Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
NAFASI YA VYAMA NA TAASISI MBALIMBALI KATIKA MAKUZI YA KISWAHILI
#1
NAFASI YA VYAMA NA TAASISI MBALIMBALI KATIKA MAKUZI YA KISWAHILI 

Kwa Mukhtasari

IKIWA idara ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), awali
ikiitwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ni miongoni mwa taasisi kongwe
zaidi za lugha nchini Tanzania na Afrika Mashariki. Madhumuni yake ni kusimamia
usanifishaji na maendeleo ya Kiswahili.

Japo Kiswahili
kimeendelea kubaki nembo ya Afrika, mjadala usio na mwisho kuhusiana na ni ipi
lugha ya kufundishia katika shule na vyuo nchini Tanzania ni ithibati kwamba
Kiswahili hakijapokezwa hadhi inayostahiki katika mengi ya mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati.

TUKI, kwa sasa TATAKI,
ilianzishwa mnamo 1930 ikijulikana kama International-Territorial Language
(Swahili) Committee kwa nchi tatu za Afrika Mashariki na baadaye ikaitwa Kamati
ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Mnamo 1964, kamati
ilifanywa kuwa sehemu ya UDSM na baadaye ikaitwa Chuo cha Uchunguzi wa
Kiswahili. Tangu 1970 kimepewa jina la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
(TUKI). Mwaka 2009, TUKI iliungana na iliyokuwa Idara ya Kiswahili ya UDSM na
kuunda taasisi kubwa zaidi inayoitwa TATAKI.

Majukumu ya taasisi hii
awali yalikuwa ni kutafiti nyanja zote za lugha ya Kiswahili, fasihi na
utamaduni na kuchapisha matokeo ya utafiti huo.

Hivyo pamoja na Baraza
la Kiswahili Tanzania (BAKITA), TUKI ni mlinzi wa usanifu wa lugha ya Kiswahili
katika Tanzania. Baada ya kuungana na Idara ya Kiswahili, sasa TATAKI
inafundisha Isimu, Fasihi na Historia ya Lugha ya Kiswahili.

Inafundisha Kiswahili
kama lugha ya pili hasa kwa wageni kutoka nje ya ulimwengu wa Waswahili na
kuendeleza utungaji wa kamusi mbalimbali zinazohusiana na Kiswahili.

BAKITA

Ni taasisi ya serikali
iliyoundwa kwa sheria ya Bunge Na.27 ya mwaka 1967 kwa madhumuni ya kukuza
Kiswahili. Kutokana na sheria hii, Baraza ndilo mratibu wa kusimamia asasi zote
na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

BAKITA imekuwa na
mchango mkubwa katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili kupitia
majukumu yake.

Miongoni mwa majukumu
ya Baraza hili kama yalivyofafanuliwa katika sheria hiyo ni kuratibu na
kusimamia maendeleo na matumizi ya Kiswahili nchini pamoja na kushirikiana na
vyombo vingine vinavyojihusisha na maendeleo ya Kiswahili.

Huhimiza matumizi ya
Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida, huandaa vipindi mbalimbali
redioni ili kuhimiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili, hushirikiana na
mamlaka zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi, hutoa huduma za
tafsiri na ukalimani kwa serikali, mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali
na asasi nyingine pamoja na kuidhinisha vitabu vya Kiswahili vitakavyotumika
shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa.

TAKILUKI

Taasisi ya Kiswahili na
Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa mnamo 1979 kwa lengo la kukuza na
kueneza Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar.

Inajishughulisha na
kuratibu, kuendesha mafunzo ya Kiswahili visiwani Zanzibar, kuhariri miswada
mbalimbali ili kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili na kufanya tafiti za Kiswahili
katika nyanja zake zote, hususan sarufi na fasihi.

TAKILUKI inatoa ushauri
wa kitaaluma kwa watunzi wa vitabu ili waweze kuandika kazi zenye ubora, na
kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili kuandaa na kuendesha semina, warsha
na kozi fupifupi za Kiswahili.

CHAUKIDU

Chama cha Ukuzaji wa
Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kina makao makuu katika Chuo Kikuu cha
Wisconsin-Madison, Marekani.

Madhumuni yake ni
kuwajumuisha pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea
kasi ya malengo mahususi kama vile kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo
lugha hii inatumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na
utafiti wa maarifa ya aina zote mathalan uandishi na utangazaji wa habari,
uandishi na uchapishaji wa vitabu na majarida pamoja na utayarishaji wa safari
za mafunzo katika Afrika Mashariki na Kati.

Husambaza habari na
matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali na teknolojia ya mtandao
wa kompyuta kuhusu vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana
na Kiswahili. CHAUKIDU inaelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia,
kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.

Vilevile inashauri ama
kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani
iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera mwafaka za kukiendeleza kadri ya
uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya serikali na watu wake kijamii, kisiasa,
kiuchumi, kiutamaduni na kielimu.

CHAWAKAMA

Chama cha Wanafunzi wa
Kiswahili katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA), kilianzishwa
mnamo 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo lote la Afrika
Mashariki kupitia kwa wanafunzi wanaosoma Kiswahili vyuoni.

Wanachama wa chama hiki
ni wale wanaosomea taaluma za Kiswahili ila wapenzi wa Kiswahili pia wanaweza
kujiunga nacho.

Mara kwa mara,
CHAWAKAMA huandaa makongamano kwa lengo la kuwapa wanachama nafasi ya kujadili,
kuimarisha, kuendeleza na kukuza vipawa vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili,
kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa Kiswahili, kueneza Kiswahili ndani na
nje ya nchi, kushirikiana na vyama vingine katika juhudi za kuendeleza na
kuimarisha Kiswahili ndani na nje ya nchi wanachama, kuwaunganisha wanafunzi wa
Kiswahili Afrika Mashariki na Kati katika kukikuza Kiswahili pamoja na
kushirikiana na asasi mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa
Kiswahili.

CHAKAMA

Chama cha Kiswahili
Afrika Mashariki (CHAKAMA) ndicho cha tatu kwa umaarufu zaidi miongoni mwa
wasomi, wataalamu na wahadhiri wa vyuo vikuu baada ya CHAUKIDU na Chama cha
Walimu wa Lugha za Kiafrika (ALTA) ambacho haundaa makongamano yake jijini
Bayreuth, Ujerumani.

Kwa pamoja na Chama cha
Kiswahili cha Taifa (CHAKITA), CHAKAMA huchapisha jarida la chama na machapisho
mengine ili kusaidia kueneza taaluma za Kiswahili.

Aidha, huhifadhi
kumbukumbu za wataalamu wa Kiswahili kwa nia ya kutumia katika kufanikisha
malengo ya chama na wadau wa Kiswahili pamoja na kuratibu makongamano na
mijadala mbalimbali inayohusiana na taaluma za Kiswahili.

Chama huandaa
makongamano kila mwaka ambalo linawakutanisha wanachama wote katika vyuo
mbalimbali katika nchi husika.

Katika makongamano
hayo, mada mbalimbali zinazohusu Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa
lakini pia maazimio mbalimbali huchukuliwa kuhusu maendeleo ya chama. Makala
mbalimbali huandikwa na kuchapishwa kwa minajili ya kusomwa na watu mbalimbali.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)