04-11-2022, 10:41 PM
HISTORIA YA UKUTA KWA UFUPI (USANIFU WA KISWAHILI NA USHAIRI TANZANIA) MALENGO YAKE NA UMUHIMU WAKE
Makala
HISTORIA KWA UFUPI YA UKUTA (USANIFU WA KISWAHILI NA USHAIRI TANZANIA) MALENGO YAKE NA UMUHIMU WAKE
Mada iliyowasilishwa na Ndugu Abdallah Ahmad Seif (Ngome Imara) katika kongamano la CHAWAKAMA lililofanyika Tarehe 30/8/2012 – 01/09/2012
Ngozi, Burundi
Chama au chombo cha UKUTA (Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania), kiliasisiwa Tarehe 29/3/1959 Mjini Dar es salaam na wapenzi wa Lugha ya Kiswahili pamoja na Ushairi, Mwenyekiti wa chama Taifa akiwa marehemu Mahamoud Hamdouny (Jitukali), aliyekuwa mshairi maarufu katika ukanda huu wa Afrika ya mashariki na pia mjuzi mkubwa aliyebobea wa lugha ya Kiswahili ambaye maskani yake yalikuwa mjini Dodoma.
Watu wengine maarufu ambao walikuwa ni waasisi wa chombo hichi UKUTA, ni akina Mzee Mathias Mnyampala, Shaaban Robert, Sheikh Kaluta Amri Abeid, Mzee Akilimali (Snow white), Mzee Mwinyikhatibu Mohammed, Mzee Said Shomari Kaniki na wengineo wengi.
Mara baada ya Tanzania (Tanganyika) kupata Uhuru, UKUTA ulipata nguvu zaidi baada ya kuongezeka wadau wengi wapenzi wa Lugha ya Kiswahili, akiwemo Rais wa kwanza wa Tanzania marehemu Mwl. Julius Kambarage Nyerere, ambae alikuwa mdau mkubwa wa Lugha ya Kiswahili na pia Mshairi alieumudu vema Ushairi.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati huo ndiye aliyekuwa mlezi wa chama cha UKUTA, na kwa nafasi yake alitoa chumba kimoja katika jengo la Anatouglo Dar es salaam ili kitumike kama ofisi kuu ya UKUTA. Ofisi hiyo ipo mpaka leo na inaendelea kutumika kwa kazi mbalimbali za kiofisi za UKUTA.
UKUTA ilifungua matawi Mikoani, na hivyo kuwa chombo kilichokuwa karibu na wananchi, na hivyo hamasa ya watu kukienzi Kiswahili ikawa iko juu kutokana na mipango madhubuti iliyokuwepo wakati huo.
MALENGO YA UKUTA
Malengo ya UKUTA ni kama yalivyoainishwa katika katiba yake ambayo ni pamoja na:-
i) Kulinda, kuhifadhi na kustawisha Lugha ya Kiswahili, Ushairi na Utamaduni wake.
ii) Kufanya kazi zitakazostawisha Ushairi kuwa sehemu ya mitaalaa ya Kiswahili nchini na nje ya nchi na kukuza Kiswahili kwa kuzingatia Lugha za kibantu.
iii) Kuhamasisha na kuamsha ari na kuwasaidia watu wanaotaka kuwa mafundi wa lugha ya Kiswahili katika taasisi za elimu na jamii kwa ujumla.
iv) Kuhamasisha na kuamsha ari za wale wanaotaka kutunga vitabu vya fani mbalimbali za elimu kwa lugha ya Kiswahili na vya Ushairi na kutafuta njia za kuchapisha kazi zao.
v) Kutunza, kulinda na kutangaza kazi za Kiswahili zilizotungwa na watunzi waliokwisha kutangulia mbele ya haki.
vi) Kusisimamia matumizi sahihi na sanifu ya Lugha ya Kiswahili na kukosoa na kuelekeza pale Lugha ya Kiswahili inapokosewa ili matumizi sahihi ya Kiswahili yabaki katika unyoofu wake.
vii) Kufasiri matangazo, maandishi, vitabu, filamu, kazi za sanaa kutoka Lugha za kigeni, Asili kwenda Lugha ya Kiswahili.
viii) Kutoa huduma ya ufasiri na ukalimani katika mikutano ya Kitaifa na kimataifa.
ix) Kushirikiana na taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi yetu katika kukiendeleza Kiswahili.
UMUHIMU WA UKUTA
UKUTA ni chombo muhimu kutokana na malengo kiliyonayo katika uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili na sanaa ya Ushairi.
Hivyo ni muhimu kwa wadau wa Kiswahili kujiunga na chombo hichi, kuanzia wanafunzi wanavyuo, na watu wengine wa kada mbalimbali.
Kwani mnapokuwa katika chombo kilichosajiliwa na kutambulika na chenye historia adhimu katika Tasnia ya Kiswahili, inakuwa ni rahisi kuunganisha nguvu zenu kupitia chombo hicho na kuweza kuyafikia malengo yenu.
Kwa kuzingatia changamoto nyingi zinazowakwaza wadau wa Lugha ya Kiswahili kutokana na kukosa msukumo kutoka Serikalini, ni vyema wadau wa Kiswahili wakiunganisha nguvu kupitia katika chombo, wanaweza kuyafikia malengo yao, tofauti na mtu ukiwa mmoja mmoja, siyo rahisi kusikika na kutekelezewa jambo lako hata kama hicho unachokidai kina mantiki ndani yake.
CHANGAMOTO ZILIZOIKUTA UKUTA
Changamoto zilizoikuta UKUTA na kusababisha kulegalega, kwa sehemu kubwa zilichangiwa na viongozi wenye mamlaka katika utawala wa nchi kutokipa uzito Kiswahili katika umuhimu wake, na hivyo kusababisha hata zile taasisi zilizokuwa zinasimamia malengo ya kukiendeleza Kiswahili zipoteze mwelekeo.
Taasisi hizo kama UKUTA zilizokuwa na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya Lugha ya Kiswahili, zilishindwa kujiendeleza kwa ufanisi kwa sababu ya kukosa nyenzo muhimu, ikiwa ni pamoja na fedha.
Serikali iliyopaswa kuzisaidia taasisi hizi kwa maendeleo ya lugha adhimu ya Kiswahili, haikuchukua wajibu wake huo muimu, na hivyo kuziacha taasisi hizi katika hali ngumu, zikikabiliwa na ukata, na hivyo kukwamisha malengo ambayo taasisi hizi zilikuwa zimejiwekea.
Lakini kwa kuwa UKUTA ni taasisi yenye malengo mazuri kwa mustakabali endelevu wa lugha ya Kiswahili, WANAUKUTA waliendelea na juhudi zao. Pamoja na kukosa uungwaji mkono kutoka katika mamlaka za utawala, juhudi za kukiendeleza Kiswahili pamoja na sanaa ya utunzi wa Mashairi ziliendelezwa hadi kufanikisha kuchapisha vitabu kadhaa vya mashairi na hata vitabu vingine vya Kiswahili vyenye maudhui mbalimbali yenye kuifaidisha jamii.
Mfano wa vitabu hivyo ni, DIWANI YA MLOKA ambayo kwa miaka mingi kuanzia 1998 hadi mwaka 2008 ilitumika kufundishia shuleni. Pia kuna vitabu kama ADHA YA UKIMWI, ELIMU YA JAMII NA CHEMSHA BONGO na vingine vilivyotungwa kwa Lugha ya Kiingereza vyenye maarifa ya kutosha, vilivotungwa na MWANAUKUTA ambaye ni Katibu wa UKUTA tawi la Dodoma, ndugu Charles Mloka.
Vingine ni BAHARI YA HEKIMA YA USHAIRI kilichotungwa na Mshairi maarufu nguli, Amiri Sudi Andanenga.
Kwa kuwa juhudi za kuliendeleza jambo lolote, huwa zipo kwa wahusika wenyewe wenye jambo lao hilo. Wadau wa Kiswahili Dodoma tuliamua mwaka 2000, kukutana na kulihuisha tena wa tawi la UKUTA kwa malengo ya kuendeleza Lugha yetu ya Kiswahili na sanaa ya utunzi wa Mashairi baada ya tawi hili lililoanzishwa mwaka 1960 kusuasua hasa mwishoni mwa mwaka 1990.
Hivyo Januari mosi mwaka 2000, tawi la UKUTA Dodoma llilifanya uchaguzi na kupata viongozi wapya kama ifuatavyo:-
Mwenyekiti - Mariam Ponda
Makamu/M/Kiti - Ramadhani Nyembe
Katibu - Charles Mloka
Katibu Mwenezi - Abdallah Hancha
Mwenezi Msaidizi - Abdallah Seif
Mweka Hazina - Saleh Seif
Mohammed Kajembe - Mjumbe
Halidi Jumanne - Mjumbe
Mohamed Kiwipa - Mjumbe
Ayoub Seif - Mjumbe
Zainabu Issa - Mjumbe
Said Yasini - Mjumbe
Hamisi Biliyetega - Mjumbe
Justina Mwaja - Mjumbe
Mussa Kazimiri - Mjumbe
Juma Kidogo - Mjumbe
Said Kaniki - Mlezi
Kwa sasa angalau, kuna mwangaza unaojitokeza wa Lugha hii ya Kiswahili na hata Sanaa ya Ushairi kupata msukumo kutoka kwa viongozi wenye mamlaka ya utawala. Kwani kongamano la UKUTA lililofanyika Mjini BUKOBA, Mkoani KAGERA, Tarehe 31 Machi hadi Tarehe 01 Aprili mwaka 2012, mkuu wa Mkoa huo Mheshimiwa FABIAN MASSAWE alibeba jukumu la kuufadhili mkutano huo kwa juhudi zake, na hivyo kuonesha angalau sasa viongozi wameanza kutambua umuhimu wa uwepo wa taasisi za uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili na kuelewa kwamba zinahitaji kuwezeshwa na kuungwa mkono ili kufikia lengo la Kiswahili kufahamika vyema kwa wadau kitaifa na kimataifa ili kiwe hazina kwa maendeleo endelevu.
UKUTA Dodoma imejipanga kutumia fursa zitazojitokeza za uungwaji mkono kwa umakini na ufanisi. Tayari tuna mipango ya kutoa vitabu vya mashairi na vitabu vingine vya Kiswahili vyenye maarifa na maelimisho kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM) na St. John, na tayari maandalizi ya kazi hizo yameshaanza kufanywa.
Hivyo tunawakaribisha wote walio tayari katika kuliendeleza jahazi letu la Kiswahili, kuungana nasi ili kufanikisha malengo yetu ya kukifanya Kiswahili kuwa kweli ni hazina ya Afrika kwa maendeleo endelevu.
SANAA YA USHAIRI
Sanaa ya Ushairi ni katika tanzu za fasihi za Lugha ya Kiswahili. Ushairi ni Sanaa yenye historia ndefu na inaenda sanjari na historia ya Lugha ya Kiswahili.
Ushairi umeanza chungu ya miaka, kwa ushahidi wa tungo za mashairi za Bwana Muyaka bin Haji.
Kwamba Ushairi umeanza miaka mingi kabla ya wageni kuja katika janibu yetu ya Afrika Mashariki. Hivyo basi Ushairi umeanza kuwepo kabla wageni kutuijia kwenye pande zetu hizi na hivyo kuwa ushahidi tosha, kuwa ushairi asili yake inaenda bega kwa bega na Lugha ya Kiswahili ambayo asili yake ni Kibantu. Hivyo Sanaa ya ushairi tunapaswa kujivunia nayo kwani inatokana na sisi wenyewe. Ushairi kwa miaka mingi umetumika katika kuielimisha jamii kwa maswala mbalimbali pia kuiburudisha.
Katika Tanzania, washairi waliandika mashairi mbalimbali katika kuhamasisha kudai uhuru wa Tanganyika na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika harakati hizo. Hata baada ya Uhuru mashairi yalitumika katika kuwajenga watu kuwa na uzalendo na nchi yao, na kuhamasisha watu kufanya kazi kwa bidii ili taifa liweze kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.
Itoshe kusema, ushairi una faida kubwa katika jamii, kwani unaonya, unaelimisha, unahamasisha mambo mazuri na pia kuburudisha. Hivyo ni muhimu watu kujifunza Ushairi ili waweze kutunga mashairi na pia kuyasoma na kusikiliza, kutokana na faida lukuki zilizosheheni katika sanaa hii ambayo huwa imepangwa katika mpango unaovutia na kusisimua.
Ni vizuri sanaa hii ikarithishwa na kuendelezwa vizazi hadi vizazi kwa kuwafundisha watu waijue na waipende kutokana na umuhimu na uadhimu ilionao, ukizingatia ina mchango mkubwa katika uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili.
Shairi hupangwa kwa urari wa mizani na vina, huku maudhui yaliyotawala katika shairi yakiwa na mvuto na msisimko mkubwa kutokana na mpangilio wa maneno yenye kufanana katika miishilio yake. Ama hakika Sanaa hii ya Ushairi tunapaswa KUIDUMISHA.
Nimalizie kwa kusoma shairi hili nililolitunga ili kumpongeza na kumuusia mshairi mwezetu ndg Mohamed Mkagile Mandai baada ya kufunga ndoa “MAISHA YA NDOA YA MKAGILE” lililotoka katika gazeti la Uhuru Februari mwaka 1993 kama mfano wa shairi zuri la kuvutia na lenye kudhihirisha uzuri na uadhimu wa Sanaa ya Ushairi.
MAISHA YA NDOA YA MKAGILE
1. Mkagile wa mandai, umeshaoa kijana,
Usia ninatumai, huu nitaounena,
Najua huukatai, nawaombea rabana,
Maisha yawe mwanana, Mkagile wa Mandai.
2. Ndoa natoa madai, ni safari ndefu sana,
Epukeni ulaghai, dunia ulojazana,
Mpende wako nisai, nae akupende bwana,
Hili jambo la maana, Mkagile wa Mandai.
3. Tamaa ni haifai, hiyo ni kuepukana,
Ridhini Siwahadai, kitakacho patikana,
Mwenda pole hajikwai, faraja huja kufana,
Tamaa heri haina, Mkagile wa Mandai.
4. Dhana kamwe haizai, jambo lenye muamana,
Muwe hilo hamtwai, la mambo kudhaniana,
Penye dhana hapang’ai, ushwari huwa hamna,
Mzingatie kwa kina, Mkagile wa Mandai.
5. Dhana kama hamwambai, nayo mkiambatana,
Welewano haukai, kutadumu kuzozana,
Itazuka jitimai, msisikizane tena,
Hatima mtaachana, Mkagile wa Mandai.
6. Maisha nawapa rai, muishi kwa kupatana,
Kama maji na karai, kama nywele na kitana,
Ni kama suti na tai, daima mkirandana,
Mambo mkiridhiana, Mkagile wa Mandai.
7. Kamwe msijikinai, mdumu kuelewana,
Furaha haisinyai, mkiwa mmeshibana,
Faraka haiwavai, kama mkishikamana,
Katika zote namna, Mkagile wa Mandai.
8. Nasi panapo uhai, tutakuja kuwaona,
Mje tukirimu chai, na vitu vya kutafuna,
Mikate jamu mayai, na vingi vyenye kunona,
Tukija kwenu bayana, Mkagile wa Mandai.
9. Atowapa vurumai, Mungu ampe laana,
Afe kwa kizaizai, na maitiye kuchina,
Kisha iliwe na tai, kuzikwa iwe hakuna,
Ataeleta fitina, Mkagile wa Mandai.
10. Beti kumi baibai, kwa nguvuze Rahmana
Mpewe mengi malai, neema kila aina,
Muishi hamfubai, muwapate wema wana,
Kwaheri ya kuagana, Mkagile wa Mandai.
Muwasilishaji – Abdallah Ahmad Seif - 0754 - 870196 au 0716 - 903355
Katibu Mwenezi Msaidizi UKUTA – Dodoma
Don Bosco – Ngozi – Burundi
31/8/2012
Umuhimu wa Kiswahili katika jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMA)
Mada hii iliwasilishwa katika kongamano la Kiswahili lililoandaliwa na CHAWAKAMA na CHAWAKIRWA lililofanyika mjini Kigali Novemba 12-16 2008. Imeandikwa na Cyprian Niyomugabo, PhD katika Sayansi za Kiisimu (Lugha za Kafrika). Mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Kigali-Rwanda (KIE).
UTANGULIZI
Si rahisi kuzungumzia umuhimu wote wa jambo lolote lile, na hivi ni vigumu kutaja umuhimu wote wa Kiswahili mnamo dakika hizi 15 ninazopewa, lakini nitajaribu. Kiswahili ni lugha ya kiafrika ambayo ni maarufu sana humu Afrika na nje ya bara la Afrika. Asili ya lugha hii ni Afrika ya mashariki sehemu za mwambao au upwa (pwani) wa Afrika ya Mashariki kando kando ya bahari ya India. Kiswahili ni lugha yenyewe na watu wake ni Waswhili na utamaduni na utu ni Uswahili.
1. FASILI YA KISWAHILI
Kiisimu, lugha ni mfumo wa sauti nasibu za binadamu (sauti hizo ni herufi: vokali/irabu na konsonanti). Kiisimu jamii, tutasema ya kwamba lugha ni chombo cha mawasiliano katika jamii za binadamu. Kuwasiliana kwenyewe ni kupashana habari kwa kutumia maneno yaani lugha.
ü Kiswahili ni lugha: ni mfumo wa sauti nasibu, vilevile chombo cha mawasiliano kama lugha yoyote ile.
ü Asili ya Kiswahili ni Afrika ya Mashariki: Ingawa kitovu cha Kiswahili ni Afrika ya Mashariki, kiwakati uliopo Kiswahili ni cha sisi sote.
ü Kiswahili ni lugha ya Kiafrika. Namba yake ni G40 katika tipolojia/ uainishaji wa lugha ya AE Meeussen.
ü Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Tanzania, nchini Kenya na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
ü Kiswahili ni lugha rasmi nchini Tanzania, nchini Kenya, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika umoja wa Afrika ( na bado haijawa lugha rasmi katika JAMA).
ü Kiswahili ni lugha ya umahiri maana lugha iliyovuka mipaka ya kitaifa na kuwa lugha ya kimataifa. Kama asemavyo Calvet (1988:14), “lugha inayozidi kuongeza idadi ya wazungumzaji wake na idadi ya dhima zake ni jumuia lugha inayotapakaa”. Leo Kiswahili kinasemekana kuwa ni lugha ya saba katika lugha za ulimwengu na ni lugha inayoongewa na takribani watu zaidi ya milioni 100.
2. DOKEZO LA KIHISTORIA: MUHTASARI WA HISTORIA YA KISWAHILI KATIKA JAMA
Nianzie labda kwa porojo isemayo ya kwamba Kiswahili kilizaliwa Unguja (Zanzibar), kikakulia na kulelewa Tanganyika (Tanzania Bara), kikapatwa na ugojwa huko Kenya, kikalazwa hospitali na kufia Uganda na kuzikwa Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya sasa hivi) na tuongeze labda kikafufukia hapa Rwanda leo hii. Ni porojo ambayo inaukweli wake kihistoria.
Wakati wa harakati za uhuru wanasiasa walijaribu sana kutumia Kiswahili kama kiungo kati yao na wananchi.
TANZANIA: TAA (Tanganyika African Association) chama hiki kilianzishwa DSM na kusambaa nchi nzima. Chama hiki kilikuwa na katiba yake katika Kiswahili. Kiswahili kikatiliwa mkazo sana. Mnamo mwaka 1954 TAA kikabadiliswa na kuwa TANU (Tanganyika African National Union) na kiongozi akawa Mwalimu J.K Nyerere. Mara nyingi mikutano yake ya hadhara alitumia Kiswahili bila ya mkalimani katika juhudi zake za ukombozi. Mnamo mwaka wa 1955 kiswahili kilianza kutumiwa Bungeni na 1961 TANU kikafanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa. TANU kilijaribu sana kukikuza na kukitumia Kiswahili na watu wakaanza kujivunia lugha hii. Wakati wote huu Kiswahili kilikuwa ni chombo muhimu cha ukombozi wa kisiasa nchini KENYA:
Nchini Kenya Kiswahili kilipigwa vita sana na magavana wa kizungu, mathalani 1900 Sir Charles Elist aliyekuwa Gavana alihimiza lugha za makabila mengine na hakutaka Kiswahili kitumiwe. Lengo lake kubwa ni kuifanya Kenya iwe chini ya wazungu na kusiwe na kiungo chochote cha lugha ya kiafrika. Na hali hii ya kukipiga vita iliendelea sana na mnamo mwaka wa 1935 Kiingereza kikawa ndiyo lugha ya mitihani katika shule ya msingi. Hata hivyo wanasiasa walijaribu sana kukitilia mkazo Kiswahili toka awali na polepole kikaanza kuwaunganisha wananchi katika harakati za ukombozi. Kumbukeni kazi ya Mhe. Rais Jomo Kenyatta, kumbukeni kazi ya MAUMAU n.k.
UGANDA: Kiswahili ni lugha ya kwanza ya kigeni kutumiwa nchini Uganda. Kiswahili kilianza kupendelewa na wakoloni hapo awali japo Ukristo ulikipinga maana ulikinasibisha na Uislamu. Mathalan Gavana wa Uganda, W.F Gowers, 1927 alihimiza Kiswahili kitumiwe Kiswahili kitumiwe Uganda huku akipingana sana na mfalme Kabaka Daudi wa Uganda ambaye alitaka Kiganda kitumiwe, Kiswahili hata hivyo kilifahamika bila kupata nguvu sana. Na hata katika harakati za ukombozi Kiswahili hakikutumika sana ukilinganisha na nchi nyenzake za Afrika Mashariki.
RWANDA-BURUNDI nchini Rwanda, Kiswahili ndiyo lugha rasmi ya kwanza ya kigeni. Mtawala Mjerumani, mfanyabiashara wa kiarabu, dini ya Islamu na Wamisionari wa kizungu, kati ya hawa wanne si rahisi kusema ni nani ameleta au ametumia kwanza Kiswahili nchini. Kazi nyingi zilizogusia mada hii hazikutoa mwanga wa kutosha juu ya swali hili. Ukweli wa mambo ni kwamba Kiswahili kiliingia rasmi Rwanda mwishoni mwa karne ya 19 wakati wa utawala wa Mjerumani. (Taz. NIYOMUGABO C. 1992). Burundi Kiswahili kiko kwani historia ya Rwanda na burundi wakati wa ukoloni si tofauti.
ZAIRE (DRC), Kiswahili kilisambazwa mashariki mwa Zaire na Tiputipu (Mtipura) kabla ya 1860 akifanya safari za biashara na Kiswahili chake kule kinajulikana kwa jina la Kingwana na ni lugha ya Taifa tena ni lugha rasmi nchini humo.
3. UMUHIMU WA KISWAHILI KATIKA JAMA
Katika Isimujamii, lugha haichukuliwi kama mfumo unaotenganishwa na mazingira yake ya matumizi; ndiyomaana hapa tutaona jinsi lugha inavyofanyakazi katika jamii ya wazungumzaji wake. Kuhusu rai hii tunasema ya kwamba luha haiwezi kuchunguzwa nje ya wale wanaoitumia kwa sababu ni sehemu muhimu ya maisha ya watu. Mabadililko katika lugha ni sehemu moja ya mabadiliko katika jamii nzima yaani katika utamaduni wake. Dhima ya madhumuni ya lugha katika jamii yatakuwa mengi. Yanayojitokeza kuwa muhimu sana ni haya yafuatayo: kusudi la kwanza la lugha katika jamii ni kuwa chombo cha mawasiliano. Kuwasiliana kwenyewe kunatarajia kuleta uelewano na ujirani mwema kati ya watu wa jamii au` kati ya jamii na nyingine. Waishio katika hali ya usalama katika jamii, maendeleo yanawafikia haraka haraka.
· Kiswahili ni chombo cha kujenga uhusiano, ujirani mwema na urafiki kati ya watu na watu. Kujua lugha nyingi ni kujiongezea uwanja wa kujipatia marafiki na kuweza kujifunza mengi kutoka kwao. Ni chombo cha kuleta amani na utulivu kwani na amani ni mojawapo ya msingi wa maendeleo katika jamii yoyote ile. Na kama tunaoimba katika Kanisa ni kwamba kunako urafiki, upendo na uhusiano Mungu yupo. Sasa Mungu yu hapa katika kongamano hili.
· Kiswahili ni chombo cha elimu: kwa kupitia mfumo wa elimu za kijadi au za kisasa.
· Kiswahili ni chombo cha starehe na burudani: nyimbo zinazopendwa katika Kiswahili, kuweza kufanya utalii kwa kutumia Kiswahili.
· Kiswahili ni silaha ya ukombozi na kitambulisho cha Waafrika: Tazama kazi iliyofanywa na TANU, MAUMAU, maandishi ya Shaaban Robert katika pambo la lugha, “Titi la mama ”. titi hilo ni lipi? Ni Kiswahili.
· Kiswahili ni kiungo cha Waafrika: Kwa Waafrika kusini mwa jangwa la Sahara, matumizi ya lugha za kigeni yamekuwa yakikuzwa kwa sababu mbalimbali mojawapo ni kukosekana lugha ya kuunganisha watu wengi wa makabila tofauti.
· Kiswahili lugha isiyo na ukabila: Ukabila, maana , matendo au mawazo ya mtu yaliyotawaliwa na kuthamini kabila lake tu na kubagua makabila mengine, ni kizuizi kikubwa sana kwa maendeleo ya Afrika. Kwa hiyo Kiswahili kimekuja kama lugha ambayo haina mwenyewe kiukabila kwani ni ya sisi sote.
· Kiswahili hupatia watu kazi: wakalimani wa Kiswahili katika UA, walimu, wauza vitabu, wanahabari.
· Kiswahili chombo cha maendeleo: Sheila Ryanga Kenyatta University amesema: “Kila lugha yoyote ile katika kila taifa iwe ni ya umahiri, iwe inatumika kwa uchache inadhima yake na nafasi yake kama chombo cha maendeleo ya nchi upande wa uchumi uongozi bora…..”. Hadhi na thamani ya lugha hutokana na hadhi ya wazungumzaji wake. Lugha ya watu maskini hadhi yake itakuwa ya umaskini. Lugha ya watu tajiri kimaendeleo, kiutamaduni, kiteknolojia,….itakuwa ni lugha yenye hadhi kubwa. Kwa hiyo ili tuendeleze Kiswahili ipasavyo lazima sisi wanachi wa JAMA tufanye kazi, tutumie bidii sana kwa kusoma hasahasa nyie vijana kwani ukesho wa JAMA ni nyie. Kama asemavyo Mnyarwanda utakachokula kesho unakitayarisha leo.
4. MIKAKATI YA KUKUZA KISWAHILI KATIKA JAMA
Taasisi za dola zinazohusika na ukuzaji wa Kiswahili katika JAMA inapaswa kukutanika pamoja kwa shuguli ya kueneza lugha ya Kiswahili na huu ni wakati mzuri wa kuchunguza sera za JAMA kiwakati uliopo katika harakati za utapakazaji wa Kiswahili. Hatua ya kwanza ya kuweza kufikiri juu ya ukuzaji wa lugha fulani ni kujua waziwazi umuhimu wake. Umuhimu wa Kiswahili katika JAMA unajulikana kinagaubaga. Yafuatayo ni kama mapendekezo:
· Kiswahili kiwe chombo cha kisiasa cha kweli: Utambulisho wa Waafrika: Mhe. Rais Joaquim Chissano wa Msumbiji (Rais mstaafu) ndiye Rais wa kwanza kuhutubia kikao cha wakuu wanchi wanamemba wa Umoja wa Afrika (AU) katika Kiswahili. Wakati huo alikuwa mwenyekiti wa umoja huo. Niwakumbushe ya kwamba kabla ya hotuba yake katika Kiswahili, lugha rasmi za UA zilikuwa Kiarabu, Kifaransa, Kingereza na Kireno. Alipozungumza katika Kiswahili na alikuwa anafanya ukalimania yeye mwenyewe. Wakati Rais Chissano alipozungumza Kiswahili kwa mara ya kwanza viongozi wengi na hata mabalozi walipatwa na mshangao na tangu wakati huo azimio likachukuliwa ili Kiswahili kiwe mojawapo ya lugha rasmi za umoja huo. Na sasa hivi Rais Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amabaye amechukua uenyekiti wa UA kutoka kwa mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais John Kufor wa Ghana aliwahutubia wakuu wenzake katika Kiswahili mnamo kikao cha mwisho cha mwezi Januari 2008. Hatua za Marais hawa zilikanganya wenzao kwani ilkuwa mazoea kwa wakubwa wa Afrika kutumia lugha za kigeni na kuonyesha umahiri na ubingwa wao katika lugha hizo za kigeni. Nikumbushe kwa kupitia ya kwamba mpaka sasa hivi kwa mujibu wa katiba ya JAMA lugha ya Kiingereza ndiyo lugha rasmi inayotumiwa na Kiswahili kimeelekezwa kutumika kama lugha ya mawasiliano, ambapo jitihada za kukifanya kiwe lugha rasmi zinaendelea. Hapa kuna maoni tofauti: (a) Kiswahili kiwe lugha ya JAMA peke yake tu. (b) Kiingereza kiwe peke yake lugha rasmi katika JAMA. © Kiswahili na Kiingereza, lugha hizi mbili zichukuliwe kama lugha rasmi za JAMA. Hali ya uwili lugha (hali ya ulugha mbili) au ulumbi (ulugha nyingi) iingizwe katika JAMA (mfano Kiswahili-Kiingereza-Kifaransa/Kiswahili-Kiingereza/Kiarabu….). Nyie mnaonaje? Mnipashe. Mimi maoni yangu ni yafuatayo:
· Sera ya lugha na upangaji wa lugha: Sera ya lugha ni taratibu mbalimbali za kuratibu matumizi ya lugha katika jamii. Upangaji wa lugha ni jitihada za kuweka sera mbalimbali za lugha ambao husaidia kutatua tatizo la mawasiliano katika jamii. Tunajua ya kwamba mradi wa upangaji wa lugha si jambo rahisi. Kwani kweli sera ya upangaji wa lugha katika jamii/jumuia fulani huonekana mara nyingi kama jaribio gumu kwani inazingatia uteuzi wa kiitikadi na kutilia maanani maoni ya kijamii, kistadi na kiutekelezaji. Wakati umefika ili kuwepo sera ya nafasi ya kila lugha katika JAMA maana kuonyesha nafasi ya kila lugha kufuatana na umuhimu au dhima zake katika jamii. Kudhihirisha nafasi za lugha za kiasili (makabila/makundi), lugha za taifa, lugha za ukanda, lugha za kimataifa. Ingawa Kiswahili kimefikia hatua ya lugha inayozungumzwa na wengi na yenye dima nyingi katika JAMA, si kumanisha kuwa hakuna vipingamizi vya uenezaji wake. Kizuizi chake cha kwanza ni mapambano ya kilugha. Taasisi za dola zinazojihusisha na ukuzaji wa lugha ya kiswahili zifanye kazi bega kwa began a ACALAN (African Academy of Languages) maana Akademia ya lugha za Afrika ya UA.
· Kiswahili kiwe chombo cha elimu cha kweli: Kiswahili kiwe chombo cha kufundishia katika viwango vyote vya masomo lakini tusisahau na lugha nyingine. Taz. Upangaji lugha.
· Kufuta kasumba za ukoloni: kasumba ni mabaki ya fikra za kikoloni kichwani mwa mtu. Kuna waafrika wengi sana ambao wanafikiri ya kwamba kujua au kuzungumza lugha za kiafrika, lugha za kishenzi, lugha duni, lugha za akinayake, lugha ambazo ndani yake kuna umasikini… ni aibu na ni kukosa akili. Mhe George Mkuchika (Mb), Waziri wa Habari utamaduni na michezo, Tanzania, akizungumzia kuhusu ukuzaji wa lugha ya Kiswahili na lugha za kiafrika kwa ujumla amesema “Mada hii ni mada muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho nchi zetu za kiafrika zimekwishajipatia uhuru wa kujitawala na kujiamulia mambo yetu wenyewe na kwamba kazi kubwa iliyoko mbele yetu kwa sasa ni kuelekeza jitihada zetu katika kujikomboa kifikira, kiutamaduni na kiuchumi mambo ambayo yalikandamizwa na kudidimizwa wakati wa kipindi cha ukoloni, kwa hiyo kwa kupitia dini na utawala walijitahidi kuwatia wenyeji kasumba ili waone kila walichonacho ni cha kishenzi; kuanzia lugha, dini, utamaduni, teknolojia, dawa na mengineyo. Somo hili walilotoa lilifanikiwa sana na likawa ni sehemu au viambajengo vya ukoloni”. Kwa wakati mwingi mradi wa kukuza lugha za kiafrika kwa jumla na kiswahili hasahasa hupingwa kwa sababu idadi ya watu wengi wanaochukua madaraka katika nyanja mbalimbali za taifa walisomea katika mfumo wa ufundishaji wa kikoloni. Baadhi ya hawa ni watu ambao machoni mwao kuwa na mradi wa kukuza lugha ya kiafrika ni upotezaji wa wakati na pesa.
· Kutafsiri vitabu na maandishi mengine katika Kiswahili: Ili Waafrika wa kila kiwango cha ujuzi wanufaike na maendeleo ni lazima ujuzi wote (teknolojia, sayansi, falsafa…) viwekwe katika Kiswahili kutoka lugha ambazo jamii zake zimepiga hatua kimaendeleo kama Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kidachi, Kijapani n.k. Vilevile ni lazima kazi za uandishi na utangazaji wa vitabu na utafiti wa kila aina katika Kiswahili yatiliwe maanani. Kwani kama asemavyo Senkoro (1987) “elimu na maarifa mbalimbali ni mali ya watu wote duniani”.
· Kuweka nguvu zaidi katika utungaji kamusi na ukuzaji wa istilahi. Ili lugha iwe na uhai lazima iweze kutafsiri dhana zote na fikra zote katika lugha hiyo ili iweze kuwa chombo cha kweli cha maendeleo ya kila aina. Kwa upandea wa Kiswahili tunapongeza sana kazi iliyofanywa na TUKI pamoja na BAKITA.
· Kufungulia milango “viswahili” vingine. Kiswahili sanifu lazima kifungulie milango launi nyingine ya Kiswahili hasahasa cha Afrika ya Kati.
· Kuongezeka idadi ya makongamano kuhusu ukuzaji wa Kiswahili kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa.
ASANTENI NYOTE!
MAREJELEO
Calvet, L.J. Les langues vehiculaires, PUF, Paris, 1981.
Chimerah, R.M. Kiswahili past present and future Horizons, Nairobi 2009.
Kagabo, J.H.L. Islam et les “Swahili” au Rwanda, Paris, 1988.
Khalid Abdallah, the liberation of Swahili, Nairobi, 1977.
Massamba, D.P.B. Historia ya Kiswahili 50BK hadi 1500 BK, Nairobi, 2002.
Mmallavi, A.P.W. Lugha katika jamii, EAPH, DSM, 1977.
Niyibizi, S. Le Swahili au Rwanda: Aspects historique, linguistique et sociolinguistique, Butare 1980.
Niyomugabo, C. Nafasi ya lugha ya Kiswahili katika uwanja wa dini nchini Rwanda: Mkabala wa kiisimujamii, Ruhengeri 1992.
Senkoro, F.E.M.K. Fasihi na jamii, DSM, 1987.
Shihabudin Chiragdin na M. Mnyampala (1977) Historia ya Kiswahili OUP, Nairobi.
Tuli R.S.K. (1985) Chimbuko la Kiswahili kukua na kuenea kwake, Arusha Tanzania.s

Mwl Maeda