MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
SEMANTIKI NA PRAGMATIKI: TAALUMA YA MAANA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SEMANTIKI NA PRAGMATIKI: TAALUMA YA MAANA
#1
SEMANTIKI
NA PRAGMATIKI: TAALUMA YA MAANA
 
SEMANTIKI
 
Dhana ya Semantiki
Etimolojia ya neno semantiki inatokana na maneno mawili ya Kigiriki yenye maana ya “sema”= maana na “ticos” = ishara. Hivyo, semantiki ni ishara za maana ama zenye maana. Kiisimu semantiki ni taaluma inayohusika na maana katika tungo ama maana
za maneno.
      a) Semantiki hutafiti maana za fonimu, mofimu, maneno na tungo.
     b) Maana hushughulikiwa katika viwango vyote vya lugha, kama vile sauti, maneno na sentensi.
Maana ya maana
Hakuna jibu la mkato au jibu rahisi linaloelezea juu ya maana ya maana, dhana ya maana ni telezi, kutokana na utelezi huo wanaisimu mbalimbali wameeleza maana ya maana kama ifuatavyo.
1.     Maana kama dhana (Richard na wenzake, 1925) wanasema maana ni ile dhana na dhana hii ni ya msemaji yaani msemaji huwa na dhana fulani kabla hajasema.
Udhaifu: si rahisi kuwa na dhana inayofanana kati ya msemaji na msikilizaji. Baadhi ya maneno ya lugha hayana dhana mahususi hadi yatumike na maneno mangine.
Mfano: pia, na, kadhalika
2.     Maana kama mwitiko (Bloomfield na C. Morries) wanasema maana ni mwitiko wa msikilizaji. Wao wanatazama tabia ya binadamu anapoitikia neno fulani linavyotamkwa.
     Udhaifu: si rahisi wasikilizaji zaidi ya mmoja kuitika katika maana moja.
3.     Maana ni matumizi : Wanazuoni wa msimamo huu wanasema maana ya neno hutokana na matumizi yake katika mfumo wa lugha. Neno kama lilivyo halina maana kama haliko kwenye matumizi au muktadha. Maana ya neno inabadilika kulingana na muktadha.
Udhaifu: lugha inatazamwa kama kapu lenye maneno mengi yanayotumika kwa wakati mahususi na kuchukua maana kwa wakati huo. Kitu ambacho si kweli.
4. Maana ni kitaja/kiwakilishi/kirejelee majumui : Wanaisimu katika mtazamo huu wanasema maana ya neno ni kile kitu halisi kinachowakilisha kitu husika. Maana ya neno iwe katika kitu halisi kinachoweza kutambuliwa kupitia milango ya fahamu (kuona, kuonja, kunusa, kugusa, kushika). Wanazingatia
uhalisi wa umajumui au maisha. Dhima ya lugha ni kupambanua vitu mbalimbali katika ulimwengu unaomzunguka mtu.
     Udhaifu: kuna maneno yasiyowakilisha kitu katika mazingira yanayotuzunguka. Mathalani, kuwa, na, pia, katika, wa, n.k. kuna maneno yanarejelea vitaja zaidi ya kimoja.
5.     Fasili nyingine za maana ya maana
Kwa mujibu wa TUKI (1990: 39) wanasema maana ya maana ni fahiwa (sense) ya neno au kirai ama dhana, matumizi au kitajwa.
v Maana ni maelezo yanayotumiwa kukitambulisha au kukifafanua kitu
v Maana ni kusudio au dhamira ya mtu
v Maana ni ishara au dalili ya jambo
v Maana ni thamani, umuhimu au nafasi ya kitu au jambo fulani kwa mtu
v Maana ni sababu Katika mikabala yote hii hakuna mkabala unaojitosheleza lakini kila mmoja una ukweli ndani yake. Katika kufasili maana ya maana ni vyema kuunganisha mikabala hii ili kueleza vizuri maana ya maana.
Swali: Kuna ugumu wa kufasili maana ya maana. Jadili.
Aina za Maana
Maana zinaweza kuainishwa katika makundi mawili kama ifuatavyo:
     a) Maana ya msingi
     b) Maana za ziada
1. Maana ya Msingi/Kiini/Mantiki/Dhana
Maana ya msingi ni fasili ya umbo la kiisimu ya kikamusi, maana ya msingi haitegemei muktadha wala hisia. Pia, hujulikana kama maana ya kikamusi au
maana tambuzi.
Sifa za Maana ya Msingi
a)     Ni ya kudumu, haibadilikibadiliki
b)    Huthibitishwa kisayansi. Mfano: mvulana na msichana
c)     Haitegemei muktadha, maana inapatikana moja kwa moja kutokana na umbo la kiisimu na uhusianishaji.
d)    Ndiyo inayojenga uhalisia wa lugha
e)     Ndiyo chanzo cha maana za ziada
2.     Maana za Ziada
   Maana ya ziada ni fasili ya umbo la kiisimu inayotegemea muktadha na hisia za mzungumzaji ama msikilizaji. Hutokana na maana ya msingi. Maana hii huhsishwa na kitajwa cha msingi.
    Ni kundi la maana kwa sababu hutegemea uelewa, uzoefu na tajiriba ya mtu mmojammoja katika kutumia lugha, kuielewa lugha na hata kuichanganua lugha. Kundi hili lina maana nyingi kama ifuatavyo:
Aina za Maana za Ziada
a)     Maana Dhana (Conceptual meaning) Ni maana inayotokana na sifa za ziada za kitaja (kirejelee), maana hii hutokana na mwelekeo ama mwenendo wa kitu kinachorejelewa (kitaja).
– Ni kutumia neno la msingi kuwakilisha maana fulani katika muktadha fulani.
– Ni maana inayotokana na athari za kihistoria au utamaduni na mazoea ya wazungumzaji wa lugha. Mfano: mwanamke = mpole, dhaifu, mvumilivu, chombo cha starehe. Mwanaume = jasiri, laghai, anatumia nguvu.
b)    Maana Mtindo (Stylistics Meaning)
Hii ni maana ya kimuktadha; ni maana inayotokana na matumizi ya lugha katika muktadha wa kifasihi ama mahali fulani
ambapo wazungumzaji wanataka kuficha mazungumzo yao. Maana mtindo huangalia
mzungumzaji katika muktadha wake.
Mfano: vyuoni = bumu, madesa,
             Daladala = vichwa, mawe, wa
kusoma, mchawi
c)     Maana mwangwi/Akisi (Reflective Meaning)
Hii ni maana inayopewa kitu kwa
kufananisha na kitu kingine. Maana inapinduliwa na kuwa kinyume chake.
Mfano: mtu anapomwita mpenzi wake
mtoto/baby/honey/malaika
Mshenzi wa hisabati/namba
d)    Maana dhamirifu/dhamira (Thematic meaning)
Maana dhamira ni maana ambapo neno
hubeba dhamira/dhima ya tungo nzima au kitabu. Katika maana dhamira msisitizo
huwekwa katika neno moja tu, ambalo huwa limebeba ujumbe. Maana hii inpatikana
kutokana na namna mtumiaji wa lugha anavyopanga maneno yake katika sentensi.
Aghalabu, ni ile taarifa ambayo mhusika anaiona kuwa ndiyo muhimu kuiweka
mwanzoni.
Mfano: Shati moja ni shilingi
elfu kumi tu.
            Shati moja tu ni shilingi
elfu kumi.
e)     Maana hisia (Affective/emotive meaning)
Hii ni maana inayotokana na hisia na
mtazamo wa mzungumzaji au mwandishi au msomaji juu ya kitu. Anaweza akawa na
furaha, huzuni, upendo, hasira ama mtazamo chanya ama hasi. Maana hisia mara
nyingi hubadilika kutegemea kiimbo hata kama maneno ni yaleyale.
Mfano: neno “mpole”
f) Maana Kolokesheni/Ambatani/Tangamano (Collocative meaning)
Ni maana inayotokana na ujirani wa
maneno kwenye tungo. Kuna baadhi ya maneno ambayo maana zake hupatikana kwa
kuwa pamoja na maneno maalumu; kinyume chake haiwezi kukubalika katika hali ya
kawaida. Maneno au mfuatano wa  maneno
katika lugha una ujirani wa ki – usilisila (neno fulani hutokea na neno fulani
katika tungo.
Mfano: nomino + kitenzi, nomino +
kivumishi, kitenzi + kielezi. Nomino nazo zinabagua aina za vivumishi kwa
mfano:
Mvulana mtanashati                *Msichana
mtanashati
Msichana mrembo                    *Mvulana mrembo/mlimbwende
Mti unatikisika                         *Mtoto anatikisika
Mtoto anatetemeka                  *Mti
unatetemeka
Maneno haya yana maana lakini inategemea
neno hilo limechaguliwaje katika tungo.
Dhana ya uhusiano wa kifahiwa na maana za Maneno/Msamiati
Uhusiano wa umbo moja la kiisimu na
linguine ndio unaotupatia semantiki ya kimuundo (mahusiano ya kifahiwa/kimaana
(sense relations) katika lugha). Maneno ya lugha hayakai hovyohovyo, bali kuna
ushikamano wa aina mbalimbali kimaana; yaani, kifahiwa (maana) zake kuwa na
uhusiano wa maana mbalimbali. Uhusiano huo ni pamoja na ule wa sinonimia,
antonimia, homonimia, polisemia na haiponimia.
1.     Mahusiano ya Sinonimia/usinonimia/usawe (Synonyms)
Ni
mahusiano ambayo umbo moja la kiisimu linarejelea maana sawa na umbo/maumbo
mengine ya kiisimu. Ni hali ya maneno mawili/zaidi kuwa maana ileile/ sawa.

Ni uhusiano wa kileksika au kimsamiati
ambapo huwa kuna maumbo tofauti katika lugha ambayo maana zake ni sawa. Ni
maneno yanayotofautiana kimaumbo lakini yanafanana au kulingana kimaana. Mfano:
(i) pesa = fedha = hela = mshiko;
            (ii) mahaba = mapenzi
           (iii) mganga = tabibu = daktari
           (iv) Start = begin = commence
Maneno haya yana maana ileile lakini katika
matumizi yanatofautiana kulingana na muktadha lakini kwa kurejelea maana ileile
moja. Mfano: waziri wa fedha = waziri wa pesa.
2.
Mahusiano ya Antonimia/unyume (Antonyms)
Ni mahusiano ya kiukinzani, umbo moja la
kiisimu linakuwa na maana iliyo kinyume na umbo moja la kiisimu. Ni uhusiano
ambao maneno katika lugha ambayo maana zake ni vinyume. Kinachokusudiwa kusemwa
hapa ni kwamba maana za maneno hayo huwa zinapingana.
Mfano: fupi = refu, cheka = lia, penda =
chukia, joto = baridi, embamba = nene.
3.
Mahusiano ya Homonimia (Homonyms)
Ni mahusiano ambayo umbo moja la kiisimu
hurejelea maana zaidi ya moja na maana hizi hazina mahusiano ya karibu. Maumbo
sawa ya kiisimu yanaitikwa na maana mbalimbali.

Ni uhusiano wa kimsamiati unaohusu
maneno tofauti yaliyosadifu maumbo sawa lakini yanayotofautiana kimaana.
Kufanana kwa maumbo hayo ni kwa kusadifu tu.

Maneno hayo huwa hayana usuli mmoja wala
histiria.

Maneno mawili au zaidi yanayofanana kwa
maumbo kutofautiana kwa maana

Mfanino: paa = kuruka, sehemu ya juu ya
nyumba, aina ya mnyama.
Maana
hizi zinatofautiana wala hazina mahusiano yoyote. Uhusiano wa homonimia
husababisha kuleta utata katika tungo.
4.
Mahusiano ya Kipolisemia (Polysemy)
Polisemia ni hali ya maneno kuwa na
maana zaidi ya moja. Katika polisemia maneno huwa yana uhusiano wa kihistoria.
Huu ni uhusiano unaohusu umbo moja la neno lenye maana mbalimbali. Umbo moja la
kiisimu huwakilisha dhana zaidi ya moja zenye mahusiano kimaana.
Kichwa = mkuu wa familia, sehemu ya juu
ya mwili, sehemu ya mbele ya gari, mkuu/kiongozi. Maana zilizochanuza zina
mahusiano.
5.
Mahusiano ya Haiponimia (Hyponyms
Ni mahusiano ya kamaumbo. Maana ya umbo
moja la kiisimu imo ndani ya maana ya umbo moja la kiisimu. Kutumia umbo moja
la kiisimu kufafanua maana za maumbo mengine.

Uhusiano wa kimsamiati ambapo maana
fulani ya neno ni sehemu ya maana kuu ya neno.

Neno lenye maana kuu huitwa maana
jumuishi ili hali maneno yenye maana ndogo huitwa haiponimu.
Mfano: Tunda = (ndizi,
chungwa, parachichi, (ndizi = kisukari, mkono wa tembo)
Kisukari ni aina ya
ndizi na ndizi ni tunda. Haya ni mahusiano ya kidarajia zaidi. Darajia ya chini
inafafanuliwa na darajia ya juu.
PRAGMATIKI
 
Dhana ya Pragmatiki
Kwa mujibu wa Morris
(1938) anaeleza njia tatu za uchunguzi wa ishara ambazo ni; mahusiano ya ishara
zenyewe (sintaksia), ishara na kirejelewa (semantiki) na ishara ya kimuktadha
(Pragmatiki). Vilevile, Schiffrin (1938 & (1994) anasema Pragmatiki ni
taaluma ya semiotiki ambayo
huchunguza ishara na maana zake ndani ya muktadha wa jamii husika. Semiotiki
inashughulikia hasa sehemu nne katika lugha yaani, ishara, kirejelewa, ufasiri
na mfasiri.
Kwa upande wake Crystal
(1987) anasema Pragmatiki huchunguza mambo ambayo huongoza uchaguzi wa lugha
katika maingiliano ya jamii au mtagusano wa kijamii na athari ya uchaguzi huo
kwa wengine.
TUKI (1990) wanasema
Pragmatiki ni taaluma ya isimu jamii ambayo huchanganua lugha kwa kutegemea
maoni ya mtumiaji hasa uchaguzi wa miundo ya maneno yanayoleta vikwazo vya
kijamii, anavyokabiliana navyo katika kutumia lugha na athari za kijamii za
matumizi ya lugha. (Matumizi ya lugha kutokana na muktadha).
Yule (1996) anasema
Pragmatiki ni mtalaa unaochunguza maana ya msemaji. Hujihususha na kufasiri
kuhusu kile watu wanachomaanisha katika muktadha fulani; na jinsi ambavyo
muktadha huathiri kile ambacho kinasemwa.
Kinadharia tunaweza
kusema chochote lakini katika hali halisi kuna sheria za kijamii ambazo
zinafuatwa kwa kujua au kutojua (consciously
or unconsciously) ambazo huongoza jinsi tunavyozungumza. Kwa mfano hakuna
sheria zinazokataza mizaha kwenye matanga au zinazotuongoza kuwa wanyenyekevu
na urasimi tunapozungumza na viongozi wetu kazini. Miktadha kama hii ndiyo
inayoleta maana ya kipragmatiki.
Pragmatiki katika Matini
Baadhi ya wanaisimu pia
hushughulikia maana katika kiwango cha matini, uchunguzi wa maana katika
kiwango cha matini huitwa pragmatiki. Pragmatiki
ni taaluma ya kisasa iliyoanza hivi karibuni, ambayo imetokana na semantiki. Pragmatiki
huangalia wale wanaozungumza lugha na kile kinachozungumzwa (language users s/v language uses).
Pragmatiki imejikita katika kuangalia kusudi la kile kinachowasilishwa (yaani
ujumbe) katika mawasiliano, kwa maneno mengine, huangalia kusudio la mhusika/msemaji
katika mawasiliano.
Kuna kanuni
zinazotumika kuonesha kusudio la msemaji, kanuni hizi ni muhimu sana katika
taaluma ya tafsiri na ukalimani kwani ni lazima uweke kusudi la mzungumzaji.
Kusudio hilo hutafsirika kwa kutegemea muktadha. Hivyo, maana ya kipragmatiki
hufungamana na muktadha. Kipragmatiki maana ya maneno inaweza kuwa tofauti
kabisa na maana ya maneno kisemantiki. Mtu anapoongea anakuwa na nia fulani ya
kufikisha ujumbe. Mtu anaweza kutoa ujumbe ambao maana yake inaachana na maana
ya msingi ya maneno aliyoyatumia. Kwa mfano: “leo kuna baridi sana!” (Maana
iliyokusudiwa = kuvaa sweta/ kufunga madirisha). “Ninahisi kiu!” (= Ninunulie
maji). Muundo wa tungo hizi hauleti maana iliyo ndani ya tungo. Ujumbe ulio
ndani ya tungo ni wa kubabia. Maana hii inategemea sana nafasi, mahali, na watu
wanaohusika. Unapofasili unatakiwa kufasili kulingana na muktadha ambao
unahoji: kusudio hasa la mzungumzaji ni lipi? Vinginevyo, utatoa fasili ya
kikasuku.
Upacha wa Semantiki na Pragmatiki
Ni kweli pragmatiki na
semantiki ni mapacha wasioweza kutenganishwa, kwa kuwa wanalenga kuishughulikia
maana ili kuweza kurahisisha mawasiliano ndani ya jamii. Kigezo cha kuwa
mapacha ni kuonesha kuwa wanafanana japo kuwa wanaweza kutofautiana kulingana
na tabia zao. Haya yanathibitishwa kwa kutumia vigezo vifuatavyo:
Kigezo cha Kimaana
Semantiki na pragmatiki
zote ni matawi ya isimu ya lugha ambayo yanatumika kupambanua maana, semantiki
hujikita katika kueleza maana mbalimbali za maneno hasa maana za msingi
zilizomo katika kamusi. Mfano, Sungura ni mnyama mdogo mwenye masikio mmafupi. Pragmatiki
ni tawi ambalo hujikita katika kueleza maana mbalimbali za maneno kulingana na
muktadha wa neno au maneno yalivyotumika. Mfano neno Sungura katika pragmatiki
linaweza kuwa na maana zifuatazo: mjanja, laghai, mwenye akili nyingi,
asiyeshindwa.
Kigezo cha Matawi ya Kiisimu
Semantiki ni taaluma ya
isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa maana za maneno au tungo
katika lugha (Massamba, 2009: 75) na Pragmatiki ni taaluma ya isimu
inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa lugha katika mawasiliano. Lengo
kuu la taaluma hii ni kuchunguza namna lugha inavyotumiwa na wasemaji wake
katika mazingira halisi 9Massamba 2009:71), matawi haya ni ya isimu kwa sababu
huchunguza lugha ya mwanadamu kisayansi.
Kigezo cha Matumizi
Matawi yote yanajihusisha
na uchambuzi wa maana, maana ndio kipengele muhimu zaidi katika uchunguzi wa
lugha ya mwanadamu, hii ni kwa sababu kazi kuu ya lugha ni mawasiliano na
mawasiliano huhususha upashanaji wa habari kwa ujumla ambapo hueleweka katika
maana ya tamko, Semantiki ni tawi ambalo hulenga zaidi kuangalia maana ya
msingi ambapo mtumiaji wa lugha huelewa kile kilichokusudiwa bila ya kuwa na
maana ya ziada, na katika pragmatiki maana hutumika na kutafsiriwa kulingana na
muktadha, mfano neno jembe kisemantiki huwa na maana kuwa ni kifaa
kinachotumika kuchimbia ardhi (TUKI, 2010) lakini ki-pragmatiki neno hilo
linaweza kuwa na maana zifuatazo; mkali, hodari au mtu asiyekwama katika jambo
lolote.
Kigezo cha Utata
Matawi yote huibua
utata katika tungo, utata unaweza kutokea katika neno, kirai, kishazi au
sentensi, utata hutokea pale ambapo neno au sentensi inakuwa na maana zaidi ya
moja katika semantiki. Mfano: (i) paa – mnyama/ -paa la nyumba au kitendo cha
kuelea angani/ -paa kuondoa magamba ya samaki (ii) amelalia uji – amelala juu
ya uji au – amekunywa uji kisha akalala. Kutokana na neno au sentensi hizo
tunapata utata katika mazungumzo, na pia katika pragmatiki mzungumzaji huibua
maana nyingi katika muktadha fulani. Mfano: mpe jiko – mpe mke, -kifaa cha kupikia.
Kigezo cha Muktadha na Mazingira
Matawi yote huzingatia
muktadha na mazingira, mazingira ni maeneo au upeo ambamo kipashio fulani cha
kiisimu huweza kutokea kufanya kazi na muktadha ni sehemu maalumu ambayo
kipengele fulani cha kisarufi hujikuta ndani mwake na kuathiriwa kihasi au
kichanya. Semantiki huchunguza zaidi maana kimazingira ambamo maana halisi
hupatikana kwa mfano: Tufunge ofisi –
kufunga mlango wa ofisi baada ya saa za kazi. Niletee kisu – yaani kifaa kikali
kinachotumika kukatia.
Kwa uhalisia wake
pragmatiki hujikita katika maeneo ambayo wazungumzaji huelewana wenyewe kwa
wenyewe, kwa mfano muktadha wa shuleni, mahusiano kati ya mwanafunzi na
mwalimu. Mfano, kipragmatiki; Tufunge
ofisi – kutoroka shule kabla ya muda wa kutoka shuleni. Niletee kisu inaweza
kuwa – niletee mke/binti mrembo.
Kigezo cha Ukongwe
Semantiki ndiyo
iliyotangulia kuwepo ambapo pragmatiki ni tawi lililoibuka baadaye, (Semantiki
ni kongwe na pragmatiki ni changa). Semantiki ilianza kutumika mwanzoni mwa
karne ya 19. Tawi hili liliasisiwa na mwanataaluma wa isimu aliyeitwa Michael
Brill na pragmatiki ilianza kutumika baada ya kuona kama semantiki inapwaya
katika baadhi ya maeneo katika taaluma ya lugha ikizingatiwa nia ya
mzungumzaji, muktadha wa mazungumzo n.k. Hii ilianza kutumika katika miaka ya
1938 na ilianza kushughulikiwa na mwanaisimu Charles Morris.
Kigezo cha Tafsiri
Katika semantiki
tafsiri ya neno au semantiki iliyotumiwa huzingatia maana ya msingi mfano, neno
“simba” maana ya msingi ni: Mnyama mkubwa wa porini wa jamii yap aka mwenye
manyoya ya rangi ya majani makavu na ambaye hula nyama (TUKI, 2010:375). Lakini,
pragmatiki tafsiri (maana ya neno) hutokea kutokana na muktadha ambapo
mzungumzaji na mpokeaji walipo mfano, simba – neno hili huweza kutoa maana
zifuatazo: Kijana mwenye nguvu/mkali/hodari au katili.
Kiini na Uhifadhi
Semantiki imejikita
kimaandishi zaidi wakati Pragmatiki ipo kimazungumzo zaidi. Hii ni dhahiri kuwa
maadamu pragmatiki huchunguza maana ya msemaji kulingana na muktadha basi
uhifadhi wake uko kichwani mwa mtumiaji lugha kulingana na hitaji lake. Semantiki
inaweza kuwa imejikita zaidi katika maandishi kwa sababu ya urasmi wake.
Kigezo
cha Umilisi
Katika semantiki
msikilizaji hapaswi kuwa mmilisi au mmahiri sana wa lugha kwa kuwa semantiki
hujikita katika maana za msingi, ambazo hueleweka kwa maarifa ya kawaida ya
lugha. Pragmatiki inataka msikilizaji kuwa na umilisi wa kutosha ili atambue
maana za ziada ambazo msemaji anakusudia. Awe anajua maana za ziada kulingana
na mazingira ambapo maana hiyo ilivyo inaweza kutafsiriwa tofauti tofauti
kulingana na mazingira mbalimbali inamosemwa lugha husika.
Kwa mfano katika mazingira
ya kawaida ni vigumu mtu asiye mmilisi kiasi cha kutosha kutofautisha maneno
majani, kulingana na matumizi ya aina mbalimbali na watumiaji mbalimbali. Mfano,
vijana wanaweza kuwa wanasema; Nipe majani au Jamaa ana majani sana huyu! Hii ina
maana kuwa mmoja anaomba dawa za kulevya hususani bangi, na katika sentensi ya
pili mmoja anaomba hela. Kwa kuwa katika semantiki maana hukitwa katika maana
ya msingi ya kamusi msikilizaji anaweza kuelewa majani kama magugu, maotea
katika uso wa ardhi.
Baadhi
ya Tofauti kati ya Semantiki na Pragmatiki
Semantiki hueleza maana
kwa kuzingatia misingi ya lugha yenyewe (Explains
meanings purely in language – internal terms). Wakati, pragmatiki hueleza
maana kulingana na  mahusiano ya
kiusemezano yanayokuwepo kati ya msemaji na msikilizaji (explains meaning as negotiated between speaker and listener).
Semantiki huichukulia
lugha kuwa ni mfumo dhahania wa alama (Looks
at languages as an abstract system of signs). Wakati, Pragmatiki
huichukulia lugha kuwa ni chombo cha mawasiliano kinachoweza kutumiwa kadri ya
matakwa ya msemaji (looks at language as
a tool for communication).
Semantiki huelezea
maana ya msingi tu (Describes literal
meaning only). Wakati, Pragmatiki hueleza maana iliyokusudiwa na msemaji na
ile inayoeleweka kwa msikilizaji (describes
intended and understood meaning).
Kwa kuhitimisha
semantiki na pragmatiki ni mapacha wawili ambao aidha wanafanana au
wanatofautiana kwa kuwa kilengwa chao ni kimoja. Kwa hiyo mtumiaji wa lugha
anapaswa kuzifahamu taaluma zote mbili kwa kuwa ni vigumu kupata maana katika
semantiki tu, bali maana nyingine huhitaji kuhusishwa na muktadha husika. Hivyo,
semantiki na pragmatiki ni lazima ziende sambamba kwa sababu ya uelewa wa lugha
kwa wazungmzaji kuwa tofauti na pia mazingira tofauti, pia lugha iwe na maana
toshelevu miongoni mwa wazungumzaji ni lazima maana na mazingira husika
yazingatiwe.
Umuhimu
wa Semantiki na Pragmatiki
Inatajwa kuwa semantiki
na pragmatiki ni muhimu katika isimu kama vilivyo vipengele vingine, yaani,
fonolojia, mofolojia na sintaksia. Kwa nini? Hii ni kwa sababu lengo la sheria
za kifonolojia, kimofolojia na kisintaksia ni kuunda tungo zenye maana (ambayo
huchunguzwa katika kiwango cha semantiki na pragmatiki).
Aidha, inatajwa kwamba
maana ndicho kipengele muhimu zaidi katika uchunguzi wa lugha ya mwanadamu. Kwa
nini? Hii ni kwa sababu kazi kuu ya lugha ni mawasiliano na mawasiliano
huhusisha kupashana ujumbe ambao hueleweka katika maana ya tamko. Ujumbe hudhihirika
katika maana na ufafanuzi wa maana zilizobebwa na vipashio vya lugha
vinavyohusika kama vile fonimu, neno, sentensi na aya/matini.
Semantiki huchunguza
namna ambavyo vipashio vya lugha huhusiana ili kuleta maana timilifu. Semantiki
ndiyo makutano ya taaluma hizi. Naye, Leech (1981) anasema wakati fonolojia,
mofolojia na sintaksia zinahusu maumbo na miundo, semantiki na pragmatiki zinaangalia
maana ya miundo na maumbo hayo katika lugha. Nao, Habwe na Karanja (2007:202)
wanasema kuwa kwa ujumla, semantiki na pragmatiki hujishughulisha na masuala
yafuatayo: Maana na uainishaji wa maana za maneno, maana za tungo, taratibu za
kuchambua maana, etimolojia ya maana za maneno, uhusiano wa kimaana katika
sentensi na nadharia za uchambuzi wa maana.
ZOEZI
1.     Jadili
kwa kina dhana ya maana katika taaluma ya semantiki.
2.     Kwa
kutumia mifano kuntu jadili mahusiano ya maana za maneno katika taaluma ya
semantiki.
3.     Linganisha
na linganua taaluma ya semantiki na Pragmatiki.
4.     Jadili
tofauti za kimsingi zilizopo katika semantiki na Pragmatiki.
5.     Fafanua
maana na mahusiano yafuatayo ya kifahiwa:
a)     Homonimia
b)    Sinonimia
c)     Haiponimia
d)    Antonimia
e)     Polisemia
6.     Kwa
kutumia mifano kuntu jadili aina zifuatazo za maana.
(i) Maana ya msingi    (ii) Maana ya ziada
MAREJELEO
 
Zabroni, T. P (2016) Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam. Karljamer Publishers,
Ltd
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)