Hadithi Fupi … SIKU MBAYA KWANGU
…Mungu wangu, kwanini nahukumiwa bila makosa???…. …
Mtunzi: Hakika Jonathan
..Kama kawaida yangu sikua na tabia ya kuchelewa kazini, niliamka mapema bila shaka ilikua saa kumi na moja usiku. Sikutaka kumsumbua mke wangu mama Dayana kwani alichoka sana na shughuli za nyumbani siku iliyopita, niliandaa maji mwenyewe na kisha kuelekea bafuni kuoga….
Bila kupoteza muda ilikua yapata saa moja kamili asubuhi, nilifika ofisini kwangu mapema sana kabla hata ya wafanyakazi wengine hawajafika.Mazingira ya kampuni yetu ya Usafirishaji wa mizigo ilikua kimya sana kwa muda ule kwani masaa ya kazi yalikua hayajafika. Nikiwa na mzigo mzito wa kukamilisha mahesabu ya pesa iliyopatikana siku iliyopita ilinibidi niwahi mapema sana kazini.
“Vipi muhasibu mbona leo mapema sana, “nilikutana na swali kutoka kwa mlinzi aliyekuwa akinifungulia mlango wa geti kuu la kuingilia ndani ya kampuni yetu. “Majukumu tu ndugu yangu ,”….nilimjibu mlinzi na kisha kuelekea ofisini. Jua lilizidi kuangaza na kuwa kali huku ndege wa angani wakiruka na kuipendezesha dunia vema. Ilikua yapata saa mbili asubuhi simu yangu ilianza kuita, kutokana na shughuli kunibana simu iliita zaidi ya mara tatu bila kuisikia huku mimi nikiwa bize na compyuta yangu.
“Halooo habari za asubuhi ndugu yangu, samahani nilikuwa mbali na simu sikuweza kuisikia ikiita ” ,nilizungumza maneno hayo kwa ustaarabu mkubwa baada ya kupokea simu yangu, na kisha kupokea taarifa iliyokua mbaya kwangu. “Kuwa na amani ndugu yangu, unaongea na uongozi wa shule ya secondari Agrey. Mwanao Dayana tumemfukuza shule baada ya kugundua ni mjamzito ” , sauti ambayo haikuwa ngeni kwangu ilipenya masikioni mwangu na kunipa mawazo na hasira kali dhidi ya mwanangu niliempenda sana Dayana.
Sikuwa na hamu tena ya kuendelea na kazi kwa siku hiyo kutokana na taarifa niliyoipokea kunivuruga akili yangu. “Naona siku hizi umekua mzembe na mwizi sana, pokea malipo ya upuuzi wakoo “,bosi wangu aliingia kwa fujo sana ofisini kwangu na kisha kutupa mezani bahasha kubwa.Nikiwa mwenye hali ya unyonge niliifungua bahasha ile kwani nilitegemea kukuta nyaraka za kiofisi zilizohusiana na mahesabu ya kampuni hali ambayo ilikuwa kinyume kabisa na matarajio yangu. “,What….. ..! nimefukuzwa kazi kwa kosa la kuiba pesa za kampuni…..Mungu wangu nimekukosea nini? leo hii mimi naitwa mwizi!!! “,nilizungumza maneno ya kumlaumu mungu wangu baada ya kusoma barua ya kufukuzwa kazi, huku nikiwa sioni sababu ya kweli iliyonifanya nikose kazi kwani daima nilikua mfanyakazi mwaminifu na mwenye bidii sana hali iliyokuwa kinyume na malipo niliyopata.
Bila kujitambua nilitoka ofisini kwa jazba na kisha kuwasha gari langu kuelekea nyumbani, sikuwa na haja ya kuomba msamaha kwani niliamini kulikua na mkono wa mtu uliyosababisha mimi kufukuzwa kazi kwa ajiri ya manufaa ya watu wachache. “,Ipo siku bosi atanikumbuka na kuona thamani yangu…”,nilitamka maneno hayo moyoni mwangu huku nikiendesha gari langu kwa kasi sana hali iliyowaacha midomo wazi watu walokuwa pembeni ya barabara. Nikiwa na hasira pamoja na huzuni kwa mwanangu kufukuzwa shule sababu ya ujauzito na mimi kufukuzwa kazi, mawazo yalikisumbua kichwa changu kwani akaunti yangu haikuwa na pesa hata senti mara baada ya kumaliza ujenzi wa nyumba yangu kwasababu nilichoshwa na maisha ya kupanga. Paaaaaaaaaaah!!!! Mlio mkubwa ulisikika na gari langu kuyumba sana,” mungu wangu nimegonga mtoto wa watu “,nilifinya breki na kisha kutoka haraka nje ya gari langu kumchukua mtoto na kumuwahisha hospitali. ” ,Apigweee huyoo apigweee! ” ,zilisikika kelele za wananchi wenye hasira walotaka kunijeruhi kwani walishuhudia mwendo kasi niliokuwa nao.
Nilimfikisha mtoto katika hospitali ya taifa Muhimbili ili apatiwe matibabu huku nikimshukuru mungu kwani kwa upande wangu sikupata majeraha yoyote. ” ,Pole sana kaka ajari hutokea bila kutegemea usijilaumu sana mtoto atapona, tumemfanyia upasuaji na anaendelea vizuri tunaomba baada ya siku tatu uje na milioni kumi za matibabu ” ,.Daktari alizungumza na kisha kuniruhusu kuondoka huku mtoto akiuguzwa na wazazi wake baada ya kupokea taarifa kutoka katika vyombo vya habari vilivyozungumzia ajari hiyo.
Nilirudi nyumbani kwa unyonge na uchovu sana,kichwa kiliuma nikitafakari namna ya kupata pesa kulipia matibabu ya mtoto na bahati mbaya nilikua nimefukuzwa kazi. Nilistaajabu kukuta milango ya nyumba yangu kukiwa wazi na ukimya ukitawala sana ndani ya nyumba yangu.. Ilibidi nifunge geti baada ya kumaliza kuingiza gari langu ndani hali iliyozidi kunitia hofu kwani mlinzi hakuwepo getini usiku ule wa saa tatu na haikuwa kawaida yake.
Nikiwa na hasira na mtoto wangu Dayana nilielekea chumbani kwake na kukuta mlango ukiwa bado umefungwa hali iliyoashiria alikuwa bado hajafika pale nyumbani. Ghafra meseji iliingia kwenye simu yangu na kisha kuisoma kwani nilitegemea simu kutoka hospitalini muda wowote kunifahamisha juu ya maendeleo ya mgonjwa wangu, “Samahani baba mimi ni Dayana mwanao mpendwa, nimeamua kutorudi nyumbani kutokana na aibu niliyokupatia nimeamua kwenda kuolewa na mwanaume aliyenipatia ujauzito. Nawapenda sana wazazi wangu “,nilimaliza kusoma meseji na kisha kuishiwa nguvu kabisa kwani ujumbe ulikua mzito sana. “,Mama Dayanaa….. mama Dayana, uko wapi mke wangu ” ,nilianza kumuita mama Dayana nimweleze mkosi uliotupata lakini sikuweza kusikia akinijibu. Nilielekea chumbani kwetu na kukuta mlango ukiwa wazi huku mama Dayana akiwa hayumo, nikiwa katika hali ya mshangao nilishtuka kusikia kelele za mwanamke na mwanaume wakioga ndani ya bafu ambalo halikutumiwa na mtu yoyote zaidi ya mimi na mama Dayana kwani bafu lilikuwa chumbani kwetu.
“What..!!!… mama Dayana unafanya nini na Beka???…” Nilitamka maneno kwa hasira baada ya kushuhudia mke wangu akioga na mlinzi wa geti la nyumba yangu aliyeitwa Beka.Nilikosa cha kufanya kwani nilimpenda na kumuamini sana mke wangu lakini kanilipa mabaya, wema wangu wote nilioufanya duniani nililipwa mabaya. Nilihukumiwa kwa makosa ambayo sikuweza kufanya…. “Mke wangu, mwanangu, bosi wangu, mbona mmenifanyia hivi?? ” ,nilizungumza maneno hayo moyoni mwangu na kisha kudondoka chini na kupoteza fahamu.
***MWISHO **
Fundisho
“Maisha ni safari ndefu tumwombe mungu atutie nguvu “