MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MCHANGO WA WAANDISHI WA RIWAYA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MCHANGO WA WAANDISHI WA RIWAYA
#1
Mchango wa Waandishi wa Riwaya

R.S. Mabala
Quote:
Quote:
Kila mwandishi ni mwandishi mwanasiasa.
Swali la pekee la kujiuliza ni: siasa gani na ni siasa ya nani.
Ngugi wa Thiong’o
 
Lugha na Fasihi
Mjadala kuhusu lugha na fasihi hapa Tanzania una sura tofauti sana tukilinganisha na nchi nyingine za Afrika kwa sababu ambazo sote tunazifahamu. Ijapokuwa wapo bado waandishi wachache ambao wanapendelea kutumia Kiingereza, kwa waandishi walio wengi hakuna mjadala tena kuhusu suala hili kama linavyowatatiza waandishi wengi kama kina Ngugi wa Thiong’o.
Hali hii ni ya kimaendeleo kwa sababu waandishi na wahakiki Watanzania wanaweza kuzama moja kwa moja katika uandishi wenyewe bila kupoteza nguvu nyingi katika mijadala mirefu kuhusu lugha ipi itumike. Vilevile waandishi hawana tatizo kuhusu wasomaji, maana lugha wanayoitumia ni ile ambayo wasomaji wote wanaijua. Kwa hiyo wana nafasi nzuri ya kuweza kuifikia jamii nzima, tofauti na Ngugi ambaye, bila kuwa na wafasiri, analazimika kuchagua ama Kiingereza, ili aweze kuongea na watu wa kila taifa ndani ya Kenya, japo wasomi wachache tu; ama Kikikuyu ili awafikie wakulima na wafanyakazi kama anavyodhamiria, Japo Wakikuyu tu. Ndiyo maana Ngugi anasisitiza umuhimu wa kuwa na wafasiri wawezao kufasiri kazi zake katika kila lugha ya Kenya.
Hata hivyo, nafasi hii ya kipekee aliyo nayo mwandishi Mtanzania lazima itafakariwe vizuri maana ni rahisi kwa mwandishi kujiona yu mwandishi wa umma kwa sababu tu anatumia lugha ya umma bila kutafakari yaokanayo na matumizi ya lugha hiyo. Iko hatari ya mwandishi kuridhika kwamba iugha ndiyo kigezo pekee cha mwandishi wa kimapinduzi. Hali hii hasa yahusu kizazi kipya cha waandishi ambacho kimerithi mafanikio yanayotokana na mapambano ya ‘vaandishi wakongwe kukipa Kiswahili nafasi na hadhi yake kama lugha ya Watanzania. Katika mapambano kama hayo mtu huelewa zaidi umuhimu wa lugha, pia matumizi na maudhui yanayobebwa na kuwasilishwa na lugha hii. Kwa mfano, msimamo thabiti wa Ngugi umetokana na mapambano hayo. Katika kitabu chake Decolonising the Mind anasisitiza mambo mawili muhimu:
Quote:
(a) Mwandishi Mwafrika anayedai kwamba hawezi kuandika bila kutumia lugha ya kigeni ni sawasawa na mwanasiasa ambaye anasema kwamba Afrika haiwezi kuendelea bila ubeberu. Tena mwandishi huyu yuko nyuma zaidi kuliko wamisionari na tabaka la vibepariuchwara ambao wote, kutokana na masilahi yao, wanatambua umuhimu wa kutumia lugha za watu ili waweze kufikisha ujumbe wao hata kama ujumbe wenyewe si wa kimaendeleo.
Quote:
(b) Kutumia lugha za Afrika ni hatua ya kwanza ya lazima, lakini ni hatua ya kwanza tu. Kutumia lugha hii hakutachochea mabadiliko wala maendeleo ya maana iwapo haitatumika kuendeleza mapambano ya wafanyakazi na wakulima dhidi ya ubeberu.
Na anaendelea; “Kwa maneno mengine, waandishi wanaotumia lugha za Kiafrika wanapaswa kujihusisha upya na mila za kimapinduzi za wakulima na wafanyakazi wakijitayatisha katika mapambano yao ili washinde ubeberu na kujenga mfumo madhubuti zaidi wa kidemokrasia na kijamaa.”1
Hoja hii ya Ngugi ni nzito sana na sitegemei kwamba kila mwandishi anaweza kulenga hivyo katika kila analoliandika. Lakini hoja hii, katika muktadha wa dondoo letu la kwanza – kwamba kila mwandishi, akubali asikubali, anahusika na siasa – ni msingi mzuri sana katika kuangalia na kupima mafanikio ya waandishi wetu.
Mwandishi na Jwnii
Kutokana na maneno ya Ngugi hapo juu, yafaa vilevile kukumbuka maneno ya wananadharia wawili wengine ambao waliandika katika mazingira tofauti. Kwanza, Lenin alimwandikia Maxim Gorky baada ya Mapinduzi ya mwezi Oktoba 1917:
Quote:
Ukitaka kuchunguza, sharti uchunguze kutoka chini, ambapo yawezekana kuangalia vizuri kazi ya kujenga maisha mapya katika makazi ya wafanyakazi, mikoani au vijijini.2
Hii inafanana na usemi wa Bertolt Brecht aliyesema kwamba mwandishi sharti “atazame mdomo wa umma.”3
Hapa tunaona kwamba Lenin na Brecht, kama wananadharia wote wa kijamaa, waliona hatari ya mwandishi kujitenga na jamii. Lenin alimwandikia Gorky kwa sababu wakati ule Gorky, ambaye daima huko nyuma alikuwa akiakisi maisha ya wafanyakazi, alikuwa ameanza kulowea makao makuu akishirikiana na waandishi na wasomi wenzake tu kiasi kwamba alianza kujitenga na umma. Brecht kadhalika aliona umuhimu wa kuwakumbusha waandishi na waigizaji hatari hiihii. Na hapa Tanzania hatari hii ipo vilevile kwa baadhi yetu. Uwezo wetu wa kuona, kuelewa na kuakisi jamii barabara umeanza kufifia kutokana na kujitenga kwetu na jamii au kushirikiana na aina au tabaka fulani tu ya watu, au kuchunguza kutoka juu.
Lengo la Makala
Lengo la makala haya basi, ni kuangalia baadhi ya waandishi ambao wameamua kuandika kuhusu matatizo, migongano, mapambano na maendeleo ya Tanzania baada ya kupata uhuru. Hivyo sitaweza kuangalia wale ambao lengo lao ni kustarehesha, wakiendeleza, kudekeza na kukuza fikra potofu katika jamii kama anavyotahadharisha Ernest Fischer:
Quote:
Kuigeuza sanaa kuwa biashara tu ili kuburudisha na kuridhisha nafsi ni hatari sana kwa sababu wakati vitabu vya aina hii vinajifanya kuwa vinamkomboa binadamu kumbe vinamdhalilisha.4
Hata baada ya kufinya uwanja wa makala haya, bado hatuwezi kusema kwamba kutalii huku katika mada kunatosheleza, ila tu katika riwaya ambazo napenda kuzingatia mielekeo fulanifulani inajitokeza. Unaweza kuzigawanya riwaya hizi katika mafungu matatu:
Quote:
(a) Riwaya zinazohusu Tanzania na suala la ukombozi kwa jumla nje na ndani ya Tanzania.
Quote:
(b) Riwaya zinazoangalia hasa tabia ya watawala wa nchi.
Quote:
© Zile zinazoangalia matatizo ya jamii ya tabaka la nchini, hususan katika vijiji.
Nimeamua kuangalia riwaya hizi kwa misingi mitatu mikubwa:
Quote:
1. Haitoshi kusema kwamba fasihi inaakisi jamii. Kama anavyosema Ngugi:
Quote:
Quote:
Fasihi haiakisi hali halisi tu bali hujaribu kumshawishi msomaji kujenga msimamo fulani kuhusu hali halisi hii. Kwa hiyo suala siyo je, ameakisi Jamii? Bali je, ameakisi kutoka wapi na ana shabaha gani katika uakisi wake?5
Quote:
Quote:
Nikinukuu shairi moja fupi kabisa la mwandishi mashuhuri wa Afrika ya Kusini, Dennis Brutus, anasema:
Quote:
Quote:
Quote:
Kioo kinahudumia
Mtazamaji anakielekeza.6
Quote:
2. Yawezekana na yatokea mara kwa mara kwamba mwandishi anaweza, bila kujitambua mwenyewe,
Quote:
Quote:
(i) kuonyesha mambo ambayo hakudhamiria
(ii) kuonyesha mambo ambayo yanapingana na yale aliyodhamiria kuonyesha.
Quote:
Kwa hiyo yawezekana kutokea mgongano kati ya ujumbe wa wazi aliodhamiria na ule uliofichika ambao pengine hakudhamiria au aliutambua kwa mbali.
3. Ijapokuwa makala haya yanaangalia hasa maudhui ya riwaya hizi, ni wazi kwamba suala hili haliwezi kutengwa na fani anayoitumia mwandishi.
Mafanikio ya Riwaya
Mafanikio yanaonekana katika ule ujumbe wa wazi. Waandishi wameongelea dhamira nyingi zenye maana na umuhimu sana hapa Tanzania.
Kwanza riwaya zimechochea na kuendeleza fikra za ukombozi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Kwa mfano, Pepo ya Mabwege na Njama vimesaidia kuwapa Watanzania mwamko na urazini mkubwa zaidi. Katika Njama mwandishi ametumia fani ya kina James Hadley Chase ambazo huhusu uhalifu na upelelezi kupanua mawazo kuhusu ukombozi wa Afrika ya Kusini, uonevu wa makaburu na mbinu zao.
Pili, zimefichua na kukosoa wapinga maendeleo ambao wamejivisha ngozi ya kondoo na wanatumia nafasi zao kama viongozi kujinufaisha wenyewe na kuihujumu Tanzania. Dhamira hii inaonekana katika riwaya karibu zote, k.m. Pepo ya Mabwege, Sudiya Yohana, Nguzo Uhondo, Nyota ya Huzuni, na kadhalika. Bila kuogopa, wameonyesha uozo mbalimbali ndani ya jamii, jinsi viongozi walivyo na vyeo vingi, k.m., Sir Henry Mwapeker na Mzee James Katika Pepo ya Mabwege; na mbinu wanazotumia ili kujijenga na kujiimarisha mpaka wote wanawaogopa. Hata polisi wanaogopa kufungua kesi ya Kalenga dhidi ya Waziri. Hali hii yaonekana hadi uongozi wa kijijini. Kwa mfano, katika Njozi Iliyopotea wanakijiji wote wanaogopa mwanzoni kumpinga Jumbe Mpwite kwa kuwa ni Mwenyekiti na anaye mganga wake.
Vilevile waandishi wamekazana kuonyesha ulaghai wa watu kama hao. Mzee James anagombea ubunge kama mjamaa. Joseph katika Sudi ya Yohana anahubiri kuhusu ukombozi wa Mwafrika na anapenda kusaidia ndugu zake huku akiwa mstari wa mbele katika kuhujumu kijiji chake na kuharibu maisha ya nduguze. Katika Njozi IliyopoteaLupituko anatumia nguvu kujenga siasa ya ujamaa ili kuridhisha silika yake ya ukatili na kuonyesha uwezo alio nao. Kadhalika itikadi ya Mambosasa katika Gamba la Nyokaimejaa kujitetea kwingi na visingizio vya kuridhisha nafsi yake.
Tatu, riwaya hizi zimeweza kuangalia kwa undani na kufundisha juu ya matatizo yanayolikabili tabaka la wanyonge.
Mojawapo ni kuhusu uongozi mbaya. Viongozi wengi ni vidikteta vidogo kama Lupituko au Katibu Tarafa Kagunda ambao wanaonea wananchi. Lupituko anahamisha familia kikatili kwa sababu mtoto wa kike alimkataa na baadaye anaua msichana mwingine katika kujaribu kumnajisi. Katika Sudi ya Yohana Kagunda kadhalika alimfunga mwanamke aliyemkataa. Katika Gamba la Nyoka Mambosasa anapokea hongo kutoka kwa wafanyabiashara.
Uongozi huu ulionekana hasa katika kipindi cha kuanzisha vijiji. Mara nyingi vijiji vilijengwa mahali pabaya kwa sababu ya wivu wa pimapima au hongo wanazopewa na makabaila au matajiri. Vilevile nguvu zimetumika kuhamisha watu bila sababu yoyote.
Athari za udhanifu katika jamii, ukiwa uchawi au Ukristo, unaonyeshwa pia. Katika Mirathi ya Hatari tunaona jinsi uchawi unavyotishia jamii nzima hadi hapo wachawi wote wanapoteketea. Hali kadhalika katika Gamba la Nyoka tunaona jinsi imani za wanakijiji zilivyoruhusu Mmarekani asiye hata Padre kupenya, kuchokoza vita kati ya wanakijiji na serikali, na kusababisha vifo vingi na baadaye kuua wengine kwa kutia sumu kisimani.
Katika Sudi ya Yohana, Amina anamsifu na kumshukuru Yohana kwa kusema:
Quote:
Mwenyezi Bwana ndiye kakutuma uje uniokoe, hakunitupa mimi mja wake. Si haki kumlaumu bali kuomba kujaziwa mema zaidi.7
Nne, riwaya zimeonyesha vijana wengi wanavyokimbilia mjini, kwa mfano, Matika na Chonya katika kitabu cha Shida. Hii yaweza kutokana na mila (kwa mfano Matika alikimbia kuozwa kwa nguvu); au fikra finyu kuhusu maisha ya mjini na nafasi za kupata kazi na kuishi kwa raha.
Tano, riwaya hizi zimefaulu kuonyesha matatizo ya wanawake katika jamii. Mara kwa mara wanawake wanaonyeshwa kuwa chombo cha uchu na ulafi wa wanaume. Familia ya Nyalindele inahamishwa kwa nguvu kwa sababu Nyalindele anamkataa Katibu Kata. Tulilumwi anakufa kwa sababu hiyohiyo; Losia analeweshwa na kudanganywa na kuachwa na mimba hadi anaamua kujiua. Agnes, mke wa Yohana, ananajisiwa kwa nguvu na shemeji yake. Matika anapokimbilia mjini analazimika kuwa malaya; Josina naye ananajisiwa baada ya kupewa dawa za kulevya. Mkewe Zautwa nave anafungwa kwa sababu ya kumkataa Katibu. Wanawake wanaonyeshwa wakidharauliwa kupita kiasi. Anavyosema Lukova katika Njozi Ilivopotea:
Quote:
Mke ni kama ngalawa. Matumizi yake makubwa na faida yake kidogo daima imaji mkukuu; hufaa lakini haiaminiki.8
Hata wanapojitahidi kujitetea au kubaki na msimamo wao wanaadhirika vibaya. Mara nyingi mwisho wanahesabiwa kuwa vyombo vya starehe tu.
Sita, waandishi nao wametoa ufumbuzi wa aina mbalimbali wa matatizo wanayoyaonyesha. Kwa mfano, mwishoni mwa Njozi Iliyopotea wanavijiji wameshagundua ubaya wa Jumbe Mpwite, na wanasimama imara kwa pamoja dhidi yake na wenzake. Katika Gamba la Nyoka mwandishi anaonyesha vizuri sana kwamba watakaoendeleza maisha ya wakulima ni wakulima wenyewe, si wahubiri kutoka nje, wawe wa siasa au dini:
Quote:
Wana mapinduzi halisi ni wale waishio vijijini wanaoathiriwa na upepo wa wakati unaowasukuma mbele kutoka walipokuwa. Kwao maisha ni maisha. Wanatazama kwa uangalifu kila badiliko linalohusu maisha yao kama watazamavyo kwa uangalifu na matumaini makubwa mimea yao ikikua9
Mara nyingi pia waandishi wanapenda kuonyesha maadui wakifichuliwa au kuteketezwa kama katika Pepo ya Mabwege.
Kwa kweli maelezo haya ya mafanikio yamekuwa mafupi mno na ya jumla, maana lengo la makala haya halikuwa kuangalia mafanikio haya ya wazi kwa undani sana. Lakini isingefaa kuzama kwenye matatizo tu bila kutambua kwamba waandishi hawa wamekwisha kutoa mchango mkubwa.
Matatizo ya Riwaya
Mafanikio ya dhamira za waandishi yameathiriwa mara nyingi na mambo makuu manne:
Quote:
(a) Kushindwa kuonyesha uhalisia kamili.
Quote:
(b) Kuzama katika nadharia ya ubinafsi bila hata kujitambua.
Quote:
© Falsafa na mtazamo wa kukata tamaa katika maisha – mtazamo kwamba maisha ni matatizo tu; mfululizo wa mateso usio na mantiki wala utatuzi.
Quote:
(d) Waandishi kupenda kusisitiza hoja zao kwa kuhubiria watu.
Uhalisia
Katika riwaya zao waandishi kwa ujumla wamefuata mtindo wa uhalisia, yaani wamedhamiria kuakisi jamii jinsi ilivyo, mara nyingi wakiwa na lengo la kuikosoa jamii ili ijirekebishe. Katika hali hii, lazima matukio na wahusika viwe vya kuaminiwa. Iwapo msomaji husita kupokea yanayotokea, riwaya huanza kuchechemea.
Mtiririko wa Vituko
Udhaifu huu unaonekana mara a kwa mara katika riwaya. Kwanza kuna matukio mengi ambayo yanapunguza uzito wa dhamira. Kwa mfano katika Pepo ya Mabwege, Josina, Kalenga na Hamisi ambao walikuwa wameachana siku nyingi wanakutana kwa bahati tu wakati mambo yameiva. Kalenga anapokwenda kumshitaki Mzee James, asingefika popote bila kufika ghafla kwa Hamisi ambaye hajaonanana Kalenga miaka kumi na nne lakini sasa amerudi na bahati nzuri amepandishwa cheo sana kiasi cha kuweza kumsaidia Kalenga moja kwa moja. Vilevile katibu wa Mzee James ni Blandina ambaye ndiye alikuwa mchumba wa Hamisi walipokutana Urusi, na ni huyuhuyu ambaye mbele ya Josina na Kalenga “anaponda” mvulana wake kwenye kituo cha basi kwa sababu ya kupewa lifti na mkwasi. Matukio kama haya labda yaweza kukubalika lakini utatuzi wa matatizo yote katika riwaya unakuwa kana kwamba ni wa juujuu tu na wa kulazimisha. Kalenga ameshachukiwa na wakubwa, wakiwemo Mhariri Mkuu wa gazeti analofanyia kazi. Msimamo wake wakati huu umekwishakua, na hata kufukuzwa amefukuzwa kazi, lakini katika siku chache zilizobaki anaachiwa gazeti awe mhariri mkuu. Anatumia nafasi hii vizuri kufichua njama kadha wa kadha na maadui wa taifa wanakamatwa. Basi ufumbuzi mzima wa riwaya. wategemea kitu ambacho kiko nje ya uhalisia.
Kadhalika katika Njama, mtiririko wa vituko wategemea Willy Gamba au wenzake wa Sierra Leone kuwepo, kwa bahati tu, mahali na wakati unaofaa kila mara. Mfano ni Willy anavyomwokoa Zabibu nukta chache kabla ya kuchinjwa. Kadhalika Willy anapokwenda Sierra Leone anatokea kukutana na mtu atakayemfaa katika mapambano ya baadaye.
Mtiririko mzima wa Njama unamtaka msomaji afumbe macho ili asione mambo yasiyoaminika. Kwa mfano, mauaji makubwa yanafanywa na kundi la majasusi wasaliti lakini kila mara wanapomkaribia Willy wanamwonya tu na hivyo kumpa nafasi ya kuwamaliza wote mwishoni. Vilevile shabaha yao ghafla inageuka kuwa mbaya kila wakimlenga yeye. Hivyo umaarufu wote wa Willy Gamba unatokana na mwandishi kwenda nje ya uhalisia.
Mtiririko wa Gamba laNyoka nao haufuati uhalisia katika sehemu muhimu. Kwa mfano, maisha ya Mambosasa na Mamboleo hayaeleweki. Wamerudishwa kijijini kwa sababu ya tabia zao mbaya na upinzani wao dhidi ya serikali. Sasa yashangaza kwamba japo hawajaonyesha kuwa wamejirekebisha wanaruhusiwa kugombea uongozi wa kijijini. Halafu baadaye ingawa bado matendo yao hayakubaliki kwa watawala (k.m., wanampiga Padre Madevu, wanakula fedha za kijiji, na wanahongwa na watu binafsi hadi kijiji chenyewe kinawakataa), Mamboleo anachaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya. Kwa hiyo matukio yanaonekana yanatukia tu kwa amri ya mwandishi ambaye yeye, kama Mungu, anaweza kuamua afanye lolote lile na dunia aliyoiumba. Hata mwanzoni mwa riwaya watu wa Kisole, katika kuamua kukataa kuhamia kijiji kipya wanaua wanamgambo karibu mia moja lakini zaidi ya kukalishwa juani kwa muda wa saa chache na kuhamishwa kwa nguvu siku inayofuata, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi yao, au viongozi wao. Hivyohivyo, Madevu anapoua watu ishirini kwa sumu hatuoni hatua yoyote ya maana inayochukuliwa. Mikasa hii ya hatari katika jamii inapita sawasawa na mkasa wowote mwingine kama vile mtu anavyowatembelea wakwe zake! Uzito wa mikasa na vipi jamii inalichukulia jambo hili zito hatuonyeshwi. Badala yake tunaona tu kwamba Tina anajuta kumwua Madevu bila hata kukumbuka wanakijiji wenzake waliokufa.
Upande wa Njozi Iliyopotea yaelekea kwamba mwandishi anataka kutuonyesha kwamba viongozi wanatumia vibaya madaraka yao lakini uzito wa hoja hii unapungua kutokana na kwenda nje ya uhalisia. Hii inaonekana hasa katika kesi ya Lukova baada ya kumpiga Katibu Lupituko.
Lupituko, akiwa ni kiongozi wa serikali, alikuwa na nafasi ya kutosha kummaliza Lukova kwa kuonyesha jinsi Lukova, kama ‘mpinga mapinduzi’, alivyomwingilia katika kazi yake na kumpiga akiwa kazini. Lupituko angeweza kula njama na hakimu na kumwadhiri Lukova sawasawa. Mashtaka dhidi ya Lukova ni makubwa: wizi wa kutumia nguvu, kuwa na meno ya tembo kumi na moja na ngozi tatu za chui bila kibali, kuwa na bangi masanduku mawili, na kuwa na bunduki ya serikali iliyoibiwa. Mashtaka kama hayo yanahitaji ushahidi wa kutosha na yanaweza kubatilishwa kabisa na wakili mahakamani, lakini utetezi wake tu ni kwamba ndugu na marafiki wanasema kwamba Lukova hana tabia ya namna hii. Hivyo:
Quote:
(a) Mashtaka yenyewe yameongezwa kupita kiasi
Quote:
(b) Utetezi upande wa mshtakiwa ni mdogo mno. Iwapo wakili kweli alimwonea huruma na kuamua kumtetea ipasavyo, anastahili kufukuzwa kazi kwa kushindwa kubatilisha mashtaka yasiyo na ushahidi.
Quote:
© Ushahidi wa Kiligilo usingekuwa na maana yoyote hata kama angeweza kusema bila kuondoka kwa ghadhabu. Kwa hiyo dhana ya kwamba rafiki yake alihukumiwa kwa sababu Kiligilo alishindwa kumtetea haipo kabisa. Kutokana na hayo, uzito wa hoja ya mwandishi unapunguzwa.
Mifano kama hii inaonekana katika karibu kila riwaya. Katika Sudiya Yohana Joseph anazidi kumdhulumu ndugu yake kuanzia kumwingilia mke wake kwa nguvu, hadi kumkatalia nafasi yake ya kusoma ng’ambo, na mwisho kumfukuzisha kazi. Licha ya yote haya bado anategemea kwamba Yohana atakubali kumwendeshea kampuni yake. Vilevile migomo ya wafanyakazi inapachikwa tu kwa kuwa mwandishi anataka kuonyesha mwamko wa wafanyakazi.
Uchoraji wa Wausika
Kukosa uhalisia upande wa wahusika nako kunaathiri sana dhamira ya mwandishi. Tukianzia kwa Mambosasa na Mamboleo katika Gamba la Nyoka, ni kweli kwamba hawa ndugu wawili wana migongano mikubwa ndani yao kutokana na kulewa itikadi na ukatili wao, lakini mwandishi ameshindwa kuoanisha vipengele mbalimbali katika tabia zao. Mara twaambiwa wamefanya mema mengi katika jamii, kwa mfano, kufichua wenye maduka wanyonyaji na wapimaji wa pamba walaghai; kujenga visima vizuri kwa kushirikiana bega kwa bega na serikali katika operesheni vijiji, n.k.; mara twaambiwa kwamba ni wapinzani wakubwa ambao walimpiga mwalimu wa siasa J.K.T. na kusambaza karatasi ya uchochezi kambini. Upande wa mapenzi, Mambosasa anajiambia:
Quote:
“Sina muda wa mapenzi. Mapenzi ni mojawapo kati ya mambo ambayo hayapasi kuambatana na tabia njema ya mwanamapinduzi halisi.”10 Lakini hapohapo tunafahamishwa kwamba sababu nyingine ya kurudishwa kwao kijijini ni kwamba walimnajisi msichana. Hivyohivyo katikati ya mjadala mzito juu ya matatizo ya ujamaa Mambosasa anauliza: “Mamboleo umekwishashika maziwa ya msichana mdogo?”11
Ni kweli kwamba binadamu amejaa mikinzano ya kila aina, lakini lazima kuwepo na uhusiano na mfungamano kamili wa wahusika hao ambao utafanya tuyaamini mabadiliko haya ya tabia ya mara kwa mara. Hali hii inaathiri hata wahusika wengine. Mara nyingi pia tabia za wahusika hazionekani kwa vitendo kiasi kwamba kunakuwepo na mgongano. Kwa mfano, katika Njozi Iliyopolea mwandishi anataka kujenga dhana ya kwamba Kiligilo ni mcbapakazi na mpenda haki anayewafunulia wanakijiji haki zao na kujenga umoja thabiti katika kuendeleza kijiji. Hayo yote tunaambiwa moja kwa moja na mwandishi mwenyewe, hatuyaoni sana katika vitendo vya Kiligilo. Kinyume chake mara nyingi anachelewa kuamka na kwenda kazini; mara tu baada ya kufika kijijini na kuanza kazi, anapata matatizo na anapotea mwezi mzima. Hajaonyesha tabia yoyote inayotudhihirishia kwamba maneno ya mwandishi ni kweli. Hivyo inaonekana kwamba mwandishi analazimisha hoja zake.
Hata hivyo Kiligilo angalau ni binadamu, kinyume na Willy Gamba ambaye kwa uwezo wake anafanana na miungu, na kama miungu walivyo anaabudiwa, hasa na wanawake. Anatamba mwenyewe, “mimi huwa sielewi kwa nini binadamu hawa hutokea kunipenda mara tu nionyeshapo uso wangu.13
Na kweli. Kwa mfano, Zabibu anaambiwa kwamba mpenzi wake ameuawa. Wakati huohuo mara amekwishampenda Willy:
Quote:
Niko tayari kukusaidia kwanza kwa sababu umeniokoa pia kwa sababu unapeleleza kifo cha mpenzi wangu na tatu nafikiri wewe ni kijana mwenye kupendeka.13
Ikifika usiku anakwenda kulala na Willy.
Mfano huu unaonyesha uhalisia hafifu katika uchoraji wa wanawake. Nisingependa kusema mengi maana mada hii ina siku yake, lakini kwa ujumla wanaonekana binadamu dhaifu kupita kiasi. Katika Njama, mapenzi yao hubadilika mara moja. Mfano mwingine ni Margret. Mara atokeapo mwanamume shujaa basi tunaona mara moja msichana huyo “ameshakwisha” japo wakati huo anaomboleza kifo cha mpenzi wake. Hata kama wako wasichana ambao nao wana nguvu, kama vile Veronica, bado haifuti wazo kwamba wanawake ni chombo cha starehe, hasa kwa mtu kama Willy ambaye mwandishi anatuambia kwamba anastahili warembo hao kwa sababu ya kazi ngumu anayoifanya.
Hata katika riwaya nyingine, wanawake huonyeshwa wadhaifu kupita kiasi na rahisi kudanganywa au kulazimishwa. Hata jitihada za baadhi yao kusimama imara zinaishia ukingoni tu. Josina anapewa dawa za kulevya na kunajisiwa. Losia, msichana mwenye tabia nzuri ajabu, ambaye wakati wote akiwa shuleni hakuteteleka hata kidogo, anadanganyika kirahisi na pombe ya siku moja na kuamka kesho yake kitandani mwa mwanamume bila hata kujitambua alifikaje pale. Tena hapohapo anabeba mimba na mwisho kuona njia ya pekee ni kujiua. Ameshindwa. Mama Liganga naye anasimama imara kujitetea lakini matokeo yake anafungwa miaka mitatu na kugeuka malaya anapofunguliwa. Mkewe Yohana naye analazimishwa na Joseph. Kuna mifano mingine mingi. Ni kweli kwamba waandishi wanataka kuonyeshajinsi wanawake wanavyoonewa, lakini mwishoni inaonekana kwamba hata wale wanaotaka kusimama imara wanashindwa wote. Kwa hiyo watabald dhaifu tu.
Mwisho, upande wa wanawake, mara nyingine tunalazimishwa kujiuliza kama wanawake wasio na uzuri kupita kiasi wana nafasi kalika jamii. Hali hii yajitokeza hasa katika Njama. Kila msichana ni mrembo kupita kiasi, ambaye hajawahi kuonekana, na ni haohao wenye uwezo. Hii ni kurahisisha mambo kupita kiasi na inadhalilisha uwezo na tabia za wanawake. Katika riwaya nyingine hali hii siyo mbaya sana lakini hujitokeza hapa na pale.
Mauaji
Riwaya nyingi zimejaa mauaji. Katika Njama Willy anaua karibu watu mia moja peke yake. Katika Pepo ya Mabwege, Josina na Master Peter wanakufa. Katika Njozi IliyopoteaLosia Lukova, Tulilumwi, na Lupituko wanafariki; na katika Mirathi ya Hatari wanakufa watu wengi sana. Huenda hali hii inatokana na:
Quote:
(a) kutaka kumshawishi msomaji kwa kutumia vituko visivyo vya kawaida
Quote:
(b) haja ya kuipatia riwaya tamati yenye kuridhisha. Hata hivyo mauaji nayo yakizidi uhalisia hupungua.
Kutia Chumvi Nyingi
Mauaji ni mfano mmoja tu wa jinsi waandishi wanavyotia chumvi kupita kiasi. Njama inatupa mfano halisi mwingine:
Quote:
“Nilijiviringisha hewani namna ambayo wote walishangaa; risasi zao zote zikanikosa. Wakati uleule nikaachia za kwangu nikawapata wote nao wakaanguka chini.14Au kwingine tunaambiwa kwamba Willy anaweza kuruka futi nane, ambayo ni zaidi ya rekodi ya dunia. Kutokana na chuku za namna hii, mhusika haaminiki.
Hali hii inaonekana mara nyingine mwandishi anapotaka kusisitiza hoja yake. Kwa mfano hadithi nzima ya Amina anavyoachwa pale kwenye kituo cha basi huku akitaka kujifungua. Mwandishi anataka kutuonyesha jinsi jamii ilivyoharibika lakini lengo na msisimko wa sehemu hii unapotea.
Mwisho waandishi wengi wanapenda kutuinia tashititi, ucheshi, n.k., ili kuwasilisha ujumbe wao. Kwa mfano, katika Pepo ya Mabwege mwandishi anaonyesha jinsi watumishi wa hoteli wanavyowakimbilia Wazungu hadi wanagonganisha vichwa na mmoja anapoteza jino. Vivyohivyo kanisani Josina anapomkataa Peter, matendo ya watu kuhusu jambo hili yanatiwa chumvi sana. Tashititi kwa kawaida hutegemea utiaji wa chumvi lakini ili ifanikiwe inapaswa iwe sehemu kamili ya muundo na mtiririko wa hadithi kwa jumla.
Udhanifu
Udhanifu huonekana hasa katika tamati za riwaya. Mwandishi anapenda kuonyesha hali ya maendeleo au kuondoa waovu, kwa hiyo anapachika tamati nzuri ambayo mara nyingine inakwenda kinyume na yaliyotokea awali. Pepo ya Mabwege ni mfano mzuri. Tumeshaonyesha kwamba kufichuliwa na kuondolewa kwa uovu ndani ya jamii kunategemea Kalenga kuwa Mhariri Mkuu kinyume cha hali halisi. Matokeo yake ni kwamba wema unashinda, jamii inasafishwa, na Kalenga anapandishwa cheo kuwa Mhariri Mkuu. Kwa hiyo inavyoonekana uozo haukutokana na mfumo hata kidogo, bali umetokana na watu wachache tu wenye nia mbaya ambao wametumia nafasi zao kwa faida yao. Sasa kizazi kipya kimeshika hatamu, kwa hiyo hakuna matatizo yoyote wala haja ya kufanya mabadiliko katika jamii.
Katika Shida, Chonya na Matika wanarudi katika kijiji cha Paradiso. Mapambano yamekwisha. Katika Gamba la Nyoka mwandishi anakwepa udhanifu huu. Anaonyesha matatizo kadha wa kadha yanayokabili uanzishaji wa vijiji vya ujamaa, lakini mwishoni mapambano yanakwisha hivyohivyo. Viongozi wabaya vijijini na wilayani wanaondoka, trekta inafika, na mabomba ya maji – mpaka tunaelezwa hata kazi za kila kamati kijijini. Kwa hiyo baada ya dhiki, faraja yapatikana moja kwa moja. Katika Mirathi ya Hatari wachawi wote wanateketea. Si kwamba tamati nzuri ya matatizo haiwezi kupatikana, ila tamati hizi zinaishia katika ndoto kwa sababu:
Quote:
(a) mara nyingine hazitokani na yaliyotangulia; na
(b) zinakuwa nje ya maisha ya kila siku ya jamii. Harakati zinatoweka.
Kwa kifupi, lengo la sehemu hii ya “udhanifu” ni kuonyesha jinsi udhaifu wa uhalisia unavyoathiri sana dhamira za waandishi, maana mahali ambapo msomaji anashindwa kukubali uakisi wa wahusika na hali halisi basi na dhamira ya mwandishi nayo haitakubalika.
Ubinafsi
Ijapokuwa waandishi wanaonyesha jamii ikipambana na waovu, mapambano haya daima hutegemea nguvu ya watu wachache sana. Umma haupo. Mfano halisi ni Njama.Ijapokuwa mwandishi anasema kwamba riwaya ni: “Kwa ajili ya wale wote ambao wamejitoa mhanga katika kupigania uhuru wa bara hili la Afrika,”16 dhamira inayojitokeza ni kwamba bila Willy Gamba na uwezo wake wa kujiviringisha kwa namna ya ajabu, ukombozi wote ungekwama. Wapigania uhuru wenyewe wamepigwa butwaa pamoja na kamati ya ukombozi na polisi. Hawana nguvu yoyote. Hata mwishoni mahali ambapo imeeleweka wazi mahaini wako wapi na ni kiasi tu cha kuwazingira na kuwakamata bado ni Willy tu na Sherriff, Eddy na Isaac ambao wanakwenda peke yao kuteketeza kundi zima la wahalifu. Hivyo dhana inayopatikana hapa ni kwamba ukombozi wategemea nguvu ya binadamu wachache wenye vipawa vya ajabu. Kazi ya umma ni kukaa na kushangilia na kushukuru hawa wachache kwa kuwaokoa wao wasio na akili na uwezo wowote.
Huu ni mfano mmoja wa dhamira zilizojificha, dhamira zenye kuhitilafiana na zile zilizo wazi. Mapema katika riwaya mwandishi anaeleza kwa ufasaha umuhimu wa mapambano ya umma na jinsi vyama vya kupigania uhuru vinavyojitahidi, lakini hadithi yenyewe inaonyesha kwamba mbele ya mbinu za hali ya juu ya makaburu, umma hauwezi kitu.
Dhana nyingine inayotokana na hiyo ni kwamba hawa binadamu wachache wa ajabu wanastahili maisha ya ukwasi wa hali ya juu kutokana na mchango wao. Hivyo Wasichana warembo “wanawaangukia” kila dakika, wanaweza kusafiri dunia nzima kupumzika kama Willy alivyokwenda Sierra Leone, maisha yao ni.kula katika hoteli za kitalii na kunywa pegi nyingi za wiske. Hapo vilevile twaambiwa kwamba lipo tabaka la juu linalostahili maisha haya mazuri lakini siyo tabaka la umma.
Katika Pepo ya Mabwege hali hii haijitokezi kiasi hicho lakini ipo. Mwapeker na James ni watu wakubwa katika jamii na nyadhifa zao ni nyingi lakini wanaangushwa na jitihada za Kalenga peke yake akisaidiwa na Hamisi na watu wengine wachache. Kwa hiyo hapa vilevile mapambano ni kati ya wale waovu wakubwa na watu wachache wanaowaona. Ni vita vya mafahali, sisi wengine twabaki ni watazamaji tu.
Kwa ujumla nguvu ya wafanyakazi haionekani kabisa. Hata wale wasaidizi wa Kalenga waliosoma naye wana kazi nzuri katika jamii, k.m. mwandishi wa habari, inspekta wa polisi, mwalimu – wote wamepata nafasi ya kusafiri nje. Kwa hiyo karibu ni wa tabaka lilelile la kina Mwapeker. Labda tofauti ni kwamba hiki ni kizazi kipya lakini nafsi zao ndani ya mfumo ni zilezile, na mfumo unabaki palepale. Mwapeker na James wanajenga himaya yao kwa kutumia watu binafsi wanaowafahamu, na Kalenga na wenzake wanawaangusha kwa kufanya hivyohivyo. Tunaweza kujiuliza kama Hamisi angemsaidia Kalenga iwapo hawakusoma pamoja. Vilevile ni jambo la ajabu kwamba wote wenye msimamo imara wanatoka nje ya Tanzania au wamekwenda ng’ambo. Katika Njama Willy anasaidiwa hasa na watu wa Sierra Leone. Ni vizuri sana kuonyesha umoja wa Afrika lakini Watanzania nao hawana uwezo huu isipokuwa Willy na wenzake katika upelelezi? Katika Pepo ya Mabwege kadhalika, Kalenga amesoma Nairobi na kufanya kazi Msumbiji, Josina kasoma Cuba, na Hamisi Urusi. Waliosoma Tanzania wanaonekana hawawezi kupata urazini huo mkubwa.
Ubinafsi unaonekana vilevile katika dhamira ya wahusika wengi ya kulipiza kisasi. Willy anamfuata Shuta kumlipizia kisasi Veronica. Kalenga naye anasukumwa na nia ya kumlipizia kisasi Josina. Vilevile katika Sudi ya Yohana mwandishi anaona kwamba njia pekee ya kutatua matatizo yanayojitokeza katika jamii ni Yohana kwenda kumchoma kisu Joseph. Zautwa alikuwa hoi kwa sababu alishindwa kulipiza kjsasi. Mdogo wake Wakili Mwakipusi naye aliishia kulipiza kisasi. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo waandishi wanaleta dhana ya kwamba kila mtu binafsi akiamka namna hiyo basi hata kama jamii haibadiliki angalau haki fulani itakuwa imetendeka; kilio cha wanyonge kitakuwa kimesikika na mwovu atakuwa ameadhirika hata kama mfumo ulioruhusu uovu huu umebaki palepale.
Kusema yote hayo hakuna maana kwamba mwandishi wa makala haya anataka kuona wafanyakazi wakiamka na kupigana moja kwa moja wakiwa na urazini mkubwa na mikakati ya hali ya juu. Hii itakuwa kinyume cha uhalisia tena. Lakini yawezekana kwamba waandishi hao wameathiriwa na elimu yao na nafasi zao katika jamii kiasi cha kuona mapambano upande wa tabaka la kati tu, na mapambano ya mtu binafsi kutetea haki zake kazini, shuleni, na kadhalika, bila kuona na kushiriki katika mapambano ya walio wengi ambayo yanaendelea siku hadi siku. Tukitumia mfano mmoja wa tamthiliya, tunaona kuwa katika mchezo wa mafuta wafanyakazi wanagoma lakini mara tu wanapofukuzwa kazi na kuona njaa ya siku mbili wanarudi na kulamba miguu ya tajiri wao. Hii ni tofauti na waandishi wengine mashuhuri wa Afrika, k.v., Sembene Ousmane, Ngugi wa Thiong’o na Alex la Guma ambao daima wanatambua kwamba umma upo na nguvu unazo hata kama hawaamki wote kwa pamoja na kupambana kila wakati. Kwa hiyo mapambano ya mtu binafsi yanapewa nafasi yake katika mapambano mapana na mazito zaidi ya jamii nzima.
Kukata Tamaa
Waandishi wengine wanaonyesha vizuri sana matatizo ndani ya jamii lakini yaelekea kwamba matatizo haya hayatokani na mfumo wa jamii uliojengeka bali hulka za binadamu. Mambo yakiwa hivi, basi hakuna matumaini ya kuleta mabadiliko ndani ya jamii. Dunia ni tambara bovu. Labda tungoje ya mbinguni. Kwa mfano katika Gamba la Nyoka,maisha ya Mambosasa na Mamboleo yanabadilika siku hadi siku bila kueleweka. Inavyoonekana maisha hayana mantiki kabisa: Mamboleo ghafla anapandishwa kuwa Mkurugenzi bila kufanya lolote la maana. Mwenzake anarudishwa kuwa Mwalimu vilevile bila sababu yoyote ya kuonekana tofauti na mwenzake. Mkuu wa Wilaya anakalia barua ya Mambosasa tu bila sababu wakati Mamboleo anapewa ya kwake.
Katika Njozi Iliyopotea kadhalika tunaona jamii na wema katika jamii wakizidi kudidimizwa na mwandishi. Si kwamba tunatakiwa kuona kwamba wema wanashinda kila mara, la hasha, lakini ni kama mwandishi amedhamiria kutuonyesha kwamba maisha ya binadamu ni kuwa mpweke tu. Kiligilo na Mzee Malongo wanaelewana mara moja kwa sababu ya upweke wao, lakini kila Kiligilo akiwa na tegemeo la kuondoa upweke, tegemeo hili linavunjiliwa mbali. Mpenzi wake Losia anadanganywa na mwisho anajiua. Lukova anaonewa kwa mashitaka ya ajabu na baadaye anakufa ghafla kutokana na ugonjwa unaozuka jela. Matumaini ya Kiligilo kwa Tulilumwi yanakatishwa na ukatili wa Katibu Lupituko mpaka Kiligilo anaishia kupata kichaa. Mwandishi anatuonyesha kwamba kweli njozi imepotea kabisa.
Mahubiri
Mara nyingi mwandishi anaamua kufikisha ujumbe wake kwa njia ya mahubiri, ambayo mara nyingine yanapingana na uhalisia. Kwa mfano, katika Mirathi ya Hatari mhusika mkuu anaamua kuwahubiria wachawi palepale ndani ya pango lao. Katika Njama mwandishi anafikisha ujumbe wake sehemu ya mwanzo ya kitabu kwa kutueleza historia yote ya nyuma ya Afrika ya Kusini na sababu ya mapambano – Vero, Sherriff na Willy ambao wote wanajua mambo hayo fika inabidi wahutubiane ili sisi wasomaji tupate ujumbe sawasawa. Hali hii inatokea vilevile katika Pepo ya Mabwege kati ya Josina na Kalenga. Katika Gamba la Nyoka mwishoni, mwandishi anaamua kuingilia kati kuhakikisha kwamba kweli tunaelewa sawasawa. Hatari za hali hii ni kwamba:
Quote:
(a) riwaya hugeuka hotuba na kupoteza nguvu yake ya kutufanya sisi kuona na kusikia kwa namna ya pekee yale yanayojitokeza katika jamii.
Quote:
(b) Huu ujumbe wa hotuba huhitilafiana na ujumbe unaotokana na vitendo vilivyoelezwa awali.
Tamati
Kazi ya msanii, kwa kuwa inagusa hisia zetu zote, ina uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa katika urazini na msimamo wa wasomaji. Hivyo wajibu wa mwandishi ni mkubwa. Inafurahisha kuona jinsi baadhi ya waandishi wa riwaya walivyobeba wajibu huu; wamekazana kuakisi na kuelimisha jamii, na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa.
Hata hivyo, mara nyingi ujumbe na dhamira zao vinaonekana zaidi katika maelezo yao ya wazi mwandishi anapoingilia mwenyewe au kwa kupitia kwa mhusika mmojawapo. Lengo la makala haya limekuwa ni kuonyesha kwamba ili aweze kufanikisha zaidi dhamira anayoikusudia, mwandishi wa riwaya anapaswa kuzingatia zaidi jinsi muundo mzima wa riwaya unavyochangia kutoa ujumbe wake; na iwapo ana nia ya kuwakilisha umma katika maandishi yake yafaa ajichunguze zaidi anaiandikia jamii kwa mtazamo gani na wa nani ili pasiwe na mgongano kati ya ujumbe ulio wazi na ule uliofichika.
Tanbihi
1. Ngugi wa Thiong’o, (1986) Decolonising the Mind. Currey, London, uk. 29 – 30, tafsiri yangu.
2. V. Lenin, (1981) On Literature and Art. Progress Publishers, Moscow, uk. 226, tafsiri yangu.
3. D. Craig (ed) (1975) Marxists on Literature. Penguin, Harmondsworth, uk. 14, tafsiri yangu.
4. E. Fischer, (1969) Art Against Ideology. Braziller, New York, tafsiri yangu.
5. Ngugi, (1981) m.y.k. uk. 6 – 7, tafsiri yangu.
6. D. Brutus, (1978) Stubborn Hope. Heinemann, London, uk. 79, tafsiri yangu.
7. C.S.L. Chachage, (1981) Sudiya Yohana. DUP, Dar es Salaam, uk. 18.
8. C.G. Mung’ong’o (1980) Njozi Iliyopotea. TPH, Dar es Salaam, uk. 28.
9. E. Kezilahabi (1979) Gamba la Nyoka. Eastern African Publications, Arusha, uk. 150.
10. Kezilahabi, (1979) uk. 46.
11. Kezilahabi, (1979) uk. 58.
12. A.E. Musiba, (1981) Njama Continental Publishers, Dar es Salaam, uk.
13. Musiba, k.h.j., uk. 129.
14. Musiba, k.h.j. uk. 170.
15. Musiba, k.h.j. Kwenye jalada la nyuma.
Bibliografia
Balisidya, N. (1981) Shida. DUP, Dar es Salaam.
Brutus, D. (1978) Stubborn Hope. Heinemann, London.
Craig, D., ed. (1978) Marxists on Literature. Penguin, Harmonds worth.
Femia, J.V., (1981) Gramsci’s Political Thought. O.U.R, Oxford.
Fischer, E., (1969) Art Against Ideology. Braziller, New York.
Gugelberger, G., (Mh.) (1985) Marxism and African Literature. Currey, London.
Kavanagh, R.M., (1985) Theatre and Cultural Struggle in South Africa. Zed, London.
Kezilahabi, E., (1979) Gamba laNyoka. Eastern African Publications, Arusha.
Lenin V., (1982) On Literature and Art. Progress, Moscow.
Mung’ong’o, C.G., (1977) Mirathi ya Hatari, TPH, Dar es Salaam.
Quote:
(1980) Njozi Iliyopotea. TPH, Dar es Salaam.
Musiba, A.E. (1981 Njama. Continental, Dar es Salaam.
Mruma I., (1980) Nguzo ya Uhondo. TPH, Dar es Salaam.
Mwakyembe, H., (1981) Pepo ya Mabwege. Longmans, London.
Ngugi wa Thiong’o (1981) Writers in Politics. Heinemann, London.
Quote:
(1986) Decolonising the Mind. Currey. London.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)