Makosa Yaliyozoeleka katika Matumizi ya Kiswahili Sanifu
Sehemu ya Hamsini na Saba
Ipi ni Sahihi Kati ya “Jina Langu ni Issaya Simon Lupogo” na “Majina Yangu ni Issaya Simon Lupogo”?
Kumekuwa na matumizi ya ruwaza hizi katika miktadha mbalimbali ya matumizi ya Kiswahili sanifu. Vilevile, kumekuwa na mjadala kuhusu suala hilo; kila upande ukitetea kwamba wapo sahihi. Hili ni jambo linalotakiwa kuwekwa sawa ili kuondoa hali ya kuwapo kwa namna mbili za matumizi ya kirai hicho pasi na msingi wowote.
Mjadala wowote wa kitaaluma hutumia hoja zenye mashiko (zinazoshawishi) ili kufikia hitimisho au suluhisho muafaka wa mgogoro wowote.
Tuzame kidogo katika data. Je, ili mtu atoe jibu la kutaja jina lake (majina yake❗), kunakuwa na swali gani?
Kiingereza:
What is your name? may you tell us your name?
Kimatengo:
Liina lyaku wa nya (jina lako ni nani)? au agukema wa nya (wanakuita nani)?
Kizigua:
Wetangwa yuhi (unaitwa nani)? au idizina dyako ndihi (jina lako ni lipi)?
Kizaramo:
Twaga jako nani (unaitwa nani)?
Kihaya:
Eibala lyae ulyoa (jina lako ni nani)? au noyetwa oha? (unaitwa nani)? au eizina lyae nilihya (jina lako ni lipi)?
Kijapani:
Anata wa dare desu ka /貴方は誰ですか (wewe unaitwa nani)?
Kibena:
Yuve nani (wewe ni nani)? au litawa lyaho nani (jina lako nani)?
Kwa hivyo, ukizingatia uulizaji wa maswali katika sampuli ya lugha hizi, unaona dhahiri kwamba zinalenga mtu atoe jibu la kutaja jina lake ambalo huwa ni moja; mfano, ninaitwa Issaya Simon Lupogo au jina langu ni Issaya Simon Lupogo.
Aidha, kama lengo lingekuwa ni kumtaka ajibu kwa kutaja majina yake zaidi ya moja (mengi), hata namna ya uulizaji ingekuwa na ruwaza muafaka; jambo ambalo halijajitokeza katika lugha yoyote katika sampuli iliyotumika.
Pia, kutokana na uchanganuzi huo, ni dhahiri kwamba kusema “majina yangu ni Issaya Simon Lupogo” haina mantiki inayoweza kushawishika kirahisi. Inafahamika kwamba wanaotetea suala hilo (majina yangu ni…) wanajenga hoja kwamba kwa kuwa jina hilo linakuwa ni muunganiko wa jina la kwanza na la mwisho (ukoo) au jina la kwanza, la kati, na la mwisho; basi wanazitazama sehemu hizo kama majina yanayojitegemea. Mantiki ya jambo hili ni rahisi sana kuhojiwa. Mathalani, maswali yafuatayo yanaweza yakawa magumu kwa wanaoamini katika hili: kama mtu ni mmoja, iweje jina lake lisomeke katika wingi?, inakuwaje vipande vinavyounda jina moja vichukuliwe kama majina yanayojikamilisha ilhali kukamilika kwake ni mpaka yaungane yote?
Hoja nyingi ya msingi ni kwamba kama “majina yangu ni….” ingekuwa ni sahihi, basi katika kuyataja majina hayo panapaswa kuwa na kiunganishi/kihusishi “na” pamoja na alama nyingine za uakifishaji, mathalani, koma/mkato.
Mfano:
Majina yangu ni Issaya, Simon, na Lupogo❗
Ninaamini hii si ruwaza inayotumika; kama haitumiki ruwaza hiyo, madai ya “majina yangu ni…” ni batili na hayana mashiko kisarufi na/au kiisimu.
Kwa hivyo, ni dhahiri kwamba hoja ya kutetea “jina langu ni Issaya Simon Lupogo” ina mashiko kuliko huo upande mwingine.
Mwl. Issaya Lupogo – Chuo Kikuu Mzumbe
+255712143909
lupogoissaya1@gmail.com
#Fuatilia pia makala hizi katika gazeti la Mwananchi kwenye ukurasa wa Kiswahili Adhimu kila Jumanne#