Utangulizi: Katika mada hii unatarajiwa kuelewa maana ya mawasiliano na jinsi mchakato wa mawasiliano unavyofanyika. Utaelewa dhana ya lugha na vipengele muhimu vinavyokamilisha maana ya lugha. Utaelewa dhima kuu za lugha, matumizi na umuhimu wake. Vilevile katika mada hii utajifunza juu ya lafudhi na matamshi mbalimbali ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili.
Matumizi na Umuhimu wa Lugha
Lugha kama Chombo cha Mawasiliano
Mawasiliano ni mchakato wa kuhawilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa mawazo, hisia, malengo, tabia, matarajio, mitazamo kupitia mazungumzo, ishara na maandishi. Ni ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi ambazo zinaweza kuwa viumbe hai au kinyume chake. Sasa hapa sisi tutajikita katika mawasiliano yanayofanywa baina ya viumbe wanaotumia lugha (ambao kimsingi ni binadamu).
Maana ya MawasilianoLugha ni nyenzo muhimu sana katika mawasiliano ya binadamu. Ulishawahi kujiuliza kwamba mwasiliano yangekuwaje pasipokuwepo lugha? Mwalimu angekua anatumia mtindo gani kukufundisha darasani au wewe ungemwombaje kalamu rafiki yako? (Unasema ungewasiliana kama wanavyowsiliana watu wasiosikia au kuzungumza?) Hao pia wanawasiliana hivyo kwa sababu wana maarifa ya lugha.
Mafumbuzi ya kisayansi na teknolojia, yote haya yasingewezekana pasipo kutumia lugha, usingeweza kusogoa (kuchat) na marafiki zako kwenye facebook, usingeweza kumwandikia ujumbe rafiki yako kupitia simu yako na kadhalika.
Umeona sasa jinsi lugha ilivyo muhimu katika mwasiliano? Kabla hatujaona umuhimu huu hebu tuangalie maana/maana ya lugha.
Kuna mitazamo mbalimbali juu ya maana ya lugha lakini kwa ujumla lugha inaweza kumaanawa kama mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku ili kuelezea hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.
Kulingana na maana hii tunaweza kubainisha maneno ya msingi yanayojitokeza katika maana ya lugha, maneno hayo ni pamoja na haya yafuatayo:
Lugha ni mfumo
Kila lugha ya mwanadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa maana. Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno, maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya. Mfano; k+u+k+u – kuku
Mtoto + anatembea – mtoto anatembea.
Katika muunganiko huu wa maneno na miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria zinazodhibiti mfuatano wa kila kipashio. Kuna kanuni zinazodhibiti mfuatano wa sauti, mfuatano wa mofimu, mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi. Kwa maana hiyo, lugha ya mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu maalumu ambazo zikikiukwa basi kunakuwa hakuna utimilifu wa lugha husika. Sheria hizi zinazotawala mpangilio wa viunzi za lugha hiyo ndizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha fulani kuelewana.
Lugha ni mfumo wa sauti nasibu
Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno (kwa mfano jiwe) na kitu chenyewe tunachotumia katika ujenzi na matumizi mengine (maana na kirejelewa). Hii ina maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapa. Kwa mfano neno “jiwe” hakuna watu waliokaa na kusema kuanzia leo hili litaitwa jiwe. Vile vile hakuna uhusiano wowote kati ya neno “jiwe” na umbo linalorejelewa. Uhusiano wake ni wa nasibu tu na hutofautiana kutokana na lugha moja na nyingine. Jiwe mnaliitaje katika lugha yenu? Basi huo ndio unasibu wa lugha.
Lugha ni maalumu kwa mwanadamu
Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu mwenye uwezo wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanaweza kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa. Binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kuitumia katika mazingira yake na kitu ambacho wanyama hawawezi. Kwa mfano, ukimchukua paka wa china na kumleta Tanzania atatoa sauti ile ile sawa na paka wa Tanzania kwa kueleza shida ile ile au kutoa ishara ile ile.
Lugha ni mfumo wa ishara
Uishara wa lugha unamaanisha kuwa maneno huambatanishwa/huhusishwa na vitu, matendo,mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano. Hivyo basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilishwa.
Lugha hutumia sauti
Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba:
- Mtoto hujifunza kuzungumza kabla hajajifunza kusoma na kuandika.
- Mtoto hujifunza lugha moja kwa moja bila kufikiri kadiri anavyokuwa
- Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo
- Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa
- Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko kuandika
Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema kwa kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu; haya ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawasawa kwa kutumia maandishi.
Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano
Kwa kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya. Vile vile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza, kufanya kazi n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.
Mfumo wa Lugha
Hoja kuwa lugha ni mfumo inamaanisha kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali. Viambajengo au vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha.
Dhima za Lugha katika MawasilianoBaadhi ya dhima za lugha ni pamoja na hizi zifuatazo:
Ujumi: ujumi ni hali ya kutumia maneno ya lugha fulani kwa ufundi na ustadi wa hali ya juu kwa lengo la kuburudisha na kuwavutia watu wengine. Baadhi ya watu hutumia lugha kwa dhima hiyo, ili maksudi wasomaji au wasikilizaji wao wavutike na kuburudishwa na Lugha hiyo. Maeneo yatumikamo lugha yenye ujumi wa kiwango cha juu ni kwenye matangazo na kwenye fani ya utunzi wa mashairi.
Utambuzi: Ni hali ya kufikiria kwa makini, kukokotoa na kutoa majibu ya maswali tofauti ndani ya ubongo. Chombo kikuu kitumikacho kutoa majibu hayo ni lugha. Kutokana na muktadha huo tunaweza kusema kwamba lugha hutumika kama chombo cha utambuzi.
Hisia: ni fikra za ndani alizokuwa nazo kiumbe mwanaadamu. Tunapotaka kuonyesha hisia zetu na vilevile kuwavuta wengine kwa maneno mazito yanayoweza kumtoa msikilizaji machozi ya huzuni au ya furaha tunachagua maneno makali yenye hisia.
Kujielezea: Hali ya mtu kudhihirisha mambo mbalimbali aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake. Kwa mfano mtu anaposema nina furaha sana. Hapa mtu anatowa msisitizo wa kuonyesha kiwango cha furaha alichonacho, hili linafanyika kwa kutumia lugha. kwa ufupi tunachoweza kusema hapa ni kwamba lugha hutumika kwa ajili ya kujielezea.
Kuamuru: Ni kutoa maelekezo kwa njia ya kuamrisha. Kwa mfano hakimu anamuhukumu mshitakiwa kwa kumuamuru ‘Ninakufunga miaka mitatu jela’. Hapa lugha inatenda kazi ya kuamuru.
Kushirikiana: ni hali ya kutenda kitu kwa pamoja au hali ya kuwa na ubiya kwenye jambo. Lugha huwezesha watu kujenga mahusiano ya siri baina ya watu wawili au zaidi na kuweza kujitengenezea njia zao za kuwasiliana pasipo wengine kuelewa.
Kuonesha: kumuelekeza mtu kitu kwa njia ya kuashiria. Unapotaka kuonesha jambo ni lazima utumiye lugha kwa njia moja au nyengine.
Matumizi na Umuhimu wa Lugha
Lugha hutumika kama chombo, zana, kifaa au njia ya kufikia lengo fulani. Baadhi ya matumizi ya lugha ni pamoja na haya yafuatayo:
Kuwasiliana:- Lugha hutumika kupashana habari
Kuunganisha– Lugha hupatanisha na kuleta uelewano miongoni mwa wanajamii. pia lugha huweza kutofautisha jamii moja na nyengine.
Kujenga jamii- lugha huleta/huhimiza shughuli za maendeleo ya jamii, huleta amani na mshikamano katika jamii.
Kufundishia– Lugha hutumika katika kufundishia elimu.
Kutambulisha- Lugha hutumika kutambulisha jamii ya watu fulani.
Kuhifadhi- Lugha ndicho chombo cha kuhifadhi na kueneza utamaduni
Matamshi na Lafudhi ya KiswahiliMaana ya Matamshi
Matamshi ni namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu anavyozungumza lugha. Unaposema fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa unamaanisha anazungumza Kiswahili fasaha.
Neno moja linaweza kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali kutokana na sababu mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia anakotoka huyo mtu, kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au mwanasiasa, na elimu aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya watu watofautiane katika matamshi.
Dhana ya matamshi huhusisha:
Bainisha sauti za lugha ya Kiswahili
Sauti za lugha ya Kiswahili hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda sauti 24, irabu tano na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi ya kiswahili). Sauti za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano maneno “data” au “dengue” wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata kama wakiwa wanazungumza kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya
Kiswahili hutamkwa kama yalivyoandikwa.
Kwa hiyo unapotamka maneno ya Kiswahili ni sharti uzingatie sauti asilia za lugha ya Kiswahili. Kuna watu huwa wanaandika hivi “xaxa”, hii huwa unaitamkaje? Au “ucjal” huwa unaitamkaje? Kwa kufuata matamshi asilia ya Kiswahili “ucjal” itatamkwa “uchijal” sijui itakuwa ina maana gani sasa. Na pengine umekuwa ukitumia maandishi ya namna hii hata kwenye insha zako ukidhani upo sahihi au ni kwa mazoea tu, sasa kwa kuwa umejua matamshi sahihi ya Kiswahili ni yapi, utajifunza kuyatumia kwa usahihi katika maandishi rasmi na yasiyo rasmi.
Mkazo
Katika lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali, kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba’ra (njia).Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara’bara (sawa sawa), Alha’misi
Kiimbo
Ni utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika utaratibu wa utamkaji, dhana ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu ( yaani , kiwango cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj), Kwa hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au kuwa chini.
Aina za viimbo
Kiimbo cha maelezo: Kiimbo cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa takriban katika mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.
Kiimbo cha maulizo: Kiimbo cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti za kidatu kutegemeana na aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu anafundisha?
Kiimbo cha amri: kiimbo cha amri hakitofautiani sana na kiimbo cha maulizo. Kiimbo cha amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha maelezo. Mfano, njoo hapa!
Lafudhi ya Kiswahili
Lafudhi ni matamshi ya msemaji wa lugha fulani ambayo yanatokana na athari za kimazingira. Mazingira hayo yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea, kiwango chake cha elimu, tabaka lake la kijamii na kadhalika.
Lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili kwa watumiaji wengi wa Afrika Mashariki, kwa hiyo hii inafanya kuwatambua wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au maeneo wanakotoka. Kwa mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa Mwanza kwa lafudhi yao, watu wa Mtwara kwa lafudhi yao, watu wa Pemba kwa lafudhi yao au watu wa Musoma kwa lafudhi yao. Mifano:
Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuria)
Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mafaranga makumi mawili (Wakongo)
Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja kwa moja (Wasukuma)
Mbona unakuwa kinganganizi, nilishakwambia sikupendi lakini wewe bado unaningangania tu! (Wahaya)
MAWASILIANO UWILIKatika maigizo kwanza waigizaji huongea wao kwa wao lakini pia ujumbe walio naounawasilishwa kwa watazamaji; ni kwa hali hii tunapata double communication katika maigizo.
Mawasiliano kati ya waigizajiJukwaani vinashashamiri vitendo mbalimbali kama mahojiano, mafunzo, kongamano, mijadala… vinavyotukia kuhabarisha, kuhamasisha, kuhadithia… Pia muigizaji anaweza kuongea mwenewe katika kumtaarifu mtazamaji hisia, au mtazamo alio nao.
Mawasiliano kati ya jukwaa na watazamajiHali si yenye kuonekana sana maana mtazamaji nafanywa kuwa mpokea ujumbe isipokua ndani ya igizo shirikishi ambapo muigizaji anaruhusiwa kuongea na mtazamaji.
Mwl Maeda