MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
HISTORIA NA MAENDELEO YA RIWAYA YA KISWAHILI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
HISTORIA NA MAENDELEO YA RIWAYA YA KISWAHILI
#1
HISTORIA NA MAENDELEO YA RIWAYA YA KISWAHILI
Historia na Maendeleo ya Riwaya za Kiswahili
Maana hasa ya “ri waya” sio rahisi kuifafanua. Mpaka sasa kuna ubishi mkali miongoni mwa wasomi wa fasihi kuhusu mpaka kati ya “hadithi fupi” na “riwaya” kama vipengele vya fasihi-andisli Kuna wale wanaotumia kigezo cha urefu na kudai kwamba “hadithi” au “kijiriwaya” ni kisa kifupi kinachokamilika kwa idadi ndogo ya maneno. Kwa kigezo hiki, riwaya kama zile za Shaaban Robert huitwa “hadithi”au “vijiriwaya” wala sio riwaya kamili.
Kwa upande mwingine, wapo wataalamu wanaoeleza kuwa undani wa vitushi, maudhui na fani nyinginezo ndivyo vipimo muhimu zaidi vya kuieleza “riwaya” wala sio idadi ya kurasa au maneno yake. Mfano mzuri wa wasomi wenye mwelekeo huu nikama vile Mlacha (1989). Kwa mujibu wa Mlacha, riwaya ni utungo wa natharia wenye kutongoa hadithi yenye urefu fulani, visa vinavyooana na inayozingatia swala nyeti kwa muda maalum. Swala la maana ya riwaya pia limeshughulikiwa na Syambo na Mazrui(1992). Wao pia wanatoa maoni sawa net yale ya Mlacha (1989) na wanaeleza kuwa urefu au ufupi sio kigezo muhimu cha kufafanua riwaya. Wanaeleza kuwa ubunifu, ploti na matumizi ya lugha ya nathari ndizo nguzo za riwaya.
Vigezo vya riwaya vilivyotajwa hapo juu ni vya kijumla na pia vimetokana na tamaduni Kimagharibi. Lakini, kama asemavyo Mohamed (1995), vigezo vya aina hii vinakubalika mrad visipingane na miiko, miundo, sifa na mielekeo ya jamii zingine ambazo zimezalisha riwaya kutegemeamila na utamaduni wake. Jamii zilizozalisha riwaye zake za kipekee zenye kujumuisha vipengelevya kigeni na kiasili ni Waswahili.
Kazi nyingine ambayo imeshughulikia swala la historia na maendeleo ya riwaya ya Kiswahili niile ya Rollins (1993) inayoitwa A History of Swahili Prose. Kitabu hiki kinafafanua historia ya maandishi ya nathari ya Kiswahili, chanzo chake, na aina zake kutoka miaka ya mwanzo wa kame hii hadi miaka ya 1970. Kinaeleza vipengele muhimu vya nathari hiyo kuwa Bekaya, Hadithi, Kioj~ Babari na baadaye maandishi kama vile Wasifu, Simo, Masimulizi, Neno La Bekima na Ngano~Mwandishi anaeleza kwamba misingi ya nathari ya Kiswahili ni fasihi simulizi ya Kiswahili.
Pengine udhaifu mkubwa wa kazi ya Rollins ni maadai yake kwamba kila kipenge1e cha Fasihi simuliziya Kiswahili kilitokana au kiliathiriwa na tamaduni za kimashariki.
Ni kweli kuwa nyanja au tanzu za riwaya na tamthilia hazijastawi na hazina historia ndefu kamavile utanzu wa ushairi. Wachambuzi wa maandishi ya fasihi ya Kiswahili wameeleza jambo hili kwa namna tofauti. Baadhi wameeleza kuwa uandishi wa nathari umefuata sana misingi ya fasihiya kimagharibi. Wao wameonelea kuwa ushairi wa Kiswahili ulikita sana katika misingi ya fani za kimasimulizi za Kiswahili ambazo ni za tangu jadi na hii ndio sababu umestawi kuliko nathari.Wengine nao wameeleza kuwa ushairi ulizingatiwa sana kuliko nathari kwa sababu ulikuwa naumbo na mpangilio uliosaidia wasimulizi kueleza na kukumbuka maudhui yao kwa urahisi kuliko nathari.
Ijapokuwa riwaya haina historia ndefu kama ushairi katika fasihi andishi ya Kiswahili, mpaka sasakuna kazi nyingi katika utanzu huu ambazo zinastahili kuelezwa jinsi zilivyoanza na kuendelea.
Hatahivyo, kabla ya kuanza kusimulia kwa tafsili historia na maendeleo ya riwaya za Kiswahili inafaakujadili niaswala na hoja kadhaa muhimu kuhusu nadharia ya riwaya kwa jumla. Maswala nahoja hizi zimekusudiwa kutoa ufafanuzi kuhusu maana na matumizi ya neno “riwaya”.
Nadharia Kuhusu Riwaya
Katika utamaduni wa kimagharibi, hususa Uropa na Marekani, tofauti kati ya maana za maneno ” .
riwaya”, “shairi”, “tamthilia” au “hadithi fupi” ni dhahiri. Kwa hivyo, mchambuzi au mhakiki wa fasihi huyatumia maneno hayo kiistilahi bila hofu ya kutoeleweka wala kukanganya. Hata hivyo, kwamaoni yetu, hivi sivyo mambo yalivyo katika fasihi ya Kiswahili hasa kuhusu umbo na sifa za utungo unaopaswa kuitwa ‘riwaya’ au ‘hadithi fupi’. Tungependa basi kueleza jinsi maneno haya yatakavyotumika katika makala haya.
Wachambuzi wengi wa fasihi ya Kiswahili wanaamini kwamba utanzu wa riwaya ya Kiswahili umeshabihiana sana na tanzu za tungo kama “kisa”, “hadithi”, “hekaya”, “kioja”, “habari”, “wasifu”, “simo”, “masimulizi”, “neno la hekima” na “ngano”.
Pengine msomaji angestaajabu, je, iwapo jambo hilo ni la kweli, basi, riwaya ya Kiswahili ni umbo jipya la mojawapo ya tanzu zilizotajwa hapo juu au ni utungo mpya ambao ni wa kigeni katika fasihi ya Kiswahili. Lakini, pengine haitoshi kusema hivyo kwani dai kama hili halitoshi kueleza sababu za kuwepo kwa riwaya ya Kiswahili kama tuijuavyo hivi leo. Pengine njia moja ya kulirahisisha swala hili ni kusema kuwa kwa hakika hakuna sababu za kitaaluma za kudai kuwa ronayo riwaya ya Kiswahili, Kiingereza, Kirusi, Kichina, Kijapani ama Kijerumani ambayo inazo sifaza kipekee zinazoitenga na riwaya kutoka katika tamaduni nyingine hasa kimtindo na kimuundo.
Hatuna budi kujiuliza sasa, ni nini basi maana hasa ya ‘riwaya’ katika fasihi-andishi? Ni dhahiri rwamba upana na undani wa swala hili la kinadharia unakiuka upeo wa makala haya. Hata hivyo, tunaitumia dhana hii kumaanisha utanzu wa fasihi bunifu ya kinathari, kazi ya kisanaa ambayo hujaribu kuwasilisha, kupitia maandishi ya nathari, mtazamo fulani wa maisha ya mwanadamu kwa usanifu na umbuji wa kuvutia huku ikichambua au kuunga vipengele kadha vya jamii.
Kazi kama hiyo, inayo sifa moja kuu ambayo ni uwezo wake wa kumsafirisha kimawazo msoma hatua- kwa hatua kupitia msururu wa tajriba mbalimbali zenye mpangilio mwafaka na zinazooam kimantiki na pia kazi yenyewe hutoa misimamo na maelezo kuhusu maudhui yake. Kwa hivyo maelezo mwafaka, udhahiri na uelewekaji ni mojawapo wa sifa muhimu za riwaya, kama alivyotajwa Kitsao (1979) na Ohly (1981).
Baada ya kutoa utangulizi mfupi na maelezo kuhusu matumizi ya istilahi “riwaya” katika makal haya, sasa tutapiga hatua nyingine mbele na kufafanua kiini na maendeleo ya utanzu wa riwaya Kiswahili. Baadhi ya utafiti ambao umefanywa kuhusu hoja hii, mbali na ule wa Mazrui na Kazungu (1981) ameichora fasihi ya Kiswahili kama kipengele tofauti na mazingira ya utamaduni wote wa Kiswahili au tuseme kama kipengele kidogo tu cha utamaduni huo. Utafiti huu umejishughulisha sana na vipengele vya umbo na mtindo wa fasihi na kwa nadra sana msingi ya kitamaduni na kijamii ya fasihi yenyewe. .
Makala haya yataangazia riwaya ya Kiswahili kihistoria na jinsi mtazamo huu unavyooana na maudhui ya kijamii yaliyomo katika kazi tofauti. Kwa maneno mengine, haja kubwa hapa ni kugundua ” ni kwa nini na ni katika hali gani ambapo riwaya fulani ilitungwa.”
Kutokana na sababu kadhaa za kihistoria na kijiografia, kazi nyingi za nathari zilizotungwa na kuchapishwa katika mataifa jirani kama vile Tanzania, Uganda, Zaire, Zambia, Congo, Rwanda
Burundi na Somalia hazijulikani sana hapa Kenya na ni nadra kupatikana. Hali hii inaifanya juhu ya kuzitalii riwaya za Kiswahili kuwa ngumu na zenye kufinyika sana kiupeo kwani kazi kurejelewa ni haba mno. Hata hivyo, riwaya nyingi za waandishi wa Tanzania kama Said Ahmed Mohamad, Shaaban Robert, Mohamed Suleman Mohamed, E. Kezilahabi na wengineo wachache, zimewahi kuchapishwa hapa Kenya katika miaka ya hivi karibuni. Jambo hili limeimarisha kufanikisha kusambaa kwa usomaji na uchambuzi wa riwaya za Kiswahili koteAfrika ya Mashariki.
IIi kurahisisha maelezo kuhusu historia na maendeleo ya riwaya ya Kiswahili, tumeyagawa makala haya katika sehemu nne kihistoria. Sehemu hizi ni kabia ya utawaia wa kikoioni, kipindi cha uandishi wa kiwango cha chini cha nathari, kipindi cha mapambano ya ukombozi na baadaye uhuru. Mgawo huu unawiana na ule wa Mazrui na Kazungu (1981) na Arnold (1973).
Kipindi Cha Kabla Ya Ukoloni: 1850 hadi 1890
Baada ya majilio ya Waarabu, mfumo wa kijamaa wa jamii ya Waswahili ulianza kuvunjilia mbali na mahali pake kuchukuliwa na mfumo wa kibwanyenye. Maudhui ambayo yanaegemea sana upande wa dini katika maandishi ya nathari ya wakati huu yametokana na kukolea sana kwa ustaarabu wa kidini wa jamii ya pwani ya Afrika Mashariki mnamo kame za 18 na 19. Ustaara huo ulikita sana kwenye misingi ya uisiamu. Hata hivyo athari hiyo haikuigeuza fasihi hii wala kuipokonya uafrika wake. Jambo muhimu sana kuhusu kipindi hiki ni kwamba hakukuwa na utunzi wowote wa maandishi ya nathari na kama ulikuwepo, basi ulikuwa haba mno. Huu ndio wakati ambapo utanzu wa ushairi ulifikia kilele huku washairi wengi wanaosifika sana wakitoa tungo nyingi za fahari ambazo zimebakia kuwa kielelezo cha ushairi bora wa Kiswahili hadi leo. Mifano mizuri ni kama Furno Liyongo (1160-1204 AD), Muyaka bin Haji (1776-1840 AD) na Seyyid bin’ Haji (1776-1840 AD) na Seyyid S.A Nassir (1720-1820 AD)
Washairi wengineo ni kama vile Mwengo bin Athman, mtunzi wa Chuo cha Tambuka, Mwana Kupona(1810-1860), Ali Koti, Abdalla Songora, Malenga Mkilifi na Mwinyi Jitu . Je, ni kwa nini hapakuwa na uandishi wa nathari wakati huu? Kazungu na Mazrui (1981) wamelijibu swali hili kwa kue1eza kuwa ushairi ulihifadhiwa kwanza kimaandishi kwa sababu ulikuwa mgumu kukumbukika na kusimulika kuliko nathari. Nathari, wanazidi kufafanua ilikuwa ni utunzi ambao ulimpamsanii uhuru zaidi wa kubuni kivyake kila aliposimulia na hali haikuruhusiwa wala haikuwa rahisikubadilisha muundo, mtindo au maneno ya shairi. Kwa hivyo, yamkini wasanii- walihiari kuzihifadhi tungo zote za kishairi kimaandishi na huku wakihifadhi nathari katika bongo zao.
Sababu nyingine ya kutokuwepo kwa riwaya au tungo za kinathari katika kipindi hiki ni kuwa tanzukama riwaya na tamthilia ni mazao ya fasihi ya kimagharibi. Pili, kwa vile hapakuwa na wanachuoni waliofuzu kuandika nathari miongoni mwa waswahili basi hapakuwa na yeyote aliyejitoma katika uandishi huu. Pengine sababu nyingine ni kuwa, ingawa waandishi wengi wa Kiswahili wangeweza kubuni kazi za kinathari, kujieleza kwa kutumia ushairi kulikuwa ni ishara yaustaarabu na elimu. Maandishi ya nathari hayakuwa ya fahari. Jambo hili linaweza kudhihirishwa nahoja kwamba katika ustaarabu na utamaduni wa Kiarabu ambao ndio uliouletea elimu jamii ya waswahili na hati ya kuandikia ulitukuza na kuthamini ushairi kuliko utanzu mwingine wowote.
Hatakatika tamaduni nyingine ambamo elimu na ustaarabu wa Kiarabu ulikuwa na athari kuu kama katikajamii ya Wahausa, hakuna kazi nyingi za nathari zilizotungwa katika wakati huu.
Ijapokuwa kipindi hiki (1850 hadi 1890) hakikuzalisha kazi nyingi za nathari, ni kiwakilishi muhimukatika historia ya riwaya ya Kiswahili kwani kinatangulia kipindi cha uhifadhi wa masimulizi katikamaandishi ya nathari. Pia kutokuwepo na riwaya au tungo za kinathari kabla ya kuja kwa wakoloniWaingereza hapa Afrika Mashariki kulitokana na kumilikiwa taaluma ya uandishi na ushairina maulama wa Kiisilamu na wafuasi wao kama wasemavyo Syambo na Mazrui(1992).
Kipindi Cha Uandishi Haba Wa Nathari: 1890 hadi 1930
Kufikiamwishoni mwa kame ya 19, wamishenari wengi walikuwa tayari wamepiga kambi mahali pengikatika pwani ya Afrika ya Mashariki. Hawa wageni wote hawakuwa wamishenari tu bali pia wasafui na wavumbuzi ambao walipendezwa sana na utamaduni wa Waafrika waliowazunguka.
Wajerumaninao, katika juhudi zao za kuimarisha utawala wao huko Tanganyika (Tanzania bara), walihimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli za utawala. Ni katika kipindi hiki ambacho kilishuhudia uandishi na kuchapishwa kwa kazi za kwanza za kinathari za Kiswahili. Machapisho yakwanza yalikuwa ni magazeti machache ambayo yaliuza nakala chache tu kama vile, Msimulizi (1888) na Habari za Mwezi (1894). Magazeti haya yaliandikwa katika lugha rahisi ambayo haikushirikisha maneno ya kikale,jazanda, maneno mapya ama matumizi mengine ya lugha bunifu.
Licha za magazeti, kazi za kwanza za nathari zilizotungwa zilikuwa ni maandishi ya ngano au hekaya za kutokana na misingi ya sihi-simulizi. Hii ilikuwa hatua muhimu sana katika kuibua chanzo cha riwaya. Ngano na hadithi hizi zilikuwa na sura na ishara za riwaya kama vile undani wa masimulizi, uumbaji wa kiubunifu wa wahusika, ploti, mandhari na hata utata wa kimaudhui.Maandhishi haya yalitungwa na wazungu hasa wamishenari katika Kiswahili K.m. Hadithi za Unguja(1967) na Mashujaa: Hadithi za Wayunani cha C. Kingsley. Baadhi ya maandishi yalikuwa katika Kiingereza K.m. Specimen of Swahili Short Stories (1866), Swahili Tales as Told by Nativesof Zanzibar (1870) cha Kasisi Steere, Swahili Stories (1885), Kibaraka: Swahili Stories from Arab Sources(1886). Hadithi nyinginezo pia ziliandikwa kwa Kijerumani K.m. Prosa und poesieder Suaheli (1907) cha C. Velten na Anthrologie aus der Suaheli-literatur (1894).
Kazi ya kinathari ambayo ilichapishwa wakati huu na ambayo inahesabika kama ya mwanaya aina yake ni ile iitwayo Habari za Wakilindi iliyotungwa na Abdalla Hemed Liajjemi katili mwaka 1905. Kulingana na Kitsao (1979), hii “ni hadithi ya kiwango cha juu kuhusu watu waitwa Wakilindi waishio Tanganyika (Tanzania bara). Licha ya upungufu wake, Habari za Wakilindi bado ndio kazi ya kwanza ya nathari katika Kiswahili ambayo imekaribia sana riwaya ya kisas hasa kwa upande wa uumbaji wa wahusika na uwasilishaji wa mazingira ya kijamii.
Machapisho mengineo ya nathari ya wakati huu ni kama vile Habari za Pate (1913) na Habari  za Lamu. Hata hivyo nathari ya aina hii ilitupiliwa mbali katika ruiaka ya 1930 ambapo mitind mipya ya uandishi wa riwaya za Kiswahili ilianzishwa. Riwaya za kimasimulizi na kihistoria ziliana kufifia umaarufu na mahali pake pakatokea aina ya riwaya ya kimasimulizi iliyokusudiwa kusisimu na kufurahisha kama inavyoelezwa katika sehemu ifuatayo.
Kipindi Cha Mapambano Ya Uhuru 1930 hadi 1960
Hiki ni kipindi ambacho kilizalisha kazi nyingi za natharia kuliko vipindi viwili tulivyojadili. Kufia mwanzo wa miaka ya 1930, mfumo wa elimu ya Waafrika ulikuwa umepanuka sana. Kwa hivyo ilizuka haja kubwa ya kuandika vitabu vingi ambavyo vingetumiwa katika shule. Ni kutoshelea haja hii ndipo vitabu vingi vilipotafsiriwa katika Kiswahili, hasa kutoka Kiingereza. Mahiui makubwa hasa yalikuwa katika viwango vya shule za msingi; katika madarasa ya chini na ya kati
Hapakuwa na waalimu Waafrika wa kutosha waliohitimu kuweza kuandika vitabu kama hivyo.
Kwa hivyo wamishenari hawakuwa na la kufanya ila kutafsiri vitabu hivyo. Mifano ya vitabu vya aina hiyo ambavyo bado vinatumika hadi leo shuleni mwetu ni, – Mashimo ya Mfalme Suleman. Kisiwa Chenye Hazina, – Hadithi za Abunuwas, Alfu Lela Uleta na Hadithi za Esopo.
Vitabu hivi vya kutafsiriwa vilikuwa na sifa moja kuu ambayo ni kwamba ijapokuwa ni sehemu ya fasihi iliyotungwa kwa lugha ya Kiswahili, vilisimulia mazingira yasiyokuwa ya uswahilini maana vimewahi kushitakiwa kuwa ujumbe uliomo ulikusudiwa kumdunisha Mwafrika mbele ya mtu mweupe. Wazungu walikuwa pengine na nia ya kutafsiri na kuwafunza waafrika aina ya fasii ambayo ingewafanya waafrika kuendelea kuwanyenyekea wakoloni. Maudhui kama hayo yam katika kazi kama Mashimo ya Mfalme Suleman na Uhuru wa Watumwa (1934).
Baadaye, katika miaka ya 1950, waandishi wa Kiafrika kama vile Shaaban Robert walians kutunga fasihi ya kufurahisha na kuasa wasomaji wa tabaka la wasomi lililokuwa limeanza kujengeka baada ya waafrika wengi kujipatia elimu ya kigeni. Tabaka hili lilikuwa la watu kama wamishenari watawala na watumishi wa serikali. Kazi kama vile Adili na – Nduguze (1952), Kufikirika na Kusadikika zilitokea kutekeleza haja hii. Fasihi kama hii ilipendwa sana na ilichapishwa na wachapishaji wa kikoloni.
Hata hivyo ni muhimu kusisitiza hapa kuwa, kazi za aina hii hazikuwa tu na maudhui ) unyenyekevu na utiifu bali baadhi kama vile Kusadikika ziligubika mawazo yenye uzito yaliyowes kuichambua jamii kisiasa na kifalsafa. Pana ushahidi wa kutosha kudhihirisha hoja hii kutoka katika riwaya za wakati huu. Kwa mfano, wimbo huu katika Wasifu wa Siti Binti Saad unao mchomo uliolengwa kumdhihaki mtawala fulani wa Kiarabu aliyewatawala waafrika wakati huo. Kejeli yenyewe imefichika sana:
Bwana ulipoondoka
Raia tuliinama
Sote tulidhoofika
Tulihadhiri jasama
Na sasa umefika
Mwili utarudi nyama
Astahiki salama
Maulana El Amiri 3
Kwa hakika, Kusadikika ambayo ndiyo riwaya inayojulikana zaidi miongoni mwa kazi za ShaabanRobert, inayo maudhui ya kukosoa mfumo wa kisiasa katika Tanganyika ya kabla na baada yauhuru.Wachambuzi wengi hawajawahi kuyafichua na kuyafafanua maudhui haya hadi leo. Hadithi hii haipendekezi tu kuwa mawazo ya kigeni yashirikishwe katika ujenzi wa mataifa yetu machanga bali pia inafaa kuwepo na uhuru wa kujadili njia zote zinazofaa za kuyajenga mataifa haya na pale inapolazimuau inaposadifu, mawazo hata ya kutoka nchi za kigeni yashirikishwe.
Mwelekeo wa utetezi katika fasihi ya Kiswahili kwa hakika ulianza hapo awali na kuna ushahidi wakutosha wa kuthibitisha jambo hili kama ubeti huu wa Utenzi wa Maji Maji unavyodokeza:
Kilwa na Dari’s salama
Kuna wazungu nakama
Mtu hapati kusema
Nti wamezizima
Hata hivyo, ni sharti ikumbukwe kwamba kipindi hOO, hasa mwanzo mwanzo kilikuwa na nathariiliyotungwa kusifu na kustahi enzi ya watawala wa kikoloni ijapokuwa sio moja kwa moja.
Kwamfano, Shaaban Robert mara kwa mara aliwasifu sana watawala hao na hata aliona fahari kutungabaadhi ya vitabu vyake kwa heshima yao.
Kwa hivyo mwelekeo wa utetezi dhidi ya ukoloni haukuchochewa na itikadi ya kisiasa iliyokita katikafalsafa yoyote bali ilitokana kwa upande mmoja na uhasama kati ya uislamu na ukristo.
Penginewaliotunga fasihi yenye mwelekeo huo wangetosheka na mfumo uliokuwepo hapo awali – yaani ujumuiya wa kijadi kabla ya kufika kwa wakoloni wa kimagharibi.
Fasihi yenye kupinga ukoloni hasa ilianza kushika kasi na kuwa na mwelekeo imara katika miaka ya 1950. Kazi za Shaaban Robert kama vile maisha yangu na Baada ya Miaka Hamsini na hatamashairi kama Almasi zaAfrika (1960) ni mifano mizuri ya kazi za aina hii. Waandishi kama ShaabanRobert walianza kujishabihisha na waandishi wenzao kama George Benard Shaw ambao walikuwamaarufu kwa kuongoza juhudi za kupigania uhuru katika nchi zao.
Ni jambo la kushangaza sana kuwa kwa kulingana na fasihi katika Kiingereza ya wakati huu ambayoilikuwa na kazi nyingi za nathari zilizohusu juhudi za mapambano ya uhuruAfrika Mashariki, fasihiya Kiswahili haikuwa na kazi nyingi kama hizo. Mifano ya waandishi waliotumia Kiingereza naambao walitunga kuhusu vita vya uhuru ni kama Ngugi wa Thiong’o, Joe Mutiga, Jonathan Kariarana Mugo wa Gatheru. Pengine sababu moja ya ukosefu huu ni kwamba hakukuwa na wasomajiwengi wa nathari katika Kiswahili wakati huu. Pia yamkini kwamba waandishi kama ShaabanRobert waliogopa mchujo wa maandishi yao na serikali ya wakoloni na hawakutaka kuhatarisha vyeo vyao kama watumishi wa serikali. Kwa hivyo, walihiari kuendelea kutungajuu ya maudhuiya kitamaduni na maadili ya kijamii.
Bila shaka, kama anavyoeleza Wafula (1989), Shaaban Robert ni mwandishi aliyekuwa na tajriba pana ya kimaisha ambayo iliathiri sana uandishi wake. Imani yake ya utu wa Mwafrika na kimaadili ya dini ya Islamu pamoja na mazingira ya ugandamizi ya kikoloni yalinoa ubongo wa Shaaban Robert na kumwezesha kuwa na mtazamo na msimamo thabiti wa kimaisha. Hii ndiyo sababu r aliweza kubuni kazi zenye kina cha falsafa na uhalisi katika vijiriwaya vyake. Kazi za Shaaba Robert zinawakilisha hatua muhimu katika ukuaji wa nathari ya Kiswahili.
Kutokana na hali hii, vijiriwaya vingi wakati huu vilitungwa kufurahisha na kuwaidhi. Mifano ni kama, Adaza Arusi katika Unguja (1960), Kurwa na Ndoto (1960), Kisa cha Mrina Asali na Wenzake Wawili (1962), Siku ya Watenzi Wote (1963), Utubora Mkulima na vinginevyo.
Njia mojawapo ya kueleza kwa nini riwaya ya Kiswahili haikuendelea sana wakati ni kuuangals mfumo wote wa utawala wa kikoloni. Ni dhahiri kuwa waandishi wa Kiswahili walitingwa vikwazo vingi wakilinganishwa na wenzao weupe au walioandika kwa Kiingereza. Kwa hakika,  waandishi wa Kiingereza sio tu kwamba walipendelewa na kusaidiwa na wakoloni bali pia hata mashirika ya uchapishaji ambayo yalimilikiwa na wakoloni yalipendelea kuchapisha kazi za Kiingereza kuliko za Kiswahili.
Kiswahili, kwa ujumla, kilipewa hadhi ya chini kuliko Kiingereza. Kwa kiasi fulani, sababuhi inatufahamisha kwa nini waandishi kama Shaaban Robert, Swaleh Farsey na Mohamed Said Abduh ambao walikuwa na uhusiano mzuri na watawala wa kikoloni, kazi zao zilipokelewa na kuchapishwa kwa urahisi hata ingawa walikabiliwa na vikwazo kadhaa wakilinganishwa na waandishi wa Kiingereza.
Kipindi Cha Baada Ya Uhuru: 1963 hadi 1992
Utungaji wa riwaya zenye maudhui ya kitamaduni na kijamii haukukoma wakati uhuru ulipopatikani bali utunzi kama huo uliendelea kwa muda mrefu baada ya uhuru. Mifano mizuri ya kazi kama hizo ni Mtugeni (1971) kilichotungwa na Buyu, Kuishi Kwingi ni kuona Mengi cha J.B. Simba, Simba Kaishi na Wanadamu (1970) kilichotungwa na Joy Adamson na pia kitabu cha Patterson kiitwacho Simba wa Tsavo ambacho ijapokuwa kilichapishwa mnamo mwaka wa 1947, kilitolewa mara nyingi baada ya uhuru.
Katika kipindi hiki waandishi wengi walianza kujitokeza na kutunga kazi nyingi za nathari juu ya maudhui mbalimbali. Kazi nyingi zenye maudhui ya utamaduni asilia zilizuka. Kwa mfano, “Naushangilia Mlima Kenya cha Jomo Kenyatta, Kaburi Bila Msalaba, Uhuru na Baadaye, Mau Mau Kizuizini, Ujamaa Wa Mwafrika na vinginevyo. Idadi kubwa ya riwaya hizi zilikuwa na maudhui ya kisiasa na utetezi dhidi ya ukoloni na hali vingine vilikuwa na mwelekeo wa kihistoria. Athari ya maandishi haya ya kisiasa ilizua msisimko mpya ambao ulielekeza fasihi katika wakati wa mwamko (disillusionment) katika miaka ya katikati ya 1960.
Wachambuzi wa fasihi na waandishi wengi wametambua kwamba fasihi ya Kiswahili sio chombo cha pekee ambacho kinawasilisha utamaduni wa Kiswahili. Wameeleza kuwa hata fasihi katika lugha nyinginezo kama Kiingereza, Kifaransa, Kireno, Kiispaniola, Kirusi, Kichina na kadhalika haziwezi kusemekana kuwa zinawasilisha tamaduni za jamii hizo kikamilifu. Wote wanatambua kuwa riwaya ya Kiswahili inatekeleza jukumu muhimu kwani licha ya kuendeleza uzuri wa sanaa ya fasihi-tungo, pia huichambua jamii kwa tafsili. Riwaya huifunza na kuionya jamii. Kazi kama vile hadithi ya Rosa Mistika ni mfano mzuri wa riwaya kama hizi za mafunzo na maonyo kwa jamii.
Kipindi cha baada ya miaka ya kati ya 1970 kilitoa riwaya zilizo na sifa mbili kuu.
Sifa ya kwanzani juhudi kuu ya kutafsiri hasa riwaya za Kiingereza katika Kiswahili. Sehemu kubwa ya riwayahizo zilijumuika katika mkondo wa fasihi ya Kiswahili. Licha ya ugumu wa kutafsiri, riwayahizi zimeikwasisha fasihi ya Kiswahili kwa kuiboresha mitazamo na mielekeo yake na kuipanuamipaka ya maudhui na maswala yake. Wasomaji wa fasihi ya Kiswahili waliweza kutalii uwanjampana zaidi. Kazi hizo ambazo zilikuwa pamoja na riwaya, tamthilia na mashairi sharti zihesabike kama kazi asilia za fasihi ya kiswahili. Mifano ya kazi hizo za tafsiri ni Boi, Shujaa Okonkwo, Wema hawajazaliwa, Hamkani si Shwari Tena, Mwakilishi wa Watu, Njia Pa nda, UsilieMpenzi Wangu, Shamba la Wanyama na vinginevyo.
Sifa nyingineyo muhimu ya fasihi ya Kiswahili iliyotungwa katika mwisho wa muon go wa 1970,ni kuanza kujitokeza kwa aina ya fasihi ambayo tunaweza kuieleza kama “fasihi yenye msimamo wa kiitikadi”. Hii ndiyo fasihi ambayokimaudui na kimtindo, ilielekea kuwa na undani zaidi kuliko ile ya hapo awali. Fasihi hii ilianza kuonyesha mwe1ekeo wa kuzitathmini jamii zetu kwambinu za kisayansi za uchambuzi. Fasihi hii ilianza kutafuta chanzo cha baadhi ya matatizo ya jamii hizi sio tu katika ukoloni na ukoloni mamboleo bali hasa kutokana na miundo ya jamii na mifumoyetu ya kiuchumi.
Katika aina hii ya fasihi, hapakuwa na nafasi ya fasihi tumbuizi ambayo ilitungwa kwa kusudi kuula kusisimua tu kama vile kazi za waandishi kama Ndeti Somba, Mohamed Said Abdulla, Faraji Katallambula na Banzi. Udhaifu wa fasihi hii tumbuizi ulikuwa ni ufinyu wa upeo na mtazamo wakekwani wasanii hawa waliyafafanua na kuyachambua matatizo ya kijamii kama ambayo yalisababishwa na nguvu tu za kimaumbile na wala si binadamu mwenyewe. Fasihi yenye mwelekeo kama huo ilishutumiwa kwa kujaribu kuambaa uhalisi wa jamii. Aina mpya ya fasihi yenye mwamko iliendelezwa na wanariwaya mashuhuri kama vile Mohamed Suleman Mohamed, Said Ahmed Mohamed,Shafi Adam Shafi, Mwalimu Julius Nyerere, E. Kezilahabi, George Mhina, J.K. Kiimbila na wengmeo, Hii ndio aina ya fasihi anayojaribu kuifafanua F.E. Senkoro anapofasiri mawazo ya Mao Tse Tung kuhusu jukumu la fasihi tumikizi.
Anaeleza:
Ni lazima tuhakikishe kuwa fasihi na
sanaa ni sehemu muhimu ya utaratibu wote
wa mapinduzi – kwamba hizi ni nyenzo imara
wa kuwasaidia watu kumkabili adui kwa
moyo na nia moja. (tafsiri yangu)
Pia Abdilatif Abdalla anayo maoni saw a katika utangulizi wa kitabu cha Said Ahmed Mohamed kiitwacho, Sikate Tamaa:
Fasihi ni sharti iikosoe jamii wala
sio kukariri yale yaonekanayo ama
yasemwayo kuwa ndiyo yanayotokea
Kati ya riwaya za Kiswahili zilizofikia upeo wa juu zaidi katika fasihi yenye mwamko ni Donia Mti Mkavu cha S.A. Mohamed. Katika maoni yetu inaweza kuelezwa kuwa yenye mwelekeo wa ukombozi wa tabaka la mafelahi. Inatoa ufafanuzi wa mapambano kati ya makabaila na umma.
Fasihi kama hii ni ishara ya tajriba ya mwandishi anayejihisi kuwa sehemu ya umma na mapambano yao ya kujikomboa. Haidhihirishi athari zozote za kibwanyenye juu ya msanii na ni tofauti kabisa kimaudhui na fasihi ya miongo ya 1950 na 1960 iliyopendekeza mabadiliko hafifu katika mfumo wa jamii. Fasihi hii mpya inatoa mwito wa mapinduzi ya kitaaluma na yaliyopangwa mahsusi ili kuugeuza mfumo wa kiuchumi na kijamii kama suluhisho la kudumu la kipekee juu ya matatizoj jamii zetu.
Hata hivyo, inaweza kudaiwa kuwa kuanzia mwishoni mwa mwongo wa 1970 na 1980, utunzi wa nathari katika Kiswahili, hasa utanzu wa riwaya ulifikia kilele chake katika upande wa umbi mtindo na maudhui. Jambo hili linadhihirishwa na ushahidi kutokana na kiwango cha juu cha usanifu wa kimtindo na kiisimu unaobainika katika uandishi wa wanariwaya kama E. Kezilahabi na S.A
Mohamed ambao wametia fora sana katika uwanja huu katika miaka ya hivi karibuni. Licha ya kuvinjari uzuri na udhaifu wa maongozi ya siasa ya ujamaa katika taifa lake la Tanzania, E. Kezilahabi amezidi kufafanua falsafa ya udufu na upweke wa maisha (existentialism) katika jamii ya kisasa ambayo imekabiliwa na migogoro ya mabadiliko ya kisiasa na kitamaduni. Hii ndio miangaza inayopatikana kutokana na usomaji wa riwaya za Kezilahabi mbili,yaani, Gamba la Nyoka na Nagona.
Kwa upande mwingine, Said Ahmed Mohamed amezidi kuendeleza falsafa yake kuhusu maana ya uhuru na ukombozi wa kisiasa na kiuchumi katika mazingira ya ukoloni mambo-leo katika riwaya yake, Kiza Katika Nuru (1988). Pia, ameshughulikia swala la vikwazo na maonevu dhidi ya mwanamke katika jamii ya kisasa ya kiafrika katika Tata za Asumini (1990). Katika riwaya hii mwandishi huyu amejaribu kusarifu mhusika ambaye amekusudiwa kuwa kielelezo cha shujaa wa kike katika mapambano ya ukombozi wa wanawake.
Ni jambo la kushangaza kwamba waandishi hawa wawili maarufu wameathiriwa na falsafa ya kimagharibi ya udufu wa maisha (existentialism) na uhalisi wa kimaumbile (phenomenologismiy wanafalsafa kama Samuel Beckett, Jean Paul Sartre, Albert Camus na Martin Heidegger. Hata hivyo, ni kweli kwamba kazi zao zimehifadhi sifa kamili za uafrika halisi kiumbo, kimtindo, kimaudhui n pia kimazingira.lO Athari ya Kimarx, pia inapatikana katika riwaya za hivi karibuni kama vile Walenisi (1995) cha Katama Mkangi.
Kunao pia waandishi wachache wa riwaya za Kiswahili ambao, ingawaje kazi zao hazijaenea na kusifika sana hapa Afrika Mashariki, bado zina umuhimu mkubwa katika mchango wake. Mifano ya wasanii kama hao ni Shafi Adam Shafi aliyetunga Kuli (1988) na Kasri ya Mwinyi Fuad (1979).
Pia kunaye Z. Burhani aliyeandika Mali ya Maskini (1981) na Mwisho wa Kosa (1989) na pia Katama Mkangi Ukiwa na Mafuta. Hiki cha pili kilionyesha maendeleo makubwa ya falsafa ya mwandishi kutoka aandike Ukiwa, hadithi ya mapenzi. Mafuta kinachambua kwa njia ya kimafumbo maovu ya kisiasa ya kijamii katika Kenya huru. Isitoshe, riwaya ya Yusuf King’ ala, Anasa ambayo inawakilisha uchambuzi wa uchoyo wa tabaka la makabaila katika Kenya, inaweza pia kujumuishwa katika kikundi hiki.
Hitimisho
Tunaafikiana na maoni ya W.H. Whiteley kuwa fasihi ya Kiswahili haina wingi wa maandishi ya kinathari na hasa fasihi iliyotungwa kabla ya miaka 1980. Hatuwezi kusema kuwa sababu kuu iliyosababisha hali hii ni kule kuteuliwa kwa lahaja ya Kiunguja kama msingi wa Kiswahili sanifu hapo 1930. Ni kweli kuwa Kiunguja ilikuwa lahaja ambayo haikuwa na wingi wa fasihi ya kimaandishi ikilinganishwa na lahaja ya Kimvita ambayo ilikuwa na historia ndefu sana ya maandishi, hasa ushairi. Pengine upungufu huo pia ulisababishwa na athari ya ustaarabu wa Kikristo na Kiislamu, elimu rasmi ya kigeni pamoja na mielekeo iliyotokana na ukoloni.
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa fasihi ya Kiswahili sasa imezidi kukwea ngazi ya umaarufu na hata kuwezakushindana na ile ya Kiingereza. Lile pengo kuu kati ya tungo za kinathari na riwaya za kisasa linazidi kuzibwa. Kwa mfano, riwaya fupi kama vile Kiu na Rosa Mistika zimekusudiwa mtekelezawajibu huu.
Makala haya yamefafanua, ijapokuwa kwa ufupi, baadhi ya hatua muhimu ambazo riwaya ya Kiswahili imepitia katika maendeleo na historia yake na pia athari kuu ambazo ziliathiri maendeleo hayo. Athari hizi ni za ndani na pia za kutoka nje. Kwa mfano, mapendeleo ya mwandishi na kiwango chake cha elimu ni mfano mzuri wa athari kama hizo.
Pia tumetaja hapo awali kwamba kuna uhaba wa kazi za nathari hapa Kenya na Uganda zilizotungwakwa lugha ya Kiswahili. Fasihi iliyotungwa kwa kiingereza bado imezidi ile ya Kiswahili hapanchini. Jambo hili linaweza kuelezwa kama lenye kusababishwa na hali ya kutwezwa kwa Kiswahili na lugha nyinginezo za Kiafrika na kutukuzwa kwa lugha za kikoloni kama Kiingereza.
Jambohasa linalokera ni kwamba utaratibu wa kusuluhisha hali hii unakwenda kwa hatua ya polepole sana hapa Kenya na itachukua muda mrefu kabla Kiswahili hakijapata waandishi wake wa kujivunia kama vile fasihi ya Kiingereza inavyojivunia wasanii hodari wake kama Ngugi wa Thiong’o, Meja Mwangi, David Maillu na kadhalika. Wasomaji wa fasihi ya Kiswahili wanatamani kuweza kupata kazi za kinathari za aina nyingi kama riwaya za kadhia, tawasifu, usafiri na uvumbuzi, watu mashuhuri, sayansi na historia.
Maoni yetu ni kwamba fasihi ya Kiswahili itaweza kukua tu pale ambapo mwelekeo wa wananchi kuhusu Kiswahili utakuwa wenye imani na pale ambapo asasi zetu za kisiasa zitahimiza matumizi ya Kiswahili katika nyanja zote za maisha na kuonyesha juhudi kamili za kuikuza lugha hii maarufu.
Hapo tutaweza kuwa na mfululizo wa machapisho ya nathari ya kiwango cha juu yanapolinganishwa na kiwango cha fasihi bora kote duniani.
MarejeIeo
Farouk, T 1975. Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili: Kitabu cha Kwanza. Nairobi: Oxford Universe Press.
Farouk, T 1977. Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili : Kitabu cha Pili. Nairobi: Oxford Universit Press
Mlacha, S.K. na Madumulla ]’S. 1991. Riwaya ya Kiswahili. Dar es Salaam: Dar es Salaam Universe Press.
Ohamed,S.A.1995. Kunga za Nathari ya Kiswahili. Nairobi: East African Educational Publishers.
usokileM,1993.Misingi ya Uhakiki wa Kiswahili. Nairobi: East African Educational Publishers.
lIins,J.D. 1983. A History of Swahili Prose. Leiden.
Sengo, T.S.Y. na Kiango, S.D. 1974. Ndimi Zetu 1. Tanzania, Oar es Salaam: Longman.
Koro, F.K. 1982. Fasihi. Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.
Ambo, B. na Mazrui, A. 1991. Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers.
Ula, R. M. 1989. “The Use of Allegory in Shaaban Robert’s Prose Works.” M.A. Thesis. Unpublished: University of Nairobi.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)