Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
YA KALE YA KUKUMBUKWA! UPAMBAUKAO HUTWA (KWAHERINI)
#1
YA KALE YA KUKUMBUKWA!
  UPAMBAUKAO HUTWA
         (KWAHERINI)

1. Upambaukao hutwa, na kutwapo huwa giza,
Mtana hupetwa petwa, ukanyang'anywa mwangaza,
          *Yaliza haya yaliza!*

2. Na sisi ule mtana, uliotupambauza,
Ulotupa kujuana, na mengi kuyafanyiza,
Leo waanza kununa, mitima kuiumiza,
          *Laliza hili laliza!*

3. Hikumbuka tangamano, vyema tulivyolikuza,
Mi nanyi 'kawa mfano, wa lulu katika chaza, 
Kisha leo saa hino, hiona twalikatiza,
            *Laniliza! Laniliza!*

4. Hikumbuka ukarimu, na wema wenu nduguza,
Jinsi mulivyonikimu, myaka saba hatimiza, 
Nahisi najidhulumu, Tanzania kuipeza,
          *Ndipo hamba laniliza*

5. Ingawa menilazimu, na nyinyi kujiambaza,
Yondokayo ni sehemu, sehemu najibakiza,
Moyo wangu umo humu, Tanzania 'tausaza,
          *Japo hivyo laniliza!*

6. Ni yangu matumaini, kwenu nayapendekeza,
Kwamba hwenda si jioni, nuru ingajipunguza,
Pengine wingu angani, ndilo lilojitandaza,
            *Litakoma kutuliza?*

7. Na iwapo si hakika, hili nilowaambiza,
Jambo moja liso shaka, tusoweza lipuuza,
Utwao hupambauka, hauwezi ukaiza,
          *Hapo halitatuliza.*

*ABDILATIF ABDALLA,*
*S.L.P. 35110,*
*DAR ES SALAAM.*
*SEPTEMBA 8, 1979.*

*NA KUCHAPO LITAKUCHWA*
( *KWA HERI YA KUONANA* )

1. Na kuchapo litakuchwa, likafungamana giza,
Na mchana ukaachwa, usiku ukajikweza,
Asubuhi ikafichwa, jioni ikatokeza,
  *Yasikulize nyamaza.*

2. Nyamaza yasikulize, tuombeane Muweza,
Mitima aitulize, mapenzi kutujaliza,
Kwako kwetu atujaze, ya heri kutueneza,
  *Usijilize nyamaza.*

3. Pia nasi kwa mfano, kwako tukielekeza,
Tuwazapo kongamano, kwenye yale mabaraza,
Kwenye mbinu kwenye ngano, machozi watwambukiza,
      *Ndipo nasema nyamaza.*

4. Sisahau umuhimu,  mengi umeniongoza,
Hasa kwa ile sehemu, diwani nilimaliza,
Ya mwenzetu marehemu, *Nyamaume* kuikuza,
    *Nyamaza bwana nyamaza.*

5. Kilio hiki si chako, ni changu unaniliza,
Na giza hili si lako, ni langu lanikwamiza,
Mayonzi haya si yako, ni yangu yaniumiza,
        *Ukilia waniliza.*

6. Kwa heri sisemi nenda, na siwezi kukataza,
Wendapo naona inda, nagubikizwa na kiza,
Nina nyang'anywa uwanda, uga gani nitacheza,
      *Hapo kulia nyamaza.*

7. Wendako usisahau, nyuma kututumbuiza,
Kwa salamu angalau, heba ukatuliwaza,
Wemao hatusahau, buriani nanyamaza,
    *Wacha kulia nyamaza.*

*SHAABAN C. GONGA,*
*S.L.P. 9031,*
*DAR ES  SALAAM.*
*09 - 09 - 1979.*

*USHAIRI HARIJOJO?*
1. Kwa isimuye Rabana, Muumba na Muumbule,
Aliyeumba mchana, usiku uufatile,
Naomba kwake auna,  nudhumu niipangile,
*Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?*

2. Ushairi wa maana, tulorithi kwa wakale,
Wenye mizani na vina, maudhui yatimile,
Urari, lugha mwanana, Kiswahili kiso ndwele,
*Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?*

3. Ushairi wenye taji, walotufunza wavyele,
Ulosheheni umbuji, na hekima teletele,
Si leo wa mfa maji, anayepiga kelele,
*Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?*

4. Beti nne kaditama, ukomo niufikile,
Mtima unaniuma, pingiti nizionile,
Zimetanda zinavuma, ni shangwe vigelegele!
*Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?*

*KHAMIS S.M. MATAKA,*
*S.L.P 70249,*
*DAR ES SALAAM.*
*18 - 09 - 2003.*
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 2 Guest(s)