MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.

SHAIRI: “YALIYOPITA YAMEPITA” NA MATHIAS MNYAMPALA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SHAIRI: “YALIYOPITA YAMEPITA” NA MATHIAS MNYAMPALA
#1
TUJIKUMBUSHE KALE YETU
Mathias Eugen Mnyampala, mmoja wa washairi maarufu na wa daraja la juu katika ulimwengu wa Kiswahili alitunga shairi liitwalo “YALOPITA YAMEPITA”. Shairi hili alilitunga baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 akiwa na nia ya kuwaasa washairi wa wakati wake kukomesha magombano na mivutano yao ya kishairi na badala yake watunge tungo aali zenye kuadilisha jamii (ikumbukwe kuwa miaka ya kabla ya uhuru malumbano ya washairi yalishitadi sana hadi kufikia hatua ya kuwagawa washairi katika makundi). Katika shairi hilo tunamuona Mathias Mnyampala akiwataja washairi bulibuli kama ilivyo desturi ya washairi kuzinduana na kuhamasishana kwa kutajana majina (kumbe jadi hii ya kutajana majina ndani ya tungo hatuianzi siye wa zama hizi). Katika shairi hilo Mnyampala alisema:
Hapana cha upinzani, cha ugomvi na matata
Watunzi na ubishani, vile watunzi kuteta
Sasa wanayo imani, umoja wamefumbata
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Ya uhuru yatungeni, ya ugomvi yamepita
Tanganyika ni amani, nchi haina salata
Washairi unganeni, na utunzi kutakata
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Bwana Gonga muhisani, mtunzi mwenye kunata
Khamisi bini Amani, mwenye tungo za kutata
Ugomvi jama acheni, tungeni ya kumemeta
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Msanifu Makarani, mwenye tungo za kuvuta
Bwana Miraji rubani, mtunzi usiyesita
Pia na Makwayasoni, mtunzi mwenye mafuta
Ya ugomvi tuacheni, na tutunge ya uhuru
Bwana Juma Ujijini, na Adamu nawaita
Mheshimiwa wa dini, Sheikh Amri Kaluta
Wambieni suluhuni, madaraka tumepata
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Nawe Bwana Damiani, shauri hili kamata
Na kule Magharibini, ni Idrissa kakita
Waaseni ya uhuni, waungwana kutafuta
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Mandevu wa Buguruni, na Shaha wanaye Chata
Kazimoto na Imani, Kiwato na Chamatata
Tanganyika tukuzeni, kiwango tumekigota
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Mwaruka na Selemani, waacheni kuwasuta
Na Palla wa Uteteni, Bini Mchuchuli Sheta
Na adui pendaneni, hata kama ni msuta
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Shinyanga ni Khalfani, fundi kucheza karata
Na Unguja kisiwani, washairi bora sita
Kwa umoja shikaneni, pamoja kujipakata
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Tama Bwana Shaabani, na Saidi msojuta
Mahamudu Hamduni, na Snow mwenye kuseta
Nawe Bwana Saadani, na kurumbiza fuata
Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru
Shime washairi wa leo tushike busara na hekima iliyomo ndani ya shairi hilo la Sheikh Mathias Mnyampala kwani shairi lake limehifadhi mafunzo yenye adili yasiyochujuka kwa zama zote
Hassan R. Hassan
Chuo Kikuu cha Dodoma
**Wakatabahu**
Mwl Maeda
Reply

Forum Jump:

Users browsing this thread: 1 Guest(s)