Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
KIMYA CHENYE KELELE NYINGI
#1
KIMYA CHENYE KELELE NYINGI
Akulumbale huwa hapendi kupuuzwa hata kidogo, kwa sababu hiyo,  alikata shauri la kurudi huko pasipojulikana .  Kwa hakika, kusikojulikana ndiko pahala waishipo watu wasiojulikana pia. Watu hao aghalabu huwa hawana sio tu anwani za makazi  lakini pia hata  majina yao hayatambuliki kiwepesi.
Hata hivyo,  pamoja na yote hayo, huko kusikojulikana ni tofauti kabisa na kule kimya, ambako huenda watu walioharibikiwa mambo yao.
Utasikia,  hivi bwana fulani siku hizi yuko wapi?  Iwapo bwana fulani mwenyewe anayezungumziwa  atakuwa ameharibikiwa na mambo yake, majibu huwa, '  bwana yule, yupo kimya ' ikisemwa hivyo mara nyingi huwa inaeleweka kuwa,  ingawa mambo ya huyo bwana fulani yapo msegemnege lakini uhakika uliyopo  ni kwamba, walau  huko aliko yuko hai.
Hii ni kinyume kabisa na kule kusikojulikana. Huko ikiachiliwa mbali kutojulikana kwake na kwenda bila utayari wala hiyari hakuna kikingine kinachojulikana na wengi.
Ni muhimu kufahamu kuwa,  si kila mtu aliyeharibikiwa ama kuharibiwa mambo yake huchagua kwenda huko kimya.  Kuchagua kuishi huko hutegemea ubora wa ama busara na hekima au silka na hulka zilizomkuza mtu mwenyewe.
Jambo muhimu kuliko yote katika muktadha huu,  ni kule kuweza kung'amua nyakati za mapito ya kimaisha ya mwanadamu. 
Hivyo, ni muhimu kabisa kujua, ni wakati gani  mtu aende huko kimya na muda gani achague kwenda pasipojulikana kama itaonekana inafaa.
Akichagua kwenda kimya huenda akavikwa nguo upya siku za usoni. Hata hivyo,  uamuzi wowote baina ya hiyari hizi mbili ni mgumu.  Ingawa ni bora katika mazingira fulani kupoteza pua ili kuulinda wajihi. Kwani! Kama hapana budi lisilobudi hufanywa! Uamuzi wa mithili hii ndiyo hasa huitwa uamuzi wa kukata jongoo kwa meno.  Wakati fulani kimya ni kelele lakini si kila kiza ni shari.
Si budi kuzipima vizuri nyakati ili ifanyike itihari sahihi ya mtindo wa maisha kwa kuzingatia mazingira ya wakati unaohusika. Hata kiza si shari tupu na si kila kilichopinda ni kibaya.
soma_useme
********
A. A. Majid Mswahili
Chang'ombe,  Kisarawe_ Pwani
Usipitwe na Hadithi Fupi kwa Ufupi za Majid Mswahili,  kuanzia Februari Mosi, 2022, In Shaa Allah.
Anuanipepe: majidkiswahili@gmail.com
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)