06-26-2021, 05:14 PM (This post was last modified: 06-26-2021, 05:17 PM by MwlMaeda.)
Katrina Esau anafanya kila awezalo ili lugha yake ya utotoni inasalia duniani hata baada ya kifo chake
Bi Esauni, 84, ni mmoja wa watu watatu walio hai ambao wanazungumza kwa ufasaha lugha iitwayo Nuu, mojawapo ya lugha zinazozungumzwa nchini Afrika Kusini ya jamii ya San, ambao pia wanafahamika kama Bushmen.
Lugha ya N|uu inachukuliwa kama lugha asili ya taifa la Afrika Kusini.
Huku kukiwa hakuna hata mtu mmoja ambaye anaweza kuzungumza kwa ufasaha lugha hiyo isipokuwa watu wa familia yake, lugha hiyo imetambuliwa na Umoja wa Mataifa kama “lugha iliyo katika hatari kubwa ya kuangamia”.
“Nilipokuwa mtoto, nilikuwa nikizungumza tu Ki-N|uu na nikawasikia watu wengi mno wakiongea lugha hii.
Ilikuwa ni habari njema, tuliipenda sana lugha yetu, lakini hilo kwa sasa limebadilika,” anasema Bi Esau huko Upington, mji ulioko katika jimbo la Northern Cape.
Kwa karne nyingi, watu wa kabila la San, walikuwa wakitembea kwa uhuru mkubwa katika maeneo haya, wakikusanya matunda na mimea, huku wakiwinda wanyama ili kulisha familia zao.
Lakini leo, tabia hiyo ya kitamaduni ya wa- San, imekwisha kabisa, na watu wa ukoo huo wananiambia kuwa, lugha ni jambo miongoni mwa mambo machache yaliyosalia ambayo yanawaunganisha na buyu la historia yao.
Ndani ya nyumba moja ndogo ya mbao, anawafunza watoto wa mtaa huo sauti 112 na Sauti mwaliko 45 za N|uu.
“Nawafunza lugha hii kwa sababu, sitaki ipotee, mara baada ya kufa kwetu,” Bi Esau alisema.
“Nataka kuwafunza kabisa hadi waelewe, kwa sababu nafahamu hatuna muda mrefu uliosalia.”
Huu ni mwaka wa 10 kwa Bi Esau ambaye amekuwa akiendesha shule hiyo nyumbani kwake.
Watu wa jamii hii, akiwemo Bi Esau, wanazungumza Ki -Afrikaan, ambayo inafanana na liugha inayozungumzwa na walowezi wa Kiholanzi, waliofika Afrika Kusini karne ya 17 wakitokea Uholanzi.
“Tungepigwa vibaya sana iwapo ungepatikana na mzungu ukizungumza lugha hii,” amesema.
“Kwa sababu ya historia yetu, watu leo hawataki kabisa kuzungumza lugha hiyo, kwani inazungukwa na machungu makubwa.
“Tuliitupilia mbali lugha ya N|uu na tukaanza kujifunza na kuzungumza lugha ya Afrikaan, hata ingawa sisi sio wazungu- hiyo imetatiza pakubwa utambulisho wetu,” ameongeza.
Dadake Bi Esau, Hanna Koper na Griet Seekoei – wote wenye miaka 95- wanasikiza kwa makini sana, huku akizungumza kwa machungu waliyopitia wakiwa watoto wadogo.
Hawazungumzi sana lakini wanaitikia kwa kutikiza vichwa vyao, huku dada yao akiongea.
Leo hii, Ouma Geelmeid, anavyofahamika na wengi, ana matumaini ya kuondoa aibu inayoandama lugha hiyo ya N|uu.
Wakati wa mafunzo, huku akiwa na kijiti mkononi, Bi Esau anagusa majina ya Ki- N|uu katika mchoro ulio na viungo vya mwili wa binadamu, huku wanafunzi wakisoma kwa mpigo.
Sawa tu na lugha nyingi za bara Afrika, ambazo zimekuwa zakipasishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa kuzungumza tu- lakini lugha hii sasa imo katika hatari ya kuangamia.
Hadi hivi majuzi, hakukuwa na rekodi yoyote ya maandishi ya lugha hii.
Bi Esau anafanya kazi na mtaalamu wa lugha, Sheena Shah kutoka Chuo cha Masomo kuhusu Afrika na Mashariki ya Kati (Soas) Jijini London na Matthias Brezinger wa taasisi ya The Centre for African Language Diversity Centre Jijini Cape Town, Afrika Kusini ili kubuni alfabeti ya lugha ya Ki- N|uu na misingi imara ya alfabeti na sheria ya msingi ya sarufi.
“Kutokana na kazi aliyoifanyia jamii ya Ouma Geelmeid, tulielewa kuwa jamii hizi zinaitazama lugha kama kitambulisho chao, na hivyo ni kigezo muhimu mno kwa muingiliano wa binadamu,” anasema Bi Shah.
“Utambulisho wa mtu binafsi ni jambo nzuri mno, hasa sasa kote duniani.”
Chakula cha Wahadzabe cha matunda na nungunungu Tanzania
Lugha ni zaidi ya suala fulani tu la kuwasiliana na mtu mwingine, pia inafungamanishwa na tamaduni na namna maisha ilivyo katika jamii, wataalamu wananiambia.
“Unapotizama lugha za kiafrika, unaelewa kuwa wanawasilisha hali ya maisha kwa njia tofauti mno, mahusiano, maswala ya kiroho, ardhi, afya na ubinadamu,” anasema Bw Brezinger.
“Kuna upana mkubwa mno wa mawazo ujuzi na maarifa juu ya maisha, ambayo imepeanwa kutoka kizazi hata kizazi katika makabila asilia ya Afrika, ambayo mataifa ya magharibi yanafahamu vitu vichache mno na kwa hakika hawajui ni lini lugha hizi zinaangamia: pia ya namna maarifa ya kipekee pia wanapotea,” anaendelea kusema.
Ndani ya darasa, kunao watoto kama 20 hivi, wengi wao wakiwa na
umri chini ya miaka 10, na chipukizi wachace.
Mary-Ann Prins, mwenye umri wa miaka 16, ni mwanafunzi bora zaidi wa Bi Esau, ambaye ana matumaini kwamba siku moja atafunza darasa hili.
“Napenda kuelewa lugha hii. Inanifanya kujihisi kuwa ndani yake, kwamba nimeshikamanishwa na babu wa mababu zangu. Naambiwa walikuwa wakiizungumza na leo naweza kuwa sehemu ya wanaoizungumza pia,” alisema huku akitabasamu.
N|uu sio lugha pekee barani Afrika ambayo imo katika hatari ya kuangamia nchini Afrika Kusini.
Masaa matatu kutoka hapa, katika mji wa Springbok, wazungumzaji
wa lugha inayojulikana kama Nama, wamekuwa wakiishinikiza serikali ya Afrika Kusini, wakitaka kabila lao litambuliwe rasmi nchini humo.
“Ni jambo la huzuni mno kwamba watoto wetu hawawezi kuzungumza Nama. Inanivunja moyo mno, kwamba watoto wetu hawawezi kuwasiliana na wazee wao kwa lugha yao ya kiasili,” anasema Maria Damara, 95, mmojawepo wa wazungumzaji wa lugha ya Nama hapa.
“Je Siku zijazo itakuwa vipi, ni nini kitakachofanyika na watoto wetu?”
Lugha kubwa sita zinazozungumzwa nchini Afrika Kusini: Zulu: Asilimia 22.7, Xhosa: Asilimia 16, Afrikaans: Asilimia13.5, Kiingereza: Asilimia 9.6, Setswana: Asilimia 8 na Sesotho: Asilimia 7.6
Kwa ujumla, Afrika Kusini ina lugha rasmi 11. Kiingereza ndio lugha inayozungumzwa kwa wingi kama lugha rasmi na lugha ya kibiashara.