Kwa Mukhtasari Ni vyema ieleweke kwamba neno sanifu la Kiswahili ni ‘chukua’ na wala si ‘chukuwa’.
AGHALABU, huwawia vigumu sana baadhi ya wanafunzi na watumizi wengine wa lugha ya Kiswahili kutenga tofauti baina ya maneno yanayoishia kwa silabi ‘wa’ na ‘ua’.
Mfano wa maneno hayo ni ‘kuwa’, ‘kua’ na chukua. Walimu watakubaliana nami kuwa kauli kama vile: ‘Nimekua nikisoma’; ‘Nilikua nikicheza’; ‘Nimekua nikiimba’; ‘Waziri alikua akiwahutubia waombolezaji’ miongoni mwa nyingine zimetawala kazi za wanafunzi hususan wale wa shule za msingi na za upili. Mara kwa mara huwasisitizia wanafunzi kuwa neno ‘kua’ hutumiwa tu mzungumzaji atakapo kuelezea hali ya kupevuka au kuongezeka kwa kimo cha kiumbe ama kuzidi kwa jambo fulani. Mifano: Mtoto amekua na tazama karibuni ataanza kwenda shuleni.
Neno ‘Kuwa’nalo hutumiwa kuelezea kwamba mtu au kitu kimedumu katika hali fulani kwa muda au kipindi fulani. Mfano: Wanakijiji wamekuwa wakiomboleza; Waislamu wamekuwa wakifunga saumu. Pili, huonyesha hali ya kutokea, kutendeka au kufanyika kwa jambo fulani.
Kwa mfano: Mbona siku hizi Ali amekuwa mwembamba hivi? Neno lenyewe ni miongoni mwa vitenzi vya silabi moja na hujitokeza kamusini kama ‘-wa’.
Mnyambuliko walo katika kauli ya kutendea ni ‘wia’ na katika kauli ya kutendwa au kutendewa ni ‘wiwa’. Tofauti na ‘kuwa’ ambalo limetawala matumizi ya kila siku na ambalo ni nadra sana kuliepuka katika semi zetu, ‘kua’ limejibana kimatumizi.
Lakini kadiri tunavyojaribu kutatua tatizo la matumizi ya ‘kua’ na ‘kuwa’ ndivyo liibukavyo tatizo jingine jipya: matumizi ya silabi ‘wa’ mwishoni mwa maneno ambayo yanapaswa kumalizika kwa ‘ua’. Mfano mmojawapo ni ‘chukuwa’. Je, ni ‘Kuchukua tahadhari’… au ‘Kuchukuwa tahadhari’…? Japo matumizi ya ‘chukuwa’ hujitokeza katika baadhi ya kazi za waandishi wa fasihi na sarufi, si sahihi. Tunaweza kuyathibitisha madai haya kwa kuangalia mnyambuliko wa neno lenyewe. Katika kauli ya kutendea, hunyambuliwa kama ‘chukulia’ ilhali katika kauli ya kutendwa au kutendewa huwa ni ‘chukuliwa’.
Minyambuliko
Endapo ‘chukuwa’ lingekuwa neno sahihi kisarufi, basi minyambuliko yake ingekuwa: ‘chukuwia’ (kauli ya kutendea), chukuwiwa (kauli ya kutendwa au kutendewa); jambo ambalo sivyo. Katika utunzi wa mashairi, maneno kama vile ‘chukuwa’, ‘juwa’ ‘kiliyo’, ‘sikiya’ ‘semeya’, ‘ingiya’ na mengine mfano wayo hayawezi kuhukumiwa kwa kutumia vigezo vya sarufi kwani malenga huwa na uhuru mwingi ukiwamo ule wa kubadili sauti za mwishoni mwa baadhi ya maneno ili kuwa na vina vya keketo moja.
Kutokana na hali hii, utakumbana na mishororo kama huu ufuatao: Ninalotaka kujuwa, sinifitie nambiye.
Je, kunayo sababu ambayo huwafanya watu wengine kutumia ‘ua’ mwishoni mwa maneno ambayo yanapaswa kuishia kwa ‘wa’ na ‘wa’ mwishoni mwa maneno ambayo yanapaswa kuishia kwa ‘ua’? Yamkini wanaotatizwa na jambo hili hudhani kuwa mageuko ya sauti ambayo hutokea baina ya mizizi ya nomino na vivumishi au baina ya nomino na nomino yanaweza kutokea mwishoni mwa vitenzi vinavyoishia ‘ua’.Pengine.
Hebu tuliangalie jambo hili kwa kina kidogo. Waihiga G, (1999: 51) anapoelezea muundo wa vivumishi katika ngeli ya A-WA, anadai kuwa ikiwa mzizi unaanza kwa irabu, irabu |u| ya kiambishi hugeuka na kuwa nusu irabu |w| kama ifuatavyo: Mtu mu+angalifu>mwangalifu. Katika fonetiki na fonolojia, mageuko kama haya hujulikana kama usigano wa sauti na hudhihirika kupitia uyeyusho wa vokali za juu ambazo huweza kuyeyuka na kuwa (w) au (y).
Mabadiliko
Hata hivyo, tulivyodokeza hapo juu, mabadiliko yenyewe hutokea baina ya viambishi vya nomino na vivumishi, nomino na nomino au nomino na viambishi awali vya vitenzi vinavyoanza kwa vokali kama vile uliza, ua, ona, enda miongoni mwa vingine. Mageuko hayo yanajidhihirisha katika mfano ufuatao: mu + uliza> mwuliza; mu+ ua> mwua; mu+ ambia> mwambia.
Hatutarajii mageuko hayo kuathiri viambishi tamati vya vitenzi na kuzua maneno kama vile pekuwa badala ya pekua; ibuwa badala ya ibua; chukuwa badala ya chukua miongoni mwa mengine.
Zipo sababu nyingine ambazo yamkini huchangia utata utokeao wakati wa kuyatamka maneno yenye sauti tulizozitanguliza katika makala haya na ambazo zinapaswa kufanyiwa utafiti wa kiisimu.
Ni vyema hata hivyo ieleweke kwamba neno sanifu la Kiswahili ni ‘chukua’ na wala si ‘chukuwa’.