kupata wadhifa huu wa Urais, pale alipokuwa makamu wa Rais alikuwa mstari wa mbele katika kukuza Kiswahili na kwa kweli kazi imeendelea katika kipindi hiki cha siku 100 tangu awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Heko na kongole sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza lugha yetu ya Kiswahili.??

11 Matarajio
Mintarafu ya mafanikio haya ndani ya siku hizi 100, wapenzi na wadau wa Kiswahili tuna matarajio mbalimbali katika awamu ya 6

1.Kiswahili kuendelea kuwa lugha muhimu katika kuimarisha na kuchochea maendeleo ya nchi hususan dhana ya Diplomasia ya uchumi.

2.Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu.

3.Kuendelea kuhimiza matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu kwa umma.

4. Kuendelea kuifanya lugha ya Kiswahili bidhaa lugha itakayoingiza fedha.

Hizi ndizo siku 100 za utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na mchango wake katika maendeleo ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Nawashukuru wataalamu mbalimbali wa Kiswahili kwa maoni yao katika kuboresha zaidi makala haya.

Tuendelee kumtia shime Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wetu wote ambao wanaendeleza tunu ya lugha yetu ya Kiswahili ndani ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania. Kiswahili ni nyenzo ya uchumi, uti wa mgongo wa Taifa letu na utambulisho wetu. Bidhaa ya kujidaia na kutambia ulimwenguni kote.

0713400079
Mhadhiri
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere-Kigamboni
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)