MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
NADHARIA YA FONOLOJIA MIZANI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
NADHARIA YA FONOLOJIA MIZANI
#1
 Nadharia ya Fonolojia Mizani (FM)
Nadharia ya Fonolojia Mizani iliasisiwa na Liberman na Prince mwaka 1977. Katika kuchunguza ruwaza ya mkazo katika lugha Liberman (1975) aliibuka na pendekezo lake la shahada ya uzamivu ili kuitalii upya ruwaza ya mkazo katika lugha ya Kiingereza. Mwaka 1977 Liberman na Prince wakaunda nadharia yao ya ruwaza ya mkazo ijulikanayo kwa jina la nadharia ya Fonolojia Mizani.
 Liberman na Prince (1977) (kuanzia sasa LP) wanadai kuwa mkazo uko katika mfumo wa mfuatano wiani wa kimsonge ambao hupanga silabi, maneno na virai katika sentensi. LP wanabainisha uwakilishi wa mkazo katika lugha katika viwango vikuu viwili vya neno na tungo. Uwakilishi wao unatumia miti ya mizani katika jozi uwilikinzani kwa kuziwekea alama ama ya nguvu au hafifu kwa kila mwisho wa tawi. Hawakuishia hapo bali walitumia gridi ili kuonesha tofauti za nguvumsikiko kwa kila silabi zinazojenga neno au maneno yanayojenga tungo.
Haya ni mabadiliko yanayotokana na udhaifu uliojitokeza katika nadharia ya Fonolojia Zalishi. Vilevile ni tokeo la Goldsmith kufanikiwa katika kutatua tatizo la uwakilishi wa toni katika lugha zenye toni. Liberman na Prince waliona kuwa mkazo una tabia kama ya kipambasauti toni hivyo wakaamua kuuwakilisha katika rusu yake kwa kutumia miti ya mizani na gridi ili kuonesha mpishano wa msikiko na nguvumsikiko wa vipandesauti au viambajengo.
Nadharia hii ina misingi mikuu mitatu: msingi wa kwanza ni wa silabi ambao unaona kuwa silabi ni kiambajengo muhimu, ambapo LP wanaamini kuwa maneno ya lugha yoyote hupangika katika utaratibu wa silabi unaofuata utaratibu wa lugha maalumu. Msingi wa pili ni nguvumsikiko. Katika nadharia ya FM, uchanganuzi wa sauti umekitwa katika kigezo cha nguvumsikiko ambacho kinawezesha kutofautisha silabi zenye mkazo dhidi ya silabi zisizo na mkazo pamoja na kupambanua mpandoshuko wa mawimbi ya sauti wakati wa usemaji. Aidha, nadharia ya FM, huonesha mahali silabi inapoanzia na inapoishia (upeo na mpomoko wa silabi). Msingi wa tatu ni uhusiano wa ndani wa silabi ambao huoneshwa kwa kutumia matawi ya mizani (taz. Massamba 2011: 207).
Mbali na misingi hiyo, FM ina mihimili mikuu mitatu ambayo hubeba dhana ya nguvu na uhafifu. Mhimili wa kwanza ni mpangiliomsonge, ambapo vipengele vya kifonolojia huwakilishwa katika rusu zilizo katika uhusiano wa kimsonge, kwa kuanza na vipengele vikubwa zaidi kisha kumalizia na vipengele vidogo zaidi (taz. Massamba 2011:208). Uwakilishi huu unaonesha wazi uhusiano wa ndani wa vipengele vya kifonolojia. Kwa upande wa mkazo, uwakilishi huanza kwa viambajengo vikubwa ili kuona kiambajengo kipi kina nguvu na kipi ni hafifu na hatimaye, viambajengo vidogo katika mpangiliomsonge huo. Mhimili wa pili ni wa matumizi ya matawi. Nadharia ya FM hutumia rusu zinazopangika kimatawi, yanayoitwa matawi ya mizani yanayokuwa katika jozi uwilikinzani. Kila mwisho wa tawi huitwa kikonyo, matawi yanayoanzia katika kikonyo kimoja huishia kwenye sehemu mbili ambazo hujulikana kama vikonyo dada. Mhimili wa tatu ni wa uhusiano wiani wa matawi, katika mhimili huu
matawi ya kimizani huwa na uwiani wa kimsikiko ambapo tawi moja huwa na msikiko zaidi kuliko tawi lingine. Tawi linalokuwa na msikiko zaidi huwa na nguvu zaidi na hupewa alama ya N wakati lile lisilo na msikiko zaidi huwa hafifu na hupewa alama ya H (taz. Liberman & Prince 1977:257 na Massamba 2011: 209)
Misingi na mihimili hiyo tuliyoeleza hapo juu, ndiyo huongoza uchanganuzi wa mkazo katika FM. Kama tulivyokwishaeleza, msigano wa msikiko wa viambajengo katika mti wa mizani huoneshwa kwa kila kikonyo kupewa ama alama ya N (nguvu) yenye maana ya “ina nguvu kuliko”, au alama H (hafifu) yenye maana ya “ni hafifu kuliko” (taz. Massamba 2011: 210). Kwa mujibu wa LP, matawi ya mizani lazima yawe katika jozi ya uwilikinzani (taz. van der Hulst & Smith 1982:31, Hogg & McCully 1987:66 na Massamba 2010:234-235 & 2011:210-211). Hebu chunguza vielelezo vifuatavyo:
1 a) b) c) d) e) f)
N H N N H H N H H N
Kwa mujibu wa nadharia hii uchanganuzi ulio katika a) na f) ndio unaokubalika lakini uchanganuzi wa b) – e) haukubaliki kwa sababu b) na c) hakuna ukinzani, na katika d) na e) kuna tawi moja tu, hivyo unakinzana na utaratibu wa FM, kuwa sharti matawi yawe kwenye jozi.
Aidha, nadharia hii ina vipengele vya Silabi, Moti, Gridi, Egemeomkazo, na Kichwa ambavyo vitafafanuliwa hapa chini ili kuelewa dhima zake katika uchanganuzi wa mkazo.
Silabi ni kipengele muhimu katika FM kwa sababu huchukuliwa kuwa ni kiambajengo ambacho hujenga maneno ya lugha kwa kufuata utaratibu maalumu wa mfuatano wa sauti kulingana na lugha inayohusika (taz. Massamba 2011:206). Hivyo kiuchanganuzi, silabi zina nafasi kubwa kwa sababu mkazo huwekwa kwenye kilele cha silabi. Kwa sababu hiyo Liberman na Prince waliona ni kipengele muhimu sana katika uchanganuzi wa mkazo.
Moti ni kipengele muhimu katika FM ambacho kina dhima ya kutofautisha kategoria za maneno katika kuchukua mkazo. Neno ambalo lina sifa ya kileksika huwa linawekewa alama ya M (Moti), ikiwa na maana kwamba neno hilo lina sifa ya kubeba mkazo wenye nguvu, na neno lisilo la kileksika haliwekewi alama M ikiwa na maana kwamba neno hilo halina sifa ya kuchukua mkazo wenye nguvu katika mazingira yote linapotumika (taz. Liberman & Prince 1977:270, Hogg & McCully 1987:74-75 na Massamba 2011:230-231). Katika FM maneno yenye sifa ya kileksika katika lugha hupokea mkazo msingi lakini yale yasiyo ya kileksika hayapokei mkazo msingi.
Gridi ni kipengele kingine katika FM ambacho kinawakilisha muundo wa mabadiliko ya sauti. Katika uchanganuzi wa mkazo gridi hutumika kutofautisha nguvumsikiko kwa kubainisha
baina ya silabi yenye msikiko wa juu zaidi kuliko nyingine katika ngazi ya neno au neno kuliko maneno katika ngazi ya sentensi (taz. Selkirk 1984, Hogg & McCully 1987:130-132, Uhmann 1991:176, Kager 1996 na Massamba 2011:234). Hii ina maana kwamba silabi au neno lenye nguvumsikiko zaidi huwa na mhimili mrefu zaidi kuliko silabi au maneno mengine kiuwakilishi.
Egemeomkazo ni istilahi itumikayo kuelezea kizio cha mahadhi au lahani katika lugha ambazo silabi zake zenye mkazo hushuka na kupanda katika utaratibu unaofanana Crystal (1987) (taz. Massamba 2011:237). Naye Massamba (2011:237) anafasili egemeomkazo kuwa ni mfuatano wa viambajengo ambapo kile cha kushoto kabisa kina nguvu kimizani [+mkazo] na vile viambajengo vingine ni hafifu kimizani [-mkazo]. Kager (1996) anaeleza kuwa egemeomkazo linaweza kuwa kulia au kushoto kutokana na ruwaza ya mkazo mkuu/ msingi katika lugha inayohusika.
Hivyo, istilahi egemeomkazo inaweza kufasiliwa kama ni mfuatano wa viambajengo ambapo ama kile cha kushoto au cha kulia kabisa kina nguvu kimizani [+mkazo] na viambajengo vingine ni hafifu kimizani [-mkazo]. Hii ina maana kwamba mkazo mkuu unaoangukia kushoto unaruhusu viambajengo vya kushoto kuwa na nguvu kuliko vya kulia, na ule unaoangukia kulia unaruhusu viambajengo vya kulia kuwa na nguvu kuliko vya kushoto katika neno au tungo. Egemeomkazo hutusaidia kujua ruwaza ya mkazo kama imefungwa na silabi za kushoto au kulia mwa neno katika lugha inayohusika (taz. Masuba 2013:16).
Kichwa cha mizani kwa mujibu wa Liberman na Prince ni kipashio kinachomiliki mkazo wenye nguvu (N) peke yake, na ndicho chenye msikiko mkubwa zaidi katika tungo nzima. Kipashio hiki kinaitwa Kipengele chenye Hadhi Kuu (KHK) (taz. Liberman & Prince 1977:259, Hogg & McCully 1987:70, na Massamba 2011:226). Kichwa cha mizani katika uchanganuzi wa mkazo kinatumika kubainisha kiambajengo chenye mkazo msingi na msikiko mkubwa zaidi kuliko viambajengo vingine katika tungo au neno.
Sanjari na hilo, FM inachunguza pia uziadamizani ambapo inatazama viambajengo kuwa viko katika mpangilio wa kimsonge na mizani pia imejengwa kimsonge, kwa mantiki hiyo kila kiambajengo kina nguvumsikiko kwa kiasi fulani ingawa baadhi ya viambajengo vingine havitazamwi kimizani (taz. Hayes 1981).
Licha ya FVH na FM kukidhi mahitaji ya kiuchanganuzi bado nadharia zimeendelea kuibuka kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi katika uchanganuzi wa vipengele vya kifonolojia. Kutoka mwaka 1977 ilipoundwa FM, mwaka 1993 ikaundwa nadharia nyingine ya Umbo Upeo ya Prince na Smolensky. Tutaieleza katika kipengele kinachofuata.
  1. Nadharia ya Umbo Upeo (UU)
Nadhari ya Umbo upeo ilianzishwa na Prince na Smolensky mwaka (1993) kwa lengo la kuchanganulia vipengele vya kifonolojia. Lengo la nadharia hii ilikuwa ni kuboresha zaidi
nadharia ya FZ. Prince na Smolensky (kuanzia sasa PS) wanajaribu kuonesha uhusiano uliopo baina ya umbo la ndani na umbo la nje kwa kuboresha zaidi mtazamo wa CH ambao unaeleza kuwepo kwa umbo la ndani na umbo la nje. Mbali na hilo, wanaonesha ukokotozi wa umbo la nje kutoka umbo la ndani.
PS katika nadharia ya UU wanadai kuwa FZ ina kanuni nyingi sana ambazo hutumika katika ukokotozi wa umbo la nje kutoka umbo la ndani. PS walifikia uamuzi wa kuunda nadharia ya UU kutokana na udhahania uliokithiri katika nadharia ya FZ ambao ulielezwa na watangulizi wao kama Kiparsky 1968, Campbell 1974, McCawley 1974, Kenstowics na Kisseberth 1977 na Mathew 1982 (taz. Massamba 2011:244).
Wataalamu hawa wanadai kuwa umbo la ndani linatakiwa lisitofautiane sana na umbo la nje, hivyo waliona kuna haja ya kupata nadharia itakayoondoa kabisa au kuupunguza udhahania uliokithiri ulioletwa na CH katika nadharia yao ya FZ.
Mwaka 1993, PS waliamua kuunda nadharia ya Umbo Upeo, iliyoshadidiwa na McCarthy mwaka huohuo 1993. Nadharia ya UU inashughulikia kanuni za kimajumui katika lugha, uanishaji wa lugha kiisimu na upataji lugha sawa na nadharia ya FZ. Aidha, UU inachukulia kuwa lugha zote duniani zina maumbo mawili ya kifonolojia kwa maana ya umbo la ndani na umbo la nje. Nadharia ya UU inakosoa nadharia ya FZ katika ufasili wa dhana ya umbo la ndani na umbo la nje (taz. Massamba 2011:245). Nadharia ya UU inachukulia umbo la ndani kama ni maumboghafi ambayo yanaweza kuzalishwa bila ukomo wakati umbo la nje linachukuliwa kuwa ni umbotokeo ambapo hupatikana kutokana na mikinzano kati ya mashartizuizi ya lugha inayohusika.
Nadharia ya UU inaongozwa na misingi mikuu mitatu na mihimili minne. Katika ufafanuzi wetu tutaanza na misingi yake ambayo ni Zalishi (ZALI), Masharti-Zuizi (MASHA–ZU) na Tathimini (TATHI) kisha tutafuata mihimili yake.
Msingi wa kwanza wa nadharia ya UU ni ZALI (Zalishi) ambao unahusika na uzalishaji wa maumbotokeo mbalimbali yasiyo na ukomo katika lugha, ambayo huitwa maumboshindani. Kupitia maumboshindani hayo ndipo hupatikana umbo linalofikia upeo wa ukubalifu kulingana na mashartizuizi ya lugha inayohusika. Kimsingi umbo linalofikia ukomo linaweza kuvunja mashartizuizi yenye hadhi ya chini na yanayovumilika na lisivunje mashartizuizi makubwa yenye hadhi ya juu (taz. Massamba 2011:249).
Msingi wa pili ni wa MASHA–ZU (mashartizuizi) ambao unahusika na uwekaji wa vigezo na masharti kwa kila lugha ambayo huweza kuvunjwa na yale yasiyoweza kuvunjwa. Vigezo na masharti hayo ndivyo huamua ni umbo lipi linalofikia upeo wa ukubalifu. MASHA–ZU hushughulikia maumbotokeo ambayo huwekewa mashartizuizi ya hadhi ya juu na hadhi ya chini ambayo kwayo umbo moja hushinda na kufikia upeo wa ukubalifu (taz. Massamba 2011:250).
Msingi wa tatu ni TATHI (tathimini) ambao hufanya maamuzi juu ya umbo lipi kati ya maumboshindani limefikia upeo wa ukubalifu kwa kuzingatia memba yupi ambaye hakuvunja mashartizuizi ya hadhi ya juu yasiyotakiwa kuvunjwa. TATHI humchukulia memba ambaye hakuvunja mashartizuizi ya hadhi ya juu kuwa ni mshindi na ni umbo lililofikia upeo wa ukubalifu kulingana na mashartizuizi ya lugha inayohusika.
Kwa upande mwingine nadharia ya UU ina mihimili minne. Mhimili wa kwanza ni wa Umajumui ambao unajielekeza katika isimu ya lugha asilia za binadamu. Mhimili huu unadai kuwa lugha zote za binadamu zina sifa za kimajumui hivyo lugha zote za binadamu zina seti ya MASHA–ZU ya kimajumui kwa mujibu wa UU.
Mhimili wa pili ni wa ukiukwaji, katika mhimili huu MASHA–ZU ya kimajumui huweza kufuatwa au yakakiukwa kutegemea lugha inayohusika kutokana na MASHA–ZU kutofautiana kutoka lugha moja hadi lugha nyingine. Hii ina maana kwamba viwango vya MASHA–ZU hutofautiana kutoka lugha moja hadi lugha nyingine, sharti moja linaweza kuwa la kiwango cha juu katika lugha moja lakini sharti hilohilo likawa na kiwango cha chini katika lugha nyingine. Hivyo maumbo upeo hushinda kwa kukiuka MASHA–ZU ya kiwango cha chini (taz. Massamba 2011:251).
Mhimili wa tatu ni wa upangiliaji wa MASHA–ZU, ambapo mashartizuizi yote yanapangiliwa katika mpangiliomsonge unaofuata nguvu na uhafifu wa masharti hayo. Katika nadharia ya UU masharti na vigezo yanapangiliwa yapi yana hadhi ya juu zaidi na yapi yana uhafifu zaidi. Kutokana na mpangilio huo, kuna masharti ambayo hayatakiwi kuvunjwa na umbo upeo na yale yanayovumilika kuvunjwa kulingana na lugha inayohusika. Hapa Massamba (2011) anasisitiza kuwa ni muhimu sana kuwa na data toshelevu ya lugha inayoshughulikiwa ili kujua mashartizuizi yapi yana nguvu zaidi kuliko mengine katika lugha hiyo.
Mhimili wa nne ni wa usambamba ambao unahusu utoshelevu wa mpangilio wa mashartizuizi. Mhimili huu unatazama seti nzima ya maumbotokeo jinsi inavyojidhirisha katika mpangilio wote kwa ujumla wake kulingana na mpangilio wa MASHA-ZU .
Baada ya kueleza nadharia ya UU sehemu inayofuata tutajadili nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru ya Mkazo. Nadharia iliyoibuka wakati mmoja na nadharia ya UU.
  1. Nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru ya Mkazo (FVHM)
Kama tulivyokwishaeleza hapo awali (taz.§ 5.1) kwamba kumekuwa na mapinduzi ya mara kwa mara katika nadharia za kuchanganulia vipengele vya kifonolojia tangu miaka ya 1960, ambapo tangu miaka hiyo kumekuwa na nadharia mbalimbali lakini nadharia zote zikitafuta namna ya kutatua suala la udhahania.
Nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru ya Mkazo ni miongoni mwa nadharia zinazojaribu kuleta mapinduzi katika uchanganuzi wa kipambasauti mkazo. Nadharia hii
iliundwa na Hagberg mwaka 1993 ikikosoa nadharia ya Fonolojia Mizani ya 1977. Nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru ya Mkazo (kuanzia sasa FVHM) iliazimia kufanya mabadiliko kuhusu dhana zinazohusiana na mkazo ambazo ni kichwa cha mizani na maegemeomkazo katika ruwaza ya mkazo.
Nadharia imejengwa katika hoja kuu mbili: hoja ya kwanza inadai kuwa kichwa cha mizani ni uziadabileshi hivyo hakitakiwi kihusishwe kwenye nadharia ya mkazo na badala yake mkazo na sifa zake ndizo zihusishwe kwenye nadharia ambayo itajumuisha kichwa cha mizani.
Hoja ya pili inadai kuwa mkazo na maegemeomkazo ni vitu viwili tofauti ambavyo vinapaswa kutofautishwa. Hagberg anasema:
(i) Maegemeomkazo yanaweza kuwepo bila ya kuhusisha mkazo
(ii) Mkazo unaweza kuwepo bila kuhusisha maegemeomkazo
Ingawa Hagberg anakubaliana na Goldsmith (1976) na LP (1977) kuwa mkazo na toni ni vipambasauti huru katika lugha lakini bado anatofautiana nao kwa kudai kuwa maegemeomkazo yote hayana vichwa kwa asili hivyo huweza kuingia katika sifa yoyote ile ya kipambasauti.
Nadharia ya FVHM ina misingi mikuu mitatu: msingi wa kwanza ni kwamba maegemeomkazo yote hayafungamani na mkazo hivyo hujitegemea. Msingi wa pili unadai kuwa nadharia ya mkazo inahusisha mkazo na sifa zake ambamo ndani yake kuna kichwa cha mizani.
Msingi wa tatu unadai kuwa mkazo umejengwa katika mora, hapa ni kwamba mkazo umekitwa katika mora ambapo mkazo huo huwekwa halikadhalika maegemeomkazo na vichwa vya mizani huwekwa katika mora. Mbali na hilo matumizi ya alama ya nyota hutumika ili kujenga maegemeomkazo. Hebu tazama mfano ufuatao hapa chini kutoka kwa Hayes (1989) katika uchanganuzi wa mkazo.
2 Umboghafi: uundaji wa maegemeomkazo sheria mwisho: umbotokeo:
μ μμ μ μ (μμ) μ μ (μμ) μ
qa mal ti qa mal ti qa mal ti qamálti
(Chanzo cha data : Hagberg 1993:15)
Mbali na misingi hiyo nadharia ya FVHM ina mihimili mikuu miwili: Mhimili wa kwanza ni kwamba sifa za mkazo na mkazo wenyewe huangukia katikati ya vikonyo vya silabi. Mhimili wa pili ni mora kwamba katika silabi si mwanzo silabi wala mwisho silabi kinachozingatiwa ni mora, kwa maana ya wakaa utumikao katika utamkaji wa irabu inayohusika.
Hagberg anachanganua mkazo na maegemeomkazo kwa kutumia nadharia ya FVHM bila kuweka alama ya mora ingawa anajikita katika msingi wa kimora. Hebu chunguza mfano ufuatao hapa chini:
3 umboghafi uziadamizani uundaji wa egemeomkazo mkazo neno umbotokeo
Vasington vasing <ton> vasing <ton> vasing<ton> vasiˈngton
Katika mfano 10 huo hapo juu inaonesha kuwa mkazo uko katika silabi ya mwisho kasoro moja pamoja na egemeomkazo limejengwa katika silabi ya mwisho kasoro moja. Katika umboghafi kuna nusu pigo la kimahadhi kwa silabi zote. Katika uziadamizani silabi mbili tu zina pigo la kimahadhi, katika kipengele cha uundaji wa egemeomkazo silabi ya mwisho kasoro moja ina mapigo mawili ya kimahadhi. Katika sehemu ya mkazo wa neno silabi ya mwisho kasoro moja ina mapigo matatu ya kimahadhi kubainisha kuwa hiyo ndiyo silabi yenye mkazo mkuu. Kwa mujibu wa FVHM mkazo unatakiwa kuchanganuliwa kwa namna hiyo.
Nadharia hazijaishia hapo bado zimeendelea kuibuka zikiwa na lengo la kufanya mabadiliko zaidi katika uchanganuzi wa vipengele vya kifonolojia. Kuna nadharia ya Mawanda Upeo ambayo inakaribiana sana na nadharia ya UU kiuchanganuzi sanjari na FVH. Nadharia hii tutaileza zaidi katika kipengele kinachofuata.
  1. Nadharia ya Mawanda Upeo (MU)
Nadharia ya Mawanda Upeo (kuanzia sasa MU) ya Cassimjee na Kisseberth (1998) ilianzishwa ikiwa na lengo la kuboresha zaidi nadharia ya UU, kwa sababu inakubaliana na nadharia ya UU kuhusu kuwepo kwa umboghafi na umbotokeo. Cassimjee na Kisseberth (kuanzia sasa CK) wanadai kuwa nadharia ya MU inachukulia kuwa vitamkwa mbalimbali vya lugha hupangika kimawanda / kisilabi pamoja na sifa za vitamkwa hivyo pia, hupangika kimawanda (mawanda–sifa).
Nadharia ya MU inachukulia kuwa kitamkwa chenye sifa mahususi katika umboghafi lazima sifa hiyo idhihirike pia katika umbotokeo ili kitamkwa hicho kionekane kinafadhili sifa fulani na kuwa na mamlaka, ingawa sifa hizo huweza pia kuvuka mipaka (taz. Cassimjee & Kisseberth 1998: 40 Massamba 2011:266 na Masuba 2013:12). Hii ina maana kwamba sifa fulani ya kitamkwa inaweza kujitokeza katika kitamkwa kingine ama mahali pa matamshi au jinsi ya matamshi, na kuvifanya vitamkwa hivyo vitamkwe kwa sifa inayofanana, kwa mfano sifa ya unazali kutokana na usilimishaji huvuka mipaka katika utamkaji wa vitamkwa vinavyoandamana navyo.
Aidha, nadharia ya MU inatumia masharti makuu manne ambayo ni: mosi Mawanda ya Ulinganifu (MAU), sharti hili linasema kuwa ni lazima kuwepo na ulinganifu baina ya sifa za umboghafi na umbotokeo. Hii ina maana kwamba sifa yoyote iliyoko katika umboghafi lazima iwemo au ijitokeze katika umbo la nje ambalo ndilo umbotokeo.
Sharti la pili ni Muungano wa S(ifa) inayofadhili (MUSIFA), sharti hili linadai kuwa kila sifa-fadhili iko ndani ya mawanda ingawa inawezekana kusiwepo na uhusiano baina ya sifa–fadhili katika umboghafi la kitamkwa bali ikajidhirisha katika umbotokeo ili kulinda uadilifu wa lugha. Sharti hili linadai kuwa uadilifu wa lugha unaweza kuwa sifa inayofadhili isiwemo katika umboghafi lakini ikaonekana katika umbotokeo kwa mfano toni katika maneno yasiyo na viinitoni.
Sharti la tatu ni Upekee wa sifa-Fadhili (USIFA), hii ina maana kwamba, kuna sifa moja tu inayofadhili katika mawanda ya sifa kwenye mawanda ya vitamkwa ambapo mshindani wa kwanza katika maumbotokeo huchukuliwa kuwa ndiye mwenye uadilifu zaidi kuliko mshindani wa mwisho iwapo mshindani huyo anakidhi masharti ya MAU na MUSIFA.
Sharti la nne ni Sifa-Dhahiri (SIDHA) ambalo linasema kuwa kila elementi katika mawanda sifa inaweza kuelezwa kwa sifa fulani ambayo ni halisi. Hii ina maana kuwa sifa hiyo ielezwe kiuhalisia kama ipo kwa kitamkwa fulani.
Kwa ujumla hizi ni miongoni mwa nadharia ambazo zimeshika hatamu katika uchanganuzi wa vipengele vya kifonolojia.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)