MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
ODC : MUHADHARA WA KUMI NA TISA: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
ODC : MUHADHARA WA KUMI NA TISA: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI
#1
ODC : MUHADHARA WA KUMI NA TISA: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI
19.1 Utangulizi
19.2 Mhakiki ni nani?
Mhakiki ni mchambuzi na mfafanuzi wa maandishi ya sanaa hasa yale ya kifasihi. Ni jicho la jamii kwa vile katika kazi za fasihi anagundua mazuri pamoja na hatari iliyomo. Huyu ni bingwa wa kusoma na kuchambua maudhui, maadili na ujumbe uliomo katika maandishi ya fasihi.
19.3 Sifa za Mhakiki
Mhakiki anatakiwa ajue historian ya mazingira yaliyomkuza mwandishi. Mhakiki ili aweze kuifanya kazi yake anapaswa aelewe vema historia ya mwandishi na jamii yake inayohusika. Aelewe asili ya mwandishi, historia yake na utamaduni wake kwa ujumla. Kutokana na hali hii, mhakiki anaweza kuelewa kama mwandishi amefanikiwa kueleza ukweli wa maisha ya watu yaani jamii inayohusika.
Mhakiki anatakiwa kuelewa histori na siasa ya jamii inayohusika. Hii itamwezesha kuyaelewa matatizo ya jamii hiyo. Mhakiki lazima aifahamu barabara jumuiya ambayo mwandishi aliandika juu yake ili aweze kuandika uhakiki imara, ama sivyo atakwama na kuandika uhakiki dhaifu. Mhakiki anapaswa kuelewa historia ya watu ambao maandishi yao hayo yanawahusu, bila kuifahamu historia yao, itakuwa vigumu kwake kueleza bayana baadhi ya mambo ambayo mwandishi aliandika na kwa nini aliandika hivyo. Uhakiki wake ukisomwa na watu wanaoishi katika jamii hiyo si ajabu kusema yeye si mhakiki. Mhakiki, huangalia jinsi gani mwandishi ameiwakilisha hali halisi ya jumuiya na historia ya watu hao.
Mhakiki ni muhimu awe amesoma kazi mbalimbali za fasihi na siyo ile tu anayoifanyia uhakiki. Hii itamsaidia kuwa na ujuzi zaidi katika uwanja wa uhakiki.
Mhakiki anatakiwa asome tabakiki za wahakiki wengine katika uwanja wa fasihi na hata nje ya jamii yake ili kupata upanuzi zaidi katika kazi ya uhakiki. Hii itamsaidia kutoa tahakiki bora zaidi kwani atakuwa amejifunza yale yaliyo mazuri na kuepuka makosa waliyofanya wengine.
Mhakiki lazima awe na akili pevu sana ili aweze kung’amua mambo na akishayang’amua ayaandike kwa lugha rahisi ili mawazo yake yasomeke na kila mtu kwa urahisi, yaani atumie lugha ambayo itawatumika wasomaji wake.
 
Mhakiki lazima ajiendeleze katika taaluma mbalimbali ili aweze  kuwa na mawazo mengi ambayo yatamsaidia kuhakiki maandishi mbalimbali.Mhakiki hodari huichonga jamii yake kimawazo. Huiimarisha isitetereshwe au kupofushwa na waandishi wapotoshi.
 
Mhakiki anapaswa kuwa na uwezo wa kuchambua mambo kisayansi bila kutonesha hisia za wasomaji. Asiwe na majivuno na awaheshimu anaowahakiki na anaotaka wasome uhakiki wake, asichukie au kusifia tu kazi za waandishi kwa sababu zake binafsi bila kueleza ukweli wa kazi hiyo. Mhakiki ni rafiki wa mwandishi na wasomaji. Kwa hiyo, mhakiki lazima awe fudi katika kutoa hoja zake na lazima ziwe zinagonga, zenye kuibua udadisi na kuathiri.
Mhakiki anapaswa asiwe mtu wa kuyumbishwa na maandishi au maeneo ya wahakiki au watu wengine. Tunategemea asme kweli kuhusu kazi hiyo. Mahusiano baina ya mhakiki na mwandishi yasiathiri uhakiki wake.
Mhakiki anapaswa awe na uwezo wa kutumia mkabala sahihi kulingana na kazi anayoifanyia uhakiki. Mikabala humwongoza mhakiki kuchambua vema kazi za fasihi.
19.4 Dhima za Mhakiki
 
Kuchambua na kuweka wazi funzo linalotolewa na kazi ya fasihi. Hapa mhakiki anatoa ufafanuzi wa kimaudhui wa kazi ya  fasihi. Mhakiki husoma kwa uangalifu kazi ya fasihi, baada ya kusoma kwa makini, hutafakari na kuchunguza maudhui, Maadili , na ujumbe ambao mwandishi amekusudia kuwafikishia wasomaji wake na jamii inayohusika.
Kuchambua na kufafanua picha za kisanii zilizotumika katika kazi ya fasihi. Mhakiki huwasaidia wasomaji ili wasishindwe kuyaelewa maudhui barabara kutokana na kukakanganywa na usanii, matumizi, mathalani ya Ishara na baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kumkanganya msomaji ambaye hajapata utaalamu mkubwa wa kuchambua. Mhakiki kwa kufichua ishara Fulani ina maana kuwa amemsaida msomaji kupata ujumbe kikamilifu.
Kuhusu matumizi ya picha, kwa kawaida, lugha ya picha ina mguso sana na huibua hisia aina na hata kuchekesha au kuwafanya watu walie machozi. Mhakiki sharti awambie kwamba, matumizi ya picha ni mbunu mojawapo inayosaidia maudhui kuwaganda wasomaji. Picha inayochekesha, kufurahisha, kukejeli n.k. haikomei pale tu kwani baada ya kucheka n.k. msomaji huathiriwa sana kinafsia na aghalabu huachiwa funzo fulani. Hivyo mhakiki lazima achambue na kuiweka wazi funzo ambalo linatolewa na picha hiyo.
Mhakiki ana dhima ya kumshauri mwandishi ili afanye kazi bora zaidi. Mhakiki anamfundisha mwandishi juu ya yale anayoyasema yanavyoweza kupokelewa na jamii. Humwonesha msanii uzuri na udhaifu wa kazi aliyosaini kitendo hiki humfanya anavyoelekezwa na mhakiki, na hivyo humfanya awe na nafasi nzuri ya kuirekebisha kazi hiyo atakapoishulikia kazi nyingine. Kwa msingi huo mhakiki anaweza kulaumu au kusifu/ kumpongeza mwandishi wa kazi yoyoe ya kisanaa.
 
Mhakiki ana dhima ya kumwelekeza msomaji ili apate faida zaidi kuliko yale ambayo angeweza kuyapata bila dira ya mhakiki. Mhakiki huifunza jamii (wasomaji) namna ya kupokea na kuifurahia kazi ya sanaa. Vilevile mhakiki huwasaidia wasomaji kuyabaini maandishi yaliyo sumu kwa jamii. Mhakiki lazima ayafichue maandishi hayo ili yasieneze sumu kwa jamii inayohusika.
 
Mhakiki ni kiungo muhimu kati ya jamii na msanii. Mhakiki ndiye anayeitambulisha na kuelezea kazi ya msanii kwa hadhira. Vile vile mhakiki huchukua mawazo ya wasomaji na kuyapeleka kwa mwandishi. Humtahadharisha msanii kuhusu makosa aliyoyafanya katika kuikabili kazi yake na wakati huo huo anaionesha jamii udhaifu uliomo katika kazi hiyo ya fasihi.
Mhakiki ana dhima ya kukuza kiwango cha utunzi na usomaji wa kazi ya fasihi. Kutokana na ushauri anaoupata mwandishi kutoka kwa mhakiki, humfanya awe makini zaidi wakati wa kushughulikia kazi nyingine. Vile vile wasomaji wanakuza kiwango chao cha usomaji kwa kufuata mawaida ya mhakiki.
Mhakiki ana dhima ya kusema wazi kuhusu kiwango cha maandishi anayoyahakiki.Akisema wazi kwamba maandishi hayo yako katika kiwango cha chini, mara mwandishi huyo asilia atakapoamua kutunga tena, atashawishika kuandika maandishi yaliyo kwenye kiwango cha juu zaidi. Na waandishi wengine watapatiwa msukumo wa kuandika maandishi yaliyo kwenye kiwango cha juu pia. Na hivi ndivyo mhakiki anavyosaidia kukuza na kuendeleza maandishi ya taifa lake.
Mhakiki ana dhima ya kumsaidia msomaji kuyabaini maandishi yaliyosumu kwa jamii. Mhakiki sharti aseme wazi ayafichue maandishi ya namna hiyo. Kuna maandishi ambayo huwachekesha na kuwaburudisha wasomaji sababu yameandikwa kwa namna hiyo, na kumbe yaneneza sumu, na maandishi haya yanazorotesha maendeleo ya jamii, hivyo mhakiki huyafichua maandishi kama haya.
 
Mwisho, mhakiki anatakiwa kuheshimu na kuthamini kazi za waandishi na kuzifanyia haki. Jambo la msingi (lazima) kuzingatia ni kwa mhakiki afayapo kazi yake huwa vitani. Mhakiki anapaswa kujua namna ya kuwanasa wasomaji bila wao kujitambua na kuwa na uwezo au kuchambua kisayansi mambo bila kutonesha hisia za wasomaji. Anatakiwa asiwe na majivuno na aheshimu anaowahakiki na anaowataka wasome uhakiki wake, awachukue hatu kwa hatua kifalsafa hata waone vigumu, na haiwezekani kupingana naye.
 
Kwa kuhitimisha, mhakiki ni mtu muhimu sana katika kazi za fasihi. Kazi ya sanaa ya uandishi ni kama chakula kilichokwishapikwa na kuungwa vizuri. Uhakiki ni sehemu mbalimbali za ulimi zenye kuifanya jamii ikubali utamu wa chakula hicho; uchungu au ukali wa chakula hicho na igundue uchungu wa chakula hicho au ukali wake.
19.5  Uhakiki wa Fasihi
Nkwera (2003) amechunguza na kuona kwamba mara nyingine mhakiki hulazimika kulinganisha kazi za kifasihi. Kazi hizo zinaweza kuwa zinafanana au zinatofautiana. Ulinganisho huo utazingatia vipengele vyote vya fani na maudhui. Mhakiki anatazamiwa aone ubora au upungufu katika kazi na jinsi zinavyozidiana.
Vigezo vinavyotumiwa katika kulinganisha kazi za fasihi ni vile vile vya ukweli, uhalisi na umuhimu. Vigezo hivyo vitapima dhamira, ujumbe, falsafa, wahusika na matumizi ya lugha.
Uhakiki wa kazi za fasihi unajumuisha kuzingatia kazi hiyo kwa kuisikiliza au kuisoma; kuchambua vipengele vya fani na maudhui vinavyoijenga kazi hiyo. Hatimaye mhakiki atatoa maoni kuhusu ubora au ubaya wa kazi hiyo na hukumu ya kazi ipi bora kuliko nyingine.
VIPENGELE VYA UHAKIKI  1. MAUDHUI
  1. FANI
    • Uhakiki wa Maudhui
 
            Katika kuyahakiki maudhui ya fasihi, zingatia yafuatayo:
(i) Soma na uielewe habari nzima, kisha uieleze kwa muhtasari.
(ii) Itambulishe hadhira au wazo kuu la mchezo husika kwa sentensi mbili au tatu.
(iii)Onesha mapendekezo au mawaidha ya mwandishi, msimamo na mtizamo wake wa mambo kutokana na mchezo huo.
(iv) Chunguza falsafa ya maisha ambayo mwandishi anaielezea: k.m. Je, mwandishi anaelezea hali halisi ya maisha au ni nadharia tu za uchawi au ni maisha ya njozi yasiyo na ukweli ndani yake?, nk.
(v) Ainisha matatizo na migogoro inayojitokeza katika mchezo huo na sababu zake.
(vi) Mtambulishe mhusika mkuu katika mchezo mzima.
(vii) Onesha njia/mbinu zilizotumika ili kumuinua au kumuangusha mhusika mkuu.
(viii)Onesha njia/mbinu zilizotumika ili kuyakabili na kuyatatua matatizo hayo na migogoro iliyojitokeza katika mchezo huo.
(ix)Onesha majibu/matokeo ya juhudi zote alizotumia mwandishi ili kulikabili suala au tatizo linalozungumziwa katika mchezo huo.
(x)Fanya tathmini ya kupima kama mwandishi amefanikiwa, katika maelezo yake, kulifikisha lengo alilokusudia kwa hadhira lengwa.
(xi)Na kama hakufanikiwa kulifikisha lengo lake kwa hadhira husika, eleza kwa nini kashindwa.
19.5.2  Uhakiki wa Fani: Wahusika
Uhakiki wa Fani Wahusika unatakiwa ushughulikiwe kwa kuzingatia na kuchunguza mambo mawili makubwa:
  • Wahusika
Yuko mhusika mkuu au wako wahusika wakuu.
Mhusika mkuu au wahusika wakuu hutambulishwa kwa maswali matatu:
(a)Hadithi imejengwa juu ya nini?
(b) Je, mhusika huyo hutokea mara nyingi akitenda mambo, kuongea au kuzungumziwa na wahusika wenzake?
 © Je, mhusika anatoa uamuzi unaofikisha mchezo kwenye kilele au upeo wa weledi wa hadhira yake?
Wahusika wadogo nao huunda makundi matatu:
(a)  Wahusika wadogo walio maarufu au muhimu.
(b) Wahusika wadogo walio maarufu kidogo.
©Wahusika-Wadogo wanaofanya mazingira katika mchezo   ambayo yanamsukuma Mhusika-Mkuu aamue au asiamue jambo kama alivyokusudia hapo awali.
Jinsi wahusika walivyoundwa na kulelewa mambo muhimu ya kuchunguza katika kipengele hiki ni:
 (a) Sura, tabia, kazi zao maishani katika jamii, na katika mchezo.
 (b) Uhusiano wao katika Jamii:
  • Je, wanaendelezana kimaisha, au kila mmoja kivyake?
  • Je, wanagongana kitabaka, kifikra, kiuchumi, kielimu, nk?
  • Je, wanasadikika na kupokeleka na jamii yao, au na hadhira kwa jumla?
19.5.3    Uhakiki wa Fani: Muundo
Kipengele hiki kinachunguza jinsi mchezo wenyewe ulivyotengenezwa. Maswali ya kujiuliza ni haya:
(a) Mwanzo wa mchezo ni wapi na unakomea wapi?
(b) Kilele cha mchezo ki wapi; kimeanzia na kuishia wapi?
© Sehemu za mchezo ni zipi? Yaani mchezo una vitendo vingapi (sehemu ngapi) na maonesho mangapi?
(d)Ni mandhari gani yaani sura ya mahali na mzingira ya wakati yanasawiriwa katika mchezo?
19.5.4  Uhakiki wa Sanaa: Kufaulu Kwa Mtunzi
Uamuzi wa kwamba mtunzi amefaulu ama hakufaulu katika utunzi wa mchezo wake, hatuna budi kuchunguza au kujiuliza mambo yafuatayo kuhusu sanaa aliyoitumia katika mchezo wake.
(a) Je, lugha aliyoitumia mwandishi ni fasaha, (yaani ni lugha sahihi kisarufi, na ni rahisi kueleweka kwa watu wengi waliokusudiwa wauelewe mchezo wake?
(b) Je, viashiria au ishara na mifano iliyotumika ili kulijenga wazo kuu; kuunda visa, mazingira ya wakati na mahali; kubainisha ukale dhidi ya usasa (mapinduzi); nk. yamechangia kufanikisha azma ya mchezo?
© Je, ukubwa wa hadhira au jamii inayoweza kufikiwa na ujumbe wa mchezo na ikauelewa fika na kuathirika nao vibaya au vizuri, unaridhisha?
 (d) Je, maudhui yatokanayo na mchezo huu yanatoa jawabu au suluhisho la kufaa kuhusu migogoro inayojitokeza katika jamii hiyo?  Je, yanachochea zaidi vurugu akilini  kuhusu mgogoro uliopo?
(e) Je, semi zimetumiwa katika mchezo ili kusisitiza au kukejeli mambo yanayosadikiwa na kufuatwa kama kanuni au desturi katika jamii?
(f) Je, suala linalojadiliwa linawagusa watu wa kiwango gani kielimu katika jamii hiyo?
(g) Je, suala la wachache katika jamii, yaani ni tabaka dogo tu la watu?
(h) Je, suala la watu wengi katika jamii, yaani ni tabaka kubwa la watu?
(i)  Je, suala la watu wote katika jamii?
(j)  Je, suala linalojadiliwa lina umuhimu gani kwa jamii kwa wakati huu?
(k) Je, mwandishi amewatumia wahusika wake ipasavyo katika kuliweka bayana wazo kuu kwa hadhira husika, na uwe mfano bora kwa hadhira kuwaiga au kutowaiga kwa vile alivyowamulikia kwa undani maisha yao kwa vitendo na maneno yasemwayo mchezoni?
19.5.5 Uhakiki wa Kichwa cha Mchezo
Kichwa cha mchezo ni kama nembo. Kwa hiyo, nacho pia inafaa kihakikiwe. Maswali ya kujiuliza kuihusu ni kama ifuatavyo:
(a)   Je, kichwa kilichowekwa kweli kinawakilisha wazo kuu, au
         kiini cha habari?
(b) Je, ni wazo mojawapo tu linalojitokeza katika mchezo huu katika jumla ya mawazo?  au
© Ni neno tu la kuamsha udadisi wa msomaji na labda la kuwavutia wanunuzi wa kitabu chake?

Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)