MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MAKUWADI WA SOKO HURIA (CHACHAGE S. CHACHAGE) KATIKA MUKTADHA WA RIWAYA YA KIHISTORIA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MAKUWADI WA SOKO HURIA (CHACHAGE S. CHACHAGE) KATIKA MUKTADHA WA RIWAYA YA KIHISTORIA
#1
MAKUWADI WA SOKO HURIA (CHACHAGE S. CHACHAGE) KATIKA MUKTADHA WA RIWAYA YA KIHISTORIA KATIKA FASIHI YA KISWAHILI


Makuwadi wa Soko Huria (Chachage S. Chachage) katika Muktadha wa Riwaya ya Kihistoria katika Fasihi ya Kiswahili
Mugyabuso M. Mulokozi
Ikisiri
Miongoni mwa kazi bora za fasihi duniani ni zile zilizojikita katika matukio na/au mashujaa halisi wa kihistoria. Mifano mizuri ni tendi za Homer za Kiyunani, baadhi ya tamthilia za W. Shakespeare (k.m. Julius Kaisari), na riwaya mashuhuri za Kirusi za Pushkin na Leo Tolstoi. Katika fasihi ya Kiswahili, riwaya ya kihistoria haijaendelezwa sana. Miongoni mwa kazi zilizoinua kiwango cha riwaya ya kihistoria katika Kiswahili ni Makuwadi wa Soko Huria. Makala haya yataichambua riwaya hiyo katika muktadha wa riwaya ya kihistoria katika Kiswahili ili kuona mchango wa riwaya hiyo, na wa Chachage mwenyewe, katika kuuendeleza na kuukomaza mkondo huo wa uandishi wa kubuni.
_______________________________________
“Mtu huandika kitabu kimoja tu katika maisha yake.” Chachage S.Chachage
_______________________________________
“…katika kuandika historia isiyokuza ushujaa wa mtu au watu binafsi, Chachage amemkaribia mwandishi mashuhuri wa kimapinduzi, Maxim Gorky. Kwangu mimi, hili tu linatosha kumweka Chachage katika orodha ya wasanii stadi wa Tanzania, na wa Bara la Afrika” (Issa Shivji ,2002).
                        _________________________________________
1.0 Utangulizi Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria iliandikwa mwaka 1999-2000, na kuchapishwa mwaka 2002 na kampuni ya E & D. Katika mahojiano aliyoyafanya na Diegner (2004: 228), mwandishi anasema alitumia miaka mitatu (1996-1999) kufanya utafiti wa masuala yaliyomo katika riwaya hiyo. Muda huo mrefu wa utafiti ni ushahidi kuwa C.S. Chachage alikusudia kuandika kazi changamani na yenye mawanda mapana na kina cha kutosha. Makuwadi wa Soko Huria inazo sifa hizo na zaidi. Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria (baadaye Makuwadi) ilihakikiwa kwanza na Shivji (2000/2002) na baadaye Mbonde (2004). Tutazipitia kidogo tahakiki zao kabla hatujajikita katika uchambuzi wetu wa riwaya hiyo katika muktadha wa bunilizi za kihistoria katika Kiswahili.
Makala ya Shivji ni mapitio na utambulisho wa riwaya hiyo na inafanya mambo kadha muhimu: Inatupa mtazamo na mwelekeo wa kitabaka wa kisiasa-kiitikadi wa kuitazama riwaya hiyo, na hivyo kuonesha dhima na mchango wake katika kufafanua na kuendeleza harakati za wanyonge wa Tanzania na Afrika za kupambana na mifumo inayowakandamiza. Pili, tahakiki hiyo inabainisha vizuri mtanziko wa kimawazo na kivitendo wa tabaka la vibwanyenye wa Tanzania linalowakilishwa na wahusika Mjuba na Sifuni. Hili ni tabaka linaloyumba kati ya kukubali kuukumbatia ubepari na raha zake, au kujiunga upande wa mapambano na mawanio ya umma na karaha zake. Mtanziko huu, aliouelezea vizuri Amilcar Cabral mwaka 1966, bado haujasuluhika. Mchango muhimu wa makala ya Shivji ni kutupatia kiunzi cha kinadharia na kiitikadi cha kuitazama riwaya hiyo ya Chachage, maana haingii sana katika uchambuzi wa riwaya yenyewe.
Mbonde anafanya uchambuzi wa
kijadi wa riwaya ya Makuwadi kwa
kuzingatia vipengele vya dhamira, muundo na mtindo. Anabainisha dhamira muhimu
zinazojitokeza katika riwaya hiyo. Kwa upande wa muundo na mtindo, Mbonde
anaonesha kuwa Chachage anatumia kwa ufanisi mbinu-rejeshi; anachanganya
usimulizi na uandishi ili kuileta hadhira karibu na msimuliaji. Aidha, anatumia
lugha fasaha iliyosheheni tamathali, na anaonesha migogoro (labda hiki ni
kipengele cha maudhui kuliko mtindo). Mbonde anadhihirisha kuwa riwaya hiyo
inatumia historia kuakisi mapambano ya leo, na kwamba inashabihiana na ile ya
Alex Haley ya Roots (siyo The Roots) katika kupekua nasaba na
mahusiano ya kiukoo ya makabila mbalimbali ya kusini mwa Tanzania (suala la Roots kuwa riwaya nalo lina mjadala;
wengine huweza kudhani kuwa ni historia).
Kwa hakika wahakiki hawa wawili
wametupatia mahali pazuri pa kuanzia katika kuiangalia riwaya ya Makuwadi.  Makala haya hayakusudiwi kurudia yale
waliyokwishasema vizuri zaidi, bali tutajikita katika suala la Makuwadi wa Soko Huria kama bunilizi ya
kihistoria, jambo ambalo Shivji na Mbonde hawakulizungumzia sana kwa kuwa
halikuwa lengo lao. Chachage mwenyewe, katika mahojiano na Diegner
(tumekwishayataja hapo juu), analipa suala la historia uzito mkubwa kuhusiana
na riwaya yake. Lengo letu si kujadili sifa za riwaya ya kihistoria kidhahania,
bali kuonesha nafasi na umuhimu wa riwaya ya kihistoria katika kuibua riwaya
bora ya Kiswahili ya kimaendeleo, tukitumia Makuwadi
kama kielezo chetu.
2.0
Riwaya ya Kihistoria katika Fasihi ya Kiswahili
Riwaya ya kihistoria ni hadithi
ndefu ya kubuni iliyojikita katika matukio ya kweli ya historia, hasa yaliyo
muhimu kwa taifa au jamii inayohusika, kuyachanganya na matukio ya kubuni, na
kuyapangilia upya kisanii ili kutoa ujumbe fulani kwa jamii inayoandikiwa.  Riwaya ya kihistoria huwa ni jaribio la
kuoanisha mgogoro wa kihistoria na mgogoro wa kisanaa (k.m. wa kibinafsi),
ukweli wa kihistoria na ukweli wa kisanaa, na viumbe wa historia na viumbe wa
sanaa, ili kujenga simulizi yenye maana, ujumbe maridhawa na kumbukumbu ya
kudumu kwa walengwa (Lukacs, 1962; Mulokozi, 1990).
Masimulizi ya kihistoria si jambo
geni katika utamaduni wa Waswahili na Waafrika kwa jumla. Kila jamii
huwasimulia watoto wao juu ya matukio ya zamani yanayowahusu, hususani yale
yanayohusu chimbuko lao, namna walivyofika mahali walipo sasa, harakati
walizozipitia, mahusiano yao na majirani zao, na mapambano yao na maadui zao.
Masimulizi hayo huweza kuwa ni historia ya moja kwa moja, hasa kuhusiana na
matukio ya siku za karibuni, au historia iliyochanganyika na visakale
(kuhusiana na matukio ya zamani zaidi) au visakale vilivyochanganyika na
visasili (kuhusiana na matukio ya kale sana). Historia halisi husahaulika na
kuingia katika kumbo la visakale na visasili kwa kadiri muda unavyopita.  Hiyo ni tabia ya kawaida ya simulizi za
mdomo.
Katika fasihi ya Kiswahili,
simulizi za kihistoria zimekuwapo tangu kale. Vitabu vya Tarihi vinatupa simulizi zilizoandikwa kutokana na mapokeo ya
mdomo, hususani zile zinazowahusu watawala. Ni vitabu vyenye historia finyu
kulingana na malengo yake ya kuhifadhi habari za nasaba za watawala. Masimulizi
ya kihistoria yenye mapana na taarifa zaidi ni yale ya kishairi – hasa yale
yanayopatikana katika tendi. Ya zamani zaidi yanamhusu shujaa Liyongo, na
yalitolewa kwa njia ya nyimbo na mashairi, na pia tendi-simulizi ambazo sasa
zimepotea (Steere, 1870). Zipo pia tendi mashuhuri za miaka ya karibuni, kwa
mfano Utenzi wa  Vita
vya Wadachi Kutamalaki Mrima (Hemed Abdallah, 1895) na Vita vya Maji Maji (Abdulkarim Jamaliddini, 1910; TUKI, 2006),
zinazohusu mapambano ya wananchi kupinga uvamizi na utawala wa Wadachi, na Utenzi wa Vita vya Uhuru (Robert, 1961)
unaosimulia matukio na mwenendo wa Vita vya Pili vya Dunia. Sambamba na tenzi,
zimechapishwa tamthilia kadha za kihistoria tangu miaka ya 1960. Baadhi yake
ni: Kinjeketile (Hussein, 1969) na Mashetani (Hussein, 1971); Mkwawa Mahinya (Nkwera, 1968), Mukwava wa Uhehe (Mulokozi, 1979) na Harakati za Ukombozi (1982).
Ubunilizi wa kihistoria katika
umbo la riwaya hauna historia ndefu kama ulivyo katika ushairi. Kitabu cha Habari za Wakilindi (Ajjemy, 1895)
kinafikiriwa na baadhi ya watu kuwa ndicho riwaya ya kwanza ya Kiswahili. Hata
hivyo, dai hili lina walakini, kwani mtunzi wa masimulizi hayo hakuyakusudia
yawe riwaya, bali aliamini kuwa alikuwa akiandika historia ya Wakilindi,
hususani utawala wa nasaba ya kina Kimweri huko Usambara. Visasili na visakale
vinavyojipenyeza katika masimulizi hayo haviondoi ukweli kuwa yale ni
masimulizi ya kihistoria yanayotokana na simulizi za mdomo na matukio ya
kushuhudiwa na mwandishi mwenyewe, na kwamba mtindo uliotumika ni wa taaluma ya
kijadi ya usimulizi wa historia isiyopambanua visakale na historia halisi.
Hivyo tunaweza kusema kuwa riwaya
halisi ya kwanza ya historia ni ile ya James Mbotela ya Uhuru wa Watumwa (1934). Riwaya hiyo inasimulia juu ya masaibu ya
mateka waliochukuliwa utumwani na baadaye kukombolewa na meli ya Wazungu katika
miongo ya mwisho ya karne ya 19. Mengi yanayosimuliwa ni matukio ya kweli ya
kihistoria, japo bila shaka hapa na pale mtunzi katia chumvi kwa malengo ya
kisanaa. Baada ya hapo hapakutokea riwaya ya kihistoria tena hadi miaka ya 1970.
Baada ya mwaka 1970 riwaya ya
kihistoria katika fasihi ya Kiswahili imejitokeza kwa dhati zaidi. Riwaya ya
Msewe ya Kifo cha Ugenini
iliyochapishwa mwaka 1977 ilihusu kipindi cha uvamizi wa Wadachi  – kipindi ambacho kwa hakika ndicho
kilichohamasisha  kazi nyingi zaidi za
simulizi za kihistoria. Baadaye zilichapishwa riwaya mbili za.Shafi; Kuli (1979) na Kasri ya Mwinyi Fuad (1978). Riwaya hizo zilizohusu migogoro ya
kijamii-kitabaka huko Zanzibar kabla ya mapinduzi ziliisogeza mbele riwaya ya
kihistoria. Riwaya za Kezilahabi za Dunia
Uwanja wa Fujo (EALB, 1975) na Gamba
la Nyoka (EAPL, 1979) vilevile zina sifa fulani za uhistoria, hasa zile
zihusuzo mchakato wa ujenzi wa Ujamaa katika Tanzania katika miaka ya
1967-1977, japo haziingii moja kwa moja katika mkondo huo.
Riwaya za Kezilahabi zilifuatiwa
na riwaya za Said Ahmed Mohamed na M.S. Mohamed za Nyota ya Rehema (Mohamed 1978), na Dunia Mti Mkavu (Ahmed, 1980).
Hizo nazo zina sifa kadha za uhistoria, maana zinaonesha migogoro ya
kijamii-kitabaka ya kipindi cha kabla ya Mapinduzi nchini Zanzibar. Na ingawa
riwaya hizo zilitoa mchango mkubwa katika kuitajirisha na kuikomaza riwaya ya
Kiswahili, bado fani ya riwaya ya kihistoria, hadi mwaka 1990, ilikuwa bado
haijaenea sana.
Kutokana na hali hii, mwishoni mwa
miaka ya 1980 jopo dogo la wapenda fasihi, likiratibiwa na Bi. Elieshi Lema,
ambaye wakati huo alikuwa mhairiri katika Shirika la Uchapishaji Vitabu la
Tanzania (TPH), lilianza kukutana nyumbani kwa Bi. Lema mara mbili kwa wiki saa
za jioni kujadili na kupanga namna ya kustawisha riwaya ya kihistoria kwa
Kiswahili, hususani kwa ajili ya wasomaji vijana. Wanajopo walikubaliana wao
wenyewe waandike riwaya kama tano za kihistoria zenye kuzingatia matukio
yafuatayo: 1. Biashara ya Watumwa (mwandishi A. Lihamba); 2. Vita vya Wahehe
dhidi ya Wadachi (mwandishi M.M. Mulokozi); 3. Vita vya Wachagga dhidi ya
Wadachi – Mangi Meli – (mwandishi: R. Mabala), na Vita vya Maji Maji (Mwandishi
E. Kezilahabi). Wanajopo waligawiana kazi na kuanza kuandika. Walipata msaada
mdogo kutoka shirika la Kanada la Misaada ya Maendeleo kupitia Elimu (CODE)
ambalo wakati huo kiongozi wake wa ofisi ya Afrika ya Mashariki alikuwa Scott
Walter. Afisa huyo alitoa msukumo mkubwa uliowawezesha wahusika kufanya utafiti
mdogo wa uwandani kuhusiana na mada hizo. Kutokana na mchakato huo, kufikia
mwaka 1991 miswada viwili ya hadithi za historia kwa picha na maelezo
mafupimafupi ilipatikana: Miswada hiyo ni Wimbo
wa Sokomoko (A. Lihamba) kuhusu biashara ya watumwa; na Ngoma ya Mianzi (M.M. Mulokozi) kuhusu
uvamizi wa Wadachi huko Kilosa, uliofuatiwa na vita vya Lugalo vya 1891.
Punde ilionekana kuwa shughuli ya
kuandika vitabu kwa ajili ya watoto na vijana ilikuwa nzito, na huenda
isingewezekana kuratibiwa na Bi. Lema na shirika la CODE, kwa ufanisi bila kuwa
na chombo mahsusi cha kudumu. Ikapendekezwa na kukubaliwa kuwa uanzishwe Mradi
wa kuratibu shughuli hiyo ambao awali ungegharimiwa na CODE. Huo ukawa ndio
mwanzo wa kuzaliwa kwa Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania (Children’s Book Project – CBP) mwaka
1991. Vitabu viwili vya jopo hili vikawa miongoni mwa machapisho ya mwanzo ya
Mradi huo. Hivi leo jopo hilo halipo tena, na riwaya kuhusu Mangi Meli na Vita
vya Maji Maji hazijaandikwa, lakini Mradi umekua na kuzaa vitabu vingi zaidi
(kama 300) na shughuli nyingi zaidi, zikiwamo za kuratbu usomaji shuleni.
Juhudi za CBP
ziliwezesha kuchapishwa kwa riwaya tatu za kihistoria kwa Kiswahili kwa ajili
ya vijana zilizoandikwa na M.M. Mulokozi. Riwaya hizo ni: Ngome ya Mianzi (1990), Ngoma
ya Mianzi (1991) na Moto wa Mianzi
(1996). Lengo lake  lilikuwa ni kuwapa
vijana mwamko wa kupenda kusoma na kutafiti historia ya jamii zao kama njia
mojawapo ya kujenga mapenzi kwa nchi (uzalendo) na chuki kwa adui, kujiamini na
kujithamini. Bahati mbaya si waandishi wengi katika Mradi waliojitokeza
kuendeleza mkondo huu wa uandishi, isipokuwa Dumea aliyeandika novela ya Usiku wa Balaa (E&D, 2009).
.
Nje ya Mradi, uandishi wa riwaya
ya kihistoria ulifikia hatua ya juu ilipochapishwa riwaya ya Bernard Mapalala
ya Kwa Heri Iselamagazi (TPH 1992).
Riwaya hiyo ilitupeleka katika historia ya Mtemi Mirambo na warugaruga wake
katika muktadha wa ujenzi wa himaya ya Kinyamwezi kwenye karne ya 19. Ni riwaya
nzuri ambayo haijapata kutendewa haki (kwa kuchunguzwa kitaaluma na kutumika
kwa mapana) na wahakiki, watafiti na wakuza mitaala. Iselamagazi ilifuatiwa na riwaya mbili za Shafi: Vuta N’kuvute (1999) na Haini (2003). Zote mbili zinahusu
matukio yenye maana kubwa kwa majaaliwa ya Zanzibar na Wazanzibari, na
zinatuingiza katika undani wa matatizo ya mapinduzi ya Zanzibar ambayo
yaliwageuka wale waliojitoa muhanga kuyatengeneza.  Suala la utawala wa chuma (ambao dola
inajaribu kuuhalalisha kwa kurejelea historia ya mapinduzi) dhidi ya haki za
binadamu linachanganuliwa vilivyo katika riwaya ya Haini. Riwaya nyingine ya kipindi hiki iliyojaribu kusawiri
historia ya Tanzania kisanaa ni ile ya Miradi
Bubu ya Wazalendo. (1995). Riwaya hiyo, kama ile ya Kiingereza ya M.
Vassanji The Gunny Sack (1989),
ilijaribu kusimulia kisanaa historia ya Tanganyika/Tanzania tangu enzi za
ukoloni hadi kudai uhuru na ujenzi wa ujamaa, hadi kushindwa kwa ujamaa na
kustaafu kwa Mwalimu J.K. Nyerere. Kama riwaya ya Vassanji, riwaya hii inatumia
wahusika wa kutoka makundi mbalimbali ya kijamii-kitabaka ili kuonesha
majaaliwa ya makundi hayo katika Tanzania “huru”. Tunaoneshwa kuwa wafanyakazi
wa kawaida na wakulima hawakunufaika na sera za Ujamaa; walionufaika zadii ni
tabaka jipya la vibwanyenye wa dola (kina Nzoka) na wafanya biashara. Kama
anavyoeleza Mbonde (2004) kwa usahihi, ni vizuri kuisoma riwaya hii sambamba na
riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria,
maana maudhui yake yanakamilishana.
Kwa jumla tunaweza kusema kuwa
miaka ya 1990 utanzu wa riwaya ya kihistoria katika fasihi ya Kiswahili umekua
na kujipatia nafasi muhimu katika historia ya fasihi hiyo. Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria imetokea katika
muktadha huu wa kifasihi. Lakini, tofauti na riwaya zilizotangulia, Makuwadi imepanua mawanda na kutazama
hata nje ya Tanzania katika kujaribu kulifafanua tatizo kuu la kitaifa la enzi
zetu.
Kama wanafasihi waliomtangulia,
Chachage alifahamu umuhimu wa historia katika harakati za maendeleo na ukombozi
wetu. Alijua kuwa kosa kubwa mojawapo linalofanywa na matabaka tawala ya sasa
ya Afrika ni kudharau au kupuuza historia. Baadhi yamediriki hata kufuta somo
la historia katika mitaala ya shule (mfano: Tanzania wakati wa Awamu ya Tatu),
na mengi bado yanafundisha historia iliyoasisiwa na mkoloni – ile ya ustaarabu
wa mzungu na jusura zake katika bara la Afrika. Riwaya hii inatuonesha kuwa
kudharau historia ni hatari, kwa kuwa ni kukinyima kizazi kipya haki ya
kujitambua na kujua tulikotoka, tulipo na tuendako. Bila kujua matatizo yetu ya
kihistoria ya nyuma na ya leo, ni vigumu kubuni njia sahihi ya kufuata kwa siku
zijazo.  Maana adui wetu wa zamani, wa
sasa, na wa kesho bado ni yuleyule, na mbinu zake hazijabadilika sana.
Tunaposahau historia tunaishia kumkumbatia adui huyo tukidhani ni rafiki, na
madhara tunayoyapata katika uhusiano wetu naye yanazidi kuongezeka.
Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria inajaribu kuturudisha nyuma katika mizizi ya
kihistoria ya matatizo yetu ya leo ili historia hiyo iwe ni mwega wa
kutuwezesha kusonga mbele katika mapambano yetu ya kudumu ya kutafuta ukombozi
kamili na maisha bora kwa ajili ya jamii zetu. Katika kufanya hivyo, Chachage
anaturudisha katika jadi bora ya wahenga wetu ya kuhifadhi historia na
kuipokeza kwa vizazi vyao; jadi ambayo ilipigwa vita na ikakaribia kuuliwa na
tawala za kikoloni na asasi zake kwa kuwa zilitambua fika hatari za mwamko wa
kihistoria wa wenyeji kwa utamalaki wao.
Kwa ufupi, huu ndio muktadha wa
kifasihi uliochipuza riwaya ya Chachage ya Makuwadi
wa Soko Huria.  Sasa tuiangalie
riwaya yenyewe.
3.0 Makuwadi
wa Soko Huria
Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria iliandikwa na hayati Chachage S. Chachage
mwaka 1999-2000 na kuchapishwa na E &
D Publishers mwaka 2002. Hii ndiyo riwaya ya mwisho inayofahamika
aliyoiandika Hayati Chachage kabla hajafariki mwaka 2006, ingawa katika
mahojiano yake na Diegner anasema wakati huo (2004) alikuwa amemaliza kuandika
sura kama mbili za riwaya nyingine. Riwaya hii iliandikwa wakati wa kipindi cha
ukomavu wa utandawazi wa Kimagharibi na Kimashariki katika Tanzania na Afrika,
kuvamiwa kwa uchumi wa Tanzania na “wawekezaji”, pamoja na mawakala wao wa
kidini na kitamaduni kutoka Magharibi na Mashariki, kuundwa kwa utatu usio
mtakatifu wa mabepari wenyeji, mabepari wa kigeni, na viongozi wa serikali ili
kushirikiana kupora rasilimali za nchi,
na hivyo kujigeuza kwa tabaka la watawala kuwa mafisadi wakubwa na mawakala
wa ubepari wa kigeni dhidi ya wananchi. Mchakato huu uliambatana na
kufukarishwa kwa wananchi walio wengi kutokana na kufungwa kwa viwanda,
kufukuzwa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi katika maeneo yao ya jadi ili
kupisha “wawekezaji”,  kutelekezwa kwa
watoto wa maskini katika mfumo wa elimu (kuwapa baadhi yao mikopo ya elimu
badala ya ruzuku), na kuvurugika kwa vyama vya ushirika na bei za mazao ya
wakulima wadogowadogo. Mwenendo huu ulimwudhi sana Chachage, ambaye aghalabu
alikuwa akiandika makala na kuhutubia kuhusu utandawazi, ambao aliuita
“utandawizi.” Riwaya yake ya Makuwadi wa
Soko Huria ilikuwa ni mwendelezo wa mapambano yake dhidi ya ubepari na
utandawazi katika medani ya kifasihi.
3.1 Muhtasari wa Riwaya
Hadithi inaanza na “kifungua
pazia” ambacho kinaelezea kuhusu kutekwa kwa Mjuba na Sifuni (ambao ni
waandishi wa habari) na kundi la Kaboko kutokana na kuandika habari zenye
kufichua njama za kukwepa kulipa kodi. Inamalizika na “kifunga-pazia” ambapo
kesi ya kutekwa kwa Mjuba na Sifuni imepanuka na kuwa kesi ya mauaji yenye
kuhusisha masuala mengi na watu wengi, wakiwamo watu wakubwa katika uchumi na
utawala. Baina ya “kifungua-pazia” na “kifunga pazia” kuna sura 12 zenye
masimulizi kuhusu maisha, masaibu na mahusiano ya wahusika wakuu wa hadithi:
Fidelis, Mjuba, Sifuni na Binti Wenga; na wahusika muhimu wengine –  kina Amina,
Japhet Lupocho,  Joshua Lupocho,
Mooney, Alibhai, Chaurembo, Sorrenson, Sadiki Mazengo, Hakimu Mazengo, Mzee
Mrisho, Mzee Miraji, na Mzee Abdurahaman. Maisha na masaibu yao yanapambanishwa
na yale ya wananchi wa vijijini (Delta ya Rufiji na Ruhimba) kwa upande mmoja,
na mizengwe na vitendo vya mabepari wa kimataifa na mawakala wao wa ndani kwa
upande mwingine. Waandishi wa habari wanakuwa ndio kiungo na kioo cha kumulikia
uhusiano wa kihasama uliopo kati ya pande kuu mbili: upande wa wananchi
(wakulima, wavuvi, wafugaji) na upande wa mabepari wa dunia au watandawazaji
(wawekezaji, wahisani, “wataalamu”) na “Makuwadi” wao wa ndani.
Waandishi wa habari za mazingira
wenye mwelekeo wa kimaendeleo: Fidelis, Mjuba, Sifuni na Saada wanaamua kwenda
Rufiji kufuatilia suala la “Mradi wa Kamba” Rufiji, hususani baada ya
kuhudhuria Mkutano wa Wanarufiji uliofanyika Dar es Salaam kujadili Mradi
huo.  Wanaahidiwa msaada wa fedha na
wahisani kupitia kwa Sorrenson, afisa wa Kiswidi mwenye kazi ya kuratibu suala
hilo.
Safari ya Mjuba na wenzake
inawekewa vikwazo na Wizara ya Misitu na wawekezaji ambao hawataki habari za
mipango yao na mapambano yao na wananchi huko Rufiji zifahamike. Hata hivyo,
waandishi wa habari wanafanikiwa kufika Rufiji katika kijiji cha Nyamisati na
kupokewa kwa uhasama na viongozi wa kijiji hadi wanapodhihirisha kuwa wao wako
upande wa wananchi na wala hawakutumwa na wawekezaji au serikali. Wanaelezwa
masuala yote yanayohusu Mradi wa Kamba na uchumi wa delta wa mikoko na uvuvi,
na wanatembezwa katika visiwa mbalimbali kujionea wenyewe hali ilivyo.
Wanaelezwa pia historia kuhusu maisha na mapambano ya wananchi wa delta na
Tanzania nzima kupinga uvamizi na unyonyaji wa wageni.
Safari hii inatokea pia kuwa ni ya
ugunduzi kwa Fidelis, ambaye anakutana na ndugu zake waishio Rufiji ambao
alikuwa hawafahamu. Ni safari ya utakaso pia kwa wale walioikosea jamii – ama
kwa usaliti ama kwa kuvunja miiko. Wanarejea Dar es Salaam huku Fidelis akiwa
ameufahamu ukoo wake na akiwa ameandamana na baadhi ya ndugu zake wa Rufiji.
Safari hii ya Rufiji ya kusaka
habari na ufahamu kutoka kwa wananchi kuhusu matatizo yao ndiyo mkondo mkuu wa
hadithi. Mikondo mingine inahusu hadithi binafsi za wahusika wakuu, hasa
Fidelis, Mjuba, Sifuni, Amina, Binti Wenga, Japhet Lupocho,  Joshua Lupocho, Paul Mooney, Alibhai,
Chaurembo, Sorrenson, Sadiki Mzengo, na wengine. Masimulizi kuwahusu watu hawa
na wasifu wao na matazamio yao yanatuingiza katika undani wa mahusiano na hisia
zao za mapenzi na za chuki, za upevukaji wao kwa kadiri hadithi inavyoendelea,
hadi kufikia hatua ya baadhi yao kujitambua wao ni nani  (Japhet, Fidelis, Joshua, Amina), baadhi
kubadilika kimtazamo (Sorrenson, Japhet, Salama – mkewe Mjuba, na Oscar Mayowe
– mzinzi anayegeuka mlokole), na baadhi kuathirika kisaikolojia kutokana na
aibu ya usaliti na uvunjaji miiko hadi kufikia hatua ya kujaribu kujiua
(Japhet).
Hatimaye tunaona mabadiliko
mwishoni mwa hadithi: baadhi ya waovu wanaadhibiwa, wema wanatunukiwa, na
mshikamano wa wananchi na “wasomi” wapenda maendeleo unakuwa umejengeka na
kuimarika. Tunabaki na hisia kuwa msingi wa mapambano yajayo tayari umejengeka,
na kwamba “Makuwadi” na mabwana zao watakuwa na kazi ngumu sana katika
kuendeleza ajenda yao yenye madhara kwa wanyonge.
3.2 Mawazo Makuu
Muhtasari huu unaonesha kwamba
mgogoro wa riwaya hii una pande tatu: Upande wa wananchi wa Rufiji na Ruhimba
ambao ndio waathirika wa mfumo wa ubinafsishaji na uhuria unaosimikwa; upande
wa wawekezaji na mabepari wa kigeni na mawakala wao wenyeji (wa kisiasa na wa
kibiashara), ambao ndio wanaopambana na wananchi kwa sera na vitendo vyao; na
upande wa waandishi wa habari, ambao wako katikati na wamegawanyika kati ya
wale wanaowatetea wananchi (Mjuba, Sifuni, Fidelis) na wale wanaowatumikia
maadui wa wananchi (Mwenerumango, Jonathan Massawe, na Alhaji Seif Said). Kundi
hili la waandishi linawakilisha kundi au tabaka dogo la wasomi na vibwanyenye
uchwara kwa ujumla, na mgawanyiko wao unaakisi mgawanyiko halisi ndani ya
tabaka hilo miongoni mwa Watanzania. Hata hivyo, tabaka hili ndilo lenye jukumu
la kuuchunguza na kuuelezea mwenendo wa kijamii na mivuvumko iliyomo,
kutuonesha mahusiano ya kihasama ya makundi ya kijamii,  kiini chake na mustakabali wake. Hivyo
tunaiona jamii ya Watanzania na migogoro yake kupitia katika macho, mawazo,
uwezo na udhaifu wa kundi hili. Mipaka ya muono wa kundi hili la waandishi wa
habari ndio unaojenga mipaka ya muono wa riwaya hii. Je, kwa nini Chachage
kalichagua tabaka hili, ambalo aghalabu hulegalega kimsimamo na bila shaka lina
ufinyu wa kimawazo, liwe jicho letu la kuiangalia jamii yetu? Hatujui; labda
kwa kuwa yeye mwenyewe, akiwa ni msomi na mtafiti, alikuwa katika kundi hili,
au uhusiano wake na wale aliowatafiti (wakulima na wavuvi) haukuwa tofauti na
wa wahusika hawa na wananchi wanaoandika habari zao.
Mwandishi anatuonesha kuwa
ubinafsishaji na uhuria si sera zilizobuniwa na watawala wetu hivi karibuni,
bali zina mizizi yake katika historia ya kutawaliwa kwetu, ya ubeberu, ambao
kwa sasa ndio unaoitwa utandawazi. Hivyo, kupitia kwa mhusika Fidelis
Msakapanofu anatushauri turejee huko kwenye mizizi iwapo tunataka kuielewa
vyema tanzia ya Mwafrika wa leo:
“Kwa nini usianzie mwanzo wa hayo mambo, kule
yalikoanzia? Lakini, akili inaniuliza, mwanzo huo ndio upi?” (uk. 50)
Binti Wenga, na wazee wengine,
kina Mzee Mrisho, Mzee Abdurahaman na Mzee Miraji, na Bi. Khadija, wanaletwa
katika masimulizi haya wakiwa na jukumu la kuturejesha huko tulikotoka, kutupa
historia ya mababu na mabibi zetu, ya namna tulivyovamiwa na kuporwa tangu enzi
za biashara ya watumwa na ukoloni wa Wadachi na Waingereza, na mwitiko wa hao
wahenga  wetu kwa ubeberu wa wakati wao.
Riwaya, kupitia masimulizi ya
wazee hao, inatuonesha kuwa uporaji wa ardhi na maliasili za nchi hii ulianza
mapema kabisa, na ulifanywa na Wazungu na wengineo kwa zaidi ya miaka mia, na
kwamba wananchi, ambao kabla ya hapo walikuwa na maingiliano na uhusiano mzuri
wa kibiashara na kijamii, walivurugwa na ukoloni na kutenganishwa na kugeuzwa tribes. (Neno la Kiingereza “tribe”, kwa
namna walivyolitumia, halimo katika lugha ya Kiswahili, na si tafsiri ya neno
“kabila.” Tribe linabeba dhana ya
dharau na matusi ambayo haimo katika neno “kabila”). Hata hivyo, wananchi
wenyewe waligundua njama hizo za kuwagawa mapema na wakaamua kuungana ili
kupambana na adui yao.  Matokeo ya
mchakato huo yalikuwa ni Vita vya Maji Maji.
Mto wa Rufiji na matawi yake,
ambao sasa unaporwa na wageni, kina Mooney na Vangalatus, ukawa ndio kiungo
kikuu cha wananchi na barabara kuu iliyopeleka ujumbe wa ukombozi hadi pembe
zote za kusini mwa Tanzania:
Tulikuwa tunasafiri katika mto ambao maji yake
yalikuwa yamesafiri zaidi ya maili mia nne, mto mkubwa kuliko yote nchini ambao
sehemu kubwa ya maji yake yalitokea mto Ruaha ulioanzia Mbeya, mto Kilombero
ambao ulianzia sehemu za Njombe kama mto Ruhuji na mto Luwengu ulioanzia sehemu
za Ruvuma. Mto huu uliwaunganisha watu wa sehemu mbalimbali, nao wakajihisi
kwamba ni wamoja, na labda ilikuwa ni kwa sababu hii, watu wote wa sehemu hizi
waliungana pamoja wakati wa vita vya Maji Maji (uk. 219).
Hadithi hii ni kielezo cha picha
hii ya muungano wa watu kufuata Mto Rufiji: inahuisha, kupitia kwa wahusika
wakuu wa familia za kina Lupocho Msakapanofu, Wenga, na Nguvumali, muungano huo
wa Maji Maji wa jamii za kutoka Uzaramo hadi Rufiji hadi Ubena (Njombe), Songea
mpaka Mbamba Bay. Huu ni mtandao unaounganisha jamii za Wazaramo na nyinginezo
za upwa wa Mzizima kama vile Wandengereko, Wamatumbi, Wangindo, Waluguru,
Wamakonde, Wamakua, Wangoni, Wabena, Wapangwa, Wandendeule, Wamatengo, Wakinga,
n.k. Ni muungano unaojumuisha watu wa imani mbalimbali – za jadi na Uislamu.
Familia ya kina Lupocho ni kielezo cha muungano huu:  mababu na mabibi zao kutoka Mbamba Bay
(Msakapanofu na Wenga Mhalule) walikutana katika harakati za mapambano na wazee
wa Rufiji (Nguvumali na Samadi) na baadaye watoto wao wakaoana na kuzaa wana na
wajukuu ambao walisambaa kwenda kuishi Rufiji, Songea, Njombe, Tabora na Dar es
Salaam, na wakawa hawafahamiani. Hatimaye ndugu hao wanakutanishwa tena na
harakati za kupinga ufugaji wa kamba Rufiji na uuzaji wa ardhi Ruhemba. Baadhi
yao (Japhet na Amina) wanataka kuoana bila kujua kuwa ni ndugu, na wanapogundua
udugu wao inabidi lifanyike tambiko la utakaso). Hivyo historia ya familia hii
imebeba historia ya nchi na misukosuko yake.
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa
riwaya hii ni istiara ya vuguvugu la ukombozi la Maji Maji katika mazingira ya
leo: kutoka Rufiji hadi Ungoni hadi Mbamba Bay. Ni kama mwandishi anataka
kutuambia kuwa kama ambavyo babu zetu waliungana bila kujali mipaka, lugha au
kabila ili kupambana na ukoloni, sisi wajukuu zao pia tunawajibika kufuata
mfano wao na kuungana ili kupambana na utandawazi unaokuja katika umbo la
uhuria, uwekezaji wa kigeni, ubinafsishaji na ukuwadi.  Mto wa Rufiji uwe ni kiungo chetu kama
ulivyokuwa enzi za Maji Maji.
Ukombozi huu, kwa mujibu wa riwaya
hii, sharti ujengwe katika utaifa mpana ambao unavuka mipaka ya kabila, na hata
taifa, na kuwa Upanafrika (Umajumui wa Afika). Maana Afrika ni moja na Waafrika
ni watu walewale popote pale walipo. Mawazo ya Mjuba huenda yanawakilisha
mawazo ya mwandishi: Wakombozi wa kweli wa nchi yetu hawakuipigania Tanganyika
tu, bali mama Afrika:
Hao walikuwa watu kama akina Dennis Phombeah, akina
Austin Shaba, akina Oscar Kambona, na wengine – watu waliomjua mama mmoja tu
bila kujali kama walizaliwa wapi. Naye alikuwa mama Afrika (uk. 213).
Sentensi ya mwisho inakuwa na
maana zaidi tunapokumbuka (kwa wale wenye kufahamu) kuwa baadhi ya mashujaa
walioipigania Tanganyika anaowataja Chachage, kwa mfano Eric Fiah na Osare
Otango, hawakuwa Watanganyika. Osare Otango, ambaye aliendesha mapambano huko
Tanga dhidi ya walowezi, alikuwa Mmaragoli wa Kenya.
Hivyo riwaya hii inatusogeza mbele
na kutupeleka kwenye dhana ya umoja wa Afrika iliyohubiriwa na kina William du
Bois, George Padmore, Kwame Nkrumah na Julius Nyerere.
Uhuria ni zao la utandawazi, na
unakuja na sura mbalimbali. Kuna sura ya uchumi – ubinafsishaji na uwekezaji wa
kigeni. Wananchi wananyang’anywa ardhi na maeneo yao, wanapewa wawekezaji
kutoka nje. Kuna utalii – mbuga za wanyama zinabinafsishwa, wanyama wanauliwa
kwa ajili ya starehe za wawindaji matajiri kutoka Magharibi (Rais Roosevelt),
na kuna udini – makanisa ya kilokole (bila shaka kutokea Marekani) yanaenezwa
nchi nzima na kuwateka na kuwapumbaza watu. Ndoa ya Mjuba na Salama inavunjika
kutokana na kuokoka kwa Salama. Na haya yote yanawezekana kwa kuwa wapo watu –
wenyeji, wafanyabiashara na wanasiasa, ambao wako tayari kununuliwa na wageni
na kuiuza nchi kwa manufaa yao binafsi. Kina Japhet Lupocho, Chaurembo,  Jonathan Massawe, Moddy Mwenerumango,
Alibhai, Njovu Luhala – Mbunge, wako katika mkumbo huo. Hao ndio wanaoitwa Makuwadi,
yaani “washenga-nuksi” wanaosaidia kufanikisha mipango ya waporaji wa kigeni
hapa nchini.
Mh. Luhala anawakilisha wanasiasa,
na tunaona namna anavyoshiriki katika kuuza/kubinafsisha ardhi ya wananchi huko
Ruhimba, na anavyokataa kukutana nao wanapokuja kumwona Dodoma. Hatimaye,
wabunge wanapokubali kukutana na wananchi, wanadai posho, na wanapoona hakuna
posho, wanataka mkutano uishe haraka ili wawahi nyama choma mnadani!
Uhuria unaambatana na ufisadi.
Rushwa, ukwepaji kodi, magendo, uuzaji wa madawa ya kulevya, usaliti na
upotoshaji wa habari vimetawala. Mtandao wa ufisadi unawahusisha kina Alfred
Chaurembo (kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali-NGOs), Roshan Alibhai, A.
Kongoro, K. Kongoro, Maua Mutabingwa na Sadiki Mazengo. Pia, Wazungu wa
mashirika ya “hisani” wanaishi kwa anasa kwa kutumia misaada ya wakimbizi (uk.
185).
Kuna uharibifu mkubwa wa
mazingira; wawindaji wanateketeza wanyama wa pori (Roosevelt, Pretorius na
Louis); mikoko katika delta inakatwa bila mipangilio; samaki wanavuliwa na
kuuliwa ovyo.
Kuna unyanyasaji wa wanawake, na
mwenendo wa kuwanyima haki yao ya ardhi. Wanawake wa Ruhimba wananyang’anywa
ardhi yao na uongozi wa wilaya bila malipo wakati wanaume wanalipwa (uk. 45).
Kwa wananchi, uhuria huu
unaonekana kuwa wa bandia kwa kuwa unawanyang’anya wananchi haki yao na
kuwakabidhi wageni badala ya kuruhusu ushindani halali ambao unapaswa kutoa
nafasi kwa ushirikiano pia miongoni mwa umma (uk. 199). Mzawa wa Rufiji
anayeleta mitambo yake kuwekeza pale Rufiji anakataliwa na serikali wakati
mgeni (Mgiriki) anakubaliwa.
Kwa jumla, tunaweza kusema kwamba
riwaya hii inasawiri dhana ya uhuria na madhara yake kwa wananchi wa kawaida
(wakulima/wavuvi/wafugaji/ wachimba madini). Mfumo mzima wa uhuria unasailiwa
kwa mtazamo wa umma – wa walio wengi, kuonesha nani ananufaika, na nani
anadhurika. Riwaya inadhihirisha kuwa uhuria ni mkono wa utandawazi ambao nao
ni mwendelezo wa ubeberu wa tangu karne ya kumi na tisa na hata kabla.
Jina lenyewe la riwaya linabeba
ujumbe mzito: “Makuwadi (makuwadi) wa soko huria” ni usemi unaowasawiri waasisi
na waendelezaji wa mfumo wa soko huria kama watu waovu wanaohudumia mfumo
uliokosa uadilifu. “Makuwadi” ni watu wafanyao kazi ya kuwatafutia watu wengine
wenzi wa kufanya nao umalaya au uzinzi kwa ujira maalumu. Ni mawakala wa
ukahaba. Katika riwaya hii Chachage anawalinganisha mawakala wa soko huria na
mawakala hao wa uzinifu kwa lengo la kuonesha kwamba hawatofautiani katika kazi
zao na madhara yao kwa jamii. Na tunaoneshwa wazi kwamba mawakala wa soko
huria, kama walivyo makuwadi halisi, wanafanya biashara ya kuuza watu kwa mabepari wa kigeni.  Hivyo jina la riwaya hii ni kauli thabiti na
hasi ya mwandishi kuhusu mfumo mzima wa ubepari huria anaouchambua. Ili
kujinusuru kutokana na hali hii, mwandishi anatuasa turejee nyuma katika
historia yetu, tujue kwa nini haya yametokea, na tujifunze kutoka kwa wahenga
wetu namna ya kupambana na mfumo huu wakati huo huo tukibuni mbinu mpya
zinazolingana na hali na enzi zetu.
Udhaifu wa usawiri wa mgogoro mkuu
wa riwaya hii unatokana na ufinyu wa mtazamo na uwezo wa tabaka linalotumika
kuendeleza na kufafanua mapambano haya kwa msomaji – tabaka la vibwanyenye
wasomi (waandishi wa habari). Hili ni tabaka tegemezi ambalo takriban shughuli
zake za kimaendeleo zinategemea misaada ya wahisani. Fidelis, Mjuba na wenzao
wanakwenda Rufiji na kwingineko na kuchunguza madhara ya uhuria kwa msaada wa
shirika la Kiswidi la Sorrenson. Bila shirika hilo hawawezi kufanya kitu. Huu
ndio udhaifu na unyonge wa tabaka hili na asasi zake.  Hivyo ni kejeli na ni njozi kwamba chombo cha
utandawazi–mashirika ya hisani–ndicho kinachotumika kuuchambua na kuupiga vita
utandawazi huo. Je, kitafanikiwa?
Mbali na kiwango hiki cha
kijamii-kisiasa cha masimulizi ya riwaya hii, kuna kiwango cha binafsi cha
mahaba kati ya jozi mbili za wahusika, ambao wote bado ni vijana: Mjuba+Sifuni;
Makoba+Amina. Safari yao ya kutafuta maarifa na taarifa inakuwa pia ni safari
ya kujigundua kuwa wanapendana na kukomaza mapenzi yao hadi kufikia hatua ya
kuoana. Ni hitimisho murua la uhusiano wao unaojengwa katika mapambano.
Chachage S. Chachage anatumia
mbinu nyingi za kisanaa na kimasimulizi ili kutimiza malengo yake. Mbinu kuu
anayoitumia ni uchanganyaji wa ubunifu na uhistoria, yaani uchanganyaji wa
historia halisi na mambo ya kubuni, wakiwemo watu halisi na wa kubuni.  Mbinu hii inafanikiwa kuileta hadithi karibu
zaidi na msomaji, hasa wa Tanzania, kiwakati na kihisia. Tunahisi kuwa
tunachokisoma ni habari za kweli kama zile za magazetini au katika vitabu vya
historia. Watu halisi waliopata kuishi, kama Kinjikitile, Pretorius, Nguvumali
na Nyerere, na hata ambao bado wanaishi (wakati kitabu kinaandikwa), kama Issa
Shivji na Edward Barongo, wanapambanishwa na kuingiliana na wahusika wa kubuni
kama Binti Wenga, Japhet Lupocho, Mazengo na wengineo. Mchanganyiko huu
unakolezwa na mbinu ya udokezi (allusion)
ambayo inaifinya historia katika maelezo au madokezo mafupi mafupi. Hii ina
maana kwamba msomaji wa riwaya hii sharti awe na welewa mpana kiasi wa historia
na habari nyinginezo za nchi hii, vinginevyo anaweza asiupate vilivyo undani wa
baadhi ya maelezo na masimulizi. Kwa mfano, madokezo kuhusu Mganga Nguvumali,
Osare Otango, madawa na mizimu ya Maji Maji, na wapigania uhuru kama Phombeah
na Abduwahid Sykes yana maana zaidi kwa mtu mwenye fununu ya kutosha kuhusu
watu hao.
Mafanikio haya ya kimaudhui
yanaungana pia na mafanikio katika kujenga taharuki na mvuto. Riwaya hii
inasomeka vizuri na haraka, angalau kwa msomaji aliyepevuka kiasi. Aidha, mara
kwa mara mwandishi anaingiza ucheshi, lakini wenye maana, ili msomaji asichoke.
Mfano ni ile michapo ya “Padri wa Musoma” (Sura ya 6: 136-7) na “Mzungu Kala
Fenesi” (Sura ya 7: 145-7).
Matumizi ya kejeli hapa na pale
pia yanaongeza ucheshi. Kwa mfano, uk. 287 tunaambiwa: “nani asiyejua mchango
wa wawekezaji hawa katika kuinua uchumi wa nchi?” Lakini kusudi la riwaya ni
kinyume chake: ni kutuonesha mchango wa wawekezaji katika kuudidimiza uchumi wa nchi!
Riwaya hii inazo dosari kadha za
lugha na mtindo. Mathalan, neno “ibura” linatumika sehemu nyingi kama kivumishi
ilihali halipaswi kutumika hivyo. (Mfano: hali ngeni ibura ilimwingia moyoni” –
uk. 203). Kadhalika, kuna makosa mengi kiasi ya tahjia na matumizi ya lugha
ambayo yangeweza kusahihishwa na mhariri makini. Mifano ni mingi, hapa tutatoa
michache tu:
·
“Makuwadi”
badala ya “makuwadi” (mahali pengi)
·
“maaluni” badala ya “maluuni” (uk. 13)
·
“ngombe” badala ya “ng’ombe” (uk. 14)
·
“karatasi zingine” badala ya “karatasi nyingine” (uk.
19)
·
“mmojawao” badala ya “mmoja wao” (uk. 23)
·
“Al-Bussaidy na na ukoo”  badala ya “Al-Bussaidy na ukoo” (uk. 53)
·
“asili ya Kidachi” badala ya “asili ya Kiholanzi”
(uk. 53)
·
“askari wa kijerumani” badala ya “askari wa
Kijerumani” (uk. 54)
·
“mume wa baba yangu mkubwa” badala ya…?, n.k.
Hata hivyo, haya ni matatizo
madogo. Tatizo kubwa zaidi ni la usimuliaji. Mwandishi kaamua kutumia nafsi ya
kwanza ya usimulizi kupitia mhusika mmoja: Fidelis Mvumi. Usimulizi wa nafsi ya
kwanza unaitwa usimulizi-tinde, kwa kuwa una mipaka yake ambayo inamnyima uhuru
mwandishi. Mathalan, haiwezekani kuelezea mambo ambayo msimulizi hakuyashuhudia
au kuyashiriki, na wala haiwezekani kueleza, kama afanyavyo Fidelis, mambo
yaliyomo moyoni au katika fikra za wahusika wengine. Hayo yanaweza kufanywa tu
katika usimulizi maizi (omniscient)
ambao unawezekana tu katika nafsi ya tatu. Lakini  katika riwaya hii tunamwona Fidelis
akisimulia habari za mawazoni mwa wahusika wengine bila wasiwasi – yaani akiwa
msimulizi maizi ambaye kihalisi ni tinde! (Mifano; Sura ya 4.III – fikira za
Japhet. Pia kur. 212-216 – mawazo ya Mjuba na Sifuni). Hii ni dosari.
Dosari nyingine ni ile ya kutumia
wahusika kama Binti Wenga kuelezea historia na kufanya uchambuzi wa matatizo ya
maeneo yanayohusika kwa namna ambayo haielekei kusadifu uzoevu wao wa
kitaaluma. Masimulizi ya watu wa kijijini kwa kawaida huwa na umbile tofauti na
yale ya wasomi au waandishi wa vitabu (ambao hutumia marejeleo, huelezea miaka
ya matukio n.k.). Wasimuliaji wa mdomo hutumia mbinu simulizi, ambazo mara
nyingi huepuka kutaja miaka na tarehe, na si rahisi kwao kuzungumzia mambo ya
mbali kama Ulaya. Katika riwaya hii, sifa hizi zimechanganywa katika mtu mmoja,
na kumfanya msomaji aamini kwamba anayeongea si Binti Wenga bali ni Chachage
mwenyewe kupitia kwa mhusika huyo (kur. 67-8).
4.0  Hitimisho
Mbali na dosari chache hizi,
riwaya hii ni mchango wa pekee kabisa katika fasihi ya Kiswahili. Kwa hakika,
riwaya hii ni majumuisho ya kazi, fikra, mawazo, mtazamo, mawanio na harakati
za maisha za Chachage S Chachage. Ni kana kwamba alikuwa akituaga kwa
kutuandikia “wosia” au ushuhuda wa yote aliyokuwa nayo moyoni kuhusu matatizo
na mustakabali wa Tanzania na Afrika.
Marejeo
Abdallah,
H (1960), (uliandikwa kama 1895) Utenzi
wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima. (Mh. J.W.T. Allen). Dar es Salaam:
East African Literature Bureau (EALB)
Ajjemy,
A.H (1972); (1895), Habari
za Wakilindi (Mh. J.W.T. Allen). Nairobi: EALB, Allen, J.W.T 1971 Tendi. London: Heinemann
Cabral,
A (1966),  “The Weapon of Theory” (Silaha ya Nadharia). Address delivered to the first Tricontinetal Conference of the Peoples
of Asia, Africa and Latin America  held
in Havana in Janury 1966. Hotuba inapatikana katika Revolution in Guinea: Selected Texts (Mfasiri R.Handyside). New York:
Monthly review Press
Diegner,
L (2002), “Mahojiano na Chachage Seithy L. Chachage Juu ya Riwaya Yake Makuwadi
wa Soko Huria (2002)” katika  Swahili Forum 11 (2004): 227-234
Heepe,
M (1928), “Suaheli-Chronik von Pate.” M.S.O.S. XXXI: 145-92
Hichens, W (1938) “Khabar al Lamu — A Chronicle of
Lamu.” Bantu Studies 12(1):1-33
Hussein,
E (1969), Kinjeketile. Nairobi:
Oxford University Press (OUP)
Hussein,
E (1971), Mashetani. Nairobi: OUP
Kezilahabi,
E (1975), Dunia Uwanja wa Fujo. Nairobi: EALB
Kezilahabi,
E (1979), Gamba la Nyoka. Arusha: EAPL
Knappert,
J (1979), Four Centuries of Swahili
Verse. London: Heinemann
Lihamba,
A (1990), Wimbo wa Sokomoko. Dar es
Salaam: Tanzania Publishing House (TPH)
Lukacs,
G (1962), The Historical Novel. ,
Harmondsworth: Penguin Books
Mapalala,
B (1992), Kwa Heri Iselamagazi. Dar
es Salaam:TPH
Mbonde,
J.P (2004), “Chachage Seithy L.Chachage: Makuwadi
wa Soko Huria (2002)Uchambuzi na Uhakiki” Katika Swahili Forum11 (
2004): 214-226
Mohamed,
M.S (1978)  Nyota ya Rehema. Nairobi: OUP
Muhando, P Balisidya, N na Lihamba, A  (1982) Harakati
za Ukombozi. Dar es Salaam: TPH
Mulokozi, M.M (1990)
“Utunzi wa Riwaya ya Historia.” Mulika
Na.22: 1-12
________
(1990)  Ngome ya Mianzi. Dar es Salaam: MPB Press,
________ (1991)  Ngoma
ya Mianzi. Dar es Salaam: TPH
________ (1996)  Moto wa
Mianzi. Morogoro: ECOL, Morogoro
________
(1997) Utenzi wa Nyakiiru Kibi. Morogoro: ECOL
Mohamed,
S.A (1980) Dunia Mti Mkavu. Nairobi: Longman
Robert, S (1967) Utenzi
wa Vita vya Uhuru. Nairobi: OUP
Ruhumbika, G (1995)
Miradi Bubu ya Wazalendo. Dar es
Salaam: TPH
Shafi, A (1978) Kasri
ya Mwinyi Fuad. Dar es Salaam: TPH
Shafi, A (1979) Kuli.
Dar es Salaam: TPH
Shafi, A (1999) Vuta
N’kuvute. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota
Shafi, A (2003) Haini.
Nairobi: Longhorn Publishers
Shivji, I (2000) (2002) “Makuwadi wa Soko Huria.” Mulika
Na. 26 (2000): 93-97
Tolmacheva,
M (1993) The Pate Chronicle. East Lansing: Michigan State University Steere, E (1870)
Swahili Tales, as Told by the Natives of Zanzibar . London: Bell and Daldy
Vassanji, M (1989) The Gunny Sack. Oxford: Heinemann International
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)