Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SHAABAN ROBERT…..KUSADIKIKA
#1
SHAABAN ROBERT…….KUSADIKIKA

“…Magharibi ni machweo ya jua na mwezi. Pia ni upande wa dunia wenye giza limezalo nuru zote na ufupishao uoni wa macho. Auni aliyakabili mashaka haya akafanya safari kubwa sana. Baada ya miezi Mingi kupita, siku moja alikutana na vipofu wawili njiani. Vipofu hawa wote walikuwa wanaume. Kipofu mmoja alikuwa mbele na wa pili nyuma. Uso wa kipofu wa kwanza ulikuwa na furaha kama uso wa bwana arusi, akaonekana kama aliyeridhika kabisa. Lakini uso wa kipofu wa pili ulikuwa umeghadhibika na kinywa chake kilijaa manung’uniko mengi kama aliyekuwa hakuridhika hata kidogo. Kila hatua aliyokwenda alibwata akailaani bahati yake. Auni alishangaa sana kwa kuona vile, akasema moyoni mwake kuwa watu hawa wana vilema namna moja, lakini mmoja amekinai na mwingine hakukinai. Ajabu kubwa iliooje hii! Afadhali niulize ili nielewe sababu yake. Baada ya kukusudia hivyo alitamka, “Mabwana, nyinyi ni kina nani, na asili ya upofu wenu ni nini?”
Kipofu wa pili alijibu, “Bwana wangu mwema, mimi naitwa Sapa na mwenzangu ni Salihi. Salihi haombi neno akalikosa. Ameishi maisha haya tangu ujana wake, lakini vitu alivyovipata kwa maombi aliyoyafanya alikuwa hana matumizi navyo. Nilipoona hivyo nilimwambia kuwa niliota ndoto kuwa akiomba kitu chochote tena bila ya kugawana na mimi sawasawa, dua lake halitapokewa hata kidogo. Kwa sababu hii tuliafikiana kushirikiana kila kitu atakachokiomba tukaandikiana hati mbele ya kadhi. Hati ya mkataba wetu ilipokwisha andikwa nilifurahi sana kuwa shauri langu limefaulu, lakini palepale mwenzangu aliinua mikono yake juu akaomba upofu, na kabla sijatanabahi, sisi sote wawili tulikuwa vipofu. Kama yeye anaipenda hali hii, mimi naichukia kabisa. Nilidhani ataomba niwe mfalme nizungukwe na mawaziri na kuheshimiwa na raia, au niwe tajiri ili niwatumie maskini kama nguo mbovu. Fahari ya mambo haya ndiyo iliyonishawishi kufanyiza mkataba na Salihi. Kama angalikataa kushirikiana na mimi katika fahari hii, pasingalikuwa na dawa yoyote kwa sababu nilimdhihaki tu. Sina haja ya upofu huu. Nimemsihi sana aombe nirudi katika hali yangu ya zamani lakini hakubali. Tafadhali nisaidie kumnasihi, bwana.”
Kabla Auni hajalijua neno la kutumia, Salihi alisema, “Mimi naapa kuwa sikujua kama Sapa alitamani ufalme au utajiri wakati aliponiagulia ndoto yake. Laiti ningalijua nia yake ilivyokuwa, hili lisingalitokea. Ningaliomba madua mawili mbalimbali, yaani, moja langu na jingine lake na kila mmoja katika sisi angalipata haja yake. Nilipoona mambo ya dunia yamenichukiza, nilidhani kuwa na mwenzangu yamemchukiza vile vile, na kwa mujibu wa mapatano yetu nikaomba upofu ili tuishi  bila kuyaona tena. Madhali neno nililoliomba nimelipata, wajibu wangu sasa ni kushukuru. Haiwezekani kuomba niyaone tena mambo niliyoyakataa. Nikifanya hivyo, nitafanana na ng’ombe anayeutia ulimi wake puani na kuurudisha tena kinywani. Si laiki ya mwanadamu kuwa kama ng’ombe kwa neno alilolichagua kwa hiari yake mwenyewe…….”
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)