NADHARIA ZA KIJAMII - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Nadharia mbalimbali (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=14) +--- Thread: NADHARIA ZA KIJAMII (/showthread.php?tid=853) |
NADHARIA ZA KIJAMII - MwlMaeda - 08-16-2021 2.0 Utangulizi Sehemu hii inashughulika na kueleza nadharia za kijamii ambazo hutumika katika kuelewa uhusiano mbalimbali katika jamii. Nadharia hizi zinasaidia kuelewa wazi swala la lugha na jamii.
2.1 Madhumuni
Mpaka mwisho wa somo hili utaweza kutimiza yafuatayo:
1. Kueleza nadharia za kijamii.
2. Kuonesha jinsi nadharia hizo zinavyoingiliana na swala la lugha.
2.2 Nadharia za Kiisimu
Ili kuzingatia sehemu ya kijamii iliyo katika taaluma ya isimujamii, ni muhimu kuelewa mitazamo mbalimbali inayotumiwa kuchunguza jamii za wanadamu.
Katika sosholojia kunazo nadharia tatu kuu zinazoielezea jamii. Kuelewa lugha katika jamii kunahitaji pia kuzielewa nadharia hizi za kijamii. Katika mada hii tutazijadili nadharia mbili za mwnzo kati ya hizi tatu. Nadharia hizo tatu ni:
(a) Uamilifu (functionalism)
(b) Umaksi (marxism)
© Muingiliano (interaction)
2.2.1 Uamilifu
Hii ni nadharia iliyoibuka kati ya miaka ya arobaini na sitini (1940 s and 1960 s). Inaeleza kuwa jamii inaweza kuchukuliwa kama mfumo ulio na sehemu zenye uamilifu. Ili
kuelewa sehemu yo yote ya jamii (kama familia au shule), lazima sehemu hiyo ichunguzwe
kwa kuangalia uhusiano wake na jamii nzima. Kama vile mwanabiolojia anavyochunguza mchango
wa moyo katika kuendeleza maisha ya binadamu ndivyo sehemu ya jamii inavyochunguzwa kulingana na mchango wake katika kuendeleza mfumo wa kijamii. Mfumo wa
kijamii unayo mahitaji fulani ambayo yanahitaji kutekelezwa ili jamii idumu. Mahitaji haya ni
pamoja na chakula, mavazi na malazi. Uamilifu wa sehemu yo yote ya jamii
ni ule mchango wake katika kuendeleza na kuimarisha jamii hiyo
kwa jumla. Hii ina maana kwamba kuna kiwango fulani cha muingiliano kati ya
sehemu zote ambazo huunda jamii. Wanauamilifu wanadai
kuwa utaratibu na uimarikaji ambavyo huwa ni vitu muhimu vya kuendeleza
jamii hutokana na kuwepo kwa amali (za pamoja) sawa, yaani makubaliano
kuhusu mambo fulani katika jamii. Kutokana na mtazamo huu wanajamii
hushughulikia mifumo midogo ya kijamii na amali sawa zinazowaunganisha wanajamii.
Dhana zinazosisitizwa katika
nadharia hii ya elimujamii na ambazo ni muhimu kwa mwanaisimu
jamii ni pamoja na: utamaduni, ujamiishaji (socialisation), kaida, amali, hadhi na
majukumu/dhama. (i) UTAMADUNI
Utmduni hurejelea jinsi
jamii inavyoishi; yaani mkusanyiko wa mawazo na tabia wanazojifunza na
kupokeza kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Katika hali hii utamaduni ni
mpangilio wa jinsi watu wanavyoishi. Utamaduni unafafanua mambo yanayokubalika na
mfumo wa tabia katika jamii fulani. (ii) UJAMIISHAJI
Dhana hii inarejelea
njia ambazo kwazo watu hujifunza utamaduni wa jamii zao. Ujamiishaji wa
kimsingi au awali hutokea utotoni, aghalabu katika familia. Mahirimu au marika
(peer group) ni kukundi muhimu cha kuendeleza ujamiishaji. Marika humsaidia
kumkuza mtu kijamii na kiisimu. (iii) KAIDA NA AMALI
(a) KAIDA
Kaida ni mwongozo
maalumu wa jinsi ya kutenda mambo na kaida hueleza tabia zinazokubalika na zile
zinazofaa katika miktadha maalumu. Mifano ya kaida hizi inaonekana katika
mavazi ya shuleni, ya vijana,ya nyumbani, au ya dhifa mbalimbali. Katika hali ya ujamiishaji, kaida hufunzwa
kwa kutuza (kumpa mtoto peremende, maneno ya kusifia)
au kuadhibu. Baadhi ya kaida hufanywa kuwa sheria za
kutumikia umma wote. Kwa mfano, kukataza kuoga hadharani au wanawake kuhitajika
kufunika nyuso zao hadharani. (b) AMALI
Amali hutoa
miongozo ya kijumla ya mambo ambayo yanachukuliwa kuwa mazuri na
yenye thamani. Kwa mfano, katika jamii nyingi za kisasa, watu huthamini maisha
ya binadamu sana. Baadhi ya amali zinazopendekezwa ni umoja,uaminifu, upendo,
n.k.. Wanauamilifu wanaamini
kuwa ikiwa kaida hazitakubaliwa na kushirikishwa miongoni mwa
wanajamii, jamii haziwezi kushirikiana na kufanya kazi pamoja. Hivyo basi jamii
inahitaji kaida na amali za pamoja. Jambo hili limekuwa msingi wa tafiti nyingi za
isimujamii. (iv) HADHI NA MAJUKUMU
Hadhi hurejelea cheo cha mtu katika jamii (si lazima iwe kazi). Hadhi kama hizi
huenda zimerithiwa,
yaani mtu anapozaliwa anajipata ana hadhi fulani kwa mfano malkia au mfalme.
Anapoendelea kukua anajipata kuwa yeye ni mke au mume . Hadhi pia
huenda ikapatikana kutokana na juhudi za kibinafsi za mtu, kwa mfano, kujiendeleza
kitaaluma na kuwa mwalimu, daktari, mwanamichezo, n.k.
Kila hadhi
katika jamii huwa na idadi fulani ya kaida ambazo zinaeleza namna mtu aliye katika
hadhi hiyo anatakiwa kuendesha maisha yake. Kikundi hiki cha kaida huitwa
dhima au majukumu. Majukumu ya kijamii ndiyo huongoza tabia. Kufikia mwisho mwa siku, mtu huwa
ametekeleza majukumu mbalimbali: mwalimu (kazini), mama
au mke (nyumbani), mteja (benki), manju (kilabu cha starehe), n.k. Kila jukumu huhitaji tabia fulani
zizingatiwe, zikiwa ni pamoja na tabia za kiisimu. Kila jukumu la kijamii humfanya mtu achague
elementi fulani za kiisimu. Huku
akitekeleza majukumu yake atatumia lugha kwa njia tofauti tofauti.
Zoezi
Je, kwa maoni yako,
unafikiri nadharia ya uamilifu inajitokeza vipi katika jamii zetu na lugha
tunazozitumia? 2.2.2 UMAKSI
Umaksi unahusiana
na nadharia kadhaa. Tunapoongea kuhusu uhakiki wa ki- maksi, huwa tunairejelea mikabala mbalimbali ambayo misingi yake ni mawazo yanayohusishwa na Karl Marx na Friedrich Engels. Nadharia hii imepitia
mabadiliko makubwa tangu kuweko kwa wataalamu hawa. Umaksi unahusu nyanja mbalimbali kama uchumi, historia, jamii na mapinduzi. Umaksi una sifa ya kijumla inayojitokeza katika mwelekeo wake wa kuligusia kila eneo, na kuwa na la kusema kuhusu takriban kila kitu ikiwemo lugha. Mawazo ya
Karl Marx kuhusu historia na miundo ya kijamii yana nafasi kubwa katika nadharia hii. Umaksi ni falsafa yakinifu hasa kwa kuwa pana msisitizo mkubwa kwenye msingi wa hali za kiyakinifu za maisha kama mazingira ya kuishi kuliko mawazo katika maisha ya binadamu. Umaksi hauegemezi mfumo wake wa kifalsafa kwenye dhana dhahania kama urembo, ukweli au ndoto bali unayaegemeza kwenye uhalisi unaoonekana. Hebu
basi tuchunguze mawazo ya kimsingi ya nadharia hii: (1) Historia ya maisha
ya binadamu inaweza kuelezeka katika misingi yakinifu ya kiuchumi. Misingi hii
itachunguza njia za uzalishaji mali pamoja na miundo ya kiuchumi inayoathiri sio uzalishaji mali hiyo tu bali na usambazaji wake. Swala hili la uzalishaji mali na usambazaji wa mali hiyo linaunda kile ambacho hujulikana kama msingi au muundo msingi (base = infrastructure). Kwenye msingi huo ndiko kunakoegemezwa muundo wa juu au kikorombwezo (superstructure). Muundo wa juu ndio unaohusisha maadili, itikadi, dini, utamaduni ,n.k. Sifa za
muundo juu zinaathiriwa kwa kiasi kikubwa na muundo msingi. Hata hivyo mabadiliko yanayotokea katika muundo wa juu kama mageuzi katika muundo wa kiutawala huweza kuathiri muundo msingi. (2) Daima historia ya binadamu itadhihirisha au kuakisi
harakati zinazoendelea katika matabaka ya kiuchumi-jamii. Karl Maksi aliwahi kusema kuwa historia ya maisha ya binadamu ni ya harakati za kitabaka. Je, harakati hizi zinasababishwa na nini? Tunajua kuwa kitu cha msingi katika maisha ya binadamu ni kula na kunywa, kupata malazi na mavazi na mambo mengine. Tendo la
kwanza la kihistoria kwa hiyo, ni kutafuta njia ya kuyakidhi mahitaji haya ya kimsingi. Ili kufanikiwa katika lengo hilo, binadamu hulazimika kujiunga pamoja au kuunda umoja ili kuimarisha ubora na wepesi wa kuizalisha mali ya kukidhi mahitaji hayo. Muungano huo huwa na ugawaji wa majukumu au kazi ambayo ndiyo msingi wa kuundwa kwa matabaka katika jamii. Hatua ya juu ya mwendeleo huu ni ukuzaji wa mfumo wa ubepari. Katika mfumo huu, mali inamilikiwa na idadi ndogo ya watu. Watu hao wanaipata mali yao kutokana na unyonyaji wa umma na hasa wafanya kazi. Kumbuka
Zingatia maoni haya
katika muktadha wa lugha. Kwa mfano lugha- wenyeji na lugha za kigeni zilizopo hapa nchini. Kadiri mfumo
wa ubepari unavyoendelea ndivyo ubora wa uzalishaji maji unavyoongezeka na tofauti kati ya matabaka kuimarika kwa kuwa kuna watu wanaofaidika kwa njia zisizo za haki. Kufaidika huko kwa njia zisizo za haki, pamoja na mbegu za kujiangamiza zilizomo kwenye mfumo wa ubepari vinachangia kuuangusho mfumo wenyewe. Marx anaamini kuwa haya yanatokana na mfanyiko wa kiasilia wa kihistoria. Mfanyiko huo ni wa kipembuzi (dialectics). Kwa mujibu wa mawazo haya, historia huendelea kutokana na mfululizosafu wa mkinzano wa mawazo. Matokeo ya mkinzano huo ni kuzuka kwa hatua nyingine mpya ya kihistoria. Huu ndio msingi wa kile kinachoitwa upembuzi wa kiyakinifu (dialectical materialism). (3) Matamanio na
matakwa yaliyopo katika jamii na hasa tabaka lenye nguvu yanaakisiwa katika itikadi iliyopo katika jamii, jinsi na miundo ya mawazo ambayo aghalabu huwa imeshika kwa nguvu na huwapo kila mahala kiasi cha kuwa huenda wanajamii wasiitambue kwa haraka. (4) Njia ya kusaidia na
labda hata kuharakisha kuangamizwa kwa mfumo wa kibepari ni kudadisi, kukosoa, kushutumu, kulaumu na kufichua batili iliyopo katika itikadi ya kibwanyenye inayooimarisha ubepari. Dhana za kimsingi
zimeibuka katika nadharia hii: ukengeushi; ubidhaaishaji na itikadi. (i) Ukengeushi
(alienation): Ugawaji wa kazi unaishia kusababisha utengano fulani kati ya wanaohusika au binadamu. Hii ni hatua ya kimsingi ya ukengeushi . Mfumo wa kibepari unapoendelea kuboreka unasababisha hali ambapo uhusiano uliopo kati ya mfanya-kazi na tokeo la nguvu zake ni wa kitu kigeni (alien object). Watu wanaishia kukengeushwa na jamii yao kutokana na mfumo wa kiainisho (specialization) unaosisitizwa na kukuzwa na ubepari. (ii)
Ubidhaaishaji: Maksi anaitumia dhana ya bidhaa kukieleza au kukirejelea kitu kinachozalishwa sio kwa nia ya kutumiwa bali kubadilishwa katika mfumo wa kibepari wa soko. Bidhaa hizo hazitathaminiwi kutokana na kazi yake bali ni kutokana na bei zinazoweza kuvuta. Yaani msingi wa kuzitathmini sio thamani kimatumizi bali ni thamani kimabadilishano. Katika msingi huu, bidhaa zinaishia kuhusisha nguvu au kanuni fulani fiche ambazo huwavuta watu na kuwafanya wawe na mvuto mkubwa wa kukimiliki kitu fulani ambacho kinawasisimua. Huu ndio msingi wa kuabudu bidhaa (fetishism of commodities). Hii ni
sifa kuu katika mfumo wa kibepari na ni msingi wa uchumi wa kibidhaa ambapo watu husukumwa na kani za kununua na kumiliki vitu ambavyo labda hawavihitaji au wanavikinai haraka na kutamani vingine. Sifa hii ya ubidhaaishaji inaishia kuwahusu binadamu ambao hawathaminiwi kama binadamu ila kutokana na uwezo wao wa kuzalisha mali. (iii) Itikadi: Ni dhana
telezi, lakini kimsingi ni uwasilishi wa pamoja wa mawazo, fikira na tajriba hasa ikiwa vitalinganuliwa na uhalisia wa kiyakinifu vinakoegemezwa. Dhana hii
inaweza kufafanuliwa katika muktadha wa lugha pale ambapo watu wanaamini kuwa kuzungumza lugha ya mama ni dalili ya ushamba au kinyume chake kwamba kuzungumza lugha ya Kiingereza ni dalili ya kuwa mtu wa tabaka la juu. Zoezi
Kwa kuzingatia hali ya
lugha nchini Kenya, ni kwa njia gani nadharia ya Umaksi inaeleza hali hii (zingatia mvutano kati ya lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo za Kiafrika). Swali
Huku ukitumia nadharia
moja ya Elimujamii, onyesha namna lugha inavyoingiliana na jamii 2.4 HITIMISHO
Katika somo
hili tumejadili nadharia mbili za kijamii ambazo zitatusaidia kuelewa jamii. Nadharia hizi zitachangia katika kuelewa swala la lugha katika jamii. Marejeleo
Teule Eagleton, T. (1983)
Literary Theory: An Introduction. Oxford: Blackwell. Mesthrie, R.
et al (2001) Introducing Sociolinguistics, Edinberg,Edinberg Universtity Press.
Wamitila, K.W. (2002)Uhakiki wa fasihi: Misingi na Vipengele vyake. Nairobi. Phoenix Publishers Ltd. - - JoseZGR - 04-21-2022 Nadharia hulutishi / HYBRIDITY THEORY Iliasisiwa na Wanazuoni wa Kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni wamechangia sana katika kukuza taaluma ya FS ya Kiafrika. Miongoni mwa waasisi na wafuasi hawa ni pamoja na M.M.Mulokozi, Johson na Ngungi wa Thiong Katika nadharia zote zilizotangulia, wakiwemo wana nadharia za Kitaifa kulikuwa na changamoto mbalimbali. Hata hivyo, changamoto hizo zilitofautiana kutoka kundi moja la wananadharia hadi lingine. Kwa kuwa changamoto za nadharia nyingine zilikwisha jadiliwa, hapa tutajadili na kugusia tu zinazohusiana na nadharia za kitaifa |