06-26-2021, 05:41 PM
Je Wairaqw ni Wambulu? Fahamu Historia yao na asili ya jina Mbulu…
Kaka samahani je wewe ndiye coordinator wa Ohayoda blog? Kama ndivyo hebu tafadhali ufanye utafiti wa kabila la kiirak *IRAQW* na je hili jina la Wambulu origin yake ni wapi? Je hawa kama c Wabantu wametokea wapi? Maana naona kuna upotoshaji mwingi na tafiti za watu mbalimbali. I w’ll appreciate that kaka.
Baada ya kupata maombi mbalimbali ya wadau wa Ohayoda hasa ndugu Joachim John ambaye alinitumia ujumbe huo hapo juu kupitia mtandao wa kijamii wa facebook, nimeona ni vyema tukaliweka jambo hili sawa hasa kwa jamii ya nje ambayo pia haijui kama kuna kuna tofauti kati ya Wairaqw (wairak) na wambulu.
Wairaqw ni moja ya makabila matatu tu Tanzania ambalo ni jamii ya Wakushi au Wahamitiki wenye asili yao kwenye nchi za Ethiopia tofauti na wengi wanavyoamini kuwa asili yao ni mesopotamia yaani Iraq ya sasa(mengine ni Wambugu waliopo Tanga na Wagorowa au wafyomi waliopo Babati). Utafiti wa kiathropolojia na hata vinasaba (DNA) uliofanyika unathibitisha kuna uhusiano mkubwa kati ya Wairaqw na hao wakushi wa Ethipia na Eritrea, kuanzia muundo na matamshi ya lugha, miili (body structure), mavazi na hata shughuli za kila siku ikiwemo hata michezo kwani Wairaqw kama walivyo waethipia wanasifika kwa riadha na wamefanana katika kila hali
Kutokana na sababu ambazo hazifahamiki japo inaaminika kuwa ni kwa sababu ya vita au njaa ya mara kwa mara inayoikumba eneo hilo la pembe ya Afrika, kundi moja la watu lilihama kuelekea kusini kufuata bonde la ufa kwa miaka mingi sana. Walipofika kaskazini kwa Tanzania ya sasa, wakagawanyika makundi mawili ambapo kundi moja dogo lilielekea mashariki na kundi lingine likaendelea na safari yao wakifuata bonde la ufa kuelekea kusini. Kundi hilo dogo lilifika mpaka milima ya usambara Tanga na kukaa huko mpaka leo ambao ndio wanaofahamika kama Wambugu.
Inasemekana kundi kubwa liliendelea kusonga mpaka kusini mwa Tanzania hadi Iringa wakaishi huko kwa miongo mingi sana kabla ya kuamua kurudi kaskazini baada ya kuona eneo hilo haliwatoshi baada ya kustawi sana hapo. Katika thesis yake ya PHD, Dr. Jackson Makwetta ambaye ni Mhehe aliandika kuwa jina la wahehe limetokana na kabila moja dogo ambalo liliishi zamani karibu na wahehe ambalo kwa sasa lipo wilayani Mbulu mkoani Arusha (sasa Manyara) ambalo wao kila wakimwona mtu asiye wa kabila lao walimwita Hee! Hee!
Lakini pia, masimulizi ya wazee wa kiiraqw yanaanzia kwenye sehemu inayoitwa Gusir Ma/angwatay, nchi inayoelezwa kuwa ni ya baridi sana iliyopo kusini, ambapo hawakumbuki wala hakuna masimulizi yanayoeleza kabla ya kufika hapo walitoka wapi lakini wanajua baada ya kuondoka hapo wakafika sehemu inayoitwa Gusir Tiwalay yaani sehemu tuliyopigwa. Hapa ndipo historia ya Wairaqw ilipoandikwa upya na kuchukua sura nyingine kabisa, eneo hili inasemekana ni kati ya Babati, Hanang na Kondoa.
Wakiwa hapa, wairaqw walistawi sana wakiwa na ng`ombe na mazao ya kutosha, wakashamiri katika michezo na mafunzo ya kivita lakini hawakuwa na watu wa kupigana nao. Masimulizi yanaeleza kuwa katika kipindi hiki mchezo wa kupigana kwa fimbo yaani Ilgendi ulishamiri sana ambako kulikuwa na hadi mashindano ya kutafuta bingwa wa mchezo huo. Vijana wakajawa na kiburi na kuona wao ni wao, wakamshinikiza kiongozi wao aliyeitwa Haymu Tippe awaletee watu wa kucheza nao (kupigana nao) na kumteka mtoto pekee wa Haymu na kumtishia kuwa kama hatawaleta watu wa kupigana nao watamuua huyo mtoto. Japo Haymu Tippe aliwaasa hasa baada ya ramli yake kuonesha madhara makubwa yatakayotokana na vita hivyo lakini vijana hao waliushikilia msimamo wao, walidai vita.
Haymu akaenda akawafuata wadatoga lakini kabla hawajafika, Haymu alitoroka na baadhi tu ya watu wa ukoo wake (Tippe) na ukoo wa Duwe na Naman (wengine wanadai ni Masaay) ambao ndio waliomsikiliza. Waliobaki nyuma na kusubiri vita walimalizwa wote na hakubaki hata mtu moja. Katika kukimbia huko, Haymu alikuwa na mpwa wake (mtoto wa dada yake) aliyeitwa Gortoo ambapo katika kukimbia kuelekea ukingo wa bonde la ufa kwa kaskazini waligawanyika huku Gortoo akiwangoza kundi dogo kuelekea mlima Kwaraa uliopo Babati na Haymu Tippe na kundi lingine wakielekea mlima Hanang (/Anang) lakini wakaamua kukimbilia kwenye kingo za bonde la ufa eneo la Madunga na kisha kufuata kingo hizo kuelekea Kaskazini Mashariki hadi milima ya Tlahhara na Nou hadi Irqwar Daaw sehemu inayoitwa Mama Isara.
Gortoo na kundi lake wakakaa huko Kwaraa na maeneo ya Babati na ndio wakawa kabila la Gorowa au Wafyomi ambao kwa sehemu kubwa wamefanana na wairaqw isipokuwa baadhi ya matamshi ya maneno kutokana labda na mabadiliko ya mazingira lakini wanasikilizana.
Wairaqw waliishi hapo Mama Isara kwa miaka mingi sana na kuanza kuongezeka kutoka hizo koo tatu tu, wakaanza kupokea watu kutoka koo mbalimbali (assimilation) na kuunda koo mpya, mfano ukoo wa Bayo uliundwa na Wanyiramba waliofikia kwa mtu anayeitwa Bayo na kisha kuitwa Manda do Bayo! Aidha ukoo mkubwa kuliko wote wa Wairaqw ambao ni Sulle asili yao ni Wadatoga na utafiti unaonesha kuwa wadatoga wote wanaopakana na Wairaqw wanazungumza Kiiraqw na zaidi ya nusu ya hao wadatoga wanajitmbulisha kama Wairaqw tena wengi wa hao wazazi wote wawili wakiwa wadatoga.
Baada ya kukaa Mama Isara kwa miaka mingi na baada ya sera ya serikali ya kikoloni ya Kiingereza kuamua kufyeka maeneo kuondokana na mbung`o waliokuwa wanasababisha tauni, Wairaqw walianza kutoka huko milimani na kujaza maeneo ya Karatu, Mbulu, Babati, Hanang na kusonga magharibi hadi Haydom kote huku wakisonga nyuma ya Wadatoga ambao huhamahama kutafuta malisho na ndio maana majina karibu yote ya huku yanaasili ya Kidatoga.
Je Wairaqw ni Wambulu? Fahamu Historia yao na asili ya jina Mbulu…sehemu ya Pili Kaka samahani je wewe ndiye coordinator wa Ohayoda blog? Kama ndivyo hebu tafadhali ufanye utafiti wa kabila la kiirak *IRAQW* na je hili jina la Wambulu origin yake ni wapi? Je hawa kama c Wabantu wametokea wapi? Maana naona kuna upotoshaji mwingi na tafiti za watu mbalimbali. I w’ll appreciate that kaka-Joachim John Je jina Wambulu lilianza wapi? Kutokana na eneo lote walilokuwa wanaishi la Mbulu, Karatu, Babati na Hanang kuwa katika wilaya moja wakati huo yaani wilaya ya Mbulu ndipo wakawa wanaitwa Wambulu kwa kuwa wanatoka katika wailaya ya Mbulu na wote wanapatikana katika wilaya hiyo tu! Lakini kwa kuwa wilaya hizo zimegawanyika sasa hivi kuwaita wambulu haina mantiki na pia kuna makabila mengine yaliyopo Mbulu pia Lakini Je, nini maana ya Jina Mbulu? Hakuna jibu sahihi ya jina Mbulu asili yake na kuna majibu mengi, Ohayoda itayachambua yote ili kukupa mwanga na ukweli halisi Twende kazi…. Kanisa katoliki Mbulu 1. German: Neu-Trier Mbulu ni neno la Kijerumani (Neu-Trier) lenye maana ya Majaribio mapya (new trial). Wajerumani walifika Mbulu katika karne ya 19 na kuweka ngome yao (boma) hapo ambapo inasemekana kuwa Mbulu ilianzishwa siku moja na Nairobi. Kutokana na hali ya hewa ya mahali hapo kuwa nzuri na kuzungukwa na milima pande zote, wajerumani walipapenda mahali hapo kwa sababu ya kiulinzi pia japo hali ya hewa nzuri ndiyo iliyowavutia zaidi. Hivyo basi wakaweka mpango wa majaribio wa kupafanya Mbulu kuwa kama Berlin hasa ukizingatia utawala wa kijerumani ulikuwa wa moja kwa moja (direct rule) na waliweka makazi ya kudumu na walichukulia makoloni yao kama sehemu ya Ujerumani, ndiyo maana hata miundombinu waliyoyaweka ni ya muda mrefu! Japo hili laweza kuwa sahihi lakini hakuna ushahidi wowote kuwa Mbulu ni neno la kijerumani 2. Imboru Inadaiwa kuwa jina Mbulu linatokana na neno Imboru ambalo Wairaqw hulitumia wanapopataja Mbulu. Inasemekana kuwa “waswahili na wakoloni“ walilitohoa jina Imboru na kutokana na matatizo ya “r“ na L jina hilo lilibadilika hadi kuwa Mbulu na Wajerumani kushindwa kutamka Imboru. Lakini utafiti mdogo wa matamshi unaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa neo Imboru kugeuzwa kutoka Mbulu na kufanywa lionekane la Kiiraqw zaidi yaani Imboru. Mfano mzuri ni kuwa Wairaqw lazima wongeze irabu (aeiou) katika maneno yanayoanzia na M au N kisha kufuatiwa na konsonati. Mfano neno “Ngano“ wairaqw hutamka “angano“ na “mjomba“ hutamkwa “majomba“, “ngamia“ hutamkwa “angamia“ n.k Pia majina ya maeneo mengi sana yamebadilishwa baada ya “kuIraqwishwa“ mfano Haydom kutoka “Heidom“, Garoch kutoka “Garawja“ n.k Lakini kwa upande mwingine, inasemekana neno Imboru linatokana na Imbori, moja ya majina ya Kiiraqw lakini huyu Imbori alikwa nani mpaka mahali hapo paitwe kwa jina lake? Tutaiangazia katika makala nyingine lakini hii inatupa uhalisia zaidi kuwa Imbori inatupeleka karibu zaidi na ukweli kuwa Mbulu limetokna na neno Imbori. Inasemekana Imbori alikuwa binti aliyepata mimba kabla hajaolewa (doroway) ambapo alifukuzwa kwao na kuozwa kwa “Homo“ na kisha kwenda kuishi naye huko mbulu wakati huo bado wairaqw wanaishi Irqwar Daaw hawajafika Mbulu. Baada ya kuolewa ndugu zake walikuwa wakimtembelea wakisema “Aya Imborir kawaan“ na hadi hapo baadaye pakabaki hivyo. 3. Mbulu-Mtu anayeongea lugha isiyoeleweka Kamusi ya kiwahili sanifu (sijainukuu rasmi) inaelezea neno Mbulu kama mtu anayeongea lugha isiyoeleweka.Kutokana na Kiiraqw kuwa tofauti kabisa na lugha za kibantu, kuna wanaoamini kuwa Mbulu imetokana na “waswahili“ kuwaita Wairaqw kwa kuwa wanaongea lugha isiyoeleweka kwao. hata na hivyo hija hii inakosa mshiko kutokana na ukweli kuwa kuna makabila mengine yasiyo ya kibantu na wanaongea lugha isiyoeleweka na pia ni ukweli usiofichika kuwa hakukuwa na mwingiliano (interaction) baina ya wairaqw na jamii za kibantu kabla ya wajerumani kwani wamekuwa na uhusiano au mwingiliano na Wadatoga zaidi na kwa upande wa mashariki wamepakana na wamasai ambao si wabantu na wanyiramba kwa magharibi. Hoja hii inakosa mshiko kwani kwa jinsi kiswahili kinavyokua kimekuwa kikiingiza maneno mapya kwa kutohoa zaidi kuliko kuyaunda, hivyo kuweka uwezekano mkubwa sana kwa Kiswahili kulikuta neno Mbulu tayari likiwa linatumika na tayari wairaqw wakiwa wanaitwa Wambulu na hivyo kulipa maana ya mtu anayeongea lugha isiyoeleweka. Huo ni uchambuzi wangu kuhusu asili ya neno Mbulu…kama kuna mtu anamaana tofauti na hizi nilizoeleza anakaribishwa kuujulisha umma au wadau na kisha kwa pamoja tujadili kupata jibu sahihi zaidi.
Mwl Maeda