09-09-2021, 08:00 AM (This post was last modified: 09-09-2021, 08:00 AM by MwlMaeda.)
Leo hii mbalamwezi ya Kiswahili inaangazia historia ya iliyokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki) ambayo sasa inaitwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
MBALAMWEZI ya Kiswahili imekuwa ikipokea maoni mengi kutoka kwa wapenzi wa Kiswahili kuhusiana na mada mbalimbali zinazojadiliwa katika safu hii.
Nyote mnapongezwa kwa maoni yenu na kuonyesha mapenzi makubwa ya lugha ya Kiswahili. Mnapokuwa na maoni na maswali msisite kuyatoa kwani safu hii ipo kwa ajili yenu.
Leo hii mbalamwezi ya Kiswahili inaangazia historia ya iliyokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki) ambayo sasa inaitwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Lengo la kufanya hivi ni kutoa ufafanuzi mintarafu Tuki na Tataki kwa wasomaji wakiwamo walimu, wanafunzi wa shule za sekondari walioomba maelezo kuhusu matumizi ya majina haya ambapo wengine huchukulia kuwa ni taasisi mbili tofauti.
Awali ya yote ifahamike kwamba taasisi hii ni moja na siyo mbili tofauti.
Historia ya Tataki ilianza mwaka 1930 kwa iliyokuwa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki. Kamati hii ilikuwa na majikumu kadhaa miongoni mwake ni kusanifisha Kiswahili kinachotumika katika shughuli rasmi katika Afrika Mashariki.
Pia kusimamia maendeleo ya lugha hii; kusoma miswada; kusahihisha na kutoa ithibati; kuteua vitabu vya kutumika shuleni; kutafsiri vitabu vya lugha za kigeni kwa Kiswahili; kufanya utafiti katika nyanja za sarufi na fasihi; kuchapisha na kusambaza matokeo ya utafiti unaofanywa.
Mwaka 1961 UDSM ilipoanzishwa kama Chuo Kikuu Kishiriki cha London Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ilihamishiwa katika Chuo Kikuu cha Makerere , Uganda.
Ilipofika mwaka 1964 kamati ilibadilisha jina na kuitwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).
Jina hili limegonga masikio ya wengi na kuganda akilini kutokana na huduma zake.
Majukumu
Aidha, Taasisi hii imekuwa na majukumu mengi ambayo ilikuwa inayatekeleza kama vile kuratibu msamiati, kuunda istilahi mpya za kitaaluma, kufanya utafiti katika nyanja za mofolojia, sintaksia, fonolojia, isimu jamii na dialektolojia; kuratibu na kutafsiri matini za Serikali, viwanda na taasisi binafsi ndani na nje ya nchi.
Kwa nini Tataki?
Akizindua Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) Juni 2009 aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilipongeza Baraza la Chuo kwa kusimamia vyema mpango mkakati wa mageuzi ya chuo ambao ulihusisha kuunganisha idara anuwai chuoni hapo kwa lengo la kupanua wigo na kuongeza ubora katika ufundishaji, utafiti na utoaji huduma kwa jamii.
Hivyo, kutokana na mpango mkakati uliowekwa na chuo hicho kwa lengo la kustawisha huduma, iliyokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki) na iliyokuwa Idara ya Kiswahili chini ya Kitivo cha Fani za Sayansi za Jamii ziliungana na kuwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki).
Tangu mwaka huo Tataki imekuwa ikidahili wanachuo wa shahada za awali na umahiri kufundisha na kufanya utafiti. Mwaka 2014 taasisi ilianzisha programu ya shahada ya uzamivu kwa tamrihi na tasnifu.
Wafuatao ni wakurugenzi wa Tuki/Tataki tangu kuanzishwa kwake: G. Mhina (1970 – 1976), A.M. Khamisi (1976 – 1982), C.W. Temu (1982 – 1985), D.P. Massamba (1985 – 1991), S.Y. Sengo (1991 – 1994).
Wengine ni S.A.K. Mlacha 1994 – 2000), M.M. Mulokozi (2000 2006) J. G. Kiango, (2006 – 2009), A.K. Mutembei (2009 – 2013), Murugenzi wa sasa E.S. Mosha 2013 hadi sasa).