KATIKA kuchunguza lugha, wanaisimu hutumia misingi ya kisayansi kama zifanyavyo sayansi nyingine. Maswala katika isimu huelezwa kwa udhahiri usio na utata wowote. Hoja huelezwa bila kuleta vuguvugu lolote la kimaana.
Habwe na Karanja, (2003) wanaeleza kuwa utaratibu na uwazi ni dhana zinazokaribiana sana. Bila kuwa na uwazi ni vigumu kuwa na utaratibu na kinyume chake.
Utaratibu ni kufanya jambo kwa mpangilio mzuri wenye kubainika na aghalabu unaweza kuhusisha wakati, idadi, umuhimu na hata ukubwa.
Katika kushughulikia na kuelewa lugha mwanaisimu hujikuta akiwa na kazi ya kutimiza majukumu ya kueleza maana na asili ya lugha, kuchambua muundo wa lugha, kueleza uhusiano kati ya lugha na asasi nyingine za mwanadamu na kuibua nadharia mbalimbali za lugha.
Hizi ndizo sifa bainifu ambazo kwa mara nyingi hutuelekeza katika uwezo wa kutofautisha lugha zinazotumika katika kudumisha mawasiliano ya kila siku miongoni mwa wanajamii.
Umilisi (langue) ni ujuzi alionao mjua lugha kuhusu lugha yake. Ni ujuzi alio nao mjua lugha ambao upo katika ubongo wake. Ujuzi huo huhusu kanuni zinazotawala lugha hiyo husika.
Ujuzi huu humwezesha kutambua sentensi sahihi, zisizo sahihi na kupambanua sententi zenye utata. Ujuzi huo humwezeha kupuuza makosa ya kiutendaji katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, kukatisha sentensi n.k.(Rubanza, 2003).
Utendaji (parole) ni kile asemacho mjua lugha katika muktadha wa mawasiliano ikiwa ni pamoja na makosa ya kiutendaji ya bahati mbaya na yale ya kukusudiwa. Vilevile tunaweza kusema ni udhihirikaji wa ujuzi wa lugha alionao mjua lugha.
Uamilifu au utumizi (functionalism) ni elimu inayohusu muundo wa lugha kwa kurejelea kazi zake za kijamii katika mawasiliano.
Inamchukulia mtu binafsi kama kiumbe-jamii na kuchunguza namna anavyojifunza lugha na kuitumia katika mawasiliano na wanajamii wenzake.
Urasmi (formalism) ni elimu ya maumbo dhahania ya lugha na mahusiano yake ya ndani. Huzingatia maumbo ya lugha kama uthibitisho wa kimalimwengu bila kuzingatia namna jamii inavyowasiliana.
Uelezi ni mtazamo ambao huelezea ukweli wa lugha jinsi ilivyo na inavyotumika na jamiilugha husika. Na siyo namna inavyotakiwa kutumika.
Isimu elezi haiweki kanuni ngumu au sheria ngumu zozote zinazotokana na mawazo ya mtu juu ya lugha fulani bali huelezea lugha kwa kuangalia namna lugha hiyo inavyojidhihirisha yenyewe.
Huelezea sheria na kanuni ambazo mzungumzaji mzawa ameziweka kichwani na zinazoakisi uwezo wake wa lugha. Kwa kifupi, haielezi wala kuagiza namna mtu anavyotakiwa kutumia lugha bali namna lugha ilivyo na inavyotumika na wamilisi wa lugha hiyo.
Uelekezi ni mtazamo unaojaribu kuweka kanuni za usahihi wa namna watu wanavyotakiwa kutumia lugha.
Katika misingi hii, lugha rasmi hutumika pakubwa tunapokuwa waangalifu zaidi katika mazungumzo yetu.
Kadri uangalifu unavyozidi kudhihirika katika mazungumzo fulani ndivyo yanavyopata nafasi kubwa zaidi kutambuliwa kuwa rasmi. Mfumo rasmi wa lugha huzingatia matumizi ya mseto wa sentensi changamano na sahili zenye kuwasilisha maana kamilifu.
Kwa mujibu wa Joos (1961), lugha rasmi haina madakizo au mapambo na aghalabu inahusishwa na kujitambulisha kwa wageni. Hujiepusha na urudiaji isipokuwa tu pale ambapo msisitizo unahitajika. Katika kukwepa udondoshaji, lugha rasmi huzingatia kanuni zote za kisarufi na usahihi.
Lugha rasmi ni aina ya mawasiliano yanayotumika katika mazungumzo na maandishi yaliyo rasmi kama vile kwenye mazingira ya afisini, mahakamani, uwasilishaji wa maazimio, maagizo, miongozo, nyaraka muhimu za kiserikali, hati za idara mbalimbali, matangazo ya kisheria au makala ya kitaaluma.
Katika matumizi ya lugha hii, usahili na ukweli wa mambo yanayojadiliwa ni kigezo muhimu sana kuzingatiwa. Mfumo wa lugha unaotumika katika matini ya kisheria kwa mfano, ni ule unaosisitiza kabisa usahili wa lugha ili kujaribu kuzuia ufafanuzi unaogongana na sheria hizo.
Aidha, mawasiliano katika shughuli rasmi hayafanywi ovyo tu bila ya kufuata mpangilio maalum wa matukio. Badala yake, huzingatia mtiririko maalum unaokusudia kuleta ukamilifu wa maana.
Lugha huhusisha matumizi ya zana za kiisimu zinazofanana au kulingana katika kuelezea mambo. Mathalan, tuandikapo barua za kiafisi, aghalabu tunajikuta tukitumia ‘klishe’ zilezile zilizokwisha kushamiri katika mawasiliano mengi ya namna hii. Fomu za kujazwa na wahusika ni mfano mzuri zaidi.
Mazungumzo yoyote rasmi hupangwa kabla ya kuwasilishwa ili kuepuka uradidi na urejeshi mwingi. Ni mpangilio huu wa hali ya juu ndio unaoipa lugha hii jina lake.
Kuna matumizi ya istilahi maalum zinazohusu masuala ya afisini au kidiplomasia. Aidha, vyeo au nyadhifa za wahusika mbalimbali hutajwa. Huzingatia uwazi kwa kuepuka matumizi ya misimu, nahau, mafumbo au lahaja.
Kwa ujumla, lugha rasmi ni namna ya mawasiliano katika nyanja za utawala, uendeshaji wa uongozi pamoja na masuala ya kisheria. Mawasiliano haya yanaweza kutekelezwa ama kwa njia ya maandishi au mazungumzo.
Matumizi ya viungo au miondoko ya mwili pia ni mbinu ya mawasiliano iliyo na viwango vyake vya urasmi.
Kwa mfano, katika mahojiano kwa minajili ya kutafuta ajira, matumizi fulani ya viungo vya mwili yanaweza kumdhihirisha msailiwa kama asiyependezwa na kazi hiyo, asiye mwaminifu, aliye na mtazamo hasi, asiye msikivu au aliye na wasiwasi au kiasi fulani cha aibu.
Matumizi ya lugha rasmi aghalabu hutegemea matukio, wakati, idadi ya walengwa, uhusiano baina ya mzungumzaji au mwandishi na hadhira yake pamoja na uwezekano wa habari kuwa za kibinafsi au kwa ajili ya umma.