Dhana ya nadharia imejadiliwa na wanazuoni mbalimbali ambao wamekuja na mitazamo tofauti tofauti kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa Wamitila, (2003:22) “nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani : chanzo chake, muundo wake, utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje”
TUKI (2004:300) wanasema “nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani”
Fasili hii ya TUKI inafanana kwa kiasi fulani na fasili ya Mdee (2011) anayefasili nadharia kuwa ni mpango wa maneno uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo fulani. http://kapeleh.blogspot.com/2014/05/nadh...maana.html
Kwa msingi huo nadharia hubeba mawazo, dhana au maelezo yatolewayo kwa nia au lengo la kueleza hali fulani, chanzo, muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje.
Kuna nadharia mbalimbali ambazo zimejadiliwa na wanazuoni mbalimbali, baadhi ya nadharia hizo ni pamoja na nadharia ya maana, nadharia za kifalsafa, kihistoria, nadharia ya fasihi, nadharia za chimbuko la lugha ya Kiswahili, nadharia ya chimbuko na chanzo cha lugha.
Naye Wafula na Njogu (2007:7) wamefasili dhana ya nadharia kama ni jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu. Fasili hii imeegemea hasa katika nadharia ya uhakiki wa fasihi. Pia imetaja vitu muhimu kama vile, maelekezo ambayo ndiyo yanamuongoza msomaji au mhakiki ili asivuke mipaka ya mawazo ya hiyo nadharia aitumiayo ili kufanikisha kazi kwa ufasaha.
Pia Sengo (2009:1) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani. Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira au mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.
Ili kuweza kuthibitisha maelezo yaliyotolewa na wataalamu mbalimbali kuhusu dhana ya nadharia ni vyema kuangalia mfano mmojawapo wa nadharia, ambayo ni nadharia ya sarufi. Katika nadharia hii kuna wanaisimu mbalimbali wamejitokeza kuelezea nadharia ya sarufi kwa mitazamo tofauti tofauti ambayo imeweza kuibua nadharia mbalimbali za sarufi kama vile nadharia ya sarufi mapokeo, nadharia ya sarufi msonge na nadharia ya miundo virai.
Katika nadharia ya sarufi mapokeo Mgullu (1999:68) anasema ni sarufi ya kale iliyochambuliwa kwa kutumia vigezo vya lugha za Kilatini na Kigiriki zilizokuwa na mnasaba mmoja, yaani zilikuwa na asili moja. Kwa mantiki hiyo lugha za Kilatini na Kigiriki zilikuwa kama kiolezi cha kuchanganulia lugha nyingine ikiwemo lugha ya Kiswahili. Kwa mfano wanaisimu wa Kilatini waliposema kuna aina nane za maneno na baadhi yao katika lugha ya Kiswahili wakasema kuna aina nane za maneno bila kuzingatia kwamba lugha hutofautiana. Pia nadharia hii ilijikita na sentensi sahili, haikujishughulisha na miundo kwa marefu na mapana.
Baada ya kuonekana sarufi mapokeo ina udhaifu mkubwa iliibuka nadharia ya sarufi msonge. Mgullu (1999:70) anaiona sarufi hii ni sehemu ya mkabala wa kimapokeo isipokuwa mkabala huu unaiona lugha kuwa ni mfumo mkuu yenye mifumo mingi ndani yake kama vile mifumo midogo ya fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki.
Katika karne ya kumi na nane na kumi na tisa sarufi mapokeo ikafikia kilele ndipo ikaibuka nadharia ya sarufi miundo virai. Nadharia hii inadokeza kuwa tungo imeundwa na viambajengo ambavyo vina uhusiano na vipo kidarajia. Kwa mujibu wa Mgullu (1999:70) isimu muundo imejitokeza sana katika maandishi ya akina Harris, Ferdinand De Saussure, Trubetzkoy na Bloomfield.
Katika mkabala huu lugha ilionekana kuwa na viambajengo kama vile: maneno, kirai, kishazi na sentensi na kwamba viambajengo hivyo vina uhusiano mkubwa na viko katika kidarajia toka chini hadi juu. Kwa mfano
Mkulima bora analima vizuri
Katika sentensi hii kuna uhusiano wa karibu wa viambajengo vifuatavyo; N+V yaani nomino “mkulima” na kivumishi “bora”, hali kadhalika, T+E, yaani kitenzi “analima” na kielezi “vizuri”.
Katika mkabala huu dhana ya uchamko ikaibuka kuonyesha uwezekano wa kuzalisha sentensi bila kufika kikomo. Kwa mfano,
Waziri fisadi amekamatwa jana na rais akiiba fedha za wananchi.
Hivyo ili kuwa na nadharia inayokubalika katika jamii ni muhimu kuzingatia fasili ya Sengo, (2009:1) ambaye anasema kuwa “nadharia ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani”.
Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira au mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.
Kwa ujumla nadharia huchukuliwa kuwa ni dira ya kumwongoza mtafiti au mchambuzi kulikabili na kulielezea vyema jambo fulani kwa mtazamo unaotazamiwa kuwa imara zaidi kuliko ule wa nadharia nyingine. Nadharia hutoa mwongozo katika utatuzi wa jambo fulani ambalo halijaweza kuhakikishwa ukweli wake. Ni mawazo , maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kutatua au kutekeleza jambo fulani kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.