MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
HISTORIA YA KUIBUKA KWA RIWAYA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
HISTORIA YA KUIBUKA KWA RIWAYA
#1
Chimbuko la riwaya linapatikana katika fasihi simulizi, ambayo, kwa kiasi kikubwa, imebebwa na sanaa―jadi, miongoni mwa tanzu maarufu za fasihi simulizi zilizoibua riwaya ni ngano na hekaya. 
Ngano, ni sanaa ya jadi ya kisimulizi itokanayo na matukio maalumu ya kihistoria katika jamii husika. Huwa fupi na wahusika wake ni wachache; huku ikitumia mifano mingi.
Hehaya, ni hadithi za kimapokeo zenye kusisimua na kustaajabisha huku ikijumuisha kitushi zaidi ya kimoja. Huwa fupi na wahusika wake ni wachache, huku ikitumia mifano mingi. 
Kabla ya kuiangazia historia ya riwaya ya Kiswahili, ebu tutupie jicho katika kutazama historia ya riwaya kiulimwengu kwa kuangazia mabara mawili ya Ulaya na Asia.
Riwaya katika Bara la Ulaya
Riwaya ni utanzu mchanga zaidi ukilinganishwa na ushairi na tamthiliya. Tanzu za ushairi na tamthiliya zina umri karibu sawa na historia ya mwanadamu. Riwaya ilipata umbo ililonalo hivi sasa karne ya 18 huko Ulaya. Hata hivyo, mbali na umbo la hivi sasa, historia ya riwaya inaanzia karne ya 3 hadi ya 4 K.Y.M. Madumulla (2010) anadai kuwa katika miaka hiyo kuna mtaalamu aitwaye Voltaire ambaye alidai kuwa kulikuwa na kitabu kiitwacho Cyropaedeiakilichoandikwa na Myunani Xenopheno (430―355 KK). Kitabu hicho kilikuwa ni riwaya. Nchini Uingereza, uandishi wa riwaya ulizaliwa na kupata ukomavu katika kipindi kifupi.
Sababu zilizochochea utanzu wa riwaya kukomaa kwa haraka ni:
o   Elimuo   Ukomavu wa uchumi
o   Maendeleo ya sayansi na teknolojia
o   Kutulia kwa jamii zao (utulivu wa kuishi pamoja).
Riwaya Asia
Habari za historia ya riwaya katika bara hilo ni chache sana. Hivyo, historia yao inatuangazia kuwapo kwa riwaya huko toka karne ya 7. Kwa mfano, katika karne hiyo, Dandin aliandika hadithi iitwayo Dasakumarakarita iliyohusu masaibu ya wana kumi wa Mfalme. Aidha, huko Japani kulikuwa tayari na maandiko kadhaa yenye mwelekeo wa kiriwaya. Mkabala wao wa kiuandishi ulijikita katika mtazamo wa Ki ― marx hasa baada ya kuzaliwa kwa Azimio la Kikomunisti (1848). Baadhi ya kazi hizo ni pamoja na: Taketori Monogatari (850 ― 920), Utsubo Monogatari (850 ― 900), diwani ya hadithi zilizoitwa Yamoto Monogatari, Ochikubo Monogatari (Mwishoni mwa karne ya 10), sumiyoshi Monogatari (1200), riwaya ya kimapenzi iliyoitwa Gempei Seisuku (1200 ― 1250) na riwaya ya kivita iliyoitwa Taibeki (1367 ― 75). (Kwa ziada, tazama. Madumulla, 2010).
Usuli wa Riwaya katika bara la Afrika
Historia ya riwaya katika bara la Afrika ni fupi sana. Inaanzia karne ya 20. Huko Afrika ya Kusini na Afrika ya Magharibi, maandiko ya kifasihi yalianza mwishono mwa karne ya 19. Yalichagizwa sana na kuwapo kwa shughuli za kimishenari au kikoloni kwa jumla. Fani na maudhui ya kazi hizo viliakisi mazingira ya kijadi ya maeneo hayo. Kwa maelezo zaidi, rejea Madumulla, (2010:23―35).
RIWAYA YA KISWAHILI
Kabla ya kuitupia jicho dhana ya riwaya ya Kiswahili, ni vema kuimulika dhana ya Fasihi ya Kiswahili. Dhana hii imekuwa inawachanganya wanataaluma wengi. Hii kwa sababu inachanganya kwa pamoja dhana kadhaa. Dhana hozo ni:
o   Fasihi ya Kiswahili
o   Fasihi katika Kiswahili
o   Fasihi kwa Kiswahili
o   Fasihi ya Waswahili
Ili kuzielewa vema dhana za fasihi ya Kiswahili na riwaya ya Kiswahili, kwanza tunatakiwa ku mjua Mswahili.
Ponera (2010:69), Mswahili ni mtu mwenye kiwango kikubwa cha umilisi wa lugha ya Kiswahili. Vilevile, ni mtu ambaye amefungamana sana na mila na desturi za jamii ya watumiao lugha ya Kiswahili kiasi hata cha kumuathiri kifikra, kimtazamo na kiitikadi. Fasili hii inatumulikia ukweli kuhusu kuwapo kwa Fasihi ya Mswahili au Waswahili (watu). Fasihi hiyo ilisanwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili, hivyo kuwa na sifa ya kuitwa fasihi ya Kiswahili kama ilivyo kwa fasihi ya mjerumani isanwayo kwa kutumia lugha ya kijerumani; hivyo kuitwa fasihi ya kijerumani. Dhana ya fasihi katika Kiswahili au fasihi kwa Kiswahili imetokana na sababu kadhaa zikiwemo mwingiliano wa jamii mbalimbali za hapa duniani, pamoja na shabaha ya kupanua hadhira (hatimaye kupanua soko). Hii ni ile fasihi ambayo ina mahadhi ya lugha za kigeni lakini iko katika lugha ya Kiswahili (mfano. Alfu Lela U Lela, Mashimo ya Mfalme Suleimani, Safari za Guliva, Hekaya za Abunuwasi, Safari Saba za Sindbad Bharia).
Hivyo, kwa muktadha wa kozi hii, fasihi ya Kiswahili ni ile iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili na inazungumzia masuala mbalimbali yanayomhusu mswahili. Nayo ni kama vile hali ya maisha yao, mila na desturi zao, chakula chao na kaida nyinginezo. Kuwapo kwa fasihi ya Kiswahili ni ithibati tosha ya kuwapo kwa riwaya ya Kiswahili. Chimbuko lake limo katika simulizi za asili (ngano, visa kale na visa sili).
HISTORIA YA RIWAYA YA KISWAHILI
Riwaya ya Kiswahili ina hazina ndefu. Misingi yake hupatikana katika fasihi simulizi. Riwaya za kisasa zinatokana na juhudi za wageni na wenyeji. Wageni walijihusisha na kuweka msingi katika karne ya 19.
Juhudi za kwanza zilihusu kukusanya nathari za wenjeji. Kisha, ikafuata hatua ya kutafsiri ngano za wenyeji katika lugha za kigeni. Kwa mfano, mwaka 1870 Edward Steere ilianza kutafsiri hadithi kutoka Zanzibar katika lugha ya Kiingereza. Mwaka 1889 alichapisha kitabu kiitwacho Swahili Tales as Told by the Native of Zaznzibar. Hiki ni kitabu cha muhimu kwa sababu kinatoa dira kuhusu historia ya mwanzo ya riwaya za Kiswahili. Mwaka 1907 Carl Vetten alichapisha kitabu kiitwacho Prosa and Poesie de Suaheli kwa lugha ya kijerumani.
Hatua iliyofuata ni kutafsiri fasihi za kigeni kuwa ya Kiswahili. Kwa mfano, mwaka 1928 Edwin Brenn alitafsiri kitabu kiitwacho Alaza. Mifano mingine ni: Alfu Lela Ulela, Mashimo ya Mfalme Suleimani, Hadithi za Esopo, Hadithi za Mjoma Remas na Hekaya za Abunuasi. Kazi hiyo ya kutafsiri ilipamba moto tangu mwaka 1930 wakati halmashauri ya Kiswahili ya Afrika mashariki ilipoanzishwa.
TANBIHI: Kila mmoja ajibidiishe kuchunguza mchango wa wageni katika kuchipuka kwa riwaya ya Kiswahili. Miongoni mwao ni:
o Edward Steereo   Car Buttner
o   Carl Velteno   Lyndon Harries
o   Jann Knapper
o   Edwin Brenno   J.W.T. Allen
Baada ya hapo, waafrika wakaanza kutunga riwaya. Walitunga kutokana na kuhamasishwa na halmashauri hiyo ya Kiswahili. Mfano, mwaka 1934 James Mbotela alitunga riwaya ya Uhuru wa Watumwa. Riwaya hii ilisanifiwa na Halmashauri ya Kiswahili kwa sababu iliwaponda Waarabu na kuwakweza Waingereza ambao walikuwa katika Halmashauri ya Kiswahili.
Riwaya ya Uhuru wa Watumwa ni kielelezo kimojawapo cha riwaya za mwanzo za Kiswahili. Watunzi wengine wa kiafrika ni pamoja na Shaaban Robert na Abdallah S. Farsy (aliyetunga riwaya ya Kurwa na Doto: 1961).
Baadhi ya waandishi wa kiafrika baada ya uhuru walipanua wigo na kuandika juu ya mambo mengi zaidi. Mfano, zikatungwa riwaya za upelelezi. Faraji katalambula alitunga riwaya ya Simu ya Kifo. mohammed Said Abdallah alitunga riwaya nyingi za upelelezi mhusika wake mkuu aliitwa MSA. Mifano ya kazi zake ni:
o   Duniani Kuna watuo   Kisima cha Giningi
o   Mzimu wa watu wa kaleo   Mwana wa yungi Hulewa
o   Siri ya sifurio   Kosa la Bwana MSA
Kisha, watunzi wakageukia kutunga juu ya siasa wakiongea juu ya masuala mbalimbali kama vile viongozi wanafiki, mikutano ya siasa. Mifano ya kazi hizi ni: Njozi iliyopotea na Gamba la Nyoka. Kwa ujumla, wanariwaya walikuwa wanaandika juu ya masuala ya jamii wakiwa na nia ya kukosoa, kuelimisha na kadhalika. Waandishi wamekuwa wakikomaa katika kuandika kwa kuzingatia maudhui na fani inayorandana na miktadha. Kabla ya uhuru waliandika kikasuku pasipo kuchambua. Kwa mfano, Mbotela alipowasifia waingereza katika Uhuru wa Watumwa. Pia uchoraji wa wahusika umekuwa ukikomaa kutoka kipindi kimoja hadi kingine.
Maendeleo ya riwaya ya Kiswahili
Toka ichimbuliwe ama ianzishwe, riwaya ya Kiswahili imepige hatua kubwa. Umekuwepo mwondoko mpya katika maeneo kama vile ya:
o   Idadi ya kazi za riwaya
o   Ubora wa riwaya zenyewe
o   Matumizi ya lugha
o   Mwelekeo wa maudhui
o   Mabadiliko ya motifu n.k.
Maendeleo haya ya ubunilizi wa riwaya, pamoja na sababu nyingine, yamechochewa sana na ongezeko la hali ya usomi na wasomaji katika jamii ya waswahili. Mchango wa ongezeko hilo la hali ya usomi na wasomi katika jamii ya waswahili linaweza kutazamwa kupitia maeneo kama vile; Utungaji, Usomi na utafiti kuhusu masuala ya riwaya.
MAPOTE (MAKUNDI) YA RIWAYA
Riwaya kwa ujumla imegawanyika kwenye makundi makubwa mawili. Makundi hayo ni:
o   Riwaya dhati
o   Riwaya pendwa
Riwaya dhati
Sifa zake ni pamoja na;
o   Huzungumzia mambo nyeti, adhimu na yenye thamani katika jamii.
o   Watunzi wake huwa na nia ya dhati ya kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha.
o   Hukubalika na sehemu kubwa ya jamii.
o   Huwa na lugha fasaha, nyoofu, adilifu na zisizo na matusi.
o   Utolewaji wake huthibitishwa na ogani au mamlaka husika.Mifano ya riwaya dhati na watunzi wake:
Muhammed Said Abdulla (MSA)
o   Kosa la Bwana MSA
o   Kisima cha Giningio   Duniani kuna Watu
o   Siri ya Sifuri
o   Mwana wa Yuni Hulewa
o   Mzimu wa Watu wa Kale
o   Mke Mmoja Wanaume Watatu
Said Ahmed Mohamed
o   Asali Chungu
o   Tata za Asumini
o   Dunia Yao
o   Kiza katika Nuru
o   Dunia Mti Mkavu
o   Utengano
o   Babu Alipofufuka
Seti Chachage
o   Makuwadi wa Soko Huria
o   Almasi za Bandia
o   Sudi ya Yoha na
o   Kivuli
Anicet Kitereza
o   Bwana Muyombekere na Bibi Bugonoka
Shaffi Adamu Shaffi
o   Kuli
o   Haini
o   Vuta N‘kuvute
o   Kasri ya Mwinyi Fuad
o   Mbali na Nyumbani
J.K. Kiimbila
o   Ubeberu Utashindwa
o   Lila na Fila
Euphrase Kezilahabi
o   Rosa Mistika
o   Kichwa Maji
o   Gamba la Nyoka
o   Dunia Uwanja wa Fujo
o   Nagona
o   Mzingile 
Shaaban Robert
o   Kusadikika
o   Kufikirika
o   Utubora Mkulima
o   Siku ya Watenzi Wote
o   Adili na Nduguze
o   Wasifu wa Siti Binti Saad
Riwaya Pendwa
Hizi ni zile zinazovuta nadharaia na kupendwa sana na watu takriban wa marika yote. Zinahusu maeneo yafuatayo: Mapenzi, Ujambazi, Ujasusi na Upelelezi.Baadhi ya wataalamu hutilia mashaka ukubalifu na ufaafu wake katika jamii. Riwaya hizi aghalabu hujengwa na sifa zifuatazo:
o   Kujichomoza zaidi kwa fani kuliko maudhui
o   Kujengwa zaidi kwa msingi wa taharuki
o   Kuvuma ghafla na kuzima/kufifia ghafla
o   Huwa na u―mjini zaidi kuliko u―kijijini
o   Huwa na uharaka. 
Uharaka huo hujitokeza katika: 
Uhariri na Utunzi (mtiririko wa visa huwa na kasi)
o   Uzalishaji na usambazaji wake hufanywa bila udhibiti mkubwa
o   Hutumia utusi na u ajabu ajabu kama nyenzo muhimu za kusisimua hadhira.
Mifano ya riwaya pendwa na watunzi wake:
John Simbamwene
o   Mwisho wa Mapenzi
o   Kwa sababu ya Pesa
o   Mauaji Lojingi
Elvis Aristablus Musiba
o   Kufa na Kupona
o   Njamao   Kikosi cha Kisasi
o   Hujuma
o   Hofu
o   Kikomo
Eddie Ganzel
o   Kitanzi
o   Msako wa Hayawani
o   Zubaa Uzikwe
o   Zawadi ya Bwege
A.Muhoza
o   Pendo la Kifo
Mbunda Msokile
o   Nitakuja kwa Siri
o   Usiku Utakapokwisha
o   Mapambano
o   Dhihaka ya Mume
o   Amani ya Ukubwa
Ben R. Mtobwa
o   Mikononi mwa Nunda
o   Joram Lazima Ufe
o   Tutarudi na Roho Zetu?
o   Salamu Toka Kuzimu
o   Nyuma ya Pazia
o   Roho ya Paka
o   Mtambo wa Mauti
o   Dar es Salaam Usiku
Alex Banzi
o   Titi la Mkwe
o   Zika Mwenyewe
UAINISHAJI WA RIWAYA
Pamoja na riwaya zote kuangukia katika mojawapo ya makundi haya, bado zinaweza kuainishwa zaidi katika makundi mengine mbalimbali. Hata hivyo, uainishaji wa riwaya ni jambo linalosumbua sana mawazo ya wanazuoni. Pamoja na kukinzana huko, wanazuoni wanakubaliana kuwa uainishaji wa riwaya huweza kufanywa kwa kutumia vigezo anuai. Vigezo maarufu vitumikavyo ni vinne (4). Navyo ni: kwa kuzingatia fani, usimulizi, upeo wa kijiografia na maudhui.
Aina za Riwaya kwa Kuzingatia Fani
Kwa kigezo hiki, riwaya huwekwa katika makundi matatu. Nayo ni: Riwaya Sahili; Riwaya Changamani na Riwaya za Kimajaribio.
Riwaya Sahili
Sifa zake bainifu ni pamoja na;
o   Maudhui yake ni mepesi kueleweka
o   Mandhari yake huwa halisi na rahisi
o   Vitushi vyake viko wazi
o   Hutumia lugha ya moja kwa moja
o   Kwa jumla, hazina utata katika vipengele vyake
Riwaya Changamani
Sifa zake bainifu (ni kinyume cha riwaya Sahili);
o   Maudhui yake huhitaji tafakuri ili kuyaelewa
o   Vitushi vyake hutanzwa
o   Hutumia lugha isiyo ya moja kwa moja (ya mafumbo).
Riwaya za Kimajaribio
Sifa zake bainifu ni pamoja na;
o   Hutumia mbinu na utaratibu usiozoeleka katika kumbo hili la riwaya.
o   Hii inamaanisha kuwa hutumia vipengele mbalimbali vya fani na maudhui ambavyo ni vigeni. Kwa mfano, matumizi ya nafsi ya MIMI kama mhusika katika riwaya.
o   Mfano wa riwaya hizo ni Nagona na Mzingile.
Aina za Riwaya kwa Kuzingatia Upeo wa Kijiografia
Kwa kigezo hiki, riwaya huwekwa katika makundi manne (4). Nayo ni; Riwaya za Kiambo, Riwaya za Kitaifa, Riwaya za Kimataifa na Riwaya za Kidaistopia.
Riwaya za Kiambo
Huhusu masuala ya mila, desturi na mandhari maalum ya mahala fulani. Mifano ya riwaya hizi ni: Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka, Kurwa na Doto, Kisima cha Giningi na Mirathi ya Hatari n.k.
Riwaya za Kitaifa
Hujikita katika upeo wa kijiografia usiovuka mipaka ya taifa fulani. Hivyo, maudhui yake huzungukia yanayojiri, yaliyojiri au yatakayojiri katika taifa fulani.
Riwaya za Kimataifa
Hizi ni kinyume cha riwaya za kitaifa. Hujikita katika upeo wa kijiografia usiovuka mipaka ya taifa fulani. Hivyo, maudhui yake huzungukia yanayojiri, yaliyojiri au yatakayojiri katika taifa husika.
Riwaya za Kidaistopia
Hizi husawiri jografia ya jamii isiyokuwa ya kawaida, ya kidhahania. Kwa namna fulani, mandhari zake kuogofya. Baadhi ya riwaya za Shaaban Robert na Kezilahabi zinaweza kuingia katika kundi hili. Hizo ni pamoja na: Nagona,Mzingile, Kufikirika na Kusadikika.
Aina za Riwaya kwa Kuzingatia Usimulizi
Riwaya za Monolojia
Ni riwaya ambazo hutawaliwa na sauti ya mtunzi. Yaani mtunzi husimulia kwa sehemu kubwa kwenye kazi yake.
Riwaya za Barua
Usimulizi wake huwa wa kibarua. Kwa mfano, Barua Ndefu kama Hii.
Aina za Riwaya kwa Kuzingatia Maudhui
Riwaya za kihistoria
Riwaya za mwegamo huu huakisi matukio ya kihistoria. Wahusika wake husawiri kwa makini ili kutia kumbukizi ya wakati uliopita. Riwaya hizi si kitabu cha kihistoria, bali ni huakisi tu matukio ya kihistoria. Huwa na urazini wa historia ya jamii. Mifano ya riwaya za mtazamo huu ni: Miradi bubu ya Wazalendo (G. Ruhumbika), Kifo cha Ugenini (Olaf Msewe), Kasri ya Mwinyi Fuadi (Shaffi Adam Shaffi), Zawadi ya Ushindi, Kwa heri Islamagazi (Mapalala), Uhuru wa Watumwa na Moto wa Ngoma ya Mianzi (Mulokozi).
Riwaya za Kimaadili (Riwaya za kidini)
Maranyingi hudokeza mapito ya mhusika mkuu toka utoto wake. Hujaribu kueneza maadili kwa jamii. Wahusika huwekwa ili wawe chachu ya maadili kwa jamii na kupinga uovu. Kwa mfano, Adili na nduguze na Kusadikika vya Shaaban Robert. Aghalabu, hujikita katika masuala ya dini. Misingi yake hukitwa katika vitu au mambo matatu ambayo ni: Pathema (yaani makosa au kosa), Mathema (yaani mafunzo au funzo) na Catharsis (yaani utakaso).
Riwaya za Kiamapinduzi
Huwazindua wasomaji ili wapambane na udhalimu na kubomoa mifumo ya ukandamizaji iliyopo katika jamii. Hudodosa dhana za mapambano, mikinzano na matabaka, riwaya hizi maranyingi ni za kihalisia. Mifano ya kazi za kundi hili ni: Kabwela (Abdulhaman Jumbe Safari), Ubeberu Utashindwa (Kiimbika), Kuli na Haini (Shafi Adam Shafi), Kusadikika (Shaaban Robert), Utengano (S.A. Mohamed na Dunia Mti Mkavu (S.A. Mohamed).
Riwaya za Kisosholojia
Riwaya zake huchunguza na kuibua maswali ya kijamii na kupiga darubini kali katika jamii. Hukazia vipengele vihusuvyo maisha ya kila siku katika jamii (desturi, mila na mabadiliko ya jamii). Huwa na uhalisi katika vipengele vyake. Maranyingi huwa na maudhui yenye kuhuwisha. Hugusia migongano ya kijamii kama vile ukale na usasa, umji na uvijiji, familia na ndoa kwa ujumla. Kwa mfano: Kurwa na Doto (M. Farsi), Dunia Uwanja wa Fujo, Mzimu wa Babu ana Radhi (F. Nkwera), Bwana Mnyombekera na Bibi Bugonoka na Harusi (A.J. Safari).
Riwaya za Kisaikolojia
Hujaribu kufichua hali ya kisaikolojia katika jamii kwa kuwatumia baadhi ya wahusika. Maudhui yake huhusu vita vya mazoea dhima ya uhalisi. Hujadili mikinzano aipatayo mtu ki―nafsi, ki―jamii na ki―uana. Hukitwa katika kuwako kwa (Kosa/udhaifu/jambo hasi/ utata na misawajiko kwa mhusika kuu). Mfano: Tata  za Asumini (S. Ahmed) Kichwamaji(Kezlahabi).
Riwaya za Kifalsafa
Hujadili mambo yenye urazini fiche. Mtunzi hudadisi mambo mbalimbali kwa jicho la kifalsafa (udodosi wa kina). Aghalabu, hutumia lugha tata na ngumu. Miongoni mwa mambo hayo yanayododoswa ni kuishi, ukweli, maisha, utu, kifo, kuwa na kutokuwapo kwa viumbe, kuwepo kwa Mungu n.k. baadhi ya maswali ya kifalsafa yaulizwayo ni kama vile: 
o   Maisha ni nini?o   Kuwapo na kutokuwapo kwa dunia ni kwatokeaje?o   Kuishi ni nini?o   Utu ni nini?o   Kwa nini watu au vitu vipo hivyo vilivyo?o   Kwa nini mambo yapo hivyo yalivyo?Mifano ya riwaya za kifalsafa ni riwaya kadhaa za Kezilahabi. Nazo ni: Mzingile, Nagona, Rosa Mistika, Kichwamaji. Riwaya za kifalsafa zilizoandikwa na waandishi wengine ni pamoja na: Babu Alipofufuka, Umleavyo, Walenisi, Mafuta naBin―Adamu.
Riwaya Pendwa
Husisimua na huwa na mvuto wa pekee kwa wasomaji. Aghalabu, fani hujichomoza zaidi kuliko maudhui. Pia humfikirisha sana msomaji. Rejea sifa mbalimbali zilizojadiliwa katika tapo la riwaya pendwa pamoja na mifano yake.
Riwaya za kitawasifu (riwaya sira)
Hizi ni tofauti na tawasifu. Riwaya zenye mwegamo wa kitawasifu zimetungwa kama vile tawasifu. Tawasifu hueleza maisha ya mtunzi. Riwaya ya kitawasifu hueleza maisha ya mhusika aliyeteuliwa na mtunzi. Huweza kuegemea u―chanya tu na kuacha kudokeza mambo hasi. Hulenga kutoa kumbukizi ili kuwahimiza wengine kuwa kama mhusika wa tawasifu. Katika riwaya ya kitawasifu, sauti ya mtunzi husikika kupitia maisha ya mhusika. Mfano mzuri wa tawasifu ni: Maisha yangu na baada ya Miaka Hamsini na Tippu Tip.
Riwaya za kiwasifu
Hizi hutungwa kama wasifu. Mtunzi hueleza maisha ya wahusika fulani. Katika wasifu mwandishi hueleza juu ya mtu aliyewahi kuishi au anayeishi. Wakati katika riwaya ya kiwasifu mtunzu hueleza maisha ya kubuni ya mtu ambaye labda hajawahi kuishi. Mifano ya riwaya ya kiwasifu ni: Shida (Ndyanoa Balisdya), Wasifu wa Siti Binti Saad (S. Robert),Salum Addallah (J. Mkabarab), Maisha ya Seti Benjamini, Mtemi Mirambo na Mkwawa na Kabila Lake.
DHIMA ZA RIWAYA
Pamoja na dhima nyingine za fasihi, riwaya inayo dhima ya ziada. Hii ni kushawishi (Propaganda). Propaganda ni kani ilengayo kushawishi mtu au watu kuelekeza fikra zao kule ajiegemezako mtunzi, propaganda huweza kutokea katika uga wowote wa kimaisha (hata nje ya uga wa fasihi). Propaganda hulenga kuleta ushawishi kwa watu ili wapate mabadiliko ya aina tofauti; ambayo ni: Ya kimtenguo, ya kiuimarishaji na ya  kiupya. Aina hizi za propaganda huweza kudhihirika katika riwaya mbalimbali.
Kazi ya mjadala:
Soma riwaya teule kwa makini, jenga mantiki kisha onyesha ujitokeaji wa dhima ya propaganda.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)