MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
HAKIKI RIWAYA YA MIRATHI YA HATARI AU KURWA NA DOTO

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
HAKIKI RIWAYA YA MIRATHI YA HATARI AU KURWA NA DOTO
#1
HAKIKI RIWAYA YA MIRATHI YA HATARI AU KURWA NA DOTO KWA KUZINGATIA MISINGI YA FALSAFA YA KIAFRIKA YA PLACIDE TEMPELS. MAWAZO HAYA YANA NAFASI GANI KATIKA JAMII YA LEO YA KITANZANIA
Maana ya falsafa ya kiafrika kwa mujibu wa Placide Tempels, Falsafa ya kiafrika ni ile falsafa inayowashughulisha waafrika wenyewe na watu wengine ambao sio waafrika lakini wanakubaliana na mila, tamaduni za waafrika na fasihi simulizi za kiafrika.Hivyo falsafa ya kiafrika ni ile falsafa ambayo imejikita katika mifumo ya kijamii, mila na desturi na fasihi simulizi za kiafrika.
Placide Tempels alizaliwa tarehe 18/02/1906 katika mji wa Barcal huko Ubelgiji na alikufa tarehe 09/10/1977 akiwa na umri wa miaka sabini na moja huko huko Ubelgiji. Aliishi Kongo kwa miaka ishirini na tisa mpaka pale aliporejea kwao ubelgiji. Kwa kipindi chote alipokuwa Kongo alifanya kazi kuu mbili, kazi ya umishenari na uandishi.Katika kipindi chote hicho alichokaa Kongo alisoma tabia ya waafrika wanaoishi Kongo hususani kabila la Waruba, na akabaini kuwa waafrika wana tamaduni zao zilizojikita katika fasihi simulizi. Hivyo akaandika kitabu chake kiitwacho “The Bantu philosophy” (1945), katika kitabu hicho anapinga mawazo ya wazungu kwa kusema kuwa waafrika wanafalsafa yao na hivyo Tempels akatumia hoja kadhaa kutetea mawazo yake hayo, kama imani ya uchawi, hofu ya uhai na kifo, nguvu hai, suala la ndoa na dhana ya uduara.
Katika kujibu swali hili riwaya ya “Mirathi ya Hatari” ndio inayotumika. “Mirathi ya Hatari” ni riwaya ilioandikwa na C. G. Mung’ong’o (1977). Riwaya hii inajaribu kuelezea visa na mikasa ya kisihiri iliojitokeza katika jamii za kiafrika hususani katika jamii ya Njombe (Kiterevadzi) na maeneo mengine. Hivyo msanii amemtumia mhusika Gusto ambaye ndiye anayerithishwa mirathi ya hatari kutoka kwa baba yake Mzee Kazembe, mirathi hiyo ndiyo inayopelekea vifo vingi kutokea ikiwemo visasi mfano kifo cha mama yake Gusto na dada yake Nandi, pia inapelekea kifo cha mjomba ake Gusto Kapedzile. Ukiachana na vifo hivyo pia inapelekea kutokea kwa matukio mengi ya kiuchawi.
Ufuatao ni uhakiki wa riwaya ya “Mirathi ya hatari” kwa kuzingatia misingi ya kisalsafa kama ilivyoainishwa na Placide Tempels katika kitabu cha “The Bantu Philosophy” na kuonyesha uhalisia wake na faida na hasara ya falsafa hiyo katika jamii ya kitanzania.
Imani ya uchawi, Katika falsafa ya imani ya uchawi Tempels anaamini kwamba waafrika wanategemea sana nguvu za kichawi, katika kuelezea suala hilo Tempels anajaribu kuangalia jamii ya Ulaya kwamba wengi wapatapo matatizo hurudi kwa Kristo lakini jamii nyingi za Afrika pindi wapatapo matatizo hutegemea uchawi kama suluhisho la matatizo yao wanayarudisha kwenye imani za kishirikina. Falsafa hii ya imani ya uchawi imejitokeza kwa kiasi kikubwa sana katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” kwani kuna matukio mengi ambayo yanadhihirisha hilo. Mfano,  kitendo cha Gusto kukabidhiwa mirathi ya uchawi kutoka kwa baba yake. Mfano uk. 15 Mzee Kazembe anamwambia Gusto “Mwanangu nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukiutumia vyema, bali pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo, nakuachia dawa zote za milki yangu katika mizungu ya sihiri”. Pia uwepo wa kiapo cha uchawi, unadhihilika pale ambapo Gusto anaapishwa kama ni uaminifu wa kuingia katika uchawi kiapo hicho kila mtu anahitaji kiapo ndipo awe mchawi; mfano katika ukurasa wa 21 anaonekana akiapa kwa kutamka maneno, “Enyi Mahoka na Mababu…”. Pia mazingira ya vifo vyote, vinatokea katika mazingira ya utatanishi ambayo ni mazingira ya kichawi. Mfano, kifo cha Kapedzile, ambaye aliuliwa na Gusto, kifo cha Dina ambaye aliuliwa katika mazingira ya kichawi na baba yake, kifo cha mama yake Gusto Nyamidze na Nandi ambao walikuwa na Malipula kwa kutaka kulipa kisasi na kifo cha Malipula aliyeuliwa na Gusto pamoja na Mavengi katika mazingira ya Kichawi.
Katika jamii yetu ya kitanzania imani ya uchawi inajitokeza sana kwani kuna matukio mengi yanayojitokeza na yanaonekana kiuhalisia mfano watu kugandishwa katika nyumba za watu na pia kila kukicha wanaonekana wakianguka usiku na Nyungo zao, pia suala la uwepo wa misukule katika nyumba za watu. Pia baadhi ya watu kutumia hirizi kama kinga. Falsafa ya imani ya kichawi haina nafasi katika jamii kwani inasababisha migogoro mingi, maafa pamoja na kurudisha maendeleo nyuma. Hivyo wanajamii wa leo wanaaswa kuachana na imani za kichawi.
Hofu ya uhai na kifo. Hii ni hoja nyingine ya Tempels kwani anaamini kuwa Waafrika wana hofu ya uhai na kifo. Kwa kudhihilisha hili anaweza kuangalia salamu zao, na pia mtu anapopatwa na ugonjwa anaamini hawezi kupona na kifo kinamsogelea. Wazo hili limejitokeza pia katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” mfano pale Mzee Kazembe anapomueleza mwanae kuwa hali yake ni mbaya na kifo kinamkaribia uk. 15 “Siku zangu zimekwisha sidhani kama nitaishi zaidi”. Pia mama yake Gusto alikuwa na hofu na uhai wa Gusto na ndio maana akamuusia aachane na mirathi aliyokabidhiwa na baba yake kwani anaweza akapoteza maisha. uk 38 “Sipendi nimpoteze tena hata mmoja wenu kabla sijafa”.Pia suala la salamu na kujua hali ya mtu inaonesha hofu ya kifo, mfano ni pale Malipula alipokwenda nyumbani kwa kina Gusto walianza kujuliana hali uk. 57,……Nikawauliza….., “Habari za nyumbani wazee wangu”, “Nyumbani kwema tu” alijibu mzee Kindimba “Lakini hatujui ya huko nyuma”
Suala la hofu ya uhai na kifo linajitokeza sana katika jamii ya kitanzania mfano, Watanzania asubuhi wakiamka au wasipoonana muda mrefu basi hutoleana salamu na kujuliana hali, pia pale mtu anapoamua watu huwa na wasiwasi sana na uhai wake hivyohujikithirisha kumuombea dua ili aweze kupona. Falsafa ya uhai na kifo ina nafasi katika jamii kwani inawafanya wanajamii kuchukuwa tahadhari ili kuzuia kifo, pia inaendeleza dhana ya kustawisha zaidi uhai. Kwa upande mwingine falsafa hii in hasara kwani hurudisha nyuma maendeleo kwa sababu mtu ataogopa kufanya suala la maendeleo kwa kuhofia kifo ambacho kitamfanya kuacha mali zote alizochuma pia kutotimiza malengo yake.
Waafrika wanaamini katika suala la ndoa, pia hili ni wazo la Placide Tempels ambae anasema kuwa waafrika wanaamini sana katika ndoa zao na ndoa hizo hudumishwa ili kupata watoto. Uhai wa binadamu unaanzia kwenye mimba ambayo ni matokeo ya Ndoa. Wazo hili linaonekana sana katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” mfano ndoa ya Kazembe na Nyamidze watoto wanaopatikana ni nane na wanaokufa ni watoto watano ambapo uk. 5 unaonyesha hilo. Pia  familia ya Malipula na mkewe pia wana watoto. Pia mjomba wake Dina alikuwa na ndoa iliyompeleka kupata watoto katika uk.78.
Suala hili la ndoa linasawiri maisha halisi ya kila siku ya Tanzania mfano kuna ndoa za kanisani, msikitini ndoa za serikali na ndoa za kijadi. Suala la ndoa lina nafasi kubwa katika jamii kwani inaendeleza nguvu kazi inayotokana na watoto wanaozaliwa ambao wanatumika katika ujenzi wa taifa kwa sababu hujishughulisha na shughulu mbalimbali  za ujenzi wa taifa. Pia falsafa hii huunganisha jamii, vile vile inaleta heshima katika jamii. Kwa upande wa hasara ni pale inapotokea ndoa za kulazimishwa au umri mdogo, kwani kuna wazazi wanawazoesha watoto wao wakiwa bado wanafunzi.
Waafrika wanaamini katika nguvu hai, hili ni wazo jingine la Tempels kwani anasema kwamba waafrika wanaamini sana katika nguvu hai na wanaamini kwamba chanzo kikuu cha nguvu hai ni Mungu mwenyewe, nguvu hii hupitia kwa wahenga nao hupeleka kwa mizimu ambao hupeleka kwa binadamu na binadamu hupeleka kwa wanyama na mimea. Tempels anasema waafrika wanaamini nguvu ya waganga na hivyo mganga ana uwezo mkubwa wa kupunguza au wakuongeza nguvu hai kwa binadamu. Tempels anajiuliza maswali kadhaa kuhusiana na suala la waganga mfano, Dawa zawezaje kuponya?, Dawa inawezaje kuua mtu aliye mbali?, ni vipi mtu aliyekufa anaweza kuzaliwa upya?,na anasema kitendo cha kupungukiwa nguvu huitwa “Kufwa” na “Kufudwilika” katika ukurasa wa 22. Hivyo Tempels anasema kuwa majibu ya maswali yote matatu, ili uweze kujibu maswali hayo ni lazima uwe mshirika wa mambo hayo. Dhana hii inajitokeza katika riwaya ya  “Mirathi ya Hatari” mfano baada ya kufa Mzee Kazembe mke wake Nyamidze alikwenda kwa mganga kuthibitisha nini hasa chanzo cha kifo hicho uk.37. “Mwanangu leo asubuhi nilikwenda kwa mama Tamwene kuulizia kifo cha baba yako. Mganga anasema kuwa kifo chake kimetokea si kwa mapenzi ya Mungu ila kwa michezo ya binadamu wafaidio kuwaona watu wakifa” Mama Gusto alimwambia mwanawe Gusto. Pia Malipula alitaka ampeleke Gusto kwa Chikanga (Mganga) ili kubaini kama amehusika  na mauaji ya Kapedzile katika uk.60.
Jambo hili katika jamii ya sasa bado linaendelea, kwani Watanzania wengi huenda kwa waganga ili kukamilisha mambo yao, mfano kwenye masuala ya siasa, elimu, biashara, kilimo, mauaji ya albino, upigaji wa nondo, uchunaji wa ngozi yote haya yanahusishwa na waganga. Falsafa hii ina nafasi katika jamii kwani inaendeleza uhai pale mwanadamu anapojihangaisha na kutafuta tiba ya maradhi yake na hatimae anaweza kupona na kuendelea kuishi. Pia imani hii ya ya nguvu hai inaweza kupelekea migogoro katika jamii hasa waganga wa jadi wanaposhirikishwa katika kuongeza nguvu hata pamoja na kupiga ramli huzusha mgogoro katika jamii.
Dhana ya uduara, katika wazo hili Tempels anasema kuwa waafrika hupenda vitu vya umbo la uduara kwani wanaamini kuwa hivyo ndivyo vitu vizuri. Mfano katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” dhana hii inaonekana sehemu nyingi. Mfano, pale Gusto alipoingizwa kwenye pango na kukalishwa katika kigoda chenye umbo la duara katika ukurasa wa 33. Pia Gusto anapomsifia Dina kuwa ana uso wa mviringo katika ukurasa wa 30. Vile vile Mavengi anapoupitisha mgwisho wake na kuwazungushia Dina na Gusto katika umbo la duara uk.73. Hata meza ya Gusto ilikuwa ni ya mviringo.
Dhana hii inajitokeza katika jamii ya leo mfano nyumba za msonge katika kanda ya ziwa, Mikao ya kula huwa katika duara pia vyombo vingi huwa na umbo la duara kama sufuria ,Vyungu, Vinu, Nyungo za kupepetea na Ngoma. Falsafa ya uduara ina nafasi katika jamii kwani hudumisha na kuendeleza utamaduni wa mwafrika, kwani tangu zamani inaaminika kuwa kila kitu chenye uduara ni kizuri, pia kuna jamii nyingine zinazoendeleza kujenga nyumba za msonge. Hasara ya falsafa hii hushirikisha imani hii ya uduara kama ndiyo kitu pekee kizuri, kwani kuna vitu vingine ambavyo si duara na ni vizuri.
Kwa ujumla Placide Tempels ametoa mchango mkubwa sana juu ya falsafa ya kiafrika, ambaye anakubali kabisa kuwa waafrika wana falsafa yao. Mawazo yake yanapelekea kuibuka kwa wanafalsafa wengine wanaoizungumzia falsafa ya kiafrika kama vile Kwame Nkurumah, J. K. Nyerere, Kenneth Kaunda. Hivyo basi mawazo yake yana uhalisia pia yana umuhimu katika jamii ya kiafrika.
MAREJEO
Mung’ong’o C. G. (1977), Mirathi ya Hatari. Dar es salaam: Tanzania Publisha House.
Tempels, P, (1959),The Bantu Philosophy. Paris: Presence Africaine.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 2 Guest(s)