MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
UCHAMBUZI: RIWAYA YA MUNGU HAKOPESHWI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
UCHAMBUZI: RIWAYA YA MUNGU HAKOPESHWI
#1
UCHAMBUZI: RIWAYA YA MUNGU HAKOPESHWI
UTANGULIZI
Riwaya ya Mungu Hakopeshwi inaelezea maisha ya familia moja inayoishi sehemu ya mtaa wa Malindi kisiwani Unguja ambapo familia hiyo ya Bwana Ahmed Said mwenye hasira yake kali, asoambilika na asokubali kushindwa wala kutetereka katika maamuzi yake ambapo kiundani anaonekana ana siri fulani ambaye kaihifadhi katika kifua chake na hata mkewe Bi Khadija binti Najash anapomshauri hamsikilizi anaona mwanamke ni mtu wa ndani tu hana lolote la kuchangia katika familia na jamii.
MAUDHUI
Maudhui ya kitabu hiki kwa ujumla yanaelezea maisha ya Bwana Ahmed na mkewe Bi Khadija ambao ni baba na mama wa watoto wane nao ni Said, Layla, Zahra na Salah ambapo wanaishi katika maisha mazuri lakini uzuri wake ni wa kibatari ambapo unawamurikia mwanga watu wegine lakini chenyewe ni giza tupu ndani kwani maisha ya familia hii ni ya mtafaruku, mikwazano, kejeli, dharau na yaliyojaa kunyimwa uhuru wa mtoto wa kike na hata mke katika hata yale maamuzi mazito yanayohusu maisha yao.
LENGO
Lengo la muandishi ni kuonesha kua bado katika Zanzibar au Tanzania kwa jumla kuna hizi familia ambazo zina mfumo dume ambapo mwanamke hawezi kupaza sauti kudai haki yake na wala hana uhuru wa kuamua kama Bi Khadija katika uk 32 anaposema “Ahmed unakosea unaposema hivyo mtoto wa kike nae ana haki yake”.
Haki yake? Haki ya nini? Usitake kunitibua sasa! Migogoro ya utumwa anotumishwa mwanamke haina kifani na kufikia kushushwa hadhi yake kama ukurasa 33 bwana Ahmed anamwambia mkewe “ unakistaajabia kitu gani hapo kilichokua kipya kwako kachukue tambara uje ufute hapo hizo ndio kazi zenu wanawake.”
Katika kukamilisha kusudio lake mwandishi kajitahidi kuzielezea falsafa za maisha vizuri sana pamoja na changamoto zinazokabiliana nazo, kama katika ukurasa wa 11 anasema “dunia mviringo kwa kupanda na kushuka”.
Umuhimu wa kuwepo kodi za serikali pia umezungumzwa uk 9 “Muhimu kulipa kodi za serikali kwa wakati”.
Tabaka tawala anavyoamini muandishi haliwakubali sana na watu wenye asili ya kiarabu ukurasa wa 10 “Wanatudhulumu kwa maneno yao ya shutuma na chuki”.
Falsafa ya mabadiliko ya maisha imezungumziwa vyema muandishi akizungumza kuhusu baadhi za familia namna zilivyoporomoka mdomoni kwa bwana Ahmed “Iangalie familia ya Bw Salim Mahfudh Mungu amrehemu ……wamebakiwa na nini watoto maskini uk 13.
Mwandishi pia anazungumzia suala la ugumu wa ajira “wote ni wasomi wa elimu ya juu, lakini zimewafaa nini? Yule mmoja ni Mwanasheria na Yule mwengine ni mkemia lakini wote hawana ajira mpaka sasa”.
Falsafa juu ya ndoa gani inafaa imezungumzwa na mwandishi kama inavojieleza uk 29 Bi khadija anaposema “Sijakusudia kumjua kwa sura wala anafanya nini nakusudia tabia yake ikoje”?…… sura ya mtu na mali zake hazisaidii kitu katika maisha ya ndoa ikiwa tabia yake mbaya .
Falsafa juu ya umuhimu wa elimu imeelezwa vyema kuwa elimu inamfata popote anapokwenda na kumuangazia nuru ya maisha yake .Haya anadhihirisha mwandishi wa riwaya hii katika ukurasa 83 Bwana Ahmed anapoaambiwa na mkewe: “Khah! Sikufikiria kama una dhana potovu kama hizo kuwa na elimu yenye manufaa ni utajiri bora kuliko kumiliki mali, elimu ni nuru na vazi bora na heshima kwa mwenye nayo, elimu haiishi, humfata mtu kila aendapo na humsaidia kila inapohitajika. Basi vipi mali inaweza kushika nafasi ya elimu?
Falsafa ya ukweli kama nyenzo za kutetea mtu haki yake imejadiliwa na mwandishi tangu mwanzo mpaka mwisho kama ukurasa 88 Zahra anapomuambia dada yake “Ukikosa kumchagua mume sahihi ndio ushaharibu maisha yako yote”. “Hakuna njia nyengine ila useme ukweli tu”. “Layla ndugu yangu ,usitake kuukwepa ukweli ukitaka usitake ukweli unabaki pale pale kuwa bado una hisia kwa Hassan”.
Falsafa ya tabaka la kitajiri ambalo inaliona tabaka la kimaskini halina hadhi ya kuingiliana nao ubia wala change zozote zile za kuoana wala kusuhubiana .Mwandishi kalizungumzia uk 12 bwana Ahmed aliposema oh! Eti mtoto wa Ahmed bin Said aolewe na mwenye daladala. Mwenyewe nimekufa ama? Kuonesha dharau za pesa na kujitukuza.
MIGOGORO ILIYOJITOKEZA
  1. Mfumo dume ni miongoni mwa migogoro iliyojitokeza tangu mwanzo mpaka karibu na mwisho wa kitabu husasan kumkandamiza mtoto wakike na mke kumnyima haki kama vile bi Khadija anavyojaribu kumnasihi mumewe uk 113 akubali posa za Hassan na kukataa kata kata kua yeye diye mwenye maamuzi ya pekee na anasema; “Usianze somo lako, nimechoka kubishana na wewe mwenye maamuzi ya mwisho ndani ya nyumba hii ni mimi na siku zote itabaki kua hivyo, name nimeshaamua Layla atolewa na Hafidh tu sitaki kusikia tena mada hii hapa ndipo imeshafika kikomo.
  1. Mfumo dume unaomfanya Said pia awanyime ndugu zake wa kike haki na Zahra anapojaribu kujielezea anawakaripia kwa kejeli,dharau na ukali uk 108 sio kama tunatafuta mabwana…… “Nyamaza kenge we! Mnaleta mambo ya kipuuzi humu ndani kisha unajitia kidomodomo juu bado? Katika umri wenu wote mliwahi kumuona nani kafanya ujinga huo mlioufanya nyinyi”?
  1. Mgogoro kati ya mtoto wa kiume wa bwana Ahmed Said na baba yake . Mgogoro uliojitokeza baada bwana Ahmed kutaka kumuozesha Said mke na kufika kwenda kumposea na kutoa mahari bila hata kumuarifu uk 131 Said anasikika akimueleza baba yake “Ina maana umefanya yote hayo bila kuniambia chochote hata hukujali kujua ninahitaji kitu gani”? “Wewe ni mwanangu najua nini bora kwako ndio maana nikakutafutia “ “Na nikikwambia kuwa simtaki Sifati”? “Eti ? Na usimtake ana kasoro gani”? “Hana kasoro yeyote ila simuhitaji kwenye maisha yangu”
  1. Mgogoro kati ya bwana Ahmed na wazee wa Sifati kaka zake Awadh na Yahya, uk 135 “Ami Ahmed kuna habari zimetapakaa mji mzima kua Said ameondoka nyumbani na hajulikani alipo. Eti habari hizi zina ukweli wowote”? Yahya alimuuliza suali bwana Ahmed “Aaa ni kweli, lakini….musiwe na wasiwasi, kila kitu kitakua sawa…….. ni mambo ya kitoto tu. “Kwani basi hakukutaarifu”? Awadh aliuuliza huku uso kaukunja…. uk 140 “Umefanya yote haya kwa ajili ya kutudhalilisha tu kwa sababu umetuona sasa sisi ni maskini”.
Tukizungumzia migogoro yote iliyozungumzwa hatuimalizi kwani kuna migogoro kati ya Bi Maimuna na mumewe bwana Mahfudh kuna migogoro kati Hafidh mume wa Layla kuhusiana na ndoa bubu, yote imegubika katika kumkandamiza mwanamke na kumnyima haki yake.
FANI
Katika maandishi yake kijumla mwandishi amejitahidi kutumia kiswahili fasaha kinachozungumzwa “kisiwani Zanzibar na kwa jumla tukitazama kazi yake kilugha, fani imeweza kuyaibua maudhui yaliyokusudiwa na kuibeba vyema dhamira aizungumzayo katika muktadha wa kile akizungumziacho na kutoa mwanga kwa jamii iliyokusudiwa kuifahamu vyema riwaya yake.
JINA LA KITABU
Tukianza na jina la kitabu kwamba gamba la nje lina mchoro wa mwanamme jasiri lakini na ujasiri wake kazongwa na senyenge za damu na jicho moja linachiriza machozi na ujumbe uliopo “MUNGU HAKOPESHWI”.Unapoisoma riwaya hii tangu mwanzo hadi mwisho utajua kwa kweli mwandishi kajitahidi kusibu katika kitabu chake kwani kama bwana Ahmed alipompuuza baba yake na kumkimbia nayeye alikimbiwa na mwanawe Said na hakutokea hadi kumkuta maiti,kama bwana Ahmed alivyomtupa Lulu na mkungu wa mimba na yeye kulipwa, na kuja kujishtukia na aibu.Aibu ambayo imempeleka akhera mosi,lakini pili imesababisha kuoana Zahra na Ahmed ambao ni ndugu wa damu ya baba mmoja. Hafidh ,kama alivyomtoa Layla roho kajikuta na yeye anaishi na virusi vya ukimwi kwa vitimbi alivyokuwa akimfanyia mkewe huenda ikawa ni malipo na kama hilo halitoshi baba yake alikuwa ni mhimili wake wa kumuunga mkono anahangaika na maradhi ya kiharusi hana mkono wala mguu, na anatapia nafsi yake.
“MUNGU HAKOPESHWI”ni kweli Said aliwakimbia wazee wake na majukumu ya familia kuyakwepa, na mdogo wake Layla hakumjali wakati alipokuwa anahitaji sana msaaada kamkuta keshafariki hakushuhudia hata maziko yake na huyo mwanamke aliyemzuzua Farhat, alipoanguka tu kimaisha amemkimbia akafika kufanya kazi ya kupara samaki.
LUGHA ILIYOTUMIWA
Mwandishi wa riwaya katumia lugha ya Kiswahili chepesi kinachotumiwa mjini Unguja lakini hakuacha kuirashia tauria, stiari,tamathali za semi, tashbiha ambazo zimetawala tangu mwanzo wa riwaya yake mpaka mwisho hata nyengine zikawa zinajirejea.
Mathalani hazikuchusha na pengine zilimsaidia msomaji awe na hamu zaidi ya kuimaliza haraka riwaya yake.
• LUGHA ZA PICHA
Mwandishi kila sura anaivuta vyema lugha ya picha na msomaji hujihisi kile kitu kipo mbele yake. Katika ukurasa wa 5 mwandishi akiuelezea wasifu wa Bi Khadija anaeleza
“Bi Khadija alishapindukia miaka arubaini na tano lakini uzuri wake bado haujafifia uso wake ulikua na umbo la yai wenye weupe wa wekundu pua yake ndefu iliyosimama sawa sawa baina ya mashavu yenye rangi ya waridi , chini ya macho makubwa yenye kope ndefu zilizozidisha uzuri wa macho yake. Nyusi ndefu nyembamba zilizozipinda juu ya macho zilikamilisha urembo wa mwanamke huyu. Midomo membamba iliyoficha meno nadhifu yaliyopangika vyema yalizidisha urembo wake kama vile alijua ladha ya tabasamu. Mara nyingi kama si zote uso huu ulikuwa umechanua kwa tabasamu murua na kuzidisha haiba ya uzuri wake. Mwanamke huyu alikua maridhia kwa kila jambo.
Lugha za tashbiha ambazo zimetawala riwaya hii zimeshonana tangu mwanzo hadi mwisho wa riwaya na baadhi yake akurasa ” Mkasa mzima unamp
itia kwenye kichwa chake kama vile mkanda wa filamu ” uk 1
“Bwana Ahmed alijitupa kitandani kama gunia la mbatata”
“Bwana Ahmed alikua mkali kama samba jike mwenye watoto uk 4
“ Sauti kama ya punda” uk 18
“Akichagua wanaume kama anavyochagua chuya kwenye mchele “uk 21
“Zinamiminika mkononi kama maji yanavyotiririka baharini” uk 21
“Akinua miguu juu kama mtu anaetaka kupaka hina”uk 30
METHALI
“Maji yakimwagika hayazoleki” uk 3
“Kidole kimoja hakivunji chawa” uk 4
“Mganga hajigangi” uk 4
“Riziki ya mtu hailiki” uk 10
“Mungu si athumani” uk 10
“Majuto ni mjukuu” uk 12
“Hakuna siri ya watu wawili” uk 20
“Kidole kimoja hakivunji chawa” uk 101
TAURIA NA STIARI
Miongoni mwa vipengele vya lugha vilivonogesha riwaya hii ni stiari na tauria kama zinavojionesha katika kurasa tofauti
“Said mawazo yalimzidi kichwa” uk 8
“Dola inatutia kitanzi shingoni” uk 72
“Maneno yalikua yameingia kwenye moyo” uk 16
“Uchumi unakuja kuangusha stuli” uk 3
“Jicho likafanya kazi yake “ uk 21
“Kioo kimemcheza” uk 24
“Mapenzi yao…….. ikatoa mche, mche nao ukatoa mti mkubwa” uk 24
“Ukimya ulitawala ukumbini hapo” uk 26
“Heshima imekwenda likizo” uk 32
ATHARI ZA LUGHA ZA KISLAM
Kwa vile mazingira ayazungumziayo ni mjini Unguja , hivyo muandishi wa riwaya hii hakuacha kuonyesha athari za lugha za kislam kama zilivyojionesha kwa baadhi kurasa
“Usomaji wa Qur-ani uk 26
“Lailaha illa Allah “ uk 53
“Hii riziki ninavyokunywa hapa iwe sumu mwilini mwangu” uk 52
MAWAZO YA KIUJUMLA
Kwa kuhitimisha mwandishi Zainab Alwi Baharoon kwa vile hii ni kazi yake ya mwanzo amejitahidi sana kuitumia vizuri fani katika kuelezea maudhui yaliyokusudia na jamii aizungumziayo yaani mjini Unguja katika mtaa wa Malindi (na iwe popote Zanzibar) ilimradi kaweza kuzikonga roho za wasomaji wake na mimi binafsi kitabu chake kimenivutia na leo naelezea kimuhtasari tu lakini nachukua ahadi ya kukifanyia uhakiki wa kina na nina kila sababu ya kufanya hivyo kwanza ni muislamu mwenzangu,mwanamke mwenzangu na ikiwa hilo halitoshi ni msanii kama mie, hivyo nachukua fursa hii kumwambia bado mapambano yanaendelea kuzinduliwa kwa kitabu hiki leo iwe chachu ya kutoa chengine na chengine.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Muhtasari huu umetayarishwa na
Khadija Said Suleiman AL- Battashy
Kwahajitumbo ,Zanzibar
JINA LA KITABU:       Mungu Hakopeshwi
MTUNZI:                      Zainab Alwi Baharoon
MCHAPISHAJI:           Z.A. Baharoon, 2012
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)