MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MIAKA YA MWANZO YA USANIFISHAJI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MIAKA YA MWANZO YA USANIFISHAJI
#1
MIAKA YA MWANZO YA USANIFISHAJI
3.1 Kabla ya vita
Kipindi cha kuanzia 1930 hadi 1938 kilikuwa muhimu sana kwa historia ya usanifishaji wa Kiswahili.
Katika kipindi hicho, msingi imara sana uliwekwa na kukaanzishwa kiwango cha juu cha kufanya kazi. Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilihitaji msingi imara hivyo ili kuiwezesha kufanya kazi wakati wa vita. Sifa nyingi za mafanikio ya Kamati zatokana na kazi nyingi na ya kuchosha iliyofanywa na Frederick Johnson aliyekuwa katibu wa kwanza wa Kamati hiyo. Mbali na kutafsiri vitabu vingi, Johnson alifanya kazi nyingi ya kutunga kamusi za Kiswahili-Kiswahili, Kiswahili-Kiingereza na Kiingereza-Kiswahili.
Nitaanza sehemu hii kwa kujadili hali nzuri ya wakati huo iliyoisadia kamati kufanikiwa. Hasa sera ya lugha ya nchi za Afrika Mashariki wakati huo, iliwataka maafisa waliozifanyia kazi nchi hizo, wapite mitihani ya lazima ya Kiswahili. Kisha tutaijadili kazi yenyewe ambayo Kamati ilikuwa ikifanya.
Serikali zote za Afrika Mashariki, Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar ziliunga mkono Kamati kwa kuwa zote ziliwakilishwa katika Kamati. Sera ya lugha za nchi zote zilikisaidia Kiswahili kama tutakavyo- endelea kufafanua. Wafanyakazi Wazungu wa nchi hizi zote ilibidi wajifunze Kiswahili na waipite mitihani. Walioshindwa kufauli mitihani hiyo walibaki kuwa wafanyakazi wa muda wala si wa kudumu. Kwa hivyo iliwabidi maafisa wa serikali Wazungu wajifunze Kiswahili. lli kupandi- shwa cheo kazini iliwabidi wapite mitihani ya juu ya Kiswahili. Sera hii ilikipa Kiswahili hadhi. Mitihani hiyo ya Kiswahili ilisababisha mahitaji ya kuchapisha vitabu vitakavyowasaidia maafisa hao kujitayarisha kufanya mitihani hiyo. Pia vitabu hivyo vilinunuliwa kwa wingi kwa kuwa maafisa hao walitamani kupita mitihani ili wazihifadhi kazi zao. Kwa hivyo mitihani hiyo ilisaidia kukuza na kueneza Kiswahili pamoja na kuongeza idadi ya vitabu vilivyochapishwa wakati huo.
Sasa tutajadili vile sera ya lugha ilivyokuwa katika kila nchi.
Nchini Kenya, kulingana na barua ya Katibu Mkuu namba 40 ya Juni, 1, 1931, mbali na mitihani ya Wazungu waliokuwa wafanyakazi wa Jeshi la King’s African Rifles ambayo ilikuwa na maagizo yake tofauti, maafisa wengine wote Wazungu waliokuwa wakifanya kazi katika Koloni iliwabidi wafanye mitihani ifuatayo ambayo ilikuwa ya lazima.
Mtihani uliotangulia ulikuwa, mtihani wa kwanza wa mahojiano kwa Kiswahili ambao ilibidi ufanywe kabla ya mwaka mmoja kwisha tangu kuajiriwa kwa kazi isiyokuwa ya kibarua. Iwapo afisa aliyehusika hangepita mtihani huo ilimaanisha kwamba hangepata nyongeza ya mshahara ya kila mwaka na pia ingesababisha kushushwa cheo na kuwa mfanyakazi wa kibarua. Kiwango cha Kiswahili kilichohitajika ni cha kumwezesha afisa huyo kufanya kazi kwa kutumia Kiswahili pasipo mahitaji ya mkalimani.
Mtihani wa pili ulikuwa wa Kiswahili sanifu kiwango cha chini. Mtihani huu ulitahiniwa baada ya mwaka mmoja kwisha na kabla ya miaka miwili na nusu kwisha tangu afisa aajiriwe. Wale ambao hawakupita mtihani huo walichukuliwa hatua sawa na wale ambao hawakupita mtihani wa kwanza. Ili mtu aweze kupita mtihani huo ilibidi awe amefikia kiwango cha kuelewa na kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha na ujasiri.
Mtihani wa Kiswahili sanifu kiwango cha juu ndio uliokuwa wa tatu na wa juu sana kati ya hiyo mitihani ya lazima. Mtihani huo ulikuwa wa mahojiano pamoja na wa kuandika. Ulikuwa wa Wazungu wenye vyeo vikubwa na ulifanywa baada ya miaka mitatu na kabla miaka kumi haijakwisha tangu waajiriwe. Kukosa kupita mtihani huo kwa muda uliowekwa kuliathiri cheo cha afisa aliyehusika na kumaanisha kwamba hangeendelea kupewa nyongeza za mshahara. Ili mtu aweze kupita mtihani huo ilibidi aijue vizuri sarufi ya Kiswahili na aweze kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha.
Maagizo yaliyoihusu Uganda yapatikana katika tangazo la barua namba 40 ya Disemba 29, 1928 kutoka afisini mwa Katibu Mkuu. Maagizo hayo ni sawa na ya Kenya isipokuwa kwamba kuna tofauti chache nitakazoeleza. Kuhusu mtihani wa kiwango cha kwanza wa mahojiano, maafisa waliokuwa wakifanya kazi Buganda, waliruhusiwa kufanya mtihani wa Kiluganda kwa kiwango hicho, lakini maafisa waliokuwa wakifanya kazi katika sehemu zingine za Uganda ilibidi wafanye mtihani wa Kiswahili.
Maafisa waliokuwa wakifanya kazi katika tawala za mikoa na wa Idara ya Elimu ilibidi wapite mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla hawajathibitishwa kazini. Maafisa wengine wote wangethibitishwa kabla hawajapita mtihani huo, lakini baada ya kufanya kazi kwa muda wa miaka minne hawangepata tena nyongeza ya mshahara mpaka kwanza wapite mtihani huo.
Mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha juu nchini Uganda ulikuwa ukifanywa na maafisa wa tawala za mikoa, na idara za elimu, kilimo, mifugo, misitu na polisi. Maafisa wote wa idara hizi ilibidi wapite mtihani huo, la sivyo, mshahara wao haungezidi pauni 720. Nchini Uganda, maafisa wa serikali wangefanya mitihani ya kiwango cha chini na cha juu ya lugaha zingine za Uganda badala ya Kiswahili.
Nchini Zanzibar, dondoo kutoka maagizo ya serikali ya Zanzibar yanaeleza kwamba ni lazima maafisa wote wa Kizungu wapite mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla mwaka mmoja haujakwisha tangu waingie nchini. Wale ambao hawangepita mtihani huo ama hawangeendelea kuwa waajiriwa wa kudumu au hawangepata nyongeza ya mshahara ya kila mwaka. Wauguzi ambao hawangepita mtihani huo, ingebidi wasimamishwe kazi.
Wale waliokuwa wakifanya mtihani wa Kiswahili sanifu kiwango cha juu walikuwa maafisa Wazungu ambao walikuwa wafanyakazi wa kudumu. Baada ya kupita mtihani huo walipewa kiinua mgongo cha pauni hamsini (50). Mbali ya huu mtihani wa Kiswahili kiwango cha juu maafisa Wazungu wa Zanzibar walikuwa huru kufanya mtihani wa Kiarabu au Kigujerati wa kiwango hicho. Watahiniwa wa mtihani wa kiwango cha juu wa Kiswahili, Kiarabu au Kigujerati ilibidi waweke amana ya rupia arobaini na tano (45), pesa ambazo wangerudishwa wapitapo mtihani.
Maagizo yaliyoihusu Tanganyika yapatikana katika ‘Maagizo kwa watu wote kutoka Afisi ya Katibu Mkuu, Dar es Salaam, Juni 15, 1931’. Kulingana na Maagizo hayo ilibidi maafisa wa Kizungu wapite mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla mwaka mmoja haujakwisha tangu waajiriwe nchini. Wale ambao hawangepita mtihani huo hawa- ngeendelea kuwa waajiriwa wa kudumu.
Mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha juu ulikuwa ukitahini ujuzi kamili wa Kiswahili, sarufi na muundo wa lugha kwa jumla. Watahiniwa waliofaulu walitakikana waweze kueleza maagizo, sheria na kanuni za serikali vizuri kwa Kiswahili. Pia walitakikana waweze kutafsiri kwa ufasaha maandishi ya Kiswahili kwa Kiingereza na ya Kiingereza kwa Kiswahili.
Maagizo haya yote yaonyesha wazi kwamba sera ya lugha katika Afrika Mashariki wakati wa ukoloni ilikiunga Kiswahili mkono hasa wakati huo wa siku za mwanzo za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Sera hiyo ilikusudiwa kuwawezesha Wazungu kuwaelewa Waafrika wanapofanya kazi zao. Sera hii iliwaridhisha wanakamati ambao walijivunia kazi zao kwa kuona kwamba zilitambuliwa na serikali. Juhudi za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki hazikuzinufaisha shule tu, bali ziliwafaidi maafisa wa Kizungu ambao ilibidi wajitayarishe kufanya mitihani hiyo ya lazima. Ufafanuzi huu unatusaidia kuelewa ni sababu gani iliyowafanya wanakamati wawe na moyo thabiti wa kufanya kazi nyingi ngumu ya kusanifisha Kiswahili kwa kujitolea.
Sasa tutaigeukia “warsha” ili tuone machache kati ya mambo muhimu yaliyokuwa yakifanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kabla ya vita vya pili vya dunia.
Kwa kifupi kazi nyingi na ngumu ilifanywa na maafisa wa serikali na misheni kutoka Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar waliojitolea kusanifisha Kiswahili. Hawakuwa na vitabu vya kutosha vya Kiswahili ambavyo wangetegemea kuwasaidia katika kazi zao. Mjadala mfupi unaofuata watokana na Jarida la Kamati – ILC Bulletin Na. 1 ya 1930. Waonyesha baadhi ya matatizo yaliyoikumba Kamati.
Kabla ya kufikia uamuzi kuhusu msamiati sanifu, orodha za maneno zilipelekewa wahariri wa Kamati pamoja na kuchapishwa kwenye Jarida la ILC Bulletin ili kuwapa wahariri pamoja na raia nafasi ya kuyajadili.
Maoni na mapendekezo tofauti yalijadiliwa na Kamati kabla orodha iliyokubaliwa haijachapishwa kama msamiati sanifu. Maoni na mapende- kezo yaliyotolewa na wahariri kabla uamuzi haujafikiwa yalitofautiana sana kama inavyodhihirishwa hapa chini.
Kasisi B. J. Ratcliffe, mhariri wa Kenya, anapendekeza kwamba ‘irabu’ na ‘herufi’ zitumiwe badala ya kuazima ‘vokali’ na ‘konsonanti’ kutoka Kiingere- za. ‘Herufi’ ilipendekezwa badala ya ‘harufu’ ambalo lilikuwa likitumiwa kwa wingi na Waswahili wa Mombasa ili kulitofautisha na neno harufu la kawaida.
Naye katibu wa Kamati, Frederick Johnson anashuku iwapo neno irabu latumiwa na watu wengi au latumiwa na Waswahili wachache wanaoandika kwa kutumia hati za Kiarabu. Kwa maoni ya Johnson neno herufi au harufu lilimaanisha hati yoyote ya maandishi iwe vokali au konsonanti. Kisha anafikia uamuzi kwamba neno lenye kumaanisha konsonanti lilikuwa lahitajika. Hivyo ndivyo neno konsonanti lilivyoazimwa. Mengi kati ya maneno tunayoyaona kuwa ya kawaida siku hizi, ilibidi yatolewe uamuzi. Mfano mmoja ni neno shule. Kasisi A. B. Hellier, mhariri wa Tanganyika alipendekeza neno shule lililoazimwa kutoka Kijerumani badala ya neno skuli lililoazimwa kutoka lugha ya Kiingereza.
Naye Canon Broomfield alikuwa na maoni kwamba maneno yote mawili yangetumiwa kumaanisha vituo tofauti vya elimu. Broomfield aliyekuwa mhariri wa Zanzibar alipendekeza neno skuli litumiwe kumaanisha vituo na vyuo vya kufunzia walimu nalo neno shule limaanishe shule za vijijini tu.
Maoni yalitofautiana sana hivi kwamba inashangaza iliwezekanaje kamati ikaweza kutimiza mambo mengi hivyo. Tukitazama mifano ya maneno lindi na kina, twaona kwamba wahariri wote wanne walikuwa na maoni tofauti.
Bwana Morris, mhariri wa Uganda alipendekeza kwamba neno lindi litumiwe badala ya kina. Kasisi Ratcliffe wa Kenya alisema kwamba neno sahihi ingekuwa kwina wala si kina. Canon Broomfield kutoka Zanzibar alisema kwamba neno kimo lilitumiwa kumaanisha urefu wa kwenda juu na wa kwenda chini, na kwamba neno kina lilikuwa halijulikani Zanzibar.
Naye Kasisi Hellier alijaribu kutoa suluhisho kwa kusema kwamba “tukitumia kimo kumaanisha kwenda juu na kina kumaanisha kwenda chini tutakuwa tumepiga hatua mbele” (ILC Bulletin Na. 1 1930: 5).
Baada ya kusoma aya za hapo juu mtu anaweza kushawishiwa kushuku ujuzi wa kamati na wahariri wake. Maoni kama hayo yangekuwa ya haraka na yasiyo ya kweli kwa sababu watu hao walikuwa wakishughulikia karibu kila kitu, kuanzia maneno ya kawaida ya kila siku ambayo yalihitajika hadi sarufi ya Kiswahili. Wewe unayesoma kitabu hiki, jihisi u mmoja kati ya wanakamati, naye Kasisi A. B. Hillier anakufahamisha kama alivyoifahamisha Kamati kwamba:
“Sarafu za senti hamsini, senti kumi, na senti tano kwa sasa hazina majina. Ni muhimu zipewe majina ya kutumiwa shuleni na ya kutumiwa na umma.” (ILC Bulletin Na. 1, 1930: 10).
Je, kama mwanakamati ungetoa mapendekezo gani, hasa unapojua kwamba baadhi ya wasemaji wa Kiswahili walikuwa wakitumia maneno mengi kama vile “peni la senti kumi” na “peni la senti tano”? Maneno nusu shilingi kumaanisha senti hamsini, peni kumaanisha senti kumi na nusu peni kumaanisha senti tano yalikuwa ni afadhali kuliko deka na pente kutoka Kigiriki na ashara na hamsa kutoka Kiarabu ambayo yalipendeke- zwa kumaanisha senti kumi na senti tano.
Maelezo ya hapo juu yanaonyesha baadhi ya shida zilizowakumba wasanifishaji wa Kiswahili mapema katika shughuli za usanifishaji. Kufanikiwa kwao kulitokana na jitihada za pamoja za misheni wa madhehebu mbalimbali pamoja na msaada na ushirikiano wa serikali za kikoloni za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar.
Mashauriano mengine mengi kama hayo yaliyojadiliwa hapo juu yalifanywa na matokeo yake yalikuwa ni kusanifishwa kwa maneno mengi ya Kiswahili. Kamati ilitoa orodha za maneno ya Kiswahili, ikayajadili, kisha ikachapisha yale yaliyokubaliwa kama Kiswahili sanifu. Katika jarida la ILC Bulletin Na. 9 la Oktoba 1935, Kamati inajadili orodha ya maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kibantu na kutoa maelezo ya chanzo chake. Orodha hiyo inayo maneno kama vile kanzu, shamba na kizibao.
Katika Jarida hilo Johnson pia anajadili chanzo cha baadhi ya maneno naye Kasisi Hellier anayo orodha ya msamiati anaoupendekeza wa vipimo na mizani.
Katika Jarida la mwaka uliofuata, I.L.C. Bulletin Na. 10 ya 1936 kumbukumbu tatu za J. W. T. Allen, Broomfield na F. Johnson zimechapishwa. Kumbukumbu hizo ni maoni ya Kamati kumjibu Clement M. Doke aliyetoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kugawanya maneno katika kitabu cha Bantu Linguistic Terminology. Mapendekezo ya Doke yangesababisha kuwe na maandishi ya maneno kama vile waSwahili, muIngereza, mUngu, waDaudi na kwamtu badala ya Waswahili, Mwi- ngereza, Mungu, wa Daudi na kwa mtu. Kamati ilikataa mapendekezo ya Doke katika makala hayo na mengine yaliyochapishwa katika jarida la 1937.
Masuala ya kisarufi pia yalijadiliwa na kuchapishwa katika jarida la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Kwa mfano matumizi ya KA na KI yalijadiliwa na A. B. Hellier katika jarida la 1931 naye F. Johnson alijadili kinyume cha kiambishi “kuto-” katika jarida la 1933. Katika makala yake, Johnson anatoa rai kwamba neno kutoenda latokana na maneno kutoa na kwenda. Naye mwanakamati Ronald Snoxall anapinga maelezo ya Johnson na kumsahihisha kwa kueleza kwamba to katika neno kutoenda ndicho kiungo cha kinyume.
Masuala mengine kuhusu kusanifishwa kwa Kiswahili yalishughulikiwa na Kamati pia, na matokeo yake yakachapishwa kwenye jarida. Masuala hayo yalikuwa ni pamoja na kutoa sababu za kutumiwa kwa irabu zikifuatana kulikoelezwa na Broomfield mnamo 1931; kuhesabu katika Kiswahili na A. B. Hellier 1932; alfabeti za Kiswahili na A. B. Hellier 1934; mjadala kuhusu alama za kuwakifisha; pamoja na kukadiriwa kwa vitabu vya shule vya wakati huo, kulikofanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.
Mnamo mwaka 1934 ilibidi Kamati ipime kazi yake. Jambo hili lilisababishwa na kumbukumbu “Kiswahili cha Kisasa” iliyoandikwa na afisa mmoja wa Idara ya Elimu, Kenya. Baada ya kuipokea kumbukumbu hiyo, katibu alimuomba Broomfield aijibu. Kumbukumbu hiyo, majibu yake, pamoja na dondoo la gazeti Al-Islah la Mombasa zilizochapishwa katika Jarida, ILC Bulletin la 1934 tayari zimejadiliwa katika sura ya pili.
Baadhi ya makala zilirudiwa katika matoleo ya Jarida ya hapo mwanzo.
Kwa mfano, makala ya Snoxall kuhusu kitendo kutoa, ilichapishwa katika Jarida namba 6 la 1933 na kurudiwa tena katika Jarida namba 8 la 1935.
Makala iliyojadilia suala la a mbili katika maandishi ya Kiswahili katika
Jarida namba 2 la 1931, ilichapishwa tena katika jarida Bulletin namba 6,
la 1933. Kuna sababu mbili za kuchapisha upya makala hayo. Sababu ya kwanza ni kuwa ILC Bulletin lilikuwa jarida changa lililokuwa likitoa nakala chache, na lilikuwa na wasomaji wachache na waandishi wa makala za kuchapishwa hawakuwa wengi pia.Inawezekana kwamba watu ambao wangeandika makala ya kuchapishwa kwenye jarida walikuwa na kazi nyingi ya kuandika na kutafsiri vitabu vya Kiswahili ili kutosheleza mahitaji ya vitabu hivyo. Sababu ya pili ni kwamba matolea machache ya kwanza hayakuchapishwa kama vitabu bali yalipigwa taipu na kutolewa nakala. Jarida la kwanza lililochapishwa kama kitabu lilikuwa toleo namba 6 la Oktoba 1933. Kupigwa chapa huko kulipoanza, ndipo baadhi ya makala zilipoanza kuchapishwa upya ili ziweze kuwafikia wasomaji wengi zaidi.
Yale yaliyojadiliwa hapo juu ni baadhi ya mambo muhimu ya kupanga lugha kitaaluma, ambayo hujulikana pia kama “uhandisi wa lugha”, uliofanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Jarida hali- kuchapishwa katika mwaka 1937 kutokana na kifo cha Frederic Johnson aliyekuwa katibu wa kwanza wa Kamati. Johnson alifariki akiwa Aden mnamo mwezi Machi, 1937.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)