Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
NAFASI YA VYAMA NA TAASISI MBALIMBALI KATIKA MAKUZI YA KISWAHILI
#1
Kwa Mukhtasari
IKIWA idara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), awali ikiitwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ni miongoni mwa taasisi kongwe zaidi za lugha nchini Tanzania na Afrika Mashariki. Madhumuni yake ni kusimamia usanifishaji na maendeleo ya Kiswahili.
Japo Kiswahili kimeendelea kubaki nembo ya Afrika, mjadala usio na mwisho kuhusiana na ni ipi lugha ya kufundishia katika shule na vyuo nchini Tanzania ni ithibati kwamba Kiswahili hakijapokezwa hadhi inayostahiki katika mengi ya mataifa ya Afrika Mashariki na  Kati.
TUKI, kwa sasa TATAKI, ilianzishwa mnamo 1930 ikijulikana kama International-Territorial Language (Swahili) Committee kwa nchi tatu za Afrika Mashariki na baadaye ikaitwa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.
Mnamo 1964, kamati ilifanywa kuwa sehemu ya UDSM na baadaye ikaitwa Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili. Tangu 1970 kimepewa jina la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Mwaka 2009, TUKI iliungana na iliyokuwa Idara ya Kiswahili ya UDSM na kuunda taasisi kubwa zaidi inayoitwa TATAKI.
Majukumu ya taasisi hii awali yalikuwa ni kutafiti nyanja zote za lugha ya Kiswahili, fasihi na utamaduni na kuchapisha matokeo ya utafiti huo.
Hivyo pamoja na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), TUKI ni mlinzi wa usanifu wa lugha ya Kiswahili katika Tanzania. Baada ya kuungana na Idara ya Kiswahili, sasa TATAKI inafundisha Isimu, Fasihi na Historia ya Lugha ya Kiswahili.
Inafundisha Kiswahili kama lugha ya pili hasa kwa wageni kutoka nje ya ulimwengu wa Waswahili na kuendeleza utungaji wa kamusi mbalimbali zinazohusiana na Kiswahili.
BAKITA
Ni taasisi ya serikali iliyoundwa kwa sheria ya Bunge Na.27 ya mwaka 1967 kwa madhumuni ya kukuza Kiswahili. Kutokana na sheria hii, Baraza ndilo mratibu wa kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
BAKITA imekuwa na mchango mkubwa katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili kupitia majukumu yake.
Miongoni mwa majukumu ya Baraza hili kama yalivyofafanuliwa katika sheria hiyo ni kuratibu na kusimamia maendeleo na matumizi ya Kiswahili nchini pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vinavyojihusisha na maendeleo ya Kiswahili.
Huhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida, huandaa vipindi mbalimbali redioni ili kuhimiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili, hushirikiana na mamlaka zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi, hutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali, mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali na asasi nyingine pamoja na kuidhinisha vitabu vya Kiswahili vitakavyotumika shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa.
TAKILUKI
Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa mnamo 1979 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar.
Inajishughulisha na kuratibu, kuendesha mafunzo ya Kiswahili visiwani Zanzibar, kuhariri miswada mbalimbali ili kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili na kufanya tafiti za Kiswahili katika nyanja zake zote, hususan sarufi na fasihi.
TAKILUKI inatoa ushauri wa kitaaluma kwa watunzi wa vitabu ili waweze kuandika kazi zenye ubora, na kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili kuandaa na kuendesha semina, warsha na kozi fupifupi za Kiswahili.
CHAUKIDU
Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kina makao makuu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani.
Madhumuni yake ni kuwajumuisha pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi kama vile kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote mathalan uandishi na utangazaji wa habari, uandishi na uchapishaji wa vitabu na majarida pamoja na utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika Mashariki na Kati.
Husambaza habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali na teknolojia ya mtandao wa kompyuta kuhusu vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana na Kiswahili. CHAUKIDU inaelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.
Vilevile inashauri ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera mwafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kielimu.
CHAWAKAMA
Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA), kilianzishwa mnamo 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo lote la Afrika Mashariki kupitia kwa wanafunzi wanaosoma Kiswahili vyuoni. Wanachama wa chama hiki ni wale wanaosomea taaluma za Kiswahili ila wapenzi wa Kiswahili pia wanaweza kujiunga nacho.
Mara kwa mara, CHAWAKAMA huandaa makongamano kwa lengo la kuwapa wanachama nafasi ya kujadili, kuimarisha, kuendeleza na kukuza vipawa vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili, kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa Kiswahili, kueneza Kiswahili ndani na
nje ya nchi, kushirikiana na vyama vingine katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha Kiswahili ndani na nje ya nchi wanachama, kuwaunganisha wanafunzi wa Kiswahili Afrika Mashariki na Kati katika kukikuza Kiswahili pamoja na kushirikiana na asasi mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili.
CHAKAMA
Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) ndicho cha tatu kwa umaarufu zaidi miongoni mwa wasomi, wataalamu na wahadhiri wa vyuo vikuu baada ya CHAUKIDU na Chama cha Walimu wa Lugha za Kiafrika (ALTA) ambacho haundaa makongamano yake jijini Bayreuth, Ujerumani. Kwa pamoja na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA), CHAKAMA huchapisha jarida la chama na machapisho mengine ili kusaidia kueneza taaluma za Kiswahili.
Aidha, huhifadhi kumbukumbu za wataalamu wa Kiswahili kwa nia ya kutumia katika kufanikisha malengo ya chama na wadau wa Kiswahili pamoja na kuratibu makongamano na mijadala mbalimbali inayohusiana na taaluma za Kiswahili.
Chama huandaa makongamano kila mwaka ambalo linawakutanisha wanachama wote katika vyuo mbalimbali katika nchi husika.
Katika makongamano hayo, mada mbalimbali zinazohusu Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa lakini pia maazimio mbalimbali huchukuliwa kuhusu maendeleo ya chama. Makala mbalimbali huandikwa na kuchapishwa kwa minajili ya kusomwa na watu mbalimbali.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)