Nadharia ya Msambao (Diffusionism Theory) Iliongozwa na mawazo na ushawishi wa Grimms na Thompson
Ni nadharia iliyopingana na nadharia ya ubadilikaji taratibu tuliyoona hapo juu. Wana ubadilikaji taratibu waliamini kuwa;
Ikiwa ngano mbili kutoka katika jamii mbili tofauti zimeonyesha kufanana kwa namna fulani za kimuundo au kimaudui ni kwa sababu wanadamu ulimwenguni kote wanamkondo mmoja wa mawazo na kufikiri kwao ni kwa namna moja, na kwamba ngano hiyo inasawiri hatua sawa za maendeleo ya kiutamaduni katika jamii husika.
Tofauti na wanaubadilikaji, wanamsambao wangeamini kuwa; Pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea, sababu ya msingi ya kuwapo kwa mfanano huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani sana jamii hizo mbili ziliwahi kukutana kwa namna fulani, makutano baina ya jamii hizo yalisababisha hali ya kuazimana kwa baadhi ya mila na tamaduni (mawazo) mojawapo ya jamii husika. Watafiti hawa waliangalia mila na desturi za jamii zilivyokuwa zikikua na kusema kuwa zilikua kutokana na msukumo wa asili na lugha za Ulaya. Walikubaliana kwa sehemu kubwa kuwa asili ya mila, desturi na aina nyingine za utamaduni zinapatikana India, na walitaka kutafiti ni kwa kiasi gani utamaduni huu wa Indo-European ulikuwa umesambaa duniani.
Wana msambao nao walitumia mbinu ya ulinganishi kama walivyofanya wanaubadilikaji taratibu. Kazi ya utafiti ilihimizwa na wajerumani ambao ni Jacob na Wilhelm Grimm ambao walikusanya ngano nyingi kutoka India na kutoka katika nchi yao. Jacob na Wilhelm Grimm: Walitafiti ngano kutoka India na Afrika, na walihitimisha kwamba, kuna kufanana kwa ngano za India na Ulaya. Wakatoa maamuzi ya kwamba, hadithi za Kiafrika ni chimbuko kutoka kwa wazazi wenye asili na utamaduni wa India na Ulaya. Hivyo, dhana yao hiyo waliifikia kutokana na kuifanyia kazi dhana potofu, kwani kila bara lina utamaduni, mila na desturi zake. Aidha waliliona bara la Afrika kama bara ambalo halijastaarabika.
Stith Thompson: Yeye aliwaunga mkono akina Jacob na Wilhelm. Katika kitabu chake cha The Folktale (1946:438) anapendekeza kuwa panapotokea kufanana kati ya ngano/hadithi za Ulaya na za Afrika, zinaweza kuelezewa kuwa huenda hadithi/ngano hizo zililetwa na Wazungu wakati wa utumwa. Mawazo yao kwa ujumla ni kuwa;
Utamaduni
unaweza kusambaa tu kutoka katika jamii imara na maarufu tena yenye nguvu kuelekea kwenye utamaduni wa jamii iliyo kinyume chake “from superior to an inferior people)
Ikiwa kulikuwa na kufanana kwa namna yoyote katika ngano zilizopatikana Afrika na Ulaya kwa mfano, lazima moja kati ya jamii hizo ni dhaifu kuliko nyingine, na jamii dhaifu….Afrika, ilihali jamii imara… ulaya
Yote haya yangeweza kuelezwa tu kwa misingi ya ukweli kuwa jamii za Ulaya zilileta mambo hayo Afrika kutokea Ulaya kipindi cha biashara ya Watumwa (Thompson 1946:438)
Tafiti ziliendelea kufanyika baada ya Jacob, Grimm na Thompson ambapo bara la Afrika lilionekana kuwa bara lenye giza na hivyo kukaonekana haja ya kuanzisha dini ya Kikristo na teknolojia ya Ulaya barani Afrika ili Afrika iondokane na giza hilo.
Kwahiyo tunaweza kuona namna kila kitu cha Afrika ikiwemo fasihi simulizi yake vilivyodidimizwa na watawala hawa wa kikoloni.
Upungufu Tunaweza kusema kwamba, ingawa walijitahidi kuipa hadhi fasihi simulizi kwa kusisitiza upekee wa muktadha, hawakuchunguza kwa undani sifa za kisanaa za fasihi simulizi. Pia walijishughulisha na muhtasari tu wa simulizi walizochunguza, na hivyo ni dhahiri kwamba kuna vipengele vingine muhimu vya Fasihi Simulizi ya Kiafrika ambavyo havikutiliwa maanani..
Hitimisho
Bado tafiti za namna hii hapa Afrika zinaendelea lkn mkabala na malengo ni tofauti. Ule upendeleo uliokuwepo hapo zamani sasa umeondoka. Sasa wanajihusisha na kutafiti msambao wa ngano na vipengele (units) vyake ndani ya tamaduni mbalimbali, katika bara la Afrika. Kama vile asili ya ngano za Kiafrika zinazosimuliwa katika Marekani ya Kusini na Kaskazini.