SANAA ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu hulitumia kueleza hisi zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au vielelezo vyenye dhana maalum.
Kuna aina kuu tatu za sanaa. Kwanza ni sanaa ambazo uzuri wake hujitokeza katika umbo la kudumu, umbo ambalo linaweza kuhifadhiwa na uzuri wake kuonyeshwa wakati wowote. Hizi ni sanaa za uonyesho.
Nazo ni kama vile uchoraji, uchongaji, ufinyanzi na utarizi.
Sanaa za ghibu hazijitokezi kwenye umbo linaloonekana kwa macho au kushikika bali katika umbo linalogusa hisia. Mifano ni kama vile usairi, uimbaji, upigaji muziki n.k. Uzuri wa sanaa hizi umo katika kuzisikia.
Uzuri wa sanaa za vitendo umo katika umbo la vitendo, na ili kuupata uzuri huu yampasa mtu kutazama vitendo vikifanyika.
Umbo hili linalazimisha kuwepo kwa msanii na mtazamaji wa sanaa mahali pamoja kwa wakati mmoja ama sivyo sanaa haikamiliki.
Hali hii ndiyo iliyosababisha sanaa za vitendo kuitwa sanaa za maonyesho, kwa sababu lazima wakati zinapotendeka awepo mtu wa kuonyeshwa, maana uzuri wake umo katika vitendo vyenyewe.
Kwa hiyo sanaa za maonyesho ni kitendo chochote kinachohitimishwa na dhana inayotendeka, mtendaji, uwanja wa kutendea na watazamaji. Zipo nadharia tatu zinazoelezea chimbuko na asili ya sanaa za maonyesho.
MICHEZO YA KUIGIZA
Sanaa za maonyesho ni michezo ya kuigiza, ama ni michezo inayoonyeshwa kwenye jukwaa lenye pazia na taa nyingi za jadi. Huu ni mtazamo mmojawapo ambao unaaminiwa na baadhi ya wataalamu kwa kuwa unasisitiza kwamba sanaa za maonyesho lazima zichezwe jukwaani, kuwepo na pazia na taa nyingi.
Nadharia hii inatuaminisha kuwa sanaa za maonyesho ni tamthilia tu, jambo ambalo linaleta shaka kidogo.
Tamthilia ni utanzu ulioletwa na Wakoloni kwa hiyo, kuamini nadharia hii ni sawa na kusema kuwa hakuna sanaa za maonyesho zenye asili ya hapa Afrika Mashariki.
Ni sawa na kusema kuwa kabla ya ujio wa Wakoloni sisi tulikuwa hatuna sanaa zetu wenyewe. Wazo hili si kweli na ni potoshi. (Mhando & Balisidya 1976).
Mtazamo huu unatokana na fasili ya sanaa za maonyesho inayodai kuwa sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa za mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na watazamaji.
Dosari kubwa katika ufafanuzi huu imo katika neno mchezo (play). Neno hili lina maana duni likilinganishwa na hali na umuhimu wa sanaa za maonyesho zenye asili ya Kiafrika.
Tukichukua kwa mfano unyago, jando, kusalia mizimu au masimulizi ya hadithi, ambayo ni mifano ya sanaa za maonyesho zenye asili ya Kiafrika, tunakuta zile sifa zote zipo.
Isipokuwa tunajua kuwa shughuli zote hizi si mchezo na umuhimu wazo hauruhusu hata kidogo kuingiza neno mchezo. Shughuli hizi zina maana muhimu ambayo inahusu maisha ya binadamu katika jamii yake.
Ni shughuli zinazobeba wazo maalum lenye lengo la kujenga utu wa mwanajamii na kubainisha taratibu za maisha yake. Basi vipi tuseme shughuli hizi zina sifa ya mchezo?
Wazungu wanaridhika na neno hili kwa sababu sanaa za maonyesho za utamaduni wao aghalabu zinafanywa kwa masihara tu.
Sanaa za maonyesho zao zaidi ni kwa madhumuni ya kujiburudisha au pengine kutafuta kipato.
Lakini kila aina ya sanaa za maonyesho ya Kiafrika ina dhana fulani ndani yake, kwa mfano kuhusu maana ya maisha, utekelezaji wa madaraka ya kiutu uzima, ushujaa, maadili au mafunzo ya historia ya jamii.
Kwa hiyo basi sanaa za maonyesho za Kiafrika ni dhana zilizo kwenye umbo linalotendeka na katu si mchezo. Kutokana na utamaduni wa Kiafrika, tunaweza kusema kuwa sanaa za maonyesho ni dhana inayotendeka.
Na ili dhana hii itendeke anahitajika mtu wa kuitenda. Mtendaji huyu huhutaji uwanja wa kutendea hiyo dhana na wakati akiitenda wanakuwapo watazamaji.
VICHEKESHO
Wakati Mkoloni alituletea sanaa ya maonyesho ya kikwao, sisi tulishiriki katika tamthilia za Shakespeare kama washiriki au watazamaji tu.
Tamthilia hizi hazikuwa na maana yoyote kwetu kutokana na kuwa zilibeba na ziliongelea utamaduni wa Kizungu. Tulifurahishwa na vile vitendo vilivyofanywa kwenye jukwaa katika tamthilia hizi na hivyo vitendo hivi vilituchekesha tu.
Basi jambo kubwa kwa Mwafrika ikawa ni vile vichekesho na hivyo kudhani kuwa jambo muhimu katika tamthilia ni kule kuchekesha kwake.
MAIGIZO
Wazo hili limetokana na tafsiri mbovu ya neno “play” ambalo lina maana ya mchezo wa kuigiza. Inawezekana aliyetafsiri neno hili alifuata nadharia za zamani sana za drama, ambapo ilidhaniwa kuwa uigizaji (imitation) ndio kiini cha drama.
Hata hivyo nadharia hii ilitupiliwa mbali kwa vile haikudhihirisha kiini hasa cha drama. Wengi wamepotoshwa na wazo kuwa uigizaji ndio kiini cha sanaa za maonyesho kama vile neno michezo ya kuigiza linavyoonyesha.
Hivyo, hata katika kutazama sanaa za maonyesho za asili wengi wamekuwa wakitazama iwapo kuna uigizaji.
Na hapa wengi wanakwama kwani katika unyago, jando, kusalia miungu n.k hakuna uigizaji bali wanaoshiriki wanashika nafasi fulani fulani. Hivyo ni bora kutumia neno tamthilia pale tunaporejelea “play.”
Ingawa zote ni sanaa za maonyesho, zina misingi tofauti kutokana na tofauti za utamaduni wa jamii husika.