Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SHAIRI: UCHAWI
#1
UCHAWI
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi,
Huko awako gizani, mbona ya Mana hayawi,
Pasi na nguo mwilini, lake baridi mchawi,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Mchawi hupenda tabu, hapendi mambo rahisi,
Kona anaziharibu, apite kwa wasiwasi,
Mlangoni hajaribu, apite kwa urahisi,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Yake kazi kuharibu, akageuza kizazi,
Ili unapojaribu, huoni chako kizazi,
Hapo hawana sababu, mambo yao ni ushenzi,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Japo yu mtu mkubwa, chamani kuheshimika,
Tabiaye kama mbwa, anapotaka kuruka,
Na baridi atakumbwa, hana nguo kujivika,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Juzi nilipata kesi, mtu katiwa kifafa,
Matabibu na manesi, wakadhani amekufa,
Mwisho katoa kamasi, tukagundua hajafa,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Mchawi akifahamu, una kitu kumzidi,
Jua umejipa sumu, kukuroga hana budi,
Utateswa kwa awamu, ukuishe ukaidi,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Msiwaone vichaa, kidhani yote ya Mumba,
Wengine tukashangaa, ovyo waanza kuimba,
Wachawi walishakaa, kuchanganya mitishamba,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Mtu umesoma sana, Mara vyeti huvioni,
Kumbe walishagawana, watandike kaburini,
Miaka kazi hauna, uchawi ni ushetani,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Machawi yake hasara, ulie yeye acheke,
Wala haimpi fora, hadharani asifike,
Kiumbe mwenye mikwara, japo asifaidike,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Mchawi mtu wa ila, mambo yake ni kinyume,
Usiku sie twalala, yu uchi atutazame,
Na hawi tajiri wala, kiwa wongo na aseme,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Sasa ninafunga beti, utungo siendelezi,
Msijenishika shati, ati nimewapa kazi,
Naona bora niketi, kuandika nimesizi,
Jamani niambieni, akipatapacho mchawi.

Mtunzi Filieda Sanga
Mama B
Mabibo Dsm
0753738704
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)