MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
SHAABAN ROBERT KAMA MWANANATHARI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SHAABAN ROBERT KAMA MWANANATHARI
#1
SHAABAN ROBERT KAMA MWANANATHARI
1.0.HISTORIA FUPI YA MWANDISHI
1.1   UZAWA NA MAISHA YAKE
1.1.1 UPANDE WA BABA YAKE
Asili ya wazazi wa Shaaban Robert ni Tunduru-Ruvuma kwa upande wa baba yake na Tanga kwa upande wa Mama yake.
Babu yake Shaaban Robert kwa upande wa baba aliitwa Kanduru. Alikuwa mzaliwa wa Wilaya ta Tunduru, mkoani Ruvuma. Katika suala la imani ya Kidini, Kanduru alikuwa anaamini Miungu ya Ki-mizimu ambayo wakati huo iliaminika kuwa ndiyo chanzo cha yote yaliyojiri katika maisha ya binadamu. Kanduru alipofika Mzizima kwa mara ya pili ili aje kufanya kazi, alimpata mke kutoka kabila la Wazaramo. Mke huyu alikuwa Muislamu kwa sababu eneo lote la Pwani lilikuwa tayari linakaliwa na wakazi wengi waliokuwa Waislamu. Kutokana na kumhitaji binti huyu, ilimlazimu Kanduru asilimu kwanza ndipo aozwe. Hivyo, Kanduru alisilimishwa na kuwa Mwislamu, akaitwa Jumaa, ndipo akaozwa.
Baada ya muda, walipata mtoto waliyempa jina la Ufukwe, jina alilopewa na watani kwa kuwa alizaliwa ufukweni mwa bahari ya Hindi wakati mama yake alipokwenda huko kutandaza Uduvi. Pia aliitwa Selemani, jina ambalo lilikuwa rasmi kwa muktadha wa dini ya Kiislamu. Tajiri wa Jumaa ambaye alikuwa mzungu, aliamua kumpa mtoto huyu jina la Roberto kutokana na mapenzi na furaha aliyokuwa nayo. Hivyo jina hili halihusiani na dhana ya dini. Baabaye, kutokana na athari za matamshi ya lugha ya Kiingereza, jina hili la Roberto lilibadilishwa na kutamkwa Roberts. Roberto au Roberts, ambaye majina yake ya Ufukwe na Selemani yalififia, alimuoa Mwanamwema binti Mwindau na kuishi naye huko Vibambani, Tanga. Mnamo tare 01 Januari 1909, wakamzaa mtoto waliyemuita Shaaban.( Ponera 2010:26).
  1.1.2 UPANDE WA MAMA YAKE
Bibi Mwanamwema binti Mwidau alikuwa ni wa ukoo wa kina Kihere (yaani Kihere Mwalimu Kihere na Mwalimu Mwalimu Kihere), ambao wanatajwa sana katika barua nyingi za Shaaban Robert (kama zilivyo limbikizwa na kuhaririwa na M. M. Mlokozi). Alikuwa ni wakabila la Kimwamwande, na alizaliwa Msengenyeni, Tanga, mwaka wa kuzaliwa haujulikani. Alifariki mwaka 1967.
Bibi Mwanamwema aliolewa mara tatu na alijaliwa kupata jumla ya watoto 14. Mume wake wa kwanza alikuwa Bwana Kibwana. Huyu alizaa naye watoto 3, wa kiume wawili na mmoja wa kike. Watoto hao ni:
(i)  Jafari Kibwana
(ii) Mwanagani Kibwana (mwanamke)
(iii) Khatib Kibwana
Kipindi cha kabla ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914-1918). Bwana Kibwana alisafiri kwenda Uganda na hakurudi. Hivyo Bibie Mwanamwema akajikuta hana mume, na ndipo alipoolewa na Bwana Selemani au Ufukwe bin Jumaa, au jina jingine Robert. Huyu alikuwa ni Myao Upande wa baba, na Mzaramo upande wa mama, na alipewa jina la “Robert” kwa heshima ya mkulima wa Kizungu ambaye baba yake, yaani Mzee Jumaa, alikuwa akifanyia kazi.
Mwanamwema alizaa na Bwana Ufukwe mtoto mmoja tu, yaani Shaaban Robert. Baadaye wakaachana. Hata hivyo, Bwana Robert alikuwa na watoto wengine kwa wake wengine, ambao ni:
(i)   Jumaa bin Robert wa Ngamiani, Tanga
(ii)   Abdallah bin Robert wa Mnyanjani, Tanga
(iii)  Mwansaumu binti Robert wa Mnyanjani
Mume wa tatu wa Bibie Mwanamwema alikuwa ni Bwana Mwinyiulenge Mworogo. Huyu alizaa naye watoto 10-wasichana watano na wavulana watano-wafuatao:
(i)                 Mwishehe Ulenge (Mvulana)
(ii)               Mwanaidi Ulenge (msichana)
(iii)             Mwanang’andu Ulenge (msichana)
(iv)             Yusufu Ulenge (Mvulana)
(v)               Mwanahadia Ulenge (Msichana)
(vi)             Asha Ulenge (msichana)
(vii)           Mwidau Ulenge (msichana)
(viii)         Issa Ulenge (mvulana)
(ix)             Ali Ulenge (mvulana)
(x)               Maimuna Ulenge (msichana) (mulokozi: 2002:3)
1.1.3 SHAABAN ROBERT
Shaaban Robert alizaliwa tarehe 01 Januari 1909, (Wakati wa ujana wake Shaaban aliacha kuliandika jina la Roberts, akaanza kujiita Shaaban Robert), alipelekwa madrasa, shule itoayo mafunzo ya dini ya Uislamu na mama yake akiwa na umri wa miaka tisa. Huko alijifunza mambo mengi yahusuyo dini ya Uislamu kama vile Hadithi za Mtume Mohammad (ambaye ni Kiongozi wa Waislam). Alianza masomo ya elimu ya msingi mwaka 1922 katika shule ya msingi ya Kichwele (sasa inaitwa Uhuru mchanganyiko) iliyopo mjini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 13. Wakati huo, tayari alikuwa amekwishapata elimu ya dini kwa kiwango kikubwa. Aliendelea kusoma elimu hiyo ya dini hata alipokuwa anaendelea na masomo haya ya shule ya msingi. Alihitimu masomo hayo mwaka 1926 na kufaulu vizuri kwa kushika nafasi ya pili kati ya wanafunzi kumi na mmoja. Baada ya hapo, aliajiriwa na serikali ya kikoloni na kufanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali. (Ponera 2010: 27).
1.2   KAZI ALIZOZIFANYA
  • Alianza na kazi ya Ukarani wa serikali Forodhani Pangani mwaka 1926-1944.
  • Idara ya hifadhi ya Wanyamapori (Mpwapwa) mwaka 1944-1946.
  • Alifanya kazi katika Afisi ya Mkuu wa Jimbo Tanga mwaka 1946-1952.
  • Afisa wa kupima nchi Tanga (Idara ya ardhi) mwaka 1952-1960.
  • Pia kabla hajastaafu mwaka 1960, aliwahi pia kuhamishiwa Old Moshi.
Alipokuwa kazini aliheshimika katika sehemu zote alizofanya kazi kutokana na adabu, bidii na uadilifu wake.
1.3   KIFO CHAKE
Shaaban Robert alifariki tarehe 20/06/1962 katika hospitali ya Mkwakwani Tanga, Bombo na kuzikwa tarehe 22/06/1962 katika makaburi ya ukoo wa mama yake yaliyopo hapo hapo Vibambani Tanga. Alifariki akiwa na miaka Hamsini na tatu (53).
Chanzo cha kifo chake kinatajwa kuwa ni kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika. Pia wengine wanataja kuwa ni kwa sababu ya homa ya Kifua Kikuu. Alilazwa katik hospitali hiyo kwa muda mrefu akianzia katika wodi ya Kawaida kisha alihamishiwa katika wodi ya wagonjwa mahututi. (Ponera 2010:29).
1.4   MAISHA YA NDOA
Mke wa kwanza wa Shaaban Robert alikuwa ni Amina. Alimuoa mwaka 1930/1931. Aliishi naye kwa miaka kumi tu ambapo walizaa watoto wengi lakini wengi walifariki wakiwa bado wachanga.
Amina anakadiriwa kufariki mwaka 1942 (Kutokana na shairi la Amina, kutungwa Juni 1942) na kumwachia watoto wawili, ambao ni Selemani na Mwanjaa ambao walipona dhidi ya mauti ya mapema. Kutokana na ubovu wa barabara na hali mbaya ya hewa, alishindwa kusafirisha mwili wa Amina hadi Vibambani hivyo alimzika huko huko Pangani.
Baada ya kufariki Amina shaaban alitunga tenzi za Adili na Hatia kwa ajili ya Wanawe, Mwanjaa na Selemani ili zisimame pahala pa marehemu mama yao kimalezi.
Shaaban Robert alikaa takriban miaka mitatu bila ya mke hadi tarehe 14/09/1945 alipomwoa Bi Sharifa binti Hussein wa Chumbageni Tanga, ambapo pia walizaa watoto wengi ambao pia walifariki wakiwa wachanga ambapo watoto wanne tu walipona ambao ni Akili, Hussein, Mwema na Ikibali.
Baadaye Ugane ulimvaa tena Shaaban Robert, ambapo mke huyu wa pili alifariki mwaka 1955. Baada ya kifo cha mke wake wa pili alioa mke wa tatu ambaye ni Bi. Mwanambazi binti Ali. Huyu hakuzaa naye na ndiye aliyemkalia eda mara tu baada ya kifo chake tarehe 20/06/1962.
1.5   MWONEKANO WAKE  KWA JUMLA
Shaaban Robert alikuwa ni Mcha Mungu ambapo alikuwa Mwislamu aliyeyazingatia maamrisho na miongozo ya dini hiyo kama vile kusali sala tano na mengineyo.
Pia Shaaban Robert alipenda kufurahi nakushirikiana na watu katika kazi na shughuli mbalimbali za kijamii. Aliutumia muda wake mwingi kufanya kazi alizopanga na baada ya kazi alijikita katika kuandika.
   2.0 KAZI ZA KIFASIHI ZA SHAABAN ROBERT
Shaaban Robert ni miongoni mwa waandishi maarufu na wakongwe wa fasihi ya Kiswahili ambao wamejizolea umaarufu mkubwa kutokana na kuandika kazi mbalimbali za kifasihi zenye kutumia ufundi na unadhifu mkubwa wa lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa waandishi hao ni kama vile Amri Abeid Kaluta, Mathias Mnyampala, Ibrahim Hussein, Mohammed Said Abdulla, Penina Mhando na wengine wengi.
Shaaban Robert amejipatia sifa kubwa ikilinganishwa na waandishi wengine kwani ana sifa za kipekee/ upekee mkubwa unajitokeza katika vigezo vifuatavyo;
  1. Idadi ya kazi zake za kifasihi ni nyingi ikilinganishwa na waandishi wengine.
  2. Udhati, uendelevu na uhalisi wa maudhui ya kazi zake.
  3. Umaridadi wa ufundi wa uandishi wake.
Shaaban Robert ndiye mwandishi pekee aliyeandika na kuchapisha kazi nyingi zaidi za kifasihi ya Kiswahili kwa lugha ya Kiswahili (kazi zilizokwisha kuchapishwa mpaka sasa ni ishirini na nne 24).
Aliandika kazi zilizo katika makundi mawili ambayo ni Nudhumu na Nathari.
Kazi yake ya mwanzo kabisa kuchapishwa ni makala ya “Hirizi ya shilingi mia” ambayo ilitoka katika gazeti la Mambo Leo mwaka 1932. Baada ya hapo aliendelea kuandika kazi nyingi za ushairi na nathari katika Magazeti.
Kisha alitunga tawasifu yake “Maisha Yangu” (ambayo baadaye aliipanua na kuiita “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”).
Mwaka 1939 ilianza Vita vya Pili vya Dunia na kwisha 1945 wakati wote huo alitunga “Utenzi wa Vita vya Uhuru” wenye beti 3000. Baada ya utenzi huo alianza kutunga nathari kama vile Kufikirika, Kusadikika, Adili na Nduguze na kadhalika.
Hakuwahi kuandika kazi yoyote ya Tamthiliya (Ponera 2010).
1 KAZI ZAKE ZA NUDHUMU NI;
  1. Masomo Yenye Adili, (1959), Art & Lit, Nairobi.
  2. Utenzi wa Vita vya Uhuru (1961), Oxford, Nairobi.
  3. Kielezo cha Fasili, (1962), Nelson, Nairobi.
  4. Pambo la Lugha, (1966), Oxford, Nairobi.
  5. Insha na Mashairi, (1967), Nelson, Nairobi.
  6. Ashiki Kitabu Hiki, (1968), Nelson, Nairobi.
  7. Mapenzi Bora (1969) Nelson, Nairobi.
  8. Mwafrika Aimba, (1969), Nelson, Nairobi.
  9. Koja la Lugha, (1969), Oxford, Nairobi.
  10. Maisha ya Shaaban Robert, (1971), Nelson, Nairobi.
  11. Sanaa ya Ushairi, (1972), Nelson, Nairobi.
  12. Almasi za Afrika, (1972), Nelson, Nairobi.
  13. Tenzi za Maadili Mema na Omar Khayyam (1973), T PH, Dar es Salaam.
  14. 14.2.2 KAZI ZAKE ZA NATHARI
Kazi za nathari za Shaaban Robet zinajumuisha kazi za makundi yafuatayo;
(i)                 Barua.
(ii)               Insha.
(iii)             Hadithi Fupi.
(iv)             Riwaya za Kiwasifu.
(v)               Riwaya za Kitawasifu.
Sifa zilizotumika katika kutofautisha makundi haya (hususani hadithi fupi na Riwaya ni;
(i)                 Urefu (idadi ya maneno).
(ii)               Uchangamano wa vitushi (sahili na tata).
(iii)             Lugha iliyotumika katika nathari husika.
(iv)             Wahusika (idadi).
(v)               Dhamira (idadi na uzito).
(vi)             Mandhari (ukubwa na upana-Jiografia, historia, wakati).
Nathari za Shaaban ni kama hizi zifuatazo;
  1. Adili na Nduguze, (1952), Mcmillan, Londoni.
  2. Kusadikika, (1951), Nelson, Nairobi.
  3. Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, (1949), Nelson, Nairobi.
  4. Kielezo cha Insha, (1954), Witwatersand, Nairobi.
  5. Methali na Mifano ya Kiswahili, (1997), TUKI, Dar es salaam.
  6. Kufikirika, (1968), Oxford, Nairobi.
  7. Utubora Mkulima, (1968), Nelson, Nairobi.
  8. Siku ya Watenzi Wote, (1967), Nelson, Nairobi.
  9. Wasifu wa Siti binti Saad, (1967), Nelson, Nairobi.
  10. Barua za Shaaban Robert, (2002), TUKI, Dar es salaam.
2.3 UHALISI NA UBUNILIZI KATIKA KAZI ZA SHAABAN ROBERT.
Uhalisi ni ukweli wa jambo kama lilivyo, kuna ukweli wa aina mbili ambao ni;
(a)    Ukweli katika hali halisi.
(b)   Ukweli wa kisanaa (ambao husawiri mambo yaliyobuniwa na               mtunzi).
   Ubunilizi, ni utengenezaji wa ukweli wa jambo kadri afikiriavyo msanii kwa kuzingatia uwezekano na azma yake. Hivyo basi yafaa ubunilizi usipitilize kwani ni rahisi kwenda mbali na jamii halisi.
   Vipengele ambavyo ubunilizi hufanywa ni kama vile;
(a)    Mandhari. Kwa mfano katika kusadikika mandhari iliyotumika ni ya kubuni ambapo tunaona nchi ya kusadikika iko hewani inaelea, inamipaka sita ambayo ni Ardhini, Mbinguni, Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini.
(b)   Wahusika. Ambapo wahusika katika kazi za Shaaban Robert wanauwezo na sifa maalumu. Kwa mfano wanasifa za aina moja tu, kama ni mwema tu au waovu tu. Kama ilivyo kwa Waziri Majivuno, Karama na kadhalika katika kusadikika. Pia wahusika hawa huundwa kwa sifa ya kutokukata tama kwa mfano karama katika Kusadikika. Vilevile wahusika wengine siyo binadamu ni majini kama wanavyojitokeza katika Riwaya yake ya Adili na Nduguze, kuna wahusika kama vile Mrefu.
© Lugha. Katika kipengele hiki cha lugha kuna matumizi ya Taswira na tamathali za semi ambapo kwa mwandishi huyu Shaaban Robert ameonesha umahiri wa hali ya juu katika kipengele hiki, kuitumia lugha ya Kiswahili.
(d) Ushikamani, katika kipengele hiki huweza kufanywa kwa kutumia mbinu kama vile;
(i)  Ubadala mfano katika Adili na Nduguze hakumtaja sana jina la Mfalme Rai bali alimtambulisha kwa vibadala (majina mengine ya ziada).
(ii) Urejeshi/ Kisengere nyuma. Ni ile hali ya mwandishi kuelezea hadithi Fulani kwa kuanza mbele na kurejea au kulielezea tukio la nyuma (urejeshi). Kwa mfano msuko wa matukio katika nathari ya kusadikika.
(ii) Udondoshaji, katika Adili na Nduguze mwandishi                                  ameidondosha habari ya mama yao Hasidi, Mwivu na Adili.
(iv) Uunganishaji/ ujumuishaji. Mfano katika kusadikika kuna vitushi vya Salii na Sapa, safari za Ndege Mangere na kadhalika (kitushi ndani ya kitushi).
Hivyo basi kazi za Shaaban Robert zina mseto wa uhalisi na ubunilizi ambapo kazi zake za mwanzo zina kiasi kikubwa cha ubunilizi. Mfano Kufikirika, Kusadikika na Adili na Nduguze. Ambapo ubunilizi huo unajidhihirisha katika kipengele cha Lugha, Mandhari, Wahusika na namna ya kushikamanisha vitushi vyake ambapo Shaaban Robert ametumia mbinu mbalimbali kama vile Utomelezi, Taharuki, Ujadi na kadhalika.
Kazi zake za uzeeni zina ukweli kwa kiasi kikubwa sana. Kwa mfano Utubora Mkulima na Siku ya Watenzi Wote.
MBINU ZA KIBUNILIZI KATIKA KAZI ZA SHAABAN ROBERT NI;
(i)                 Ujadi.
(ii)               Ufutuhi.
(iii)             Utomelezi.
(iv)             Taharuki.
(I)                MBINU YA UJADI
Ni utumizi wa kauli za Kiutamaduni, kauli zilizozoeleka sana na jamii katika matumizi yao ya kila siku.
Vipengele vya Ujadi ni kama vile, methali, misemo, tamathali za semi. Vilevile mtunzi huweza kuiga kaida maalumu za uzungumzaji ambazo hutumiwa na wazungumzaji wa jamii yake. Mbinu hii ya ujadi husaidia kumweka mtunzi karibu zaidi na hadhira yake.
(II)             MBINU YA UFUTUHI
Ufutuhi ni hali ijengwayo na maneno, matukio au mazingira yoyote yenye mvuto au yasiyo ya kawaida yenye kuwafanya watu watabasamu au wacheke. (Ponera 2010:6).
Hii ni mbinu ambayo mtunzi hutumia maneno au hali nyingine inayoweza kusababisha hadhira yake kupata kicheko/ Ucheshi.
  Mfano: Ufutuhi wa majazi katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”.
        Mume ni mume ingawa gumegume ana sifa ya mtume;
        Na mke ni mke ingawa kikwekwe ana manufaa yake. (uk 101).
Tukio hili linazungumzia umuhimu wa maisha ya ndoa kwa mwanadamu. Majina ya “Gumegume” na “Kikwekwe” yanamaanisha sifa za kutokusikiliza na hali ya kukosa utulivu wa kiakili na kimaadili ya ndoa (Ponera 2010).
(III)          UTOMELEAJI
Ni kitendo cha kuchukua vipande vya kazi za utanzu mwingine na kuuingiza katika hadithi. Kwa mfano nathari ya Shaaban Robert ya “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”, utomeleaji umejitokeza kwa kiwango cha juu katika ukurasa wa 4-5 katika shairi la Amina, ukurasa wa 6-20 katika Utenzi wa HATI, ukurasa wa 21-35 Utenzi wa ADILI. Mbinu hii hutumika ili ku’nogesha kazi yake pia kutia msisitizo juu ya jambo Fulani.
(IV)          TAHARUKI
Ni hali ya kuwa na dukuduku la kutaka kujua nini kitafuata katika usimulijia wa hadithi au riwaya. Mbinu hii mtunzi huitumia ili kuamsha hamu ya msomaji kufatilia kisa kinachosimuliwa katika riwaya au tamthiliya fulani. Mbinu hii Shaaban Robert ameitumia kama kijenzi kimojawapo katika utunzi wake. Imejitokeza kwa kiasi kikubwa katika kazi zake nyingi kama vile “Kufikirika”, ambapo tunaona namna alivyounda matukio yake kwa namna ya kutia hamasa kuendelea kufuatilia kisa kwa ukaribu zaidi. Katika Kufikirika tunaona alivyokijenge kisa cha Mfalme na Malkia kuwa matasa, nathari hii ina muundo ufuatao; Mwanzo, Mfalme, Waganga, Matokeo ya Utabili, Mtoto wa Mfalme, Kafara, Baraza na Gereza.
  1. MAWAZO AU MTAZAMO WA SHAABAN ROBERT KATIKA MAISHA
Mtazamo ni jinsi ya kuyatazama au kuyaona mambo na mwelekeo wake. Katika kazi za Shaaban Robert zinaonesha kuwa mwandishi aliandika kwa kugusia karibu kila Nyanja ya maisha ya mwanadamu. Baadhi ya mambo hayo ni ukombozi na maendeleo ya nchi, udugu na familia, mapenzi, dini, umuhimu wa elimu, utu, ujumi wa kiafrika na kadhalika.
3.1. UTU
Maisha ya binadamu pasipo utu, hukosa thamani. Baadhi ya maswali yanayoonekana kumshughulisha Shaaban Robert katika maandiko yake ni kama vile Utu ni nini? Utu hujengwa wakati gani? na utu hupatikanaje? Utu wa mtu hujengwa na matendo yake mwenyewe kila siku. Shaaban Robert alilijua vema suala hili na alilichukulia kwa hadhari kubwa kama asemavyo katika nathari yake;
Hapa Shaaban anasema; “Wakati mmoja nilifikiri kuwa yote yaliyo azizi au bora kwa mtu ni matendo yake aliyotenda zamani; na kwa kuwa mimi sikupata kutenda tendo lo lote la maana nilijiona sawa kabisa na maskini. Wazo hili lilibatilishwa na fikira kuwa pengine ubora wa mtu huwezekana kuwa katika wakati ujao”. (Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini: uk 1)
3.2 SHAABAN NA DINI
Shaaban Robert alikuwa Muislamu hivyo aliakikisha pia wote wanaomzunguka pia wanaelekea katika njia ya kidini, Shaaban aliamini kuwa dini ndio msingi wa amani duniani, mkwa mfano aliwahusia wanawe kushika dini katika Tenzi zake za HATI na ADILI.
Kwa mfano katika Utenzi wa HATI anamwambia Mwanjaa na Walimwengu wote kwamba;
    27 Shikamana na ibada,
          Kutimiza kila muda,
          Na kesho ina faida,
          Ikisha hii dunia.
   28  Dini mali ya roho,
         Mwilini kama joho,
         Unapoteza uroho,
         Na anasa za dunia. (Maisha Yangu na Baada Ya Miaka Hamsini, uk 10).
Pia katika kitabu hichohicho ukurasa wa 22 anamuhusia mtoto wake wa kiume Selamani juu ya umuhimu wa dini katika maisha yake.
Vilevile alisisitiza uhuru wa kuabudu (Siku ya Watenzi Wote, ukurasa 111), Dhima za dini (Siku ya Watenzi Wote, ukurasa 16 na 63), Unafiki katika dini (Siku ya Watenzi Wote, ukurasa 10, 36 na 102). Hivyo basi suala hili kwa Shaaban Robert aliliona ni la msingi na lenye umuhimu mkubwa katika maisha ya Mwanadamu akiwa hai hapa duniani.
Pia alitoa maonyo na maelekezo mengi kwa mdogo wake Yusufu Ulenge juu ya suala hili la dini. Katika barua yake ya tarehe 24/07/1931 aliyomwandikia Yusufu Ulenge anadhihirisha hilo. Barua hii ipo katika Barua za Shaaban Robert 1931-1958, barua namba 5 ukurasa wa 32.
3.3  SIASA NA UKOMBOZI
Dhamira halisi ya Shaaban Robert kupitia maandiko yake haikuupenda ukoloni wala wakoloni wenyewe. Wahakiki wengi wanamtazama Shaaban Robert kuwa na mawazo ya hali mbili, uchanya na uhasi kuhusu Ukoloni. Wapo wanomwona kama mpinga ukoloni. Wengine wanamwona kama alikuwa msaliti/ mwoga juu ya ukoloni.
Katika kazi yake ya “Utenzi wa Vita vya Uhuru”, tunaona Mawazo ya Shaaban Robert juu ya Ukoloni. Utenzi huu umezungumzia tukio zima la vita hivyo. Yeye alijiegemeza katika upande wa Waingereza kama asemavyo bayana katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” ukurasa wa 64-65. Hapa Shaaban Robert anasema;
 “…. Mimi si raia wa Jerumani, ni raia wa Uingereza…”.
Hili ni mojawapo ya mambo yaliyozua mjadala kwa wahakiki kuhusu Utanganyika wake, wanadai Shaaban Robert aliwatukuza wakoloni. Maudhui ya utenzi huu huenda yaliathiriwa na lengo lake la kumtabarukia Mudir wa Elimu wa kikoloni kipindi hicho Bwana S. N. Eliufoo.
Mbali na utenzi wa Vita vya Uhuru, Shaaban Robert amezungumzia ukoloni na siasa katika kazi zake za “Kusadikika” na “Kufikirika”. Shaaban amefafanua mengi kuhusu adha za Ukoloni na Wakoloni, kwa mfano katika Tawasifu yake ya “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” ukurasa wa 50-51, anaeleza naman alivyobaguliwa yeye na watoto wake pale aliposhushwa kutoka katika Lori la Abiria cheo cha pili ili kuwapisha Wahindi waliokuwapo ambao walikosa sehemu ya kukaa kutokana na nafasi katika Lori hilo kujaa.
SHAABAN ROBERT NA SUALA LA JINSI NA JINSIA
JINSI, ni tofauti ya kimaumbile inayojidhihirisha katika via vya uzazi na hivyo kuwatofautisha watu katika makundi ya wanawake na wanamume.
JINSIA, ni dhana ya Kisosholojia. Hii inahusu mgawanyiko wa Majukumu baina ya Mwanamke na Mwanamume.
  • Shaaban Robert amelizungumzia sana jambo hili katika kazi zake zote. Katika Barua za Shaaban Robert, kuna waraka namba 11.9 katika ukurasa wa 196. Shaaban aliandika Waraka huu kwa Bwana mtengenezaji katika gazeti la Mambo Leo, aliupa jina la“UKIJUA KUOA NA KUACHA UJUE”’.
  • Vilevile suala hili amelijadili sana kwenye kitabu chake cha “Wasifu wa Siti Binti Saad”. Siti ameonekana kuwa mfano mwema wa wake watakiwao Afrika ya Mashariki na Afrika kwa ujumla.
  • Katika nathari yake ya “Kusadikika”, anasema; “…..hapana haja ya kudharau mwanamke. Wanawake ni Malaika, makao yao sawa na yale ya pepo…”
  • Pia katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”, tunamuona jinsi alivyomsifu Amina ukurasa wa 3. Vilevile anaendelea kumchora kwa kumtetea mwanamke katika ushairi wake. Kwa mfano katika Utenzi wa HATI katika “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”, pia na katika “Pambo la Lugha” katika shairi lisemalo “Mwanamke si Kiatu” (uk 19). Hivyo basi kwa ujumla maoni na kilio cha Shaaban Robert katika suala hili tunapata katika kuchunguza kazi zake zote ambapo anawatetea na kuwalalamikia wanaume kuwa ni watesi na wanyanyasaji wa wanawake. Pia katika maandiko ya Shaaban Robert hakuna andiko hata moja linalomzungumzia mwanamke vibaya.
3.5 LUGHA
Shaaban Robert katika kipengele cha lugha anabainika kama Mwalimu na mtetezi wa lugha, hii ni kutokana na maudhui yanayopatika kutoka katika kazi zake mbalimbali alizozifanya. Kwa mfano katika kitabu chake cha “Insha na Mashairi”, kuna Insha mojawapo ya “Lugha ya Tifa” (uk 25). Katika “Siku ya Watenzi Wote” (uk 41) anasisitiza umuhimu wa mtagusano wa lugha hususani katika kufanya tafsiri.
Pia katika ‘Diwana ya Almasi za Afrika”, kuna shairi la “Kiswahili 1” na “Kiswahili 2’ (uk 59-60), pia shairi la “Kitakoma Kiswahili” (uk 65). Vilevile katika barua zake anajitokeza mara kadhaa kumkosoa Yusufu kuhusu tahajia ya Kiswahili. Katika kazi hizo Shaaban Robert anajitokeza waziwazi kufundisha, kukemea na kurekebisha unapotokea upotoshaji wa matumizi ya Kiswahili.
3.6 UJUMI NA KITAMBULISHO CHA MWAFRIKA
Ujumi ni hali/ taaluma ya masuala ya kutambua uzuri na au ufahamu wa kitu.
Shaaban Robert alikuwa Mwafrika, aliupenda Uafrika wake na mambo yote yaliyoambatana na hali hiyo. Ithibati za kuuthamini Uafrika wake inajitokeza katika kazi zake mbalimbali kama vile;
“Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” uk 98-100, kupitia utenzi wa ADILI kajitambulisha kuwa yeye ni Mwafrika. Pia katika uk 50 anasema “…Abiria Waafrika tulikua mimi na watoto wangu…”
Pia katika “Wasifu wa Siti Binti Saad” anabainisha utamaduni na Falsafa ya mwafrika wa Kiafrika.
Majina ya Diwani zake “Almasi za Afrika” na “Mwafrika Aimba”, licha ya majina humo pia kuna mashairi yasemayo juu ya suala hili. Kama vile “Istaklahi ya Tanganyika” na ‘Fahari ya nchi yangu”. Hivyo Shaaban Robert ni Mzalendo wa dhati kwani katika kazi zake anaonesha hilo kwa kutete nchi yake na bara lake, rangi yake, utamaduni wake (Kiswahili alichokipenda ni sehemu ya utamaduni), Mila na Desturi zake, Vyakula vya Kiafrika pamoja na Wanawake wa Kiafrika.
3.7 SHAABAN ROBERT NA MAPENZI
Shaaban Robert amejadili kwa kina mapenzi katika vipengele vya maana halisi ya Mpenzi, aina za mapenzi, wapi kwa kuyapata mapenzi, mtazamo wake kuhuzu watu wanavyo ya chukulia mapenzi, faida na hasara za mapenzi.
Mapenzi anayoyajadili Shaaban Robert ni Pamoja na yale ya Kiumbe kwa Muumba wake, mzazi kwa mtoto au mtoto kwa mzazi, ndugu kwa ndugu, Ya ndoa, Jamii na Wananchi kwa nchi yao, Mapenzi ya dhati na ya chati. Katika diwani yake ya “Mapenzi Bora” suala hili la Mapenzi limejadiliwa kwa undani sana.
Mapenzi ya ndugu kwa ndugu tunayaona katika nathari ya “Adili na Nduguze”, ambapo Adili alikuwa akiwapenda sana ndugu zake Mwivu na Hasidi kiasi cha kuwagawia mali zake nusu kwa nusu pale walipofilisika.
4.0 ITIKADI YA SHAABAN ROBERT
Itikadi ya Shaaban Robert ni Usoshalisti uliopea, ijapokuwa si katika hali ya kuufikia Ukomunisti. Itikadi hiyo inasawiri hatua ya juu ya Usoshalisti unaoelekea kwenye Ukomunisti (Chuachua 2010: 180)
5.0 FALSAFA YA SHAABAN ROBERT.
Shaaban Robert anaamini kuwa wema hushinda dhidi ya ubaya. Hii inajidhihirisha katika kazi zake nyingi ambazo mwisho wake huonesha watendewao ubaya huwashinda waovu na kupata haki. Mfano kama inavyojidhihirisha katika Kusadikika, Kufikirika, Adili na Nduguze na kadhalika.
  1. MCHANGO WA SHAABAN ROBERT KATIKA FASIHI YA KISWAHILI.
Shaaban ni kiungo dhabiti baina ya fasihi ya kale na ya sasa. Shaaban Robert ni miongoni mwa waandishi wa mwanzo katika fasihi ya Kiswahili na waliotumia nguvu kubwa katika uandishi ilikuitoa fasihi ya Kiswahili sana sana utanzu wa nathari kutoka katika hali ya kihekaya na kuuingiza utanzu huu ili usawiri maisha halisi ndani ya jamii ya waswahili.
Shaaban Robert ni mmoja kati ya waasisi wa uandishi wa nathari za kitawasifu katika fasihi ya Kiswahili kupitia tawasifu yake ya “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”. Tawasifu hii yenye sehemu kuu mbili yaani “MAISHA YANGU” na ‘BAADA YA MIAKA HAMSINI”, inajumla ya kurasa 124. Katika sehemu ya kwanza ya Tawasifu hii (MAISHA YANGU), imebeba sehemu kumi na tatu (13) ambazo ni Umri, Maisha ya nyumbani, Utenzi wa Hati, Utenzi wa Adili, Mke wa pili, Idara ya forodha, Uhamisho, Mapumziko, Abiria cheo cha pili, Idara ya utunzaji wa Wanyama, Naondoka Mpwapwa, Idara ya Utawala na Nilikuwa mshairi. Sehemu ya pili (BAADA YA MIAKA HAMSINI), inasehemu zifuatazo Bima, Siasa, Mwandishi, Ukinzani, Kustaafu, Msuso, Upigishaji chapa na Matukio.
Shaaban Robert, pia ni mmoja kati ya waandishi waliochangia sana katika maendeleo ya nathari ya   Kiswahili. Baadhi ya nathari bunilizi zake ni; Adili na Nduguze, (1952), Kusadikika, (1951), Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, (1949), Kielezo cha Insha, (1954), Methali na Mifano ya Kiswahili, (1997), Kufikirika, (1968), Utubora Mkulima, (1968), Nelson, Nairobi. Siku ya Watenzi Wote, (1967), Nelson, Nairobi. Wasifu wa Siti binti Saad, (1967).
Alikuwa na mchango mkubwa, katika fasihi ya Kiswahili. “Wasifu wa Siti Binti Saad”. Ni moja kati ya nathari za kwanza kabisa za kiwasifu. Nathari hiyo inaeleza Maisha ya mwanamuziki mashuhuri wa Taarab Afrika ya Mashariki “Siti Binti Saad”.
Ndiye aliyeizindua hadhira ya kazi za fasihi ya Kiswahili kuhusu matumizi ya vionjo vya fasihi simulizi katika fasihi andishi.
Ni miongoni mwa waandishi wa wakati wake walioandika na kuchapisha kazi nyingi zaidi za fasihi ya Kiswahili.
HITIMISHO
Shaaban Robetr ni miongoni mwa wanafasihi waliyoiletea heshima kubwa tasnia ya fasihi ya Kiswahili. Kazi zao zimekuwa Lulu na mwongozo kwa wanafasihi wanaochipukia katika uga wa fasihi ya Kiswahili. Msimamo wake wakuwa mwanamapokeo ulikuwa ni msimamo wa wastani kwani sio wakati wote alizitumia kanuni za kimapokeo, alizitumia kanuni hizi pale ilipobidi na pale alipotaka kuziacha aliziacha.Vilevile Shaaban Robert kupitia kazi zake amewasaidia wanazuoni wengi kufikia malengo ya kielimu, waandishi wakongwe kama E. Kezilahabi ametumia nathari za Shaaban Robert katika tasnifu yake ya Shahada ya Uzamili.
                                       MAREJELEO
Robert, S, (1949), Maisha Yangu na Baada ya Miaka HamsiniNelson, Nairobi.
                 (1951), Kusadikika, Nelson, Nairobi.
                 (1952), Adili na Nduguze, Mcmillan, Londoni.
                 (1954),  Kielezo cha Insha, Witwatersand, Nairobi.
                 (1967), Siku ya Watenzi Wote, Nelson, Nairobi.
                  (1967), Wasifu wa Siti binti Saad, Nelson, Nairobi.
                  (1968), Kufikirika, Oxford, Nairobi.
                 (1968), Utubora Mkulima, Nelson, Nairobi.
                 (1997), Methali na Mifano ya Kiswahili, TUKI, Dar es                                          Salaam.
                 (2002), Barua za Shaaban Robert, TUKI, Dar es salaam.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)